HALI YA KABURI NA VITISHO VYAKE

Maelezo

Mada hii inazungumzia hali za watu wema na waovu Makaburini na vitisho vya Kaburi.

Download
Tuma maoni kuhusu ukurasa huu kwa msimamizi

Maelezo ya Kina

  بسم الله الرحمن الرحيم

  HALI YA KABURI NA VITISHO VYAKE.

  Imeandaliwa na Abubakari Shabani Rukonkwa.

  Imepitiwa na Yunus Kanuni.

  Kaburi ni sehemu ya kwanza anayopitia mtu kuendea Akhera, na kaburi ya mtu ima itakuwa ni sehemu ya bustani ya Pepo akiwa mtu huyo ni mwema au sehemu ya shimo la Moto akiwa mtu huyo ni muovu kutegemea na jinsi vile alivyoishi duniani.
  Kuna Hadithi inayothibitisha maneno haya kama alivyosema MtumeRehma na amani ziwe juu yake,katika Hadithi iliyopokelewa na Abi Said Al-Khudrriyyi Radhi za Allah ziwe juu yake. na kutolewa na Ttirmidhi, “
  "إِنَّمَا الْقَبْرُ رَوْضَةٌ مِنْ رِيَاضِ الْجَنَّةِ أَوْ حُفْرَةٌ مِنْ حُفَرِ النَّارِ"

  “Kwa hakika kaburi ni bustani katika Mabustani ya Peponi au shimo katika mashimo ya Motoni.”
  Pia katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar Radhi za Allah ziwe juu yake na iliyotolewa na Muslim, kasema:
  "إِنَّ أَحَدَكُمْ إِذَا مَاتَ عُرِضَ عَلَيْهِ مَقْعَدُهُ بِالْغَدَاةِ وَالْعَشِيِّ إِنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ فَمِنْ أَهْلِ الْجَنَّةِ ، وَإِنْ كَانَ مِنْ أَهْلِ النَّارِ فَمِنْ أَهْلِ النَّارِ ، يُقَالُ : هَذَا مَقْعَدُكَ حَتَّى يَبْعَثَكَ اللَّهُ إِلَيْهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ"

  "Hakika mmoja wenu akifa anaoneshwa kikao chake katika Pepo asubuhi na jioni akiwa (huyo aliekufa) ni mtu wa Peponi basi ni mtu wa Peponi, na akiwa (huyo aliekufa) ni mtu wa Motoni basi ni mtu wa Motoni.

  Anaambiwa hiki ni kikao chako mpaka Mwenyezi Mungu atakapokufufuwa siku ya Kiyama.”

  Na Sayyidna Uthman bin Affaan Radhi za Allah ziwe juu yake alikuwa kila anaposimama kwenye makaburi alikuwa akilia mpaka machozi yanalowanisha ndevu zake.

  Masahaba wenzake walimuuliza:
  “Kwa nini ukikumbushwa Pepo na Moto hulii, lakini unalia ukisimama kaburini?” Akajibu:
  “Nimemsikia Mtume SAW akisema, kutokana na Hadithi iliyotolewa na Ttirmidhi, “
  "الْقَبْرُ أَوَّلُ مَنَازِلِ الآخِرَةِ ، فَإِنْ يَنْجُ مِنْهُ فَمَا بَعْدَهُ أَيْسَرُ مِنْهُ ، وَإِنْ لَمْ يَنْجُ مِنْهُ فَمَا بَعْدَهُ أَشَدُّ مِنْهُ"
  “Kaburi ni mahali pa mwanzo pa Akhera, basi ikiwa (mtu) ataokoka napo (na kusalimika na adhabu ya kaburini, basi kila kitu) baada ya hapo kitakuwa chepesi kwake.

  Na kama (mtu) hakusalimika napo (basi kila kitu) baada ya hapo kitakuwa kigumu kwake (mpaka siku ya Kiyama).”
  Pia kasema: “Na nimemsikia Mtume S.A.W. akisema, “
  "مَا رَأَيْتُ مَنْظَرًا قَطُّ إِلاَّ وَالْقَبْرُ أَفْظَعُ مِنْهُ"
  “Sikuona sura ya kutisha kuliko kaburi linavyotisha.”

  Ingawa kaburi inatisha kwa giza na adhabu zake, lakini kwa mtu ambae amekufa akiwa Mwislamu na katika radhi za Mola wake huwa katika neema kaburini mwake baada ya kujibu maswali atakayoulizwa humo kaburini. Malaika humwambiya:

  “Lala usingizi wa harusi.”
  Kisha yanaletwa matandiko ya Peponi, na anavalishwa mavazi ya Peponi, na linapanuliwa kaburi lake dhiraa sabini, na linafanywa bustani katika mabustani ya Peponi.

  Kisha linafunguliwa dirisha lenye kuleta hewa nzuri ya kutoka Peponi, na anaoneshwa makao yake ya Peponi asubuhi na jioni.

  Kwa hiyo akiona neema zote hizo alizopewa husema:
  “Mola wangu kiharakishe Kiyama, ili nirejee kwa watu wangu na mali yangu.”

  HALI YA KAFIRI AUBMTU MUOVU KABURINI.

