SABABU 33 SINAZO MFANYA MUISLAM AWE NA UNYENYEKEVU KATIKA SWALA

Maelezo

Kitabu hiki kinazungumzia Sababu 33 za Unyenyekevu katika Swala na Mambo yanayo ondoa Unyenyekevu atika Swala.

Download
Tuma maoni kuhusu ukurasa huu kwa msimamizi

Maelezo ya Kina

بسم الله الرحمن الرحيم

 SABABU 33 ZINAZOMFANYA MUISLAM AWE NA UNYENYEKEVU KATIKA SWALA.

 UTANGULIZI

Kila sifa kamilifu nizake Allah mtukufu ambae katuchagulia uislamu kuwa ndio dini ya kweli, na akaifanya starehe ya muislamu kuwa inapatikana katika swala.

Swala na amani zimuendee Mtume Muhammad s.a.w. ambae kaletwa na Allah ili kutufafanulia dini hii na kuwa ndio kiigizo chema, na ziwe juu ya Ahali zake na maswahaba zake na wote wenye kumfuata mpaka siku ya Qiyama.

Baada ya kumshukuru Allah mtukufu na kumtakia rehma mtukufu wetu wa daraja Mtume Muhammad s.a.w. kuna mambo mengi ambayo yanayo mfanya muislam asiwe na unyenyekevu katika utekelezaji wa ibada ya swala.

Unyenyekevu katika swala ni moja katika sababu za kukubaliwa swala, muislamu anapo kosa unyenyekevu katika swala inaweza kuwa sababu ya kuto kukubaliwa swala.

Hayo yamekuja katika hadithi mashuhuri kwa jina la (Musiu swalah) yani Hadithi ya asie juwa kuswali.

Hadithi hiyo nikama ifuatavyo:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه أَنَّ النَّبِيَّ صلى الله عليه وسلم دَخَلَ الْمَسْجِدَ , فَدَخَلَ رَجُلٌ فَصَلَّى , ثُمَّ جَاءَ فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ : ارْجِعْ فَصَلِّ , فَإِنَّك لَمْ تُصَلِّ . فَرَجَعَ فَصَلَّى كَمَا صَلَّى , ثُمَّ جَاءَ فَسَلَّمَ عَلَى النَّبِيِّ صلى الله عليه وسلم فَقَالَ : ارْجِعْ فَصَلِّ , فَإِنَّك لَمْ تُصَلِّ - ثَلاثاً - فَقَالَ : وَاَلَّذِي بَعَثَكَ بِالْحَقِّ لا أُحْسِنُ غَيْرَهُ , فَعَلِّمْنِي , فَقَالَ : إذَا قُمْتَ إلَى الصَّلاةِ فَكَبِّرْ , ثُمَّ اقْرَأْ مَا تَيَسَّرَ معك مِنْ الْقُرْآنِ , ثُمَّ ارْكَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ رَاكِعاً , ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَعْتَدِلَ قَائِماً , ثُمَّ اُسْجُدْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ سَاجِداً, ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ جَالِساً . وَافْعَلْ ذَلِكَ فِي صَلاتِكَ كُلِّهَا .

رواه البخري رقم (760)ومسلم (397)

Maana ya hadithi hii nikwamba:

((Kutoka kwa Abuu Hurayra radhi za Allah ziwe juu yake hakika Mtume s.a.w. aliingia msikitini-akaswali alipomaliza kuswali akakaa pembezoni mwa msikiti-kisha akaingia bwana mmoja akaswali, baada ya kuswali akaenda kumsalimia Mtume s.a.w, Mtume akamwambia: rudia swala kwani haujaswali chochote, akarejea kuswali akaswali kama alivyo swali mwanzo, kisha akaenda kumsalimia Mtume s.a.w. akamwambia: rudia swala kwani hauja swali chochote, akarudi kuswali akaswali kama alivyo swali mwanzo, kisha akaenda kwa Mtume s.a.w. akamsalimia, akamwambia mtume: rudia swala kwani haujaswali chochote, mara ya tatu.

Akasema yule bwana ninamuapa Allah ambae kakutuma kwa haqqi sijui kuswali zaidi ya hivyo naomba unifundishe,

Mtume s.a.w. akasema: utakapo simama kwaajili ya swala toa takbira, kisha soma sura nyepesi katika Qur’an, kisha rukuu mpaka utulizane katika rukuu, kisha inuka mpaka uwe sawasawa katika kusimama, kisha sujudu mpaka utulizane katika sijda, kisha inuka kutoka katika shida mpaka utulizane katika mkao, kisha Mtume akamwambia: Fanya hivyo katika swala yako yote))

(Albukhary No760 na Muslim No397).

