SIFA ZA MKE MWEMA

 Utangulizi

Himidi zote ni Zake Allaah. Tunamhimidi na kumtaka msaada na kumuomba mswamaha na tunatubu Kwake. Tunajikinga kwake kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Mwenye Kuongozwa na Allaah hakuna wa kumpoteza. Mwenye Kupotezwa na Allaah hakuna wa kumwongoza.

Nashuhudia ya kwamba hapana mola anayestahiki kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah Mmoja asiyekuwa na mshirika. Nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja Wake na Mtume Wake, Swalah na salaam zimwendee yeye, ahli zake na Maswahabaha zake wote.

Amma ba´ad...

Maudhui ya Risaalah hii iliyo na anuani ”Sifa za mke mwema” hayamuhusu tu msichana mdogo ambaye yuko katika njia ya kutaka kuolewa na anataka kujua sifa ambazo mke anatakiwa kuwa nazo ili ajiandae nazo, kuishi nazo na kuzitimiza.

Vilevile hayamuhusu tu mwanamke ambaye ameolewa ambaye anataka kuwa na sifa za mke mwema ili aweze kuzidhibiti na kuishi nazo katika maisha yake.

Vilevile hayamuhusu tu mwanamke mwenye upungufu ili aweze kutibu upungufu wake na kujisahihisha mwenyewe na ndoa yake tukufu.

Ni wito na ukumbusho ulio jumla kuliko hivyo.

Ni ukumbusho kwa baba ambaye anataka wasichana zake na wanawake ambao wako katika usimamizi wake wapate kukuwa vizuri na malezi mazuri na ndoa ambayo inaafikiana na Matakwa ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kupitia kalima hii itakuwa ni usaidizi kwake kuweza kuwakumbusha vidhibiti vya Shari´ah na sifa ambazo inatakikana kwa msichana kukuwa juu yake.

Kadhalika ni ukumbusho kwa mama ambaye ni mchungaji katika nyumba yake na wasichana wake na kuwatengeneza. Wasichana wengi wanakuwa kwa tabia na sifa mbalimbali ambazo wamepata kutoka kwa wamama zao.

Kadhalika ni ukumbusho kwa walinganiaji ili waweze kuliwekea uzito hili, kutiliia umuhimu na kufanya juhudi katika kueneza sifa hizi tukufu, tabia zilizosifiwa na kazi iliyobarikiwa ili ziweze kupatikana kwa wasichana na wanawake katika jamii ya imani na majumbani. Hili ni khaswa hivi leo wakati mwanamke ameshambuliwa kwa njia ambayo kamwe haijawahi kuonekana hapo kabla. Inafanyika kwa kutumia namna na njia mbalimbali. Malengo ni kutaka kumpotezea mwanamke heshima yake, utukufu wake, ukamilifu wake, fadhila zake, uzuri wake, imani yake, tabia yake na wema wake.

Hapo kabla ilikuwa ni vigumu sana kwa mwanamke kufikiwa na propaganda zinazoharibu, matamanio ya udanganyifu na maoni yaliyofungamana. Hilo lilikuwa likitendeka ima kwa kupitia rafiki mbaya au mfano wa hayo. Ama leo mwanamke anafikiwa na uchafu na uharibifu wote wa duniani nyumbani kwake. Hahitaji kutoka nje kwa ajili ya hilo. Sasa mwanamke anaweza kukaa chumbani mwake mbele ya TV, intaneti au magazeti machafu na akapata uchafu na shari zote katika moyo wake na fikra zake. Ili aweze kuwa mwema, mtwaharifu, mwenye Dini na mwenye kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) analazimika kufunga madirisha, njia na mwanya wa kila shari na uharibifu.

Mwanamke ana majukumu makubwa kwa wale watu ambao anawasimamia. Suala hili linahitajia kuliwekea umuhimi mkubwa kabisa.

Katika kivuli cha hali hii na upungufu wa ukumbusho na ukumbusho wa imani, tabia nzuri na maelezo mazuri ambayo mwanamke anatakiwa kuwa nayo, wanawake wengi wamekuwa wadhaifu. Wametumbukia katika kuwa na upungufu katika haya na Dini na kuanguka katika upungufu mwingi na kuathirika.

Kalima hii ni kama tulivyosema ni kuhusu sifa za mke mwema. Ninamuomba Allaah Mtukufu, Mola wa ´Arshi kubwa, afanye iwe ya kheri na manufaa na afanye iwe ni ufunguo wa kheri ufunge shari na uongoze nyoyo, uzitengeneze nafsi na ufanye kuwepo mawasiliano na Mola wa walimwengu ili Radhi Zake na Mapenzi Yake viwezi kufikiwa na kuepuka yale yanayomkasirikisha na kumghadhibikisha (Jalla wa ´Alaa).


 Kanuni ya sifa za mke mwema

Wakati tunapozungumzia kuhusu sifa za mke mwema na wema hatutakiwi kupuuza kanuni kubwa ambayo ni kanuni ya msingi ya kufikia wema, nayo ni kwamba wema hauwezi kufikiwa isipokuwa kwa mambo mawili:

Jambo la kwanza ni uafikishaji wa Allaah (Jalla wa ´Alaa), uongofu Wake, msaada Wake, usahali Wake na uafikishaji. Mwenye Kuongoza ni Allaah. Ndiye Muwafikishaji. Mambo yote yako Mikononi Mwake (Jalla wa ´Alaa). Allaah (Ta´ala) Kasema:

مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِ ۖ وَمَن يُضْلِلْ فَلَن تَجِدَ لَهُ وَلِيًّا مُّرْشِدًا

“Ambaye Allaah Amemhidi, basi yeye ndiye aliyehidika. Na Anayempotoa (kwa vile mwenyewe ametaka kupotoka), basi hutompatia mlinzi wa kumuongoza.”[1]

وَاللَّـهُ يَدْعُو إِلَىٰ دَارِ السَّلَامِ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ 

“Na Allaah Anaitia kwenye Daarus-Salaam (nyumba ya amani, Peponi), na Anamhidi Amtakaye kwenye njia iliyonyooka.”[2]

Uongofu uko Mikono Mwake, wema uko Mikononi Mwake na uafikishaji uko Mikononi Mwake. Anayotaka huwa. Asiyotaka hayawi.

