99 - Surat Az-Zalzalah ()

|

(1) Itakapo tetemeshwa ardhi kwa mtetemeko wake!
Ikitisika ardhi kwa mtikiso mkubwa, na ikasukika kwa ukomo wa kutisika na kusukika kunako mkinika na ikaweza kuchukua!

(2) Na itakapo toa ardhi mizigo yake!
Na ardhi ikatoa yote yaliomo katika ndani ya tumbo lake, ikiwa khazina au maiti walio kwisha zikwa!

(3) Na mtu akasema: Ina nini?
Na binaadamu akasema kwa kushtuka na khofu: Ardhi hii ina nini hata inatikisika hivi, na inatoa vilivyomo tumboni mwake, ndio Saa imefika?

(4) Siku hiyo itahadithia khabari zake.
Siku hiyo ardhi itamsimulia mtu khabari zake zilio mshitua,

(5) Kwa sababu Mola wake Mlezi ameifunulia!
Kwani Mlezi wake na Muumba wake atakuwa kaifunulia, kaipa Wahyi, na kaiamuru itetemeke na ijisuke suke, ndio ikafanya upesi kutekeleza amri.

(6) Siku hiyo watu watatoka kwa mfarakano wakaonyweshwe vitendo vyao!
Siku hiyo watu watatoka makaburini mbio, nao wamo katika mtafaruku, wapate kuziona hisabu zao na malipo yao aliyo waahidi Mwenyezi Mungu.

(7) Basi anaye tenda chembe ya wema, atauona!
Basi mwenye kufanya hata kitu chenye uzito wa punje ya mchanga cha kheri ataiona katika daftari lake, na atapata malipo yake.

(8) Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!
Na mwenye kufanya shari ya uzito wa chembe ya mchanga ataiona kadhaalika, na atapata malipo yake. Wala Mola wako Mlezi hatamdhulumu yeyote.