Subhana Allah! Tatizo lililo mpata swahaba huyu linaonyesha kuwa alikuwa akiswali haraka haraka bila unyenyekevu, nahii ni dalili inayo thibitisha kuwa swala isiyokuwa na unyenyekevu haipokelewi asilimia 90%.

Tatizo la ukosefu wa unyenyekevu limekuwa nitatizo sugu katika swala nyingi za waislamu, swala zingine zimempita hata huyu Swahaba aliyerudishwa mara tatu na Mtume s.a.w.

Ndugu zangu huu nimsiba mkubwa kua tunapoteza umri katika swala zisizo na manufaa nasisi.

Nisababu gani ambazo zinamfanya muislam awe na unyeyekevu katika swala?

Katika kitabu hiki tutazungumzia sababu 33 zinazo mfanya muislamu awe na unyenyekevu katika swala.

Tunamuomba Allah mtukufu aturuzuku ikhlaswi katika kauli na matendo atusamehe yale tuliyo yatenda kwasiri na dhahiri, Amiin.

 SABABU 33 ZINAZO MFANYA MUISLAMU AWE NA UNYENYEKEVU KATIKA SWALA.

Niwajibu kwa kila muislamu azijuwe sababu zinazo mfanya awe na unyenyekevu katika swala, ili awe na ufanisi wakutosha katika utekelezaji wa swala yake, ufafanuzi wa sababu hizo nikama ifuatavyo:

 1.NIKUFANYA MAANDALIZI KWA AJILI YA SWALA.

Hii nisababu ya kwanza katika sababu 33 zinazo mfanya muislam awe na unyenyekevu katika swala.

Muislam anatakiwa ajiandae mapema na kujipamba kwa ajili ya kwenda kuongea na Mola wake katika swala.

Maandalizi ya swala yanapatikana katika mambo yafuatayo:

A. Kufatilizia muadhini pindi unapo sikia Adhana.

B. Kusoma dua iliyo thibiti baada ya adhana.

C. Kusoma dua baina ya adhana na iqama, kwasababu dua baina ya adhana na iqama niyenye kujibiwa na Allah.

D. Nikutawadha vizuri nakuanza udhu kwa kusema Bismilaah rahmaani rahiim, kisha kusoma dua iliyo thibiti baada ya udhu.

E. Nikujihimiza kupiga mswaki.

F. Nikujipamba kwa kuvaa nguo nzuri zenye kupendeza.

G. Nikwenda msikitini mapema kwa utulivu na upole.

H. Kuipanga swafu ilio nyooka vizuri.

I. Nikusubiri swala.

 2. NIKUWA NA UTULIVU KATIKA SWALA.

(كان النبي صلى الله عليه وسلم يطمئن حتى يرجع كل عظم إلى موضعه) صحح إسناده في صفة الصلاة ص: 134 طبعة.11.

Imethibiti kutoka kwa Mtume s.a.w kwamba alikuwa akiswali anatulizana mpaka kila kiungo kinarudia mahala pake. Hadithi hii ameisahihisha Imam albani.

(sifa ya swala ya mtume s.a.w. uk 134).

 3. KUKUMBUKA UMAUTI KATIKA SWALA.

Kukumbuka umauti katika swala nisababu kubwa inayomfanya muislam awe na unyenyekevu akiwa katika swala.

Imethibiti katika hadithi sahihi iliyomo katika kitabu cha silsila ya hadithi sahihi ya shekh Albani kutoka kwa Anasi Bin Maliki alisema: Alisema Mtume s.a.w:

قال النبي صلى الله عليه وسلم: اذكر الموت في صلاتك، فإن الرجل إذا ذكر الموت في صلاته لحري أن يحسن صلاته. أخرجه البيهقيفي كتاب الزهد الكبير وصاحب كنز العمال، وحسنه الشيخ الألباني في السلسلة الصحيحية وفي صحيح الجامع. أخرجه الديلمى (1/431 ، رقم 1755) .