Jambo la pili ni kwamba mtu mwenyewe ajitahidi kufanya juhudi kufikia wema na kufuata sababu zake zinazopelekea katika hilo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekusanya kati ya mambo haya mawili wakati aliposema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth Swahiyh:

“Pupia katika yale yanayokunufaisha na umuombe msaada Allaah.”[3]

Maana ya “Pupia katika yale yanayokunufaisha... “ ni kwa kufanya sababu zinazonufaisha na njia za kunufaisha ambazo hufikiwa kwazo wema na kupitia hayo unafikiwa uongofu.

Maana ya “... na umuombe msaada Allaah” ni kwa kumtegemea, kumuomba msaada Wake na kutaraji kutoka Kwake (Subhaanahu wa Ta´ala) kuwa Atakuwafikisha, kukupa ustawi na kukusaidia kufikia wema na msimamo. Hii ni kanuni kubwa ambayo ni pamoja na viumbe wote.

Kanuni nyingine ambayo ni lazima kuitanabahisha, nayo ni kuwa asli ya wema, elimu yake na njia ya kuuendea ni Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili hiyo ni wajibu kwa kila ambaye anakumbusha na analingania katika wema na mtengenezaji kujengea kila kitu juu ya Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jalla) na Sunnah za Mtume Wake Mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Ta´ala) Anasema:

إِنَّ هَـٰذَا الْقُرْآنَ يَهْدِي لِلَّتِي هِيَ أَقْوَم

“Hakika hii Qur-aan inaongoza katika yaliyonyooka kabisa.”[4]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya Sunnah na uongofu wake:

“Nimewaachia mambo mawili ambayo mkishikamana nayo hamtopotea; Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu.”[5]

Kujengea juu ya hayo maudhui yetu ni sifa za mke mwema kwa mujibu wa Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kila sifa itakayotajwa hapa itakuwa ikisapotiwa na dalili yake katika Kitabu cha Allaah au Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kanuni ya tatu na ndio msingi ambao kumejengeka juu yake ´ibaadah, fadhila na ukamilifu wote, nayo ni kumcha Allaah. Kumcha Allaah (Ta´ala) ndio msingi wa fadhila, kheri na furaha katika dunia na Aakhirah. Lililo la wajibu kwa mwanamke wa Kiislamu ajue kwamba anamuabudu Allaah na kufikia Radhi za Allaah na ujira pindi atakapoishi kwa kushikamana na adabu za Kishari´ah na kuwa na sifa tukufu. Kwa upande mwingine huenda akakosa hilo kutokana na kiasi ambacho atakavyoanguka kwa ufupi katika sifa hizi. Hili litatajwa kwa kirefu wakati itakapokuja maudhui yake.


 Mke mwema uhusiano wake na Allaah

Kitu cha kwanza nitachoanza nacho ni yaliyotajwa kuhusu sifa za mke mwema katika Suurat an-Nisaa´:

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ “Basi wanawake  wema  watiifu [kwa Allaah], wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah.”[6]

Katika sehemu hii ya Aayah Allaah Ameleta maelezo na sifa zote ambazo mwanamke mwema anatakiwa kuwa nazo. Andiko hili tukufu linatuonesha kwamba mke mwema ni yule mwenye sifa mbili:

Sifa ya kwanza inahusiana na uhusiano wake kwa Mola Wake.

Sifa ya pili inahusiana na uhusiano wake kwa mume wake.

Uhusiano wake kwa Mola Wake ni katika Kauli Yake (Subhaanahu):

قَانِتَاتٌ

“... watiifu [kwa Allaah]... “

Ina maana ni mwenye kudumu katika kumtii Allaah, anahifadhi ´ibaadah na utiifu kwa Allaah, kutilia umuhimu faradhi za Uislamu na kuacha kuyaapuza. Yote hayo yanaingia chini ya Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

قَانِتَاتٌ

“... watiifu [kwa Allaah]... “

Sehemu ya pili katika Kauli Yake (Subhaanahu wa Ta´ala):

حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“... wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah... ”

Ina maana anahifadhi haki za mume wake pindi anapokuwa hayupo na ushuhuda. Anamhifadhi katika mali zake, rafiki wa kitandani, haki zake wajibu wake:

حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ

“... wenye kuhifadhi (hata) wanapokuwa hawapo (waume zao) kwa Aliyoyahifadhi Allaah... ”

Ina maana hawezi kufanikiwa kufanya hilo kwa sababu yeye ni mtu wa sawasawa, mwenye akili, fahamu na mwerevu, isipokuwa ni kutokana na uafikishaji wa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kumrahisishia hilo. Hili linatukumbusha yale niliyotaja karibuni, nayo ni kwamba uzuri na wema ni kutokana na uafikishaji wa Allaah, usahilishaji Wake na Msaada Wake.

Katika Kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

قَانِتَاتٌ

“... watiifu [kwa Allaah]... “

kunaingia ndani yake mwanamke ambaye anahifadhi faradhi za Uislamu. Kuna Hadiyth nyingi ambazo zimepokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusiana na maana hii. Miongoni mwazo ni yale aliyopokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh”[7] yake kupitia Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali [Swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataingia mlango wowote wa Peponi autakao.”

Imaam Ahmad amepokea katika “al-Musnad”[8] yake kupitia kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke akiswali [Swalah zake] tano, akafunga mwezi wake, akahifadhi tupu yake na akamtii mume wake, ataambiwa: “Ingia Peponi kwenye mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Tunampa hongera mwanamke wa Kiislamu kwa ahadi hii tukufu na fadhila kubwa na kheri ambayo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) Amemuahidi nayo. Inahusiana na mambo mane tu ambayo anaweza kuyahesabu kwa kutumia mkono wake mmoja kwa vidole vyake na si kwa kutumia [mikono] miwili. Akiishi kwa kuyahifadhi mambo mane ataambiwa siku ya Qiyaamah:

“Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Hivi kweli mwanamke ambaye anajitamania kheri juu ya nafsi yake si awekee uzito na kutilia umuhimu sifa hizi na kudhibiti matendo haya? Anatakiwa kuhifadhi Swalah zake, Swawm, tupu na haki za mume wake ili aweze kushinda ahadi hii tukufu na fadhila na kheri hii kubwa ili aweze kuambiwa siku ya Qiyaamah:

“Ingia Peponi kwa mlango wowote wa Pepo uutakao.”

