UHARAMU WA KUJICHUBUA NGOZI NA KUUNGA NYWELE ()

Yunus Kanuni Ngenda

Mada hii inazungumzia uharamu wa kujichubuwa ngozi na kuunga nywele, madhara yake na hukumu ya kisheria katika kufanya hivyo.

  |

  UHARAMU WA KUJICHUBUA NGOZI

  NA KUUNGA NYWELE ZA BANDIA

  Imetungwa na: Yunus Kanuni Ngenda

  Imepitiwa na: Yasini Twaha Hassani

  بسم الله الرحمن الرحيم

  Sifa zote kamilifu anastahiki Mwenyezi Mungu, ambae ame muumba Mwanadam katika umbile zuri, kupita kiumbe chochote katika viumbe vyake,

  Na Rehma na Amani zimwendee kiongozi wa umma huu, Mtume wetu Muhammad (s.a.w), pamoja na watu wake na Maswahaba zake na wenye kuwafuata kwa ihsani mpaka siku ya Qiyama. Amma baad:

  Anasema Mwnyezi Mungu Mtukufu katika Qur’an tukufu: (Bila shaka tumemuumba mwanadamu kwa umbo lililo bora kabisa). (Suratu Tyn: (4).

  Mwenyezi Mungu Mtukufu ni muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo, yeye Mwenyezi Mungu anavijua vizuri viumbe vyake, kwasababu ndiye aliyeviumba, baada ya kumuumba mwanadamu kwa umbile bora hakukaa kimya; Bali akamjulisha mwanadamu tena kwa kumsifu, Ili ajijue mwanadamu kuwa yeye ni kiumbe bora, Na atosheke na namna alivyoumbwa na amshukuru Mwenyezi Mungu juu ya hilo, Amwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w), na afanye matendo mema, akiwa hivo atapata ujira usio kwisha.

  Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Isipokuwa wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha). (Surat Tyn: (6).

  Na Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuishia hapo, Akaendelea kumzungumzia mwanadamu akasema: (Ewe mwanaadamu! Nini kilicho kughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?. Aliye kuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha. Katika sura yoyote aliyo ipenda akakujenga). (Surat Al-Infitwaar: (6-8).

  Katika Aya hizo tukufu Mwenyezi Mungu anazungumza kwa mshangao mkubwa, kumshangaa mwanadam kulingana na namna alivyomumba kwa ubora na ukamilifu, cha ajabu ni kwamba baadhi ya binadam hawaja ridhika na maumbile waliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambayo ndio maumbile bora.

  Wanafanya jitihada ya kubadilisha maumbile yao ima kwa kutumia madawa wakabadilisha nywele na mwili (kujichubua) au kuunganisha nywele za bandia, na hii ni haramu haifai. Kwa nini huridhiki na maumbile alio kupatia Mwenyezi Mungu? Umezaliwa ukiwa na rangi nyeusi unaona haifai! unataka rangi nyeupe! Aliekupatia rangi nyeusi kakosea?!!!.

  Na ikumbukwe kuwa baada ya Ibilisi kulaaniwa na Mwenyezi Mungu, Alichukua ahadi nyingi sana juu ya kumpoteza mwanadam. Na miongoni mwa ahadi zake ni kwamba aliahidi atawashawishi wanadam mpaka watabadilisha maumbile halisi aliyowaumbia Mwenyezi Mungu Mtukufu.

  Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Na hakika nitawapoteza na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili maumbile ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shet'ani kuwa ni mlinzi wake badala ya Mwenyezi Mungu, basi huyo amepata khasara iliyowazi). (Surat Nisaa: (119).

  Kwa mujibu wa Aya hiyo ni kwamba yeyote anaebadilisha maumbile yake kwa namna moja au nyingine, iwe ni kujichubua ngozi, au kuweka dawa nywele ili zibadilike kama ni Mwafrika aonekane kama Mzungu, au Mchina au mfano wa hao basi mtu huyo anakua:

  1-Amepotezwa na shetani.

  2-Ni mfuasi wa shetani.

  3-Mlinzi wake ni shetani.

  4-Amepata khasara kubwa (Duniani na Akhera).

  Na kutokana na maneno ya Mtume (s.a.w), ni kwamba yeyote mwenye kufanya mambo kama hayo, ya kujibadilisha maumbile. yaani: kujiweka tofauti na alivyoumbwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu. Mtu huyo amelaaniwa na Mwenyezi Mungu.

  Imepokewa kutoka kwa Asmaa bint Abubakar (ﷺ‬.a) Akisema: (Alikuja Mwanamke mmoja kwa Mtume (s.a.w) Akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu; Mimi Nina binti yangu bi harusi amepatwa na surua, (yaani maradhi ya kudondosha nywele) na nywele zake zinaanguka, Je niziunganishe kwa nywele za bandia? Akasema Mtume (s.a.w): Amelaaniwa na Mwenyezi Mungu mwenye kuunganisha nywele na mwenye kutaka kuunganishiwa). (Yaani mwenye kuunganisha na anaeunganishwa). Ameipokea hadithi hii Imam Muslim: (3/1617).

  Na imepokewa kutoka kwa jaabir bin Abdullah (ﷺ‬.a), (Mtume (s.a.w) amekataza kwa Mwanamke kuunganisha chochote kwenye kichwa chake). Ameipokea Hadithi hii Imam Muslim: (1679).