  Na kafiri au mtu muovu huwa katika adhabu kali kaburini mwake kwa yale aliyoyachuma duniani ambayo yatamfanya ashindwe kujibu maswali ya kaburini.

  Malaika watakuwa wakimpiga na nyundo, kwa uchungu na maumivu makali atakuwa akipiga kelele na sauti yake inasikika na kila kitu ila binaadamu na Majini.
  Na laiti binaadamu na Majini wangelisikia sauti yake wangelitoka roho kwa khofu.

  Kisha linadhikishwa kaburi lake, na linafanywa giza, na linafanywa shimo katika mashimo ya Motoni.
  Halafu linafunguliwa dirisha linaloleta hewa ya moto kutoka Motoni.

  Na anaoneshwa makao yake Motoni asubuhi na jioni. Na ingawa atakuwa kwenye hiyo adhabu kali lakini juu ya hivyo atasema:
  "Mola wangu usikisimamishe Kiyama.”
  Kwa sababu huko Akhera inamngoja adhabu kali zaidi kuliko hiyo aliyonayo kaburini.


  KABURI NA GIZA LAKE.

  Hakika kaburi ni sehemu ya kutisha sana, na giza lake huwezi kulifananisha na giza lingine lolote lile unalolijua, ni giza lenye kutisha sana linalomuinamia mtu aliyestahiki adhabu ya Allah.
  Katika Hadithi iliyotolewa na Bukhari na Muslim wamesema:
  “Katika zama za Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake,kulikuwapo na mwanamke akiusimamia msikiti kwa kuufagia, siku moja Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake ,hakumuona akamuulizia, wakamwambiya yakuwa amefariki usiku kisha wakamzika.
  Akaomba kwa Masahaba wake wamuoneshe kaburi lake, alipofika kaburini pake akamuombea dua, kisha akasema,

  "إِنَّ هَذِهِ الْقُبُورَ مَمْلُوءَةٌ ظُلْمَةً عَلَى أَهْلِهَا ، وَإِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ مُنَوِّرُهَا لَهُمْ بِصَلاتِي عَلَيْهِمْ"
  “Hakika haya makaburi yamejaa giza kwa watu wake, na hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu anawanawirishia kwa Sala (dua) yangu juu yao.”

  KUBANWA NA KABURI.

  Ndani ya kaburi kuna adhabu nyingi tofauti na moja ya adhabu ni ya kaburi kuibana maiti.

  Maiti yoyote ile inapowekwa kaburini, basi hubanwa na kaburi na hii ni kwa kila maiti ikiwa ya mkubwa au ya mdogo, mwema au muovu.
  Lakini ubanaji na maumivu yake inatofautiana kati ya mja mchaMungu Mwislamu na maiti nyingine.

  Mja Mwislamu inakuwa kwake kama vile mama anavyomkumbatia mwanawe kwa huruma ili asiumie.
  Na katika Hadithi sahihi imethibitika ya kwamba ingelikuwa mtu anaokoka na adhabu ya kaburini, basi Sahaba Sa`ad bin Mu`adh Radhi za Allah ziwe juu yake,angelikuwa wa kwanza kuokoka.
  Lakini kaburi lilimbana baadaye likamwachia. Na ni nani basi huyu Sahaba? Kwa ajili ya fadhila zake mbele ya Mwenyezi Mungu Rehma na amani za Allah ziwe juuyake.

  Wakati wa kifo chake Arshi (Kiti cha Enzi cha Mwenyezi Mungu) kilitikisika na mbingu zilifunguliwa kwa ajili yake, na maiti yake ilishuhudiliwa na Malaika elfu sabini.

  Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake,kasema katika Hadithi iliyopokelewa na Ibn Umar Radhi za Allah ziwe juu yake. na kutolewa na Nnasaai, “


  "هَذَا الَّذِي تَحَرَّكَ لَهُ الْعَرْشُ ، وَفُتِحَتْ لَهُ أَبْوَابُ السَّمَاءِ ، وَشَهِدَهُ سَبْعُونَ أَلْفًا مِنَ الْمَلائِكَةِ لَقَدْ ضُمَّ ضَمَّةً ، ثُمَّ فُرِّجَ عَنْهُ"


  “Huyu ndiye Arshi ilitikisika kwa ajili yake, na akafunguliwa milango ya mbingu. Na akashuhudiwa na Malaika 70 elfu, ilimbana (kaburi) mara moja tu tena ikamwachia.”

  Pia Hadithi iliyopokelewa na Bibi Aisha Radhi za Allah ziwe juu yake, na kutolewa na Ahmad, Mtume S.A.W. kasema, “
  "إِنَّ لِلْقَبْرِ ضَغْطَةً لَوْ كَانَ أَحَدٌ نَاجِيًا مِنْهَا نَجَا سَعْدُ بْنُ مُعَاذٍ"
  “Hakika kaburi lina mkandamizo, lau kama mmoja (katika binadamu) ameokoka nalo angeokoka (Sahaba) Sa`ad bin Mu`adh.”

  Tumuombe Allah atupe taufiiq ya kufanya mema, na atupe mwisho mwema, wabilahi taufiiq.
  Usitusahau kwa dua.

  Utunzi wa kielimu: