WASIA KWA WENYE KUFUNGA RAMADHAN ()

Mada hi inazungumzia wasia muhimu kwa mfungaji yakiwemo mambo anayo takiwa kuyafanya namambo ambayo hatakiwi kuyafanya mtu alie funga.

  |

  بسم الله الرحمن الرحيم

  WASIA KWA WENYE KUFUNGA RAMADHAN

  Imeandaliwa na Raudhwah Islamic Group

  Imepitiwa na Ust.Abubakari Shabani Rukonkwa.

  Ilipokaribia kuingia Ramadhan Mtume swalla Allahu alayhi wasalam aliwausia maswahaba zake kuhusu Ramadhan, wasia tutakaouona katika mada zijazo Inshaa Allah. Na sisi tukiwa tumeuanza mwezi huu mtukufu ni muhimu kukumbushana yafuatayo ili uwe wasia wetu kwa ajili ya kufaidika na Ramadhan.


  1-Kumshukuru Allah subhanahu wataala kwa kutuwafikisha kuidiriki Ramdhan. Hakika kushukuru ni miongoni mwa ibada azipendazo Allah, na akaahidi kwa waja wake wakimshukuru basi atawaongeza neema alizowapa. Amesema Allah subhanahu wataala“Na alipotangaza Mola wenu : Kama mtanishukuru nitakuzidishieni, na mkikufuru hakika adhabu yangu ni kali sana” (Suratu Ibrahim: 7) na akasema tena katika Suratul Baqarah aya ya 152 “….na nishukuruni wala msinikufuru”.

  Uhakika hatuwezi kufikia upeo wa kushukuru neema za Allah, kwani neema zake hazihesabiki wala hazipimiki. Amesema Ibnul Qayyim rahimahullah: “Kuwafikishwa kushkuru neema za Allah, nayo ni neema inayohitaji shukrani, na kuwafikishwa kushkuru neema ya shukrani, ni neema nyengine inayohitaji shukrani, na hivyo hivyo inaendelea kua muislamu aendelee kumshkuru Allah

  mpaka mwisho wa pumzi zake”. Miongoni mwa neema hizo ni kuwafikishwa kuidiriki ramadhan, alau siku moja na usiku wake, kwani wangapi walitamani alau waweze kufunga lakini maradhi yamewaweka vitandani, hawawezi kufunga, na kula yao mpaka watumie mirija? Wangapi walitamani waidiriki ramadhan na family zao, lakini sasa wako kaburini ima katika viwanaja vya pepo au mashimo ya moto? Hatutojua neema mpaka ikiondoka. Tumepewa nafasi ya kujirekebisha matendo yetu ,kwa kuitumia vizuri Ramadhan,ili siku ya Qiyama tupate ujira mkubwa apatao mfungaji, ujira ambao mimi na weye wakati huu tumewafikishwa na Allah kuupata,na tuukimbilieni huku tukiomuomba Allah atuwafikishe tuimalize Ramadhan kwa salama, asitunyime ujira wake wote, na atuwafikishe tuidiriki Ramadhan inayokuja. Tumshukuruni Allah si kwa maneno tu, bali na kwa matendo kwa kuonesha kuithamini Ramadhan.

  2-Kufunga kwa Imani na kutarajia malipo

  Amesema Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam)katika hadith sahihi, iliyopokelewa na Bukhari,Muslim na Nasai rahimahumullah na kusimuliwa na Abu-Hurayra radhiallahu anhu :“Yoyote atakaefunga Ramadhan, kwa imani na kwa kutarajia malipo atasamehewa dhambi zake zilotangulia”.

  Kufunga kwa Imani ni kukiri kua funga ni amri ya Allah, na ni miongoni mwa nguzo za kiislamu, atakaesimamisha basi atakua ameusimamisha uislamu wake, na atakaevunja basi atakua kaubomoa uislamu wake. Allah hataki kula yetu na wala hana haja ya kukaa na njaa kwetu lakini anachotaka ni ibada na kama anavyosema katika lengo la funga ni kuwa anataka watu wawe wacha-Mungu yani wamuogope yeye Subhanah.
  Kutarajia malipo ni kutaraji kuwa kutokana na funga tunayofunga basi kuna malipo mazuri yaliyoandaliwa kwa wafungaji,na malipo ya mwanzo ni kusamehewa dhambi na mengine yanafuatia Akhera. Ni madhambi mangapi tumeyafanya ya dhahiri na siri,makubwa na madogo yote hayo yatasamehewa kwa atakaefunga kwa imani na kutaraji malipo. Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) katika Hadith inayosimuliwa na Anas(radhia Allahu anhu) :“Hakuna amali kwa asiekua na nia na hakuna na malipo kwa asiyeyatarajia” .

