104 - Surat Al-Humazah ()

|

(1) Ole wake kila safihi, msengenyaji!
Atapata adhabu kali na maangamio huyo ambaye mtindo wake ni kuwafedhehi watu kwa kauli au kwa ishara, au kuwasengenya kuwavunjia hishima zao.

(2) Aliye kusanya mali na kuyahisabu.
Ambaye amekusanya chungu ya mali na akawa kazi yake kuyahisabu tu, kwa kuona ladha huko kuhisabu.

(3) Anadhani ya kuwa mali yake yatambakisha milele!
Anadhani huyo kuwa mali yake yatamweka milele duniani, na yatamkinga na hayo anayo yachukia?

(4) Hasha! Atavurumishwa katika H'ut'ama.
Na aache dhana hiyo! Wallahi! Hapana shaka yoyote kwa vitendo vyake viovu hivyo atakuja tumbukizwa katika Moto unao vuruga kila kinacho tupwa humo!

(5) Na nani atakujuvya ni nini H'ut'ama?
Na kitu gani kitacho kujuvya nini ukweli wa Moto huu wa H'ut'ama?

(6) Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa.
Moto wa Mwenyezi Mungu ulio washwa kwa amri yake, na daima unawaka!

(7) Ambao unapanda nyoyoni.
Ambao unafikilia nyoyoni na kuzizunguka nyoyo.

(8) Hakika huo utafungiwa nao
Huo utakuwa umefungwa milango yake, na wao watakuwa wamefungwa humo ndani

(9) Kwenye nguzo zilio nyooshwa.
Kwenye maguzo yaliyo nyooka. Hawawezi kutaharaki, wala kutoka.