  Na mfano wa hii ni hizi nywele za bandia zinazojulikana katika zama zetu kwa jina la wigi (wig) au baroka. Na wenye kuunganisha nywele kwa zama zetu ni Hawa watu wa saloon.

  Na mfano wa haramu hii vilevile kuvaa nywele za kuazima kama wanavyofanya baadhi ya waigizaji wa kike na wakiume wasiokuwa na tabia nzuri kwenye tamthilia na michezo ya kuigiza.

  Na hao wasanii wamechangia kwa kiasi kikubwa sana kuihari jamii.

  Imefika mahala kwamba vijana wengi wa kike na wa kiume, kila anaekua, anatamani awe msanii wa tamthilia au mwana muziki, kwasababu amekua akiwatazama hao katika runinga, kwahiyo akajenga mapenzi ya kuwapenda na kupenda wanayoyafanya. Huu ni msiba mkubwa katika umma wa kiislamu.

  Na familia za kiislamu nyingi zimeathirika na tabia hizi za kisanii, kwasababu katika majumba kumeenea: cd za tamthilia na miziki.

  Ndio ukaona watoto wa kiislamu wameiga upuuzi na mambo ya haramu.

  Na katika hilo aelewe mzazi ya kuwa ataenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu siku ya Qiyama.

  kwa kushindwa kuwafundisha watoto wake mambo ya dini ambayo ndio kheri kubwa hapa duniani na kesho akhera, kwake yeye mzazi na kwa mtoto pia.

  Kutoka kwa Abdullah bin Omar (ﷺ‬.a), Amesema; Nilimsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w), akisema: (Sikilizeni: Nyote ni wachunga, na nyote mtaulizwa kuhusu hayo mlio yachung. Kiongozi ni mchungaji na ataulizwa juu ya alicho kichunga. Na mwanamume ni mchunga kuhusu watu wa nyumbani kwake, na ataulizwa kwa hilo. Na mwanamke ni mchunga katika nyumba ya mume wake na watoto, na ataulizwa kwa hilo. Na mfanya kazi ni mchunga katika mali ya tajiri wake, na ataulizwa kwa hilo. Sikilizeni: nyote ni wachunga na mtaulizwa kwa kile mlicho kichunga). Kapokea hadithi hii imam Muslim.

  Na huu ndio wito wetu kwa wazazi; kwamba tuwafundishe watoto wetu dini yetu ya Uislamu.

  Tuwapeleke Madrasa waisome Qur-ani, wasome na hadithi za Mtume wetu Muhammad (s.a.w), wafundishwe tabia njema za Kiislamu, tabia za Maswahaba radhi za Allah ziwe juu yao.

  Ili hata ukifariki utakua umeacha mtoto mwema ambae atakuombea dua. Nahii ni faida kubwa sana kwako mzazi.

  Mtume (s.a.w) Anasema miongoni mwa mambo ambayo yanamfaa mtu baada ya kufa ni: (Mtoto mwema ambae atakuombea dua…).

  Kwahiyo tujitahidi kuwalinda watoto wasiige tabia za kikafiri na kisanii kwa kuwaandalia mazingira ya kuwafundisha dini kama tulivyoeleza hapo juu. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ataleta kheri zake.

  Na tuna watahadharisha pia, Mama zetu na Dada zetu wa Kiislamu, kuto kuiga tabia za makafiri na wajinga kwa namna yoyote itakavyo kuwa, iwe kwa mavazi, au kwa desturi za maisha yao (namna wanavyoishi), ni haramu.

  Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na simamisheni Sala, na toeni Zaka, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukusafisheni barabara). Surat Al-Ahzab: (33).

  Namna hiyo ndivyo wanatakiwa waishi wanawake wa Kiislamu, na haitoshi kutulia majumbani mwao;

  bali wanatakiwa kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w). Na kumtii Mwenyezi Mungu ni kufuata maarisho yake, kama vile: kuswali, kufunga, kwenda Hijjah, kuwaheshimu wazazi, kutoa zaka, kuwasaidia wasio jiweza, kusoma qur-ani, kujistiri vizuri, na mfano wa hayo.

  Na kujiepusha na makatazo yake, ni (kuto kufanya) kujizuia na kila alicho kikataza (alicho kiharamisha) Mwenyezi Mungu na Mtume wake (s.a.w).

  Mfano: Ushirikina, zina, riba, wizi, uongo, kiburi, kuuwa, uchawi, kula mali ya mayatima, ulevi, kamari, rushwa, umbea, kumuudhi jirani, na mfano wa hayo.

  Na kumtii Mtume (s.a.w) ni kufuata Sunna zake, mwenendo wake (s.a.w), katika Nyanja zote.

  Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: (Na anacho kupeni Mtume chukueni, na anacho kukatazeni jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu). Surat Al-Hashri: (7).

  NA MWISHO TUNA MUOMBA MWENYEZI MUNGU MTUKUFU KUPITIA MANENO YAKE MATUKUFU, TUNASEMA:

  (Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu). Surat Al-Furqaan: (74).

  Ewe! Mwenyezi Mungu tunakuomba utujaalie tuwe ni wenye kufuata maamrisho yako na tujiepushe na makatazo yako, na utukusanye pamoja na Mtume wetu Muhammad (s.a.w) na watu wema siku ya Qiyama.

  Na Rehma na Amani zimwendee Mtume Muhammad (s.a.w) na watu wake na Maswahaba wake wote. Ameen!.