  Na tumkumbukeni Allah na ukubwa wake na kwamba akatayarisha malipo mazuri kwa wafungaji na papo hapo tuyatarajie malipo hayo.

  3-Kuchunga ulimi na mambo ya kipuuzi.

  Anasimulia kwamba amesema Mtume swalla Allahu alayhi wassalam katika hadithi iliyopokewa na Bukhari na Abu-Daud na kusimuliwa na Abu-Hurayra:“Yoyote asiewacha maneno ya upuuzi, na kuyafanyia kazi,basi Allah hana haja ya kuacha chakula chake na kinywaji chake”. Je tumeizingatia hadithi hii tukafumba midomo yetu?

  Amesema Mtume wa Allah (swalla Allahu alayhi wasallam) kuwa “Yoyote anaemuamini Allah, na siku ya mwisho basi na aseme la kheri au anyamaze” .(Muttafaqun alayhi). La kusikitisha Ramadhan ndio imekua mwezi wa porojo,Ramadhan imekua ndio mwezi wa kusengenyana, Ramadhan ndio mwezi wa watu kukaa barazani na kuanza kutaja sifa za wapita njia,na wengine kukaa maskani na kuhadithiana uongo. Tumejiweka wapi na hadithi hii?

  Tokea hapo mwanzo Allah hahitaji chakula chetu wala kukaa kwetu na njaa lakini analolitaka ni ucha-mungu,na haupatikani kwa kuzungumza ovyo,na kwa mwenye kusema uongo na kufanya upuuzi mwengine basi ni bora kwake kula kwani Allah hahitaji kulifungia tumbo akauwachia ulimi,kama kufunga basi na viungo vyote vifungwe. Hatopata hasara anaenyamaza kimya lakini hasara kwa asiweza kuumiliku ulimi wake.

  Kumiliki ulimi ni jambo alousiwa Muadh bin Jabal na kaambiwa kuumiliki ulimi ndio itakua sababu ya kutengenea matendo yote iwe sala,swaumu,hajj na hata Jihad. Aliulizwa Mtume (swalla Allahu alayhi wasallam):” Ni kipi kitachowaingiza wengi motoni ? Akajibu kua ulimi na utupu ndivyo vitakaowaingiza wengi motoni. Na akasema atakaenidhamini viungo hivyo basi na yeye amemdhamini Jannah,(Hadith imepokewa na Bukhari). Basi na tuanze kumdhamini Mtume wa Allah viungo hivi ndani ya Ramadhan hii kwa kutosema uongo,kutosengenya,kutukana na porojo nyenginezo.

  4-Kutia nia ya kuzidisha kheri, na kushindana katika mazuri.

  Muumini wa kweli hatasheki na kufunga tu ndio ikawa basi,wala hatosheki na kusali sala zake tano, kisha ikawa ndio kishamuabudu Allah. Kumuabudu Allah hakutoshi kwa dakika 25 kwa sala zote tano, ndani ya masaa 24. Allah hahitaji kupangiwa au kutengewa muda kwani muda wote ni wake na anastahiki muda wote kuabudiwa. Alipotaja pepo na starehe zake akamalizia kwa kusema na washindane wenye kushindana(Muttafifin :26) na kwengine akasema Kwa mfano wa haya nawatende watendao. (swaaffaat :61).

  Pepo inahitaji kushindaniwa kwani kama anavyosema Rasuul (swalla Allahu alayhi wasallam) kuwa “….Hakika bidhaa ya Allah ni ghali na bidhaaa ya Allah ni pepo.(Tirmidhy). Ikiwa kushindana kwenyewe sisi ndio tutaenda na sala tano tu ambazo hazina khushui ndani yake, na haikutimizwa rukuu wala sijdah, mbele ya wale ambao wanaswali mpaka kuvimba miguu yao, na kuroa ndevu zao kwa kulia na kukesha usiku mzima, kwa kumuabudu Allah hivi tutakua sawasawa? Au ndo sisi tunashindana kwa aina za vyakula na nani kapika vingi na vizurii?

  Wengi wetu kabla ya Ramadhan tulitia nia ya kuzidisha kufanya kheri, na wengine baada ya kufanya vibaya Ramadhan zilopita, tukajiapiza Ramadhan ijayo nitafanya vizuri, na nitamuabudu Allah kikamilifu, lakini tunayakumbuka haya au pia tunasubiri ya mwakani, ili tufanye vizuri kwa kua Ramadhan hii tuko na mishughuliko ya world cup, hatuna muda wa kumuabudu Allah.

