Yatupasayo kufanya katika miezi mitukufu

Maelezo

Makala hii inazungumzia: Ubora wa miezi mitukufu na mambo yanayo tupasa kufanya katika miezi hii, pia imeelezea juu ya mambo yaliyo katazwa kufanywa ndani ya miezi hii mitukufu.

Download
Tuma maoni kuhusu ukurasa huu kwa msimamizi

Maelezo ya Kina

  YATUPASAYO KUFANYA KATIKA MIEZI MITUKUFU

  < Swahili >

  Kiswahili.

  Mwandishi:

  Daudi Abubakari.

  —™

  Imehakikiwa na:

  Abubakari SHabani Rukonkwa.

  Kimerejewa na:

  Yunus Kanuni Ngenda

  مايجب فعله في الأشهر الحرم

  السواحلية

  جمعه وكتبه:

  داود أبوبكر

  المدقق :

  أبوبكر شعبان ركونكوا.

  المراجع:

  يونس كنون نغندا

  بسم الله الرحمن الرحيم

  YATUPASAYO KUFANYA KATIKA MIEZI MITUKUFU.

  Utangulizi

  Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe vyote, na rehma na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad (s.a.w) na watu wake na Maswahaba wake wote. Amma baad:

  Tumeingia Katika Miezi Mitukufu Inatupasa Kuitakasa Kwa Kuacha Maovu Na Kuzidisha Mema

  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

  {ﺇِﻥَّ ﻋِﺪَّﺓَ ﺍﻟﺸُّﻬُﻮﺭِ ﻋِﻨﺪَ ﺍﻟﻠّﻪِ ﺍﺛْﻨَﺎ ﻋَﺸَﺮَ ﺷَﻬْﺮًﺍ ﻓِﻲ ﻛِﺘَﺎﺏِ ﺍﻟﻠّﻪِ ﻳَﻮْﻡَ ﺧَﻠَﻖَ ﺍﻟﺴَّﻤَﺎﻭَﺍﺕ ﻭَﺍﻷَﺭْﺽَ ﻣِﻨْﻬَﺎ ﺃَﺭْﺑَﻌَﺔٌ ﺣُﺮُﻡٌ ﺫَﻟِﻚَ ﺍﻟﺪِّﻳﻦُ ﺍﻟْﻘَﻴِّﻢُ ﻓَﻼَ ﺗَﻈْﻠِﻤُﻮﺍْ ﻓِﻴﻬِﻦَّ ﺃَﻧﻔُﺴَﻜُﻢ}

  }Hakika idadi ya miezi kwa Allaah ni miezi kumi na mbili katika hukumu ya Allaah, tangu Alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu.

  Hiyo ndiyo Dini iliyo sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo} [At-Tawbah: 36[.

  Miezi minne hiyo imetajwa katika Hadiyth ifuatayo:

  ﻋَﻦْ ﺃَﺑَﻰ ﺑَﻜْﺮَﺓ ﺃَﻥَّ ﺭَﺳُﻮﻝ ﺍﻟﻠَّﻪ - ﺻَﻠَّﻰ ﺍﻟﻠَّﻪ ﻋَﻠَﻴْﻪِ ﻭَﺳَﻠَّﻢَ - ﻗَﺎﻝَ ﻓِﻲ ﺣَﺠَّﺔ ﺍﻟْﻮَﺩَﺍﻉ:{ ﺇِﻥَّ ﺍﻟﺰَّﻣَﺎﻥ ﻗَﺪْ ﺍِﺳْﺘَﺪَﺍﺭَ ﻛَﻬَﻴْﺌَﺘِﻪِ ﻳَﻮْﻡ ﺧَﻠَﻖَ ﺍﻟﻠَّﻪ ﺍﻟﺴَّﻤَﻮَﺍﺕ ﻭَﺍﻟْﺄَﺭْﺽ ﺍﻟﺴَّﻨَﺔ ﺍِﺛْﻨَﺎ ﻋَﺸَﺮ ﺷَﻬْﺮًﺍ ﻣِﻨْﻬَﺎ ﺃَﺭْﺑَﻌَﺔ ﺣُﺮُﻡ : ﺛَﻠَﺎﺙ ﻣُﺘَﻮَﺍﻟِﻴَﺎﺕ ﺫُﻭ ﺍﻟْﻘَﻌْﺪَﺓ ﻭَﺫُﻭ ﺍﻟْﺤِﺠَّﺔ ﻭَﺍﻟْﻤُﺤَﺮَّﻡ ﻭَﺭَﺟَﺐ ﻣُﻀَﺮ ﺍﻟَّﺬِﻱ ﺑَﻴْﻦ ﺟُﻤَﺎﺩَﻯ ﻭَﺷَﻌْﺒَﺎﻥ}

