BID’A YA MAWLIDI MAANA BID’AA NA UBAINISHO WA AINA ZAKE NA HUKUMU YAKE. ()

Yunus Kanuni Ngenda

Mada hii inazunguzia Maana ya Bidaa na aina zake

  |

  بسم الله الرحمن الرحيم

  MAANA BID'AA NA UBAINISHO WA AINA ZAKE NA HUKUMU YAKE.

  Imeandaliwa na Yunus kanuni Ngenda

  Imepitiwa na Abubakari shabani


  Himidi zote kwa Mola wa walimwengu wote, Ambaye ametuamrisha kufuata amri zake na ambaye ametukataza kuzusha,

  Sala na salaam zimwendee Mtume wetu Muhammad- swalla llaahu alayhi wasallam- ambaye Allah amemtuma awe kiigizo na atiiwe, na kwa Aali zake na kwa maswahaba zake na wale wote wanaomfuta.

  Ama ba'ad:

  Vipengele hivi ni katika kubainisha aina za Bidaa na Ukatazo wake, Ikiwa muqtadhwa wa kuandikwa kwake ni uwajibu wa Nasiha kwa Allah na kwa kitabu chake na kwa Mtume wake na kwa maimamu wa uislam na waislam kwa ujumla:

  Kipengele cha kwanza: Taarifu ya Bidaa- Aina zake na Hukumu yake.  TAARIFU (DEFINETION) YA BIDAA

  Bidaa ( Al-bidaa) katika Lugha (kilugha):
  Imechukuliwa kutoka katika neno (imetokana na neno)
  "Al-bidaa" ambalo maana yake ni ambacho hakina mfano wake kabla.


  Mfano kauli ya Allah taala:

  (بَدِيعُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ...)

  Yaani: Yeye ndiye aliyezianzisha mbingu na ardhi hali ya kuwa hazina mfano(hazikuanzishwa) kabla.

  Na kauli ya Allah-taala-:

  (قُلْ مَا كُنْتُ بِدْعًا مِنَ الرُّسُلِ.... )

  Yaani: Sema sikuwa wa kwanza niliyekuja na ujumbe kutoka kwa Allah kwa waja, bali wamenitangulia wengi katika Mitume,

  Na panasemwa :

  Fulani ameanzisha(amezua) uzushi, yaani ameanzishwa njia (kitu) ambacho hakutanguliwa (kwenye kuanzisha huko).

  Maana ya Bidaa kisheria: Njia iliyozushwa katika dini, ambayo(njia hiyo) inafanana na ya kisheria, inakusudiwa katika kufuata njia hiyo kuzidi katika kumuabudu Allah taala.
  ( Tazama Al-I3tiswaam ya Shaatibiy mjeledi 1/ uk.37)

  Na kuzua kupo kwa aina mbili:

  1- Kuzua katika mambo ya kiada(Ada) kama vile uvumbuzi wa mambo ya kisasa, hii "Mubaha", kwa sababu "Asili ya mambo ya kiada(ada) na Ibaha", kwa lugha ya kiarabu :

  "الأصل في العادات الإباحة"

  " Al-aswlu fiy-l-Ibaadaat Al-ibaahat"

  2- Na Kuanzisha au kuzua jambo katika dini ni Haramu; Kwa sababu Asili ya dini au asili ya ibada ni Tawqiyf (zilivyokuja ndio hivyo hivyo), Amesema Mtume- swalla llaahu alayhi wasallam- "Atakae zusha katika jambo letu hili(la dini) ambalo halikuwepo, Atarudishiwa".
  ( Ameipokea Bukhary na Muslim)  AINA ZA BIDAA
  Kuna aina kuu mbili za bidaa (kuzusha) katika dini:

  Aina ya kwanza:

  Bidaa ya Kauli ya Kiitikadi, kama wanayoyasema Jahmiyyat na Muu'tazila na Raafidwat (Shia) na makundi mengine ya upotevu na itikadi zao.

