102 - Surat At-Takathur ()

|

(1) Kumekushughulisheni kutafuta wingi,
Yamekushughulisheni mkaacha kutimiza yaliyo waajibu na ya ut'iifu kule kujitapa kwenu kwa wana na wafwasi, na kujifakhiri kwa mali, na hisabu, na nasaba, mpaka yakusibuni mauti!

(2) Mpaka mje makaburini!
Mpaka yakusibuni mauti!

(3) Sivyo hivyo! Mtakuja jua!
Hakika mtakuja jua matokeo ya upumbavu wenu na mapuuza yenu.

(4) Tena sivyo hivyo! Mtakuja jua!
Na hakika bila ya shaka mtakuja jua natija ya hayo!

(5) Sivyo hivyo! Lau mngeli jua kwa ujuzi wa yakini,
Ama kwa hakika lau mngeli jua kwa yakini uovu wa mwisho wenu bila ya shaka mngeli ogopa huko kushindania kurindika mali, na mngeli jitengenezea Akhera yenu.

(6) Basi bila ya shaka mtaiona Jahannamu!
Nakuapieni na nakutilieni mkazo, enyi watu, kwamba hakika nyinyi mtakuja ushuhudia Moto unao waka.

(7) Tena, bila ya shaka, mtaiona kwa jicho la yakini.
Kisha ninaapa na natilia mkazo kwamba mtauona wazi na kwa yakini.

(8) Tena bila ya shaka mtaulizwa siku hiyo juu ya neema.
Tena naapa na natilia mkazo kwamba hakika nyinyi mtahisabiwa kwa neema mlizo deka nazo na mkazistarehea.