  ﺻَﺤِﻴﺢ ﺍﻟْﺒُﺨَﺎﺭِﻱّ

  Kutoka kwa Abu Bakrah ambaye amesema: “Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema alipokuwa katika Hijjah ya kuaga (Hijjah wa mwisho): {{Mgawanyo wa nyakati umerudi kama ulivyo (wakati) Allaah Alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na mbili, minne ambayo ni mitukufu; mitatu inafuatana pamoja (nayo ni) Dhul-Qa'adah, Dhul-Hijjah na Muharram, na (wa nne ni) Rajab wa (kabila la) Mudhwar ambao upo baina ya Jumaada na Sha'abaan)). [Al-Bukhaariy[

  Hivyo tunaona kwamba ni kuanzia mwezi huu tulioingia wa Dhul-Qa'adah na miezi miwili ijayo inayofuatia kisha tena hadi tutakapojaaliwa kufika mwezi wa Rajab In shaa Allaah.

  Katika miezi yote kumi na mbili Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ameichagua hii minne na Ameifanya kuwa ni mitukufu na kusisitiza kuitakasa, na kwamba dhambi zitakazofanyika humo ni zaidi na hali kadhalika thawabu za vitendo vyema zinakuwa maradufu na zaidi. [Atw-Twabariy 14: 238[

  Ni sawa kama Anavyoonya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kufanya maasi katika sehemu tukufu Alipotaja Masjidul-Haraam (Msikiti Mtukufu Makkah):

  {ﺇِﻥَّ ﺍﻟَّﺬِﻳﻦَ ﻛَﻔَﺮُﻭﺍ ﻭَﻳَﺼُﺪُّﻭﻥَ ﻋَﻦ ﺳَﺒِﻴﻞِ ﺍﻟﻠَّﻪِ ﻭَﺍﻟْﻤَﺴْﺠِﺪِ ﺍﻟْﺤَﺮَﺍﻡِ ﺍﻟَّﺬِﻱ ﺟَﻌَﻠْﻨَﺎﻩُ ﻟِﻠﻨَّﺎﺱِ ﺳَﻮَﺍﺀ ﺍﻟْﻌَﺎﻛِﻒُ ﻓِﻴﻪِ ﻭَﺍﻟْﺒَﺎﺩِ ﻭَﻣَﻦ ﻳُﺮِﺩْ ﻓِﻴﻪِ ﺑِﺈِﻟْﺤَﺎﺩٍ ﺑِﻈُﻠْﻢٍ ﻧُﺬِﻗْﻪُ ﻣِﻦْ ﻋَﺬَﺍﺏٍ ﺃَﻟِﻴﻢ}ٍ

  }Hakika wale waliokufuru na wakazuilia Njia ya Allaah na Msikiti Mtakatifu, ambao Tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayetaka kufanya upotofu humo kwa dhulma, basi Tutamwonjesha adhabu iumizayo{

  ]Al-Hajj: 25[.

  Qataadah amesema kuhusu kauli ya Allaah:

  {ﻓَﻼَ ﺗَﻈْﻠِﻤُﻮﺍْ ﻓِﻴﻬِﻦَّ ﺃَﻧﻔُﺴَﻜُﻢ}

  )Basi msidhulumu nafsi zenu humo)

  Dhulma itakayotendeka katika miezi mitukufu ni mbaya na kubwa (au hatari) kuliko dhulma itakayotendeka katika miezi mingine. Hakika dhulma daima ni makosa, lakini Allaah Hufanya baadhi ya vitu kuwa ni vizito kuliko vingine kama Anavyopenda.”

