72 - Surat Al-Jinn ()

|

(1) Sema: Imefunuliwa kwangu ya kuwa kundi moja la majini lilisikiliza, na likasema: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya ajabu!
Ewe Muhammad! Waambie watu wako: Nimepata wahyi kwamba kikundi cha majini kimesikia kusoma kwangu Qur'ani, nao wakawaambia wenzao: Hakika sisi tumeisikia Qur'ani ya namna ya peke yake, hatujapata kusikia mfano wake kabla yake,

(2) Inaongoza kwenye uwongofu, kwa hivyo tumeiamini, wala hatutamshirikisha yeyote na Mola wetu Mlezi.
inaitia kwenye uwongofu na usawa. Kwa hivyo tumeiamini hiyo Qur'ani tuliyo isikia; na kabisa hatutamshirikisha Mola wetu Mlezi aliye tuumba na kutulea na chochote katika waja wake.

(3) Na kwa hakika utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka kabisa; hana mke wala mwana.
Na kwamba hakika cheo na utukufu wa Mola wetu Mlezi umetukuka; hana mke wala mwana.

(4) Na kwa hakika wapumbavu miongoni mwetu walikuwa wakisema uwongo ulio pindukia mipaka juu ya Mwenyezi Mungu.
Na hakika wajinga katika sisi walikuwa wakimzulia Mwenyezi Mungu maneno yaliyo kuwa mbali kabisa na ukweli na kuwa sawa.

(5) Nasi tulidhani kuwa watu na majini hawamzulii uwongo Mwenyezi Mungu.
Na hakika sisi tulikuwa tunadhani kuwa haiwi binaadamu au jini kumzulia Mwenyezi Mungu jambo ambalo si laiki naye kusifika nalo.

(6) Na hakika walikuwako wanaume katika watu walio kuwa wakitafuta kujikinga kwa wanaume wa kijini; kwa hivyo wakawazidisha madhambi.
Na walikuwako wanaume katika wanaadamu wakitafuta ulinzi kwa wanaume wa kijini. Basi hao binaadamu hawakuwazidishia majini ila kuzidi uasi na ujinga na ujeuri.

(7) Na kwa hakika wao walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, ya kuwa Mwenyezi Mungu hatamleta Mtume.
Na hakika majini walidhani, kama mlivyo dhani nyinyi, enyi binaadamu, kwamba Mwenyezi Mungu hatamfufua yeyote baada ya kwisha kufa, wala hatowaletea watu Mtume yeyote wa kibinaadamu.

(8) Nasi tulizigusa mbingu, na tukaziona zimejaa walinzi wenye nguvu na vimondo.
Na hakika sisi tulitaka kufikilia mbinguni, tukakuta kumejaa walinzi wa kimalaika wenye nguvu, na vimondo vinavyo unguza kutoka upande huo.

(9) Na hakika tulikuwa tukikaa humo katika baadhi ya makao ili kusikiliza; lakini sasa anaye taka kusikiliza atakuta kimondo kinamvizia!
Na sisi kabla ya leo tulikuwa tukikaa pande za mbinguni kwenye makao kwa ajili ya kuchunguza khabari za mbinguni. Lakini sasa mwenye kutaka kusikiliza anakuta vimondo vinamngojea kumzuia na kumteketeza.

(10) Nasi hatujui kama wanatakiwa shari wale wanao kaa kwenye ardhi au Mola wao Mlezi anawatakia uwongofu.
Na hakika sisi hatujui imekusudiwa adhabu kwa walioko katika ardhi kwa huku kulindwa mbingu hata ikazuiliwa kusikilizwa, au Mola wao Mlezi anawatakia kheri na uwongofu?

(11) Na hakika katika sisi wamo walio wema, na wengine wetu ni kinyume na hivyo. Tumekuwa njia mbali mbali.
Na hakika miongoni mwetu wapo walio wema wachamngu, na miongoni mwetu pia wapo walio kinyume na hivyo. Na hao ni walio wastani katika wema wao. Kwa hivyo sisi ni wa makundi mbali mbali.

(12) Nasi tulijua kuwa hatutomshinda Mwenyezi Mungu duniani, wala hatuwezi kumponyoka kwa kukimbia.
Na hakika sisi tumeyakinika kwamba hatutamshinda Mwenyezi Mungu popote tutapo kuwapo katika ardhi, wala hatutamshinda hata tukifanya tuikimbie hukumu yake kwendea mbinguni.

(13) Nasi tulipo usikia uwongofu tuliuamini. Basi mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi haogopi kupunjwa wala kudhulumiwa.
Na hakika sisi tulipo isikia Qur'ani tuliiamini. Na mwenye kumuamini Mola wake Mlezi basi hachelei kupunguziwa chochote katika mema yake, wala kudhulumiwa kwa kuzidishiwa maovu yake.