Msingi wa wema wa mwanamke uko katika wema wake kwa Mola Wake kwa kumtii, kujikurubisha Kwake na kudhibiti ´ibaadah Zake. Wema na msimamao huu ndio siri ya mafanikio yake, kushinda kwake na uafikishaji katika maisha yake kukiwemo na maisha yake ya ndoa, watoto wake kuwa wema na kizazi chake na kuishi kwake maisha ya baraka na mazuri.

Kwa ajili hiyo ndio maana ikawa ni jambo lililosisitizwa kwa yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri na kwa wasimamizi ambao wanawatakia wasichana wao kuwalea wanawake juu ya wema, msimamo, kuhifadhi ´ibaadah, faradhi za Uislamu na khaswa Swalah tano na kufunga mwezi wa Ramadhaan na kujitenga mbali na mambo yote yanayoathiri utwaharifu wa mwanamke na utukufu wake. Ni hayo ndio yamebainishwa katika Hadiyth hii:

“... Akahifadhi tupu yake... “

Mwanamke kuhifadhi tupu yake ni jambo linalohitajia kutoka kwake na kwa walii wake kufunga milango na njia zote kwa yale yanayoharibu, yanayopelekea katika shari na kusababisha madhambi. Hili ni jambo kubwa ambalo kwa kila yule mwenye kuitakia nafsi yake kheri anatakiwa kuilea nafsi yake juu ya hilo. Anatakiwa kuihifadhi nafsi yake daima katika kumtii Allaah, kumuabudu Allaah na kujikurubisha Kwake (Subhaaahu wa Ta´ala) kwa yale yanayomridhisha katika maneno mema na matendo mazuri. Allaah Akimneemesha mume mzuri na wa sawa, ni juu yake kumcha Allaah kwa kuhakikisha anachunga haki za mume wake tokea ile siku ya kwanza ya ndoa.

Hili linawajibisha kukumbusha juu ya suala ambalo kosa lake limekuwa ni lenye kuenea na kusambaa. Nalo linahusiana na israfu na ubadhirifu unaokuwa katika usiku ule wa ndoa na katika matumizi ya ndoa. Hili ni jambo ambalo khatari yake ni kubwa na madhara yake ni makubwa mno. Wanawake wengi wanapoelekea katika kutaka kuolewa wanachozingatia ni yale ya nje na wanawake wa rika sawa naye. Wanatazama ni nini walichofanya wanawake wengine katika ndoa mbalimbali. Wanafikiria kwa njia hiyo na hivyo kunakuwa israfu na ubadhirifu. Wanapoteza vingi na pesa nyingi katika visivyokuwa na maana. Aidha kunaweza kuwepo hata maovu na mambo ya haramu. Kwa ajili hiyo mwanzo huu unakuwa na utangulizi wa ndoa ni sababu ya ukosefu wa baraka na kheri.

Hali huwa sivyo ikiwa mwanamke na familia yake watajitenga mbali na hayo, kujiepusha na israfu, mambo ya maasi na madhambi na wakafanya matumizi kuwa rahisi na pasina israfu wala ubadhirifu. Katika hali hii huja kheri na kufikiwa baraka. Imekuja katika Hadiyth Swahiyh katika “as-Sunan” Abu Daawuud[9] imepokelewa na ´Uqbah bin ´Aamir (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Bora ya ndoa ni ile iliyo rahisi.”

Katika Hadiyth nyingine imesemwa:

“Wanawake walio na baraka zaidi ni wale wenye matumizi rahisi.”[10]

Wanawake bora ni wale walio rahisi.

Kwa ajili hii ndio maana inatakikana kwa mwanamke na kwa wazazi wake wahakikishe ndoa iwe rahisi na isiwe na ugumu, unyenyekevu na sio kiburi, nzuri na yenye utulivu na kusiwe israfu na ubadhirifu. Mambo yote haya yana taathirika katika maisha ya ndoa kwa uzuri na ubaya.

Ikiwa ndoa ni rahisi na ikafanywa kuwa sahali na kujiepusha na mamabo ya israfu, hukabiliwa na baraka na kheri.

Kama ndoa iko na israfu, ubadhirifu, maasi na aina mbalimbali ya dhambi, ni baadhi ya sababu kubwa ya kukosekana baraka na tunaomba Allaah Atukinge. Mke mwema uhusiano wake na Shetani

Sifa nyingine ambayo mke mwema anapaswa kuwa nayo ni kwamba atahadhari na Shetani aliyefukuzwa. Kazi ya Shetani katika maisha haya ni kuharibu. Anaharibu Dini, tabia, mu´amala, mshikamano, udugu na lililo la kheri. Kila siku anatuma wajumbe na askari kutimiza kazi hii. Zingatia Hatiyth hii katika “as-Swahiyh” ya Muslim imepokelewa na Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Iblisi hukiweka kiti chake katika maji. Kisha anatuma

vikosi vyake. Yule mwenye nafasi kubwa kwake ni yule

mwenye fitina kubwa. Pindi mmoja wao anamjia anamuuliza aliyofanya. Wakati anaposema aliyofanya, anamwambia: “Hujafanya kitu.” Wakati mwingine anamjia na kusema: “Sikumuacha mpaka nimehakikisha nimemfarikanisha yeye na mke wake” hivyo anamchukua na kumwambia:

“Wewe ni mzuri ulioje!”[11]

Anawatuma askari na wajumbe ili waende kuharibu. Anayekuwa karibu na yeye ni yule ambaye anasababisha matatizo kati ya watu. al-A´mash amesema kwamba Shetani anamkumbatia na kuchukua askari ambao wanafarikanisha kati mwanamke na mume wake.

Mwanamke mwema anatakiwa kufahamu na kuelewa uhakika huu. Hali kadhalika mume. Wote wanapaswa kufahamu kwamba kuna adui aliyejificha. Anakuona, lakini wewe huwezi kumuona. Anapita ndani ya mwili wako kama damu inavyopita kwenye mishipa. Anapuliza na kutia wasiwasi. Anapanga hila na njama. Anafanya yote hayo bila ya wewe kumuona. Anauzungumzisha moyo wako wewe mume na moyo wa mke. Anakuja na mashaka yanayopelekea katika uadui. Ana njia nyingi za ufanya kazi wake.