Anasema Mtume s.a.w: ((kumbukeni umauti katika swala zenu, hakika mtu anapo kumbuka umauti katika swala yake inakuwa ni karibu kwa mtu kuifanya vizuri swala yake)). Hadithi hii ameitoa Imamu Bayhaqy na akaisahihisha imamu Albany. pia kaitoa hadithi hii Imamu Daylamy (vol1uk:431).

Kukumbuka umauti katika swala ni amri ya Mtume s.a.w ili kuleta unyenyekevu katika swala, na Mtume s.a.w amefahamisha haya baada ya kupata wahyi kutoka kwa Allah.

 4. KUZINGATIA AYAH ZA QURAAN AMBAZO ZINAZO SOMWA, NA ADHKARI ANAZO ZISEMA KATIKA SWALA, NA KUJIPA BIDII KATIKA UTEKELEZAJI WA SWALA.

Mazingatio katika swala hayapatikani ispokuwa kwa kujua maana ya Aya ambazo zinazo somwa ndani ya swala, kufanya hivyo itamsaidia kupata mazingatio mpaka kuleta machozi ndani ya swala, na kuathirika kiimani kama Allah anavyo sema:

قال الله تعالى:(والذين إذا ذكروا بآيات ربهم لم يخروا عليها صما وعميانا)(الفرقان/73)

Anasema Allah mtukufu: (Nawale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu). Furqaan 73.

Miongoni mwa mambo ambayo yanayo saidia muislam kupata mazingatiyo katika Aya zinazo somwa katika swala:

A. Nikuomba hifadhi na Adhabu ya moto, pindi imamu anapo soma Aya zinazo zungumzia moto.

B. Nikumsabihi Allah mtukufu katika kila Aya ambazo zinazo zungumzia Tasbihi.

C. Nikuomba pepo pindi imamu anapo soma Aya zinazo zungumzia pepo.

Pia miongoni mwa mambo ambayo yanayo msaidia muislam kuwa katika swala kikamilifu.

A. Nikuitikia ''Amiin'' Baada ya imamu kusoma suratul Fatiha (Alhamdu) na kuna malipo makubwa kwa mwenye kusema Amiin ambayo yamethibiti katika hadithi sahihi, ambayo kaipokea Abuu Haurayrah:

عن أبي هريرة - رضي الله عنه - أن النبي - صلى الله عليه وسلم - قال: (إذا أمن الإمام فأمنوا فإنه من وافق تأمينه تأمين الملائكة غفر له ما تقدم من ذنبه) رواه البخاري.رقم(140)

Kutoka kwa Abuu Hurayra Radhi za Allah ziwe juu yake, hakika Mtume Rehma na amani ziwe juu yake alisema: (Atakapo sema Imamu Amiin basi na nyie semeni Amiin hakika yule ambae muitikio wake utakubaliyana na muitikio wa malaika, basi atasamehewa madhambi yaliyo tangulia)

Ameipokea hadithi hii na Imamul Bukhari. NO(140).

TNB: Katika hadithi hii tukufu kuna ubainifu kuwa imamu anapo soma Quraan katika swala malaika wana msikiliza na anapo maliza malaika wanaitikia, Amiin.

Pia katika mambo yanayo msaidia muislamu awe mnyenyekevu katika swala, nikusema nyuma ya imamu pindi anaposema: ((samia Allah liman hamida)).

Maana yake ni: "kamsikia Allah mjawake ambae anae msifu".

Maamuma anatakiwa kusema: (Rabana walakal hamdu).

Maana yake ni: ewe mola wetu wewe ndie mwenye sifa.

Kwasababu kufanya hivyo kuna ujira mkubwa.

 5. NIKUSOMA QUR’AN KWA VITUO VYAKE, BILA KUUNGANISHA.

Miongoni mwa sababu zinazo leta unyenyekevu katika swala nikusoma Quraan kwa vituo bila kuziunga Aya kwa pumzi moja.

Kusoma Quraan kwa kuzingatia vituo vyake inaleta unyenyekevu, na nisababu ya kupata mazingatio, nakufahamu yanayo somwa, na kufanya hivyo nikufuata sunna alio kuwa akiifanya Mtume rehma na amani ziwe juu yake.

وعن يعلي بن مملك أنه سأل أم سلمة عن قراءة رسول الله صلى الله عليه وسلم وصلاته ، قالت : مالكم وصلاته ، ثم نعتت قراءته فإذا هي تنعت قراءة مفسرة حرفا حرفا .أخرجه أحمد والترمذي والنسائي بسند صحيح.