  Akaendelea kusema:

  Allaah Amechagua baadhi ya viumbe Vyake na baadhi ya vitu kuwa bora zaidi kuliko vingine. Amechagua Wajumbe kuwa ni bora kutoka katika Malaika na kutoka binaadamu. Vile vile Amechagua baadhi ya kauli Zake kuwa ni bora kuliko nyingine, Misikiti kuwa bora kuliko sehemu nyingine za ardhi, Ramadhaan na miezi mitukufu kuwa bora kuliko miezi mingine, siku ya Ijumaa kuwa ni bora kuliko siku nyingine na usiku wa Laylatul-Qadr kuwa ni bora kuliko nyusiku zingine. Kwa hiyo takasa vile Alivyovitakasa Allaah, kwani kufanya hivyo ni vitendo vya watu wenye akili na wenye kufahamu.” [Tafsiyr ya Ibn Kathiyr.[

  MIONGONI MWA YALIYOKATAZWA KATIKA MIEZI HII MITUKUFU:

  Ni kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala:

  {ﻳَﺴْﺄَﻟُﻮﻧَﻚَ ﻋَﻦِ ﺍﻟﺸَّﻬْﺮِ ﺍﻟْﺤَﺮَﺍﻡِ ﻗِﺘَﺎﻝٍ ﻓِﻴﻪِ ﻗُﻞْ ﻗِﺘَﺎﻝٌ ﻓِﻴﻪِ ﻛَﺒِﻴﺮٌ ﻭَﺻَﺪٌّ ﻋَﻦ ﺳَﺒِﻴﻞِ ﺍﻟﻠّﻪِ ﻭَﻛُﻔْﺮٌ ﺑِﻪِ ﻭَﺍﻟْﻤَﺴْﺠِﺪِ ﺍﻟْﺤَﺮَﺍﻡِ ﻭَﺇِﺧْﺮَﺍﺝُ ﺃَﻫْﻠِﻪِ ﻣِﻨْﻪُ ﺃَﻛْﺒَﺮُ ﻋِﻨﺪَ ﺍﻟﻠّﻪِ ﻭَﺍﻟْﻔِﺘْﻨَﺔُ ﺃَﻛْﺒَﺮُ ﻣِﻦَ ﺍﻟْﻘَﺘْﻞِ}

  }Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita wakati huo ni dhambi kubwa Lakini kuzuilia watu wasiende katika Njia ya Allaah na kumkanusha Yeye, na kuzuilia watu wasende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Allaah. Na fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua{

  ]Al-Baqarah: 217.[

  MAASI MENGINE AMBAYO TUNATAKIWA TUJIKUMBUSHE KUYAACHA:

  1.Kumshirikisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kama kwenda kwa wachawi na waganga na kuwaamini wanayoyatabiri kwa watu

  2.Kuiba.

  3.Kuzini.

  4.Kulewa.

  5.Kumdhulumu mtu haki yake.

  6.Kugombana, kutukanana, kuvunjiana heshima, kudharauliana n.k.

  7.Kusengenya (Ghiybah(

  8.Kusema uongo, na kila aina ya uovu mwengine.

  MAMBO MEMA YA KUKUMBUSHANA KUFANYA KATIKA MIEZI HII MITUKUFU:

  1.Kuongeza Sunnah za Swalah,

  2.Kufunga Swawm za Sunnah kama Jumatatu na Alkhamiys, Ayyaamul-Biydhw (tarehe 13,14 na 15) na Swawm ya Nabii Daawuwd (kufunga kila baada ya siku moja)

  3.Kujielimisha mambo ya dini kwa kusoma vitabu na kusikiliza mawaidha;

  4.Kuomba Maghfirah na Tawbah;

  5.Kufanya kila aina ya dhikr (kumkumbuka na kumtaja Allaah), kwa kusoma Qur-aan kwa wingi, kumshukuru, kumtukuza, kuomba du'aa n.k.;

  6.Kuwasiliana na ndugu na jamaa;

  7.Kutenda wema kwa jirani, marafiki na watu wote kwa ujumla;

  8.Kutoa sadaka;

  9.Kulisha masikini;

  10.Kupatanisha waliogombana;

  11.Kuamrishana mema na kukatazana maovu, na mengi mengineyo katika vitendo vyema.

  Allaah Atupe tawfiq tuepukane na maasi na atujaalie tufanye mema katika miezi hii mitukufu na miezi mingine, Ameen.