  Aina ya pili:

  Bidaa katika Ibada, kama kumuabudu Allah kwa Ibada ambayo hakuijaalia katika sheria, na hiyo iko katika aina zifuatazo:

  Aina ya kwanza: Ile inayokuwa katika Asili ya ibada- Kwa kuzusha (kuanzisha) Ibada ambayo haina asili katika Sheria, kama vile kuzua Sala ambayo haina asili katika kisheria, au saumu ambayo siyo ya kisheria au sikukuu ambazo siyo za kisheria kama vile sikukuu za kuzaliwa(mazazi) na zinginezo.

  Aina ya pili: Ile ambayo ya kuzidisha mambo katika Ibada za kisheria, kwa mfano kuzidisha rakaa ya tano katika swala ya Adhuhuri au ya Alasiri.

  Aina ya tatu: Ile ambayo ni katika Sifa za kutekeleza Ibada , kwa kuitekeleza ibada katika wasifu ambao sio wa kisheria (sio uliokuja katika sheria ya kiislam), na hiyo ni katika kufanya dhikri za kisheria, kwa sauti tena kwa pamoja na kwa mahadhi,

  Aina ya nne: Kujaalia (kukhusisha) wakati maalum kwa ibada fulani ya kisheria ambayo sheria haikujaalia wakati huo kuwa maalumu kwa ibada hiyo (yaani sheria haikujaalia ibada hiyo kufanywa kwa wakati huo maalumu), kama vile kukhusisha siku ya nusu ya mwezi wa Shaabani na usiku wake kwa Saumu (kufunga) na Qiyaam (kisimamo cha usiku), hakika swaumu na qiyaam ni mambo ya kisheria lakini kuzikhusisha Ibada hizi kwa wakati katika nyakati kunahitaji dalili.

  HUKUMU YA BIDAA

  Hukumu ya Bidaa(Uzushi) katika Dini kwa aina zake zote ni haramu na ni upotevu;

  Kwa kauli ya Mtume- swalla llaahu alayhi wasallam- Ole! wenu na mambo yenye kuzushwa , hakika kila lenye kuzushwa ni bidaa, na kila bidaa ni dhwalala (upotevu),
  [ Ameipokea Abu Dawuud, hadithi namba( 4607), na Tirmidhiy, hadith namba( 2676).]

  Na Kauli ya Nabiyyi- swalla llaahu alayhi wasallama- : Atakaezua katika jambo letu hili (la dini) kitu ambacho sio katika hilo, ni wenye kurudishwa(uzushi huo),
  Na katika Riwaya nyingine: Atakaefanya amali ambayo siyo katika jambo letu, jambo hilo ni lenye kurudishwa,
  Hadithi hii imekuwa ni dalili ya kuonyesha kuwa kila kinachozushwa katika dini ni Bidaa, na kila bidaa ni upotevu(dhwalala) na ni yenye kurudishwa.


  Na maana ya hiyo: hakika bidaa (kuzusha) katika Ibada na katika Itiqadi ni haramu, na uharamu huo unatofautiana kulingana na aina ya bidaa hiyo:

  Miongoni mwazo: ni kufru iliyokuwa wazi; kama kutufu makaburi kujikurubisha kwa aliyezikwa kwenye kaburi hilo, kumchinjia vichinjo, kumwekea nadhiri na kumtaka msaada,
  Na kama vile kauli za Jahmiyyat na Muutazila wale waliochupa mipaka.

  Na miongoni mwazo: ni zile zinazopelekea kwenye Shirki, kama kujengea makaburi na kuswali kwenye makaburi hayo na kuomba dua kupitia makaburi hayo.

  Na miongoni mwazo ni zile ambazo ni ufasiki wa kiitikadi; kama bidaa ya makhawarij na Qadaria(wapingaji wa Qadari ya Allah) na Murjia katika kauli zao na Itikadi zao zenye kukhalifu dalili za kisheria,

  Na miongoni mwazo ni maasi, kama bidaa ya Utawa na ya kukaa juani kwa aliyefunga eti aipate swaumu vizuri au thawabu ziwe nyingi.

  Allah atupe mwisho mwema na atukinge na Uzushi.