Kwa ajili hii imekuja katika Sunnah jinsi ya mtu atakavyojikinga kutokana na Shetani wakati mtu anapoingia nyumbani kwake, wakati wa maingiliano, wakati wa chakula, wakati anapokuwa na hasira na mambo mengine yote ambayo mtu anahitajia kujikinga kutokana na Shetani ili Shetani asiweze kuwa na ushirikiano wowote na watu wa nyumbani kwake, nyumba yake na watoto wake. Hivyo anahitajia mtu kuikinga nafsi yake na Adhkaar zilizobarikiwa, Qur-aan Tukufu,  Du´aa zilizopokelewa na kuhifadhi utiifu na ´ibaadah za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Mke mwema anapaswa kujihadhari na kampeni za Shetani na wasiwasi wake autiao katika nasfi na ambao unaharibu uhusiano na maisha ya ndoa.

Ni familia ngapi na nyumba ambazo amefarikanisha daima kwa kumtii Shetani na kufuata wasiwasi wa Shetani? Lau kila mmoja angeliomba kinga kwa Allaah kutokana na Shetani aliyefukuzwa na kujiweka na kujitenga mbali na uchochezi wake na wasiwasi wake kusingelitokea mambo hayo na mfarakano huo.

Ni majumba mangapi kumetokea mfarakano kwa sababu ya kumtii Shetani? Kisha baadaye huyu muharibifu – askari wa Shetani – anaenda kwa Iblisi ili aweze kupata nafasi ya kuwa karibu naye pindi atakapomuhadithia alivyofarikanisha kati ya muma na mke.

Kuna kitu cha manufaa ambacho ni lazima kukumbuka. Huyu adui aliyejificha ambaye anakuona na ambaye wewe huwezi kumuona na uzowefu mkubwa. Leo wakati kunapozungumziwa baadhi ya waajiriwa wa kampuni na uzowefu wao mara nyingi huwa ni uzowefu wa miaka khamsini au sitini. Lakini uzowefu wa Iblisi wa kupotosha, kuzuia watu na njia ya Allaah na kueneza uadui kati ya watu? Ni uzowefu wa maelfu ya miaka. Ni watu wangapi wamekufa na kuzikwa baada ya kuwa ni wafungwa wa Shetani na kutumbukia katika uharibifu na upotoshaji wake?  Kwa ajili hii ndio maana ni lazima nyumba ya Muislamu ajikinge yeye mwenyewe na kuiweka mbali na Shetani aliyefukuzwa.


 Mke mwema anatakiwa kumfurahisha mume

Katika sifa zingine za mke mwema ni kwamba anamfurahisha mume wake pindi anapomtazama sura yake, muonekano wake, sifa zake na mavazi yake yamfurahishe pindi mume wake anapomtazama. Anapaswa awe ni mwenye kujiandaa kwa kumtii na kutimiza maamrisho yake bila ya kuchukia na bila ya kuwa na kiburi. Zingatia Hadiyth katika “as-Sunan” ya an-Nasaa´iy[12] imepokelewa na Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa juu ya mwanamke bora. Akajibu:

“Ni yule mwenye kumfurahisha [mume wake] pindi anapomtazama, anamtii pale anapomuamrisha na haendi kinyume juu ya nafsi yake mwenyewe na mali yake

dhidi ya anayoyachukia.”[13]

Namna hii ndivyo anavyotakiwa kuwa kwa njia ya sura na sifa. Anatakiwa kutilia uzito mkubwa juu ya sura na muonekano wake wakati anapokuwa mbele yake. Kadhalika anatakiwa kutilia uzito na kutilia umuhimu kwa kutimiza maamrisho yake, hamu yake na haja zake.

Kwa masikitiko makubwa wanawake wengi wanatilia umuhimu kujipamba na kujipodoa tu wakati wanapotaka kutoka nyumbani kwenda katika mnasaba wa sikukuu, mkusanyiko na mfano wa hayo. Lakini wakati mume anapoingia nyumbani anamkuta katika mavazi mabaya na kunuka. Nywele zimevurugika na hazikutengenezwa. Anamkuta kwa sifa ambazo zinamkimbiza kwake. Halafu anakuwa ni mwenye kuumia kwa yeye kila siku kujipamba pindi anapotoka nyumbani bila hata kupata moja ya kumi. Vipi mwanaume atamtamani mwanamke kama huyu ambaye hizi ndizo sifa zake? Ni mahaba sampuli gani ambayo atakuwa nayo kwa mwanamke ambaye yuko namna hii? Hii ni dalili inayoonesha ujinga wa mwanamke na upungufu wa akili yake kwa kuhakikisha maisha ya ndoa na mafanikio yake.

Aidha kuna wanawake wengi ambao ni waasi na wapekutevu. Wanawapuuza waume zao na kuwakasirikisha. Kunalalamikiwa sana juu ya tabia zao kwa waume zao na wengine. Mwanamke huyu anakuwa ni mwenye kuleta maisha magumu, maisha ya taabu na maisha ya udhaifu nyumbani kwake na anakuwa ni mwenye kuizika nafsi yake mwenyewe kwenye kaburi.

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh”[14] yake kupitia kwa Jaabir (Radhiya Allaahu ´anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mmoja wenu anapofika wakati wa usiku [kutoka safari] asiwajie familia yake.”

Asimshtukizie mke usiku. Kwa nini? Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ili mwanamke ambaye mume wake alikuwa hayupo aweze kujinyoa na mwanamke wa nywele zilizovurugika aweze kuchanua nywele zake.”

Hapa kuna funzo tukufu kwa mwanamke. Nalo ni kwamba anatakiwa kumkaribisha mume wake kwa ukamilifu wa usafi, sura nzuri na mkutano mzuri. Hili khaswa pale ambapo mume wake alikuwa hayupo au amesafiri. Hili linahitajia kwa mwanamke kuweza kujiandaa na kujitayarisha. Hili linahusu hata kufanya utaratibu wa nyumba na muonekano wake. Mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha) ameelezea:

“Alikuja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika safari. Nikawa nimefunika mapazia yangu kwa kusahua na yalikuwa

na picha. Wakati (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipiona akairarua na kusema: “Watu watakaokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni wale wanaoigiza viumbe wa Allaah. Tukafanya mto mmoja au

mito zaidi.”[15]

Kwa nini aliweka mapazia haya? Kwa kuwa alitaka atakapoingia (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) nyumbani akute nyumba na yeye mwenyewe katika sura nzuri.