  Na tuipambeni Ramadhan yetu kwa Qur-an na qiyamul-layl. Adhkaar na madarsa na vikao vya kheri,Tutieni nia ya kuzidisha kheri na miongoni mwa mambo tunaotakiwa kuyaazimia kuyafanya ni kutekeleza sunna ya itikafu, sunna ambayo hakuiachapo Mtume baada ya kuhamia Madina na mwaka aloiwacha ikabidi ailipe lakini ndio sunna iliyokimbiwa na wengi.

  5-Kuwahurumia wanyonge na kuacha israfu.

  Anasema Allah (subhanahu wataala) “…. Na amewanyanyua daraja baadhi yenu juu ya wengine ili akufanyieni mtihani kwa hayo alokupeni…” (An-aam 165).Na akasema tena katika Suratu-Nahli aya ya 71 “Na Allah amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika rizki, Je wale walofadhilishwa,hawarejeshi rizki zao,kwa wale wanaowamiliki kwa mikono yao ya kulia?”.

  Kutofautiana kwa kipato ni dalili za uwepo wa Allah kuonesha anampa amtakae na humnyima amtakae na kwamba kupata si kwa utashi wa mtu, bali ni mipango ya Allah. Na akawataka waja wake wasaidiane. Bila shaka miongoni mwa jamii za kiislamu tunazoishi nazo wako wanaofunga lakini wasijue wataftari nini, na wanafunga hawana daku ya kula ili waweze kufunga vizuri.

  Wanafunga kwa kua ni amri ya Allah (subhanahu wataala) lakini kipato chao na uwezo wao hauwaruhusu kufanya hivyo. Watu aina hiyo wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la huruma na wale wenye uwezo. Si vibaya kila siku kumlisha maskini mmoja kwani sadaka ya kulisha chakula ina thamani kubwa mbele ya Allah (subhanahu wataala). Na Amesema Mtume wa Allah katika hadithi inayosimuliwa na Saad bin Khalid:”Atakaemfutarisha aliefunga, basi atapata ujira sawa na wake, pasi na kupungua ujira wa mfungaji chochote”(Tirmidhy,Nasai na Ibnu-Majah).

  Ikiwa ni hivyo basi na kuftarsha kwetu tusiwasahau maskini na sio shughuli zetu za kuftarisha kujazwa matajiri na wenye uwezo wao ambao hata hicho chakula hawakihitaji. Kwa kutumia kiyasa ya hadith ya Rasuul inayosimuliwa na Abu-Hurayrah kua chakula kibaya ni chakula cha harusini, kwani wanaalikwa wasiokihitaji; basi na ftari zetu kesi ndio hiyohiyo, tunawasahau maskini na wote wanaoalikwa hawakihitaji. Tusitosheke na thawabu za kuftarisha mtu bali tutake na thawabu za kulisha maskini kwani tukialika matajiri tutapata thawabu za kuftarisha tu lakini kualika maskini itakua ni thawabu za kuftarisha na za kulisha maskini.
  Ama kuhusu israfu tumeona maudhui yake katika mada zilopita

  6-Kukumbuka njaa na kiu siku ya Qiyamah.

  Moja kati ya mambo walohusishwa Mitume na ndo ikawa kama zawadi yao hapa duniani amesema Allah subhanah “Hakika tuliwachagua kwa lile jambo zuri kabisa la kuikumbuka Akhera” (Swaad :46). Ni zawadi ambayo imewafanya kutojali maisha ya dunia ni kutoshughulishwa na starehe za duniani.

  Amesema Allah (subhanahu wataala) hii kuonesha kua kila kitu chao walikua wakifiri akhera.Na hivyo ndio anavyotakiwa muislamu wa kweli awe. Awe anafikiri akhera,kwani nguzo zote za kiislamu kuanzia sala,swaumu na hata hajji vinamkumbusha mtu mambo yatakayotokezea siku ya kiyama. Funga inatakiwa imkumbushe mtu njaa na kiu, kitakachowakuta watu wa motoni na kutokana na kiu hiyo wataomba kwa watu wa peponi kama anavyotusimulia Allah (subhanahu wataala) katka suratu A’raf aya ya 50 “Na watanadi watu wa motoni kuwaita wa peponi: Tumiminieni maji au chochote katika alivyokuruzukuni Allah. Watasema watu wa peponi: Hakika Allah ameviharamisha vyote viwili (yani chakula na maji) kwa makafiri”. Hivyo basi mtu anapokaa na njaa na kiu akumbuke kua akhera watu waovu watakaa na njaa na kiu.(Allah atuhifadhi)

  Allah atuwafikishe kuyatekeleza haya na mengineyo ya kheri.