(14) Na hakika wamo katika sisi Waislamu, na wamo kati yetu wanao acha haki. Basi walio silimu, hao ndio walio tafuta uwongofu.
Na hakika kati yetu wapo Waislamu wenye kuikubali Haki, na miongoni mwetu wapo wenye kuiacha njia ya uwongofu. Basi wenye kusilimu hao wameifuata njia ya Haki, na ni wenye kufanya jitihada katika kuikhiari njia hiyo.

(15) Na ama wanao acha haki, hao watakuwa kuni za Jahannamu.
Ama majeuri walio iacha njia ya Uislamu basi hao watakuwa ndio kuni za Jahannamu.

(16) Na lau kama wangeli simama sawasawa juu ya njia tungeli wanywesha maji kwa wingi,
Na hakika lau kuwa watu na majini wakifuata Njia ya Uislamu, wala wasende upogo wakaiwacha, basi bila ya shaka tutawanywesha maji mengi yatakayo enea nyakati za haja.

(17) Ili tuwajaribu kwa hayo. Na anaye puuza kumkumbuka Mola wake Mlezi atamsukuma kwenye adhabu ngumu.
Ili tuwajaribu tuwaone vipi watavyo mshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema anazo waneemesha. Na mwenye kukengeuka na ibada ya Mola wake Mlezi atamtia katika adhabu ya mashaka asiyo yaweza kuyachukua.

(18) Na hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu, basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.
Na imefunuliwa kwangu kwamba kwa hakika misikiti ni ya Mwenyezi Mungu peke yake. Basi msimuabudu yeyote pamoja na Mwenyezi Mungu.

(19) Na hakika Mja wa Mwenyezi Mungu alipo simama kumwomba, wao walikuwa karibu kumzonga!
Na imefunuliwa kwangu kwamba alipo simama Mja wa Mwenyezi Mungu, Muhammad, katika Swala yake akimuabudu Mwenyezi Mungu, majini walijikusanya makundi kwa makundi, wakistaajabu kwa waliyo kuwa wakiyaona na wakiyasikia.

(20) Sema: Hakika mimi namwomba Mola wangu Mlezi, wala simshirikishi Yeye na yeyote.
Sema: Hakika mimi namuabudu Mola wangu Mlezi peke yake, wala simshirikishi na yeyote katika ibada.

(21) Sema: Mimi sina mamlaka ya kukudhuruni wala kukuongozeni.
Sema: Mimi sina uweza wowote juu yenu wa kukuondoleeni madhara, wala kukuleteeni uwongofu na manufaa.

(22) Sema: Hakika hapana yeyote awezae kunilinda na Mwenyezi Mungu, wala sitapata pa kukimbilia isipo kuwa kwake Yeye tu.
Sema: Hakika mimi hapana yeyote awezae kuniondolea adhabu nikimuasi Mwenyezi Mungu. Wala sipati pa kukimbilia, kuikimbia adhabu yake.

(23) Ila nifikishe Ujumbe utokao kwa Mwenyezi Mungu na risala zake. Na wenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika hao watapata Moto wa Jahannamu wadumu humo milele.
Lakini niliwezalo ni kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu na Risala zake alizo nituma nizifikishe. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipuuza Dini ya Mwenyezi Mungu, basi hakika mtu huyo atapata Moto wa Jahannamu abakie humo milele.

(24) Hata watakapo yaona wanayo ahidiwa, ndipo watakapo jua ni nani mwenye msaidizi dhaifu, na mchache wa idadi.
Hata watakapo iona adhabu waliyo ahidiwaa, hapo basi watajua wakati itapo shuka, nani mwenye msaidizi dhaifu asiye na nguvu, na yupi mchache wa idadi. Ni wao au Waumini?

(25) Sema: Sijui kama yapo karibu hayo mnayo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi atayawekea muda mrefu.
Sema: Enyi makafiri! Sijui ni karibu hiyo adhabu mliyo ahidiwa, au Mola wangu Mlezi ataifanya iwe mbali?

(26) Yeye ndiye Mwenye kujua ya siri, wala hamdhihirishii yeyote siri yake,
Yeye ndiye Mjuzi wa ghaibu, yaliyo siri. Hapana mmoja katika viumbe vyake anaye ijua siri yake,

(27) Isipo kuwa Mtume wake aliye mridhia. Naye huyo humwekea walinzi mbele yake na nyuma yake.
ila Mtume aliye mridhia kumjuvya baadhi ya hiyo siri. Naye humwekea mbele ya huyo Mtume na nyuma yake Malaika wa kumkinga na wasiwasi.

(28) Ili Yeye ajue kwamba wao wamefikisha ujumbe wa Mola wao Mlezi, na Yeye anayajua vyema yote walio nayo, na amedhibiti idadi ya kila kitu.
Ili Mwenyezi Mungu ayajue hayo yametokea kwa kuwafikiana na alivyo kadiria, ya kwamba Manabii hakika wamefikisha Risala za Mola wao Mlezi. Na kwa hakika Yeye kesha jua kwa kufananua yote waliyo nayo, na anajua idadi ya viumbe vyote. Hapana kitu kinacho mpotea Yeye.