Katika Hadiyth hii tunapata faida kwamba mwanamke anatakiwa kutengeneza nyumba yake na kuipanga kama ambavyo vilevile inatakiwa kwake kujitayarisha maandalizi kwa njia ya kikamilifu na kukutana na mume wake kwa njia nzuri. Hizi zote ni sifa zilizokuja katika Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) za mwanamke na mke mwema.

Miongoni mwa hayo ni yale yaliyopokea at-Twabaraaniy katika “al-Mu´jam al-Awsatw”[16] kupitia Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anhu) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Je, nisiwaeleze wanawake wenu Peponi?”

Yaani mke mwenye sifa zinazosifika na kazi yenye kubarikiwa akawa ni mwenye kustahiki kuwa Peponi. Akaendelea na kusema:

“Kila mwanamke mwenye mahaba na mwenye rutuba ambaye, pindi anapokasirika au akafanyiwa vibaya au mume wake akakasirika, anasema: “Naweka mkono wangu kwenye

mkono wako. Sintosinzia mpaka utapofurahi.”

Bi maana hatofumba macho, hatolala wala kufurahi mpaka awe radhi naye.

Kwa masikitiko makubwa kuna wanawake wanaolala pasina kujali waume zao wamekasirika usiku wa kwanza, usiku wa pili, usiku wa tatu, usiku wa kumi au mwezi mzima. Kana kwamba jambo hili halimuhusu kabisa. Kana kwamba hatokuja kukutana na Allaah (Subhanaahu wa Ta´ala) na kumhesabu kwa matendo haya anayoyafanya.


 Mke mwema anatakiwa kumtii mume

Katika sifa za mke mwema ni yale yaliyopokelewa katika “as-Sunan” ya al-Bayhaqiy[17] kupitia kwa Abu Udhaynah ambaye kaeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wabora ya wanawake zenu ni wale wenye mahaba na

wenye rutuba walio na maafikiano na wanausia kumcha Allaah. Waovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa meupe kwenye mbawa na makucha.”

Zitazame hizi sifa alizo nazo mke mwema.

“...wenye mahaba... “ Hii ni sifa ambayo ni tukufu na yenye kusifiwa kwa yule mwanamke mwema na yule mke aliyebarikiwa. Bi maana kwamba anapenda na kufanya aweze kupendwa. Hakuna mwingine anayestahiki mapenzi haya kama mume. Anatakiwa kuhakikisha ampende na kuamsha hisia na huruma wake kwa maneno mazuri ya kupendeza. Anatakiwa kuhakikisha ampende kwa kutaamiliana naye vizuri na kuonekana vizuri. Mke anatakiwa kuhakikisha ameshinda kuweza kuyapata mapenzi ya mume kwa maneno yake, muonekano, matendo na tabia.

“...wenye rutuba... “ Bi maana azae watoto wengi. Ni sifa yenye kusifika kwa mwanamke. Mwanamke huyu ni katika wanawake bora. Ikiwa mwanamke yuko na ila yoyote au maradhi ni jambo ambalo halitomdhuru kwa kuwa sio jambo ambalo amezembea yeye au amefanya kwa khiyari yake. Allaah Hatomhesabu kwa hilo. Hili halimdhuru na wala haliathiri chochote katika wema wake.

Ama ikiwa mwanamke ni mwenye rutuba lakini akawa ni mwenye kuzuia ujauzito na watoto, anadhurika kwa hili. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Oeni wanawake wenye mahaba na rutuba. Mimi nitajifakhari wingi wenu kwa Ummah zingine siku ya Qiyaamah.”[18]

Linalotakikana kwa mwanamke ni kujitahidi kupata watoto na kutilia uzito katika kuwalea watoto na kuwaangalia. Vilevile ahesabu thawabu kutoka kwa Allaah kwa kupatikana katika jamii watoto wema na walinganiaji wanaotengeneza. Ahesabu hilo tokea siku ile ya kwanza anapoolewa. Azungumze baina yake yeye na Allaah Amkirimu wavulana watakaokuja kuwa maimamu wa uongofu, wanachuoni wa waislamu na walinganiaji katika kheri. Kwa hili aandikiwe thawabu kubwa kwa nia yake nzuri na kila kinachofanya hilo.

“... walio na maafikiano... “ Bi maana asiwe ni mkali na mgumu. Anatakiwa kuwa msikivu na mtiifu. Hatakiwi kuwa ni mwenye kiburi na majivuno. Hatakiwi kumdharau mume. Hatakiwi kuwa muasi na mpekutevu.

“...wanausia... “ Bi maana mwenye kumuusia na kumliwaza mume wake na kusimama karibu naye. Anatakiwa awe ni mwenye kumsaidia katika kheri na katika kumtii Allaah na kila kinachofanya kuleta furaha na mafanikio.

“... kumcha Allaah... “ Bi maana sifa hizi zinakuwa ni zenye kunufaisha kwanza pindi mwanamke atakapomcha Allaah (´Azza wa Jalla). Lau atakuwa ni mwenye mahaba, rutuba, maafikiano na mwenye kuusia kwa kutafuta mambo ya kidunia na sio kwa ajili ya kumcha Allaah, sifa hizi hazitoleta manufaa yoyote wala hazitomfaa. Sifa hizi zitamnufaisha tu ikiwa anazifanya kwa kutafuta kupata Radhi za Allaah (´Azza wa Jalla) na akaishi juu ya uchaMungu.

“Muovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao... “ Bi maana wale wenye kuonyesha mapambo yao na kutoka nje kwa kujipodoa, msafi, mzuri, kwa kujiweka manukato na kujipodoa ili Shetani aweze kumfuata nyuma yake na kuharibu jamii. Mwanamke mwenye kutoka kwa sifa hizi anafanya hivyo ili apate kuwa mmoja katika askari wa Iblisi na kumsaidia kuiharibu jamii. Malengo ni kusambaza fitina na kueneza machafu kwa waumini.

“... wenye kiburi... “ Bi maana walio na kiburi. Kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kiburi. Mwanamke anayekwenda nje barabarani na kwenye masoko na ni mwenye kuonyesha mapambo, kajipodoa, kajitia manukato na kujipendezesha hawezi kwenda hivyo wakati huo huo akawa ni mwenye haya na mnyenyekevu kwa Allaah (Ta´ala). Anatoka hali ya kuwa ni mwenye kiburi, kujiweka juu na mwenye jeuri. Anakuwa ni mwenye kuzowea, katika muonekano wake na sura yake. Hivyo kuna mafungamano baina ya kuonyesha mapambo na kuwa na kiburi kama jinsi kuna mafungamano baina ya kuwa na heshima na haya.

