KUCHUPA MIPAKA ()

Yasini Twaha Hassani

Mada hii inazungumzia kuchupa mipaka katika Dini.

  |

  إياكم و الغلو

  JIEPUSHENI NA KUCHUPA MIPAKA

  MUANDISHI SHEKH: YASINI TWAHA

  KIMEREJEWA NA SHEKH: ABUBAKARI SHABANI

  Kwajina la Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehma mwenye kurehemu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mmoja, Rehma na Amani za Allah zimuendee nabii Muhammad (s.a.w) hakuna nabii baada yake, pamoja na ahli zake na maswahaba zake na Waislamu woote watakao fuata mwenendo wake hadi siku ya kiyama. Amma baad:

  Hakika Uislamu ni Dini ya uadilifu na ya kati kwa kati na kuacha kuchupa mipaka. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wasitani). (Al-Baqara: 143). Maana yake: Waadilifu walio bora. Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Sema: Mola wangu ameamrisha uadilifu). (Al-Aaraf: 29). Na Uislamu ni Dini nyepesi yenye huruma na kuondoa uzito. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) alikuiteni Waislam tangu zamani). (Al-Hajj: 78). Na akasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo). (Al-Baqara: 286). Na akasema: (Mwenyezi Mungu hamkalifishi mtu isipokuwa kwa kadiri ya alicho mpa. Mwenyezi Mungu atajaalia baada ya dhiki faraji). (Attalaaq: 7). Na Mtume (s.a.w) alikuwa ni mfano wa kimatendo katika hii dini, kwa hakika yeye (s.a.w) alipo mtuma Mudhi pamoja na Abaa Mussa kwenda Yemen aliwahusia kwa kusema: (Fanyeni wepesi na msifanyi uzito, wabashirieni watu yalio mazuri na wala msiwakimbize, saidianeni na wala msitofautiane). Kapokea hadithi hii imam Bukhari na Muslim. Usio huu sio kwa wawili hawa tu, bali kwa kila alio lazimishwa na sheria, inaonyesha jambo hilo kauli yake Mtume (s.a.w): (Hakika Dini ni nyepesi, na hakuna atakae fanya uzito isipokuwa itamshinda, fanyeni yalio ya sawa sawa, fanyeni yalio ya karibu, wabashirieni watu yalio ya kheri). Kapokea hadithi hii imam Bukhari.

  Hakika sheria ya Uislamu inapinga kuchupa mipaka katika dini, kwa sababu jambo hilo huondoa Uislamu katika usawa na uadilifu, kwa sababu hiyo kawakataza Mwenyezi Mungu walio pewa kitabu kutochupa mipaka katika dini yao, kwa sababu kuchupa mipaka hupelekea katika ukafiri na upotevu na kumzulia Mwenyezi Mungu kwa namna nyingi za uzushi. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Enyi Watu wa Kitabu! Msipituke mipaka katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa lilio kweli). (An-Nisaa: 171). Na akawakataza Mwenyezi Mungu wajawake waumini kutochupa mipaka katika dini kwa kuharamisha yalio mazuri, na akaeleza ya kwamba vitendo hivi nivya wakeukao wasio pendwa na Mwenyezi Mungu. Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Enyi mlio amini! Msiharimishe vizuri alivyo kuhalalishieni Mwenyezi Mungu, wala msikiuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wakiukao mipaka). (Al-Maaida: 87). Mwenyezi Mungu atujaalie tuwe niwenye kufuata sheria zaka bila kuchupa mipaka, tuwe watu wa kati kwa kati,Rehma na Amani za Mwenyezi Mungu zimshukie nabii Muhammad (s.a.w) pamoja na Ahli zake na Maswahaba zake na Waislam woote hadi siku ya Mwisho.