MAMBO 10 YATAKAYOKUFANYA UWE MUME BORA

Maelezo

Mada hii inazungumzia sababu kumi zinazo mfanya mume awe bora.

Download
Tuma maoni kuhusu ukurasa huu kwa msimamizi

Maelezo ya Kina

  بسم الله الرحمن الرحيم

  MAMBO 10 YATAKAYOKUFANYA UWE MUME BORA

  Imeandikwa na Kabuga Kanyegeri

  Imepitiwa na Abubakari Shabani Rukonkwa.

  Utangulizi:

  Kila sifa kamilifu nizake Allah mtukufu alie fanya maisha yasiwe mazuri mpaka mtakapo kuwa wawili mke na mume kasha akamfanya mume ndie msimamizi wa mambo yoote katika nyumba,kasha akawaumba wanawake ili wawe pomziko na starehe kwa waume zao,anasema Allah Mtukufu:

  {Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri }Ar-Rum 21.

  Sala na amani zimuendee Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juuyake mtume ambae alikuwa nimfano mwema kwa waume bora na alikuwa nimwalimu wa waalimu, na ziwe juu ya maswahaba zake na woote watakao mfuata kwa wema mpaka siku ya Qiyama.

  Mada hii inazungumzia sababu ya kuwa mume bora nimada muhimu sana hasa katika zama hizi za utanda wazi na zama za fitna ambazo watu wameifanya halali kuwa haramu mabaya kuwa nimazuri ,NK

  Leo tunakuletea mambo haya ili uwe mume bora kwa familia yako,sababu hizi niningi sana ila tuta kuelimisha haya mambo kumi tulio kuchagulia.

  1. Vaa vizuri kwa ajili ya mkeo, uonekane nadhifu na mwenye kunukia vizuri. Kama ambavyo mume anapenda mke wake aonekane maridadi kwa ajili yake, naye pia anapenda mume wake avae vizuri kwa ajili yake. Kumbuka kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w) daima alikuwa akianza kupiga mswaki pindi anaporudi nyumbani na daima alikuwa akipenda harufu nzuri.

  2. Muite mkeo kwa majina mazuri. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akiwaita wakeze kwa majina mazuri ambayo hata wao wenyewe walikuwa wakipenda kuyasikia. Muite mkeo kwa jina zuri analolipenda zaidi kulisikia, na epuka kutumia majina yatakayoumiza hisia zake.

  3. Usiamiliane na mkeo kama nzi. Mara zote katika maisha yetu ya kila siku huwa hatukumbuki kuwa kuna nzi mpaka pale wanapotuudhi. Angalia, mkeo hukufanyia mambo mengi mema kwa siku nzima ambayo huwa huyaangalii, ila pale anapokufanyia kosa kidogo unamtazama. Usiishi naye kwa namna hii; yatambue mambo mema yote anayokufanyia.

  4. Ukiona kosa kutoka kwa mkeo, jaribu kutohamaki au kumkaripia, muongoze kwa hekma na busara, atakuelewa! Hivi ndivyo Mtukufu Mtume (s.a.w) alivyokuwa pale anapoona jambo lisilokuwa muafaka kutoka kwa wakeze. Ni njia ambayo ni wanaume wachache wa Kiislamu wameimudu.

  5. Onyesha tabasamu kwa mkeo pindi unapomuona na daima zidisha kumkumbatia. Kutabasamu ni sadaqah na mkeo naye anastahili hiyo sadaka kwa namna ya kipekee. Fikiria maisha yatakavyokuwa pale mkeo anapokuona unatabasamu kwa ajili yake! Kumbuka pia zile hadith zinazosema kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akimbusu mkewe kabla ya kwenda kuswali, hata kama akiwa amefunga.

  6. Mshukuru kwa kila analokufanyia. Kisha mshukuru tena na tena! Angalia, mkeo anakuandalia chakula, anasafisha nyumba na anafanya kazi nyingine nyingi mno. Wakati mwingine hata kumpongeza hufanyi! Usiwe hivyo, mshukuru na useme: “Ahsante mke wangu!”

  7. Muombe akuandikie mambo kumi uliyomfanyia na yakamfurahisha. Kisha mfanyie mambo hayo tena. Mara nyingi huwa ni vigumu kujua mambo yanayomfurahisha mkeo. Huna haja ya kubahatisha, muombe akwambie na kisha uyafanye hayo na mengine pia katika kipindi chote cha maisha yenu.

  8. Usiyapuuze na kuyabeza matakwa yake. Mfariji. Wakati mwingine wanaume huyadharau maombi ya wake zao. Mtukufu Mtume (s.a.w) hakuwa hivyo.

  9. Uwe mwenye kunyumbulika na fanya michezo na mkeo. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akishindana na mkewe bibi Aisha katika mchezo wa kukimbia. Mara ya mwisho umemfanyia lini mkeo jambo kama hilo?

  10.Daima kumbuka maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w): “Mbora wenu ni yule anayeitendea mambo bora familia yake. Nami ni mbora wenu kwa familia yangu.” Jaribu kuwa bora!

  Usisahau kumuomba Mwenyezi Mungu aifanye ndoa yako kuwa bora.

  Mwisho:Ninaamini kuwa umefaidika vyakutosha na utayafanyia kazi kwa idhini ya Allah.

  Ninamuomba Allah azijaze nyumba na nyoyo zetu utulivu, upendo na kuhurumiana sasa na hata milele!!!.