Mwanamke mwenye heshima anakuwa na haya kamilifu. Moyo wake unakuwa ni wenye kujaa haya. Mwanamke mwenye kuonyesha mapambo yake anakuwa amevua Jilbaab ya haya na badala yake anavaa Jilbaab ya kiburi, kujiona na kiburi. Linamdhuru yeye, maisha yake ya ndoa na maisha yake yote. Ndio maana mwenye kuwa namna hiyo akasifiwa kuwa ni muovu katika wanawake. Kasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Muovu ya wanawake zenu ni wale wenye kuonyesha mapambo yao na wenye kiburi na ni wanafiki. Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa meupe kwenye mbawa na makucha.”

Lini unaona jogoo ilio na madoa meupe kwenye mbawa zake na makucha yake? Ni zaidi ya mara kidogo sana kupata jogoo namna hiyo. Mara nyingi unaona jogoo yote huwa mweusi. Anasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakuna yeyote katika wao atakayeingia Peponi isipokuwa watakuwa ni mfano wa kiasi cha jogoo zilizo na madoa

meupe kwenye mbawa na makucha.”

bi maana ni idadi ndogo sana ya wanawake kama hawa watakaoingia Peponi. Kwa kuwa aina hii ya jogoo ni ndogo sana.

Hadiyth hii inafanana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wanawake! Toeni Swadaqah kwa wingi na mumuombe

Allaah mswamaha. Nimeona Moto nyinyi ndio wakazi

wengi wa Motoni.”[19]

Kwa nini ameona wakazi wengi wa Motoni ni wanawake? Utakaposoma katika Sunnah kuhusu sifa hizi za wakazi wabaya wa Motoni utaona kuwa wanawake wengi wanapuuza na hawajali kabisa. Kana kwamba hatosimama mbele ya Allaah siku ya Qiyaamah na kumhesabu kwa hilo. Anaweza kufikiwa na Hadiyth na ujuzi juu ya suala hili, lakini anachojali tu yeye ni matamanio yake na matakwa yake.

Kuna Hadiyth nyingi zimekuja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambazo zimetaja sifa za mwanamke anayelaumika. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) anasema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amemlaani mwanamke anayerefusha nywele na mwenye kurefushwa, mwanamke anayepiga chake (tattoo) na mwenye kupigwa chale.”[20]

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake na wanawake

wanaojifananisha na wanaume.”[21]

Mbali na Hadiyth hizi na zingine zinazomlaani mwanamke kwa sifa mbalimbali  utaona ni wanawake wangapi wanaosikia laana na kuwekwa mbali na Rahmah ya Allaah hata hivyo hawajali kabisa. Kana kwamba hawatosimama mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) na kuulizwa juu ya hayo. Kana kwamba haitokuja siku ambapo atawekwa ndani ya shimo na kufunikwa na mchanga na kusimama mbele ya Mola Wake kwa matendo yake. Anapuuza yote haya. Hafikirii lolote. Hamu yake kubwa anachojali ni kujipodoa na kujipamba hata kama kile anachokifanya ni kumuasi Allaah, kwenda kinyume na maamrisho ya Allaah na kujiweka mwenyewe katika Ghadhabu na Hasira za Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala).

Kuna sifa zenye kulaumika kumekuja ubainishaji wake katika Sunnah kwa wanawake ili mwanamke mwema aweze kuwa katika hadhari. Malengo la mwanamke kuzijua sifa hizi ni ili aweze kujiepusha nazo. Mshairi anasema:

Nimejifunza shari sio kwa ajili [ya kuitaka hiyo] shari, kwa ajili nijitenge nayo

Yule asiyetofautisha kati ya jema na shari hutumbukia ndani yake


 Mke mwema anatakiwa kutofanya upungufu katika haki za mume

Katika sifa za mke mwema ni kutofanya upungufu katika haki za mume wake. Anatakiwa kutilia uzito na juhudi katika kumtumikia. Zingatia juu ya hili ambalo an-Nasaa´iy amepokea katika “as-Sunan al-Kubraa”[22] kupitia kwa Huswayn bin Mihsan kutoka kwa shangazi yake ambaye ameeleza ya kwamba aliingia kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutekeleza haja. Baada ya kumaliza haja yake akamwambia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, wewe una mume?” Akasema: “Ndio.” Akamuuliza: “Uko vipi kwake?” Akasema: “Ninamfanyia kila kitu.” Akamwambia: “Tazama ulivyo kwake. Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.”

Ni lini mume wa mke anakuwa ni Pepo yake na ni lini anakuwa ni Moto wake?  Hapa ni lazima kwa mwanamke kufahamu uhakika huu na jambo hili kubwa.

“Uko vipi kwake?” Una ya wajibu na wewe ni mja wa Allaah. Kuna Pepo na Moto. Allaah (´Azza wa Jalla) Amekuamrisha na kukuwajibishia kutimiza haki hizi za mume. Zitimize. Zitekeleze kwa njia nzuri kabisa na kikamilifu ili kumtii Allaah na kufikia Radhi Zake (Subhaanahu). Timiza wajibu wako na muombe Allaah haki zako:

“Kwani yeye ndio Pepo yako na Moto Wako.”


 Mke mwema hamtii mume wake uzito katika matumizi

Katika sifa za mke mwema ni kutomtia mume uzito kwa matumizi na kutumia mali ya mume kwa israfu na ubadhirifu. Anatakiwa kuwa mkati na kati:

وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامً

“Na wale ambao wanapotoa huwa hawafanyi israfu na wala hawafanyi uchoyo na wanakuwa wastani baina ya hayo.”[23]

Wacha tuzingatie katika mlango huu yale ambayo Abu Sa´iyd na Jaabir wamepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kwamba siku moja alisimama na kukhutubu kwa kirefusha na akataja mambo ya duniani na Aakhirah na akasema:

“Wakati Wanawaisrael walipoangamia mara ya kwanza

ilikuwa ni mwanamke wa fakiri mmoja alikuwa akimkalifisha [mume wake] mavazi na vipodozi yale anayokalifisha mwanamke wa tajiri. Kulikuwa mwanamke mmoja mfupi ambaye alikuwa akitumia mbao mbili za miguu na alikuwa na pete yenye kufungwa ambayo alikuwa akiijaza miski. Akatoka nje kati

ya wanawake wawili warefu. Wakatuma mtu awafuate [hawa wanawake watatu]. Akawajua wale wanawake wawili warefu

 na akawa hakumjua yule mwanamke wa miguu ya mbao.”[24]