Kutoka kwa swahaba yaala Bin Maliki alimuuliza Mama wa waislam Ummu salama kuhusu kisomo na swala ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake, akasema Ummu salama: mna nini na swala yake! kisha akasifu kisomo cha Mtume rehma na amani ziwe juu yake,

Akasema: alikuwa akisoma herufi moja moja kwa vituo).

Ameitoa imamu Ahmad na Tirmidhy na Alnasaai kwa upokezi sahihi.

 6. NIKUSOMA QUR’AN KWA SAUTI NZURI.

Kusoma Qur’an kwa sauti nzuri yenye kupendeza nikatika sababu zinazo mfanya muislamu aswali kwa unyenyekevu.

Allah mtukufu amehimiza waislamu wakisoma Quraan wasome kwa sauti nzuri wakizingatia hukumu na kanuni za kusoma Quraan, anasema Allah S.w katika Qur’an tukufu Suratul Muzammil sura (73/3)

 {ورتل القرآن ترتيلا}مزمل 3

Maana ya Ayah hii nikwamba: soma Qur’an kwa utaratibu na kwa uzuri.

Katika Hadithi aliyo ipokea Swahaba Baraa Bin Azibu radhi za Allah ziwe juu yake alisema: alisema Mtume swala Allah alayhi wasalam:

(وحسنوا القرآن بأصواتكم فإن الصوت الحسن يزيد القرآن حسناً).

Maana ya hadithi hii nikwamba: Alisema mtume rehma na amani ziwe juu yake (( isomeni Quraan kwa sauti nzuri hakika sauti nzuri inazidisha Quraan uzuri)).

 7.AFAHAMU ANAE SWALI KUWA ALLAH ANAE MUOMBA ANAJIBU DUWA YAKE.

Hii nisababu miongoni mwa sababu zinazo mfanya muislam awe na unyenyekevu katika swala, pindi anapo diriki kuwa dua zote anazo omba zitajibiwa, kwahiyo hata leta mchezo katika ibada yake.

Anasema Mtume rehma na amani ziwe juu yake katika hadithi aliyo isimulia Abuu Hurayrah radhi za Allah ziwe juu yake:

عن أبي هريرة قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: قال الله تعالى: قسمت الصلاة بيني وبين عبدي نصفين، ولعبدي ما سأل، فإذا قال العبد:{ الحمد لله رب العالمين } قال الله تعالى: حمدني عبدي، وإذا قال: {الرحمن الرحيم } قال الله تعالى: أثنى علي عبدي وإذا قال: { مالك يوم الدين} قال: مجدني عبدي، وقال مرة: فوض إلي عبدي فإذا قال: { إياك نعبد وإياك نستعين } ، قال: هذا بيني وبين عبدي ولعبدي ما سأل، فإذا قال: { اهدنا الصراط المستقيم صراط الذين أنعمت عليهم غير المغضوب عليهم ولا الضالين } ، قال: هذا لعبدي ولعبدي ما سأل. مسلم في الصلاة، باب وجوب قراءة الفاتحة في كل ركعة 1/296 (395) .

Maana ya hadithi hii: kutoka kwa Abuu Hurairah radhi za allah ziwe juu yake alisema: Nilimsikia Mtume wa Allah anasema:

Alisema Mtume rehma na amani ziwe juu yake, alisema Allah mtukufu: nimeigawa swala baina yangu na mja wangu nusu mbili na mja atapata yote aliyoyaomba:

-Anapo sema: (Alhamdu lilah Rabil alamiin).

Anasema Allah mtukufu: Amenishukuru mja wangu.

-Anapo sema (Arahmani rahim).

Anasema Allah mtukufu: Amenisifu mja wangu.

-Anapo sema: (Maliki yaumidini).

Anasema Allah mtukufu: Amenitakasa mja wangu.

-Anapo sema: (Iyyaaka naabudu waiyyaaka nastaiin).

Anasema Allah mtukufu: hii nibaina yangu na baina ya mja wangu na nihaki kwa mja wangu kujibiwa na kupewa aliyo yaomba.

-Anapo sema: (Ihdina swiratwal mustaqiima swiratwalladhina an amtaalayhim* Ghayril maghdhubi* alayhim wala dhwaaalin). Amiin

Anasema Allah mtukufu: hii ni ya mja wangu na anastahiki mja wangu kupata aliyo omba.

 8. NIKUSWALI NYUMA YA SITRA (KIZUIZI) NA KUISOGELEA.