Wakati wanaisrael walipoangamia ilianza kwa mwanamke wa fakiri mmoja kumkalifisha mume wake vipodozi na mapambo ambayo mwanamke wa tajiri anamkalifisha mume wake. Tazama huyu mwanamke mfupi amevyofanya israfu, ubadhirifu wa mali katika mambo yasiyokuwa na faida, udanganyifu na kutokinaika na yale Aliyomuandikia Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Mwanamke mwenye kuvaa viatu vya kisigino kirefu anakumbusha huyo mwanamke. al-Lajnah ad-Daaimah wametoa fatwa ifuatayo:

“Kuvaa viatu vya kisigino kirefu haijuzu. Vinamtia mwanamke katika khatari. Shari´ah imemwamrisha mtu kujiepusha na madhara. Allaah (Ta´ala) Amesema:

وَلَا تُلْقُوا بِأَيْدِيكُمْ إِلَى التَّهْلُكَةِ  “Wala msijitupe kwa mikono yenu katika maangamizi.”[25]

وَلَا تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ۚ إِنَّ اللَّـهَ كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا “Wala msijiue. Hakika Allaah kwenu ni Rahiymaa (Mwenye kurehemu).”[26]

Vilevile vinamuonesha mwanamke kuwa mrefu na makalio zaidi ya alionayo. Ni udanganyifu na kuonyesha baadhi ya mapambo ambayo imeharamishwa kuyaonesha.


 Mke mwema hatakiwi kukufuru neema kwa mume wake

Katika sifa za mke mwema ni kuwa si mwenye kukufuru neema anazopewa. Kwa msemo mwingine ni  kwamba hakufuru neema ambazo Allaah (Tabaaraka wa Ta´ala) Anazompa kupitia mume wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyewashukuru watu hamshukuru Allaah.”[27]

al-Bukhaariy amepokea katika “al-Adab al-Mufrad”[28] kupitia kwa Asmaa´ bint Yaziyd al-Answaariyyah ambaye amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alinipitia wakati nilikuwa nimesimama

 na kundi la wanawake wenye umri mmoja nami. Akatusalimia na kusema: “Tahadharini na kukufuru neema.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nini maana ya kukufuru neema?” Akasema: “Huenda mmoja wenu ndoa yake ikaakhirishwa kisha baadaye Allaah Akamruzuku mume na akapata naye watoto. Wakati anapokuwa ni mwenye kukasirika siku moja anakufuru na kusema: “Sijawahi kamwe kuona kheri yoyote kutoka kwako.”

an-Nasaa´iy amepokea katika “as-Sunan” al-Kubraa”[29] kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah Hamtazami mwanamke ambaye hamshukuru mume wake wakati huo huo hawezi kujitosheleza naye [kukosa kuwa pamoja naye].”


 Mke mwema anatakiwa kumheshimu mume wake

Katika sifa za mke mwema ni kwamba anamuheshimu mume wake na anajua nafasi yake na haki zake. Kumekuja Hadiyth nyingi kuhusu hili. Moja wapo ni yale aliyopokea at-Twabaraaniy katika “al-Muj´am al-Kabiyr”[30] kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Simwamrishi yeyoye kumsujudia yeyote.Lau ningelimwamrisha mtu kumsujudia yeyote, basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mume wake.”

at-Twabaraaniy amepokea katika “al-Muj´am al-Kabiyr”[31] kupitia Zayd bin Arqam kwamba Mu´aadh amesema:

“Ewe Mtume wa Allaah! Watu wa kitabu wanawasujudia maaskofu na wakuu wao; je, tusikusujudie? Akasema: “Lau ningelimwamrisha mtu amsujudie yeyote basi ningelimwamrisha mwanamke kumsujudia mume wake. Mwanamke hakutimiza haki za mume wake mpaka pale ambapo atakapomuomba kufanya naye jimaa wakati yeye atakuwa ameketi juu ya

 tandiko dogo na akamtii.”

Haki za mume zinakuwa maradufu ikiwa ni mwema, mchaMungu, mtu wa Dini na anahifadhi ´ibaadah za Allaah na kumtii. at-Tirmidhiy na Ibn Maajah wamepokea kupitia kwa Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anhu) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mwanamke ambaye anamuudhi mume wake katika maisha haya isipokuwa mke wake katika al-Huur al-´Ayn anasema: “Usimuudhi, Allaah Akuue! Ni mgeni kwako

tu. Karibuni atakuacha na kuja kwetu.”[32]

Wanachuoni wanasema kwamba katika Hadiyth hii kuna matishio makali kwa wanawake wanaowaudhi waume zao.


 Mke mwema anatakiwa kuwa muadilifu kwa watoto wake

Katika sifa za mke mwema ni kwamba Allaah Akimneemesha kwa kumpa watoto anafanya uadilifu baina yao. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu. Fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu.”

Hadiyth hii imepokelewa na Abu Daawuud[33] na kumekuja Hadiyth nyingi kwa maana kama hii.


 Mke mwema anatakiwa kubaki nyumbani

Katika sifa za mke mwema ni kwamba anabaki nyumbani na hawi ni mwenye kutoka na kuingia nyumbani kila wakati. Anatoka nje tu wakati wa haja. Anapotoka hawi ni mwenye kujipodoa na uso ukiwa wazi. Anatakiwa kuteremsha chini macho yake na kuhifadhi tupu yake. Tumepitia baadhi ya maandiko kuhusu hilo. Moja katika dalili ni yale ambayo at-Twabaraaniy amepokea katika “al-Awsaat”[34] kupitia Saalim bin ´Abdillaah bin ´Umar kutoka kwa baba yake ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwanamke ni ´Awrah. Wakati anapotoka nje Shetani anamtazama (anamfanya) kama mabadiliko. Anakuwa yu karibu na Allaah pindi anapokuwa ndani kabisa ya nyumba yake.”


 Mke mwema hatoi siri za mume wake

Katika sifa za mke mwema ni kwamba hatoi siri za mume wake na zile za ndani kwao. Hata kama kutatokea kutengana na kutokukubaliana ni lazima kwao wote wawili kumcha Allaah (Jalla  wa ´Alaa) katika suala hili. Kuhusiana na hili amepokea Imaam Ahmad katika “al-Musnad”[35] yake kupitia Amsaa´ bint Yaziyd ambaye ameeleza kwamba alikuwa kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanaume na wanawake walikuwa wamekaa kwake. Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Pengine mwanaume akasema aliyofanya na mke wake.

Pengine mwanamke akasema aliyofanya na mume wake.” Wakanyamaza kimya. Nikasema: “Ndio, Mtume wa Allaah. Wanawake wanafanya hivyo. Wanaume wanafanya hivyo.” Akasema: “Msifanye hivyo. Hili linafanana na Shetani ambaye anapata mwanamke wa kishetani njiani na akaanza

kujamiiana naye na huku watu wanatazama.”

Amesema:

”Wanawake wanafanya hivyo. Wanaume wanafanya hivyo.”

Ameanza na wanawake kwanza kwa sababu hili hufanywa sana kati yao na huwa kwa mara kidogo sana kati ya wanaume. Mwanamke huongea na marafiki zake na maswahiba zake kuhusu mambo kama hayo ya binafsi. Wengi katika wao hawajali kuongea siri za mume na mambo yao binafsi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Hili linafanana na Shetani ambaye anapata mwanamke wa kishetani njiani na akaanza kujamiiana naye na huku watu wanatazama.”

Bi maana mwanamke na mwanaume wenye sifa kama hii na wanafichukua siri zao ni kama Shetani wa kiume ambaye amepata Shetani wa kike njiani na akajamiiana naye na huku watu wanatazama.


 Hitimisho

Hizi ni baadhi ya sifa za mke mwema ambazo nimezikusanya kutoka katika maandiko ya Allaah (´Azza wa Jalla) na Sunnah za Mtume Mtukufu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nimefanya hivyo kwa kutaraji kwa Mola (Subhaanahu) Amnufaishe kwazo yule Amtakaye katika waja Wake. Ni Yeye Peke Yake ndiye mwenye kuwafikisha.

Ninamuomba Allaah (Jalla wa ´Alaa) kwa Majina Yake Mazuri na Sifa Zake Kuu Atuongoze sote katika njia iliyonyooka, yale tunayojifunza iwe ni hoja yetu na si dhidi yetu, Atubariki katika maneno yetu, matendo yetu, wakati wetu, wake zetu, watoto wetu, mali zetu na maisha yetu yote, Atutengenezee Dini yetu ambayo ndio kinga yetu, Atutengenezee maisha yetu ya duniani ambayo tunaishi na maisha yetu ya Aakhirah ambayo ndio kituo chetu cha mwisho, Afanye uhai kwetu kuongezeka iwe ni kheri ya kila kitu na mauti iwe ni raha kwetu kutokana na kila shari, Awatengeneze wanawake wa Waislamu na wasichana wao, Awaongoze katika njia iliyonyooka, warudi Kwake kwa njia nzuri na Awaepushe na fitina zote zilizodhahiri na zilizojificha na Atuongoze sote katika kila kheri Anayoipenda na Kuiridhia. Hakika Yeye (Tabaaraka wa Ta´ala) ni Mwenye kuzisikia Du´aa, Yeye ndiye wa kuwekewa matarajio, Anatutosheleza na ni Mbora wa kuyasimamia mambo.

Wito wetu wa mwisho tunamhimidi Allaah, Mola wa walimwengu.

Swalla Allaahu was-Sallam, wa Baarak wa an´aam ´alaa ´abddihiy wa Rasuulihiy Mustwafaaa Muhammad bin ´Abdillaah. SwalawaatuAllaahi wa salaam ´alayhi, wa ´alaa aalihiy, wa Swahbihii ajma´iyn[36].[1] (18:17)

[2] (10:25)

[3] Muslim (2664).

[4] (17:09)

[5] al-Haakim (1/172). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (2937).

[6] (04:34)

[7] Kwa nambari. (3163).

[8] Kwa nambari. (1661).

[9] Nambari. (2117). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “as-Swahiyhah” (1842).

[10] Ameipokea Ahmad katika “al-Musnad”, nambari. (25120), an-Nasaa´iy katika “al-Kubraa”, nambari. (9274) kupitia Hadiyth ya ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anha)

[11] Muslim (2813).

[12] Nambari. (3231). Imaam al-Albaaniy ameisahihisha katika ”as-Swahiyhah” (1738)

[13] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[14] Nambari. (715)

[15] al-Bukhaariy, nambari. (5954), Muslim, nambari. (6107).

[16] Nambari. (1743). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “Swahiyhah”, nambari. (3370)

[17]  7/82. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (3380).

[18] Ahmad (12613), kupitia Anas (Radhiya Allaahu ´anhu). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “Irwaa´-ul-Ghaliyl” (1784).

[19] al-Bukhaariy (304) kupitia kwa Abu Sa´iyd al-Khudriy (Radhiya Allaahu ´anh) na Muslim (79) kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

[20] al-Bukhaariy (5947) na Muslim (2124).

[21] al-Bukhaariy (5885).

[22] 8913 na Ahmad (19003). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (2612).

[23] (25:67)

[24] Ibn Khuzaymah katika ”Kitaab-ut-Tawhiyd” (487). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (591).

[25] (02:195)

[26]  (04:29)

[27] Ahmad (7939) na Abu Daawuud (4811) kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anhu). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swhaiyh katika ”as-Swahiyhah” (416).

[28] 1048. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (823).

[29] 9135. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (289).

[30] 11/356. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (3490).

[31] 5/207. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika “as-Swahiyhah” (3366)

[32] at-Tirmidhiy (1174) na Ibn Maajah (2014). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (173).

[33] 3544. Imepokelewa na an-Nu´maan bin Bashiyr (Radhiya Allâhu ´anhu). Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (1240).

[34] http://www.darulhadith.com/v2/12-den-rattfardiga-hustrun-skall-stanna-hemma/ - sdfootnote1anc2890 och 8096. Imaam al-Albaaniy amesema kuwa ni Swahiyh katika ”as-Swahiyhah” (2688).

[35] 27583. Ni Swahiyh kupitia Hadiyth zingine kwa mujibu wa  Shaykh al-Albaaniy (Rahimahu Allaah) katika ”Swahiyh-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2022). Razana ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (2011).

[36] Asli ya kijitabu hichi ni muhadhara ambao nimepanga kidogo lakini hata hivyo nikaacha ubaki usulubu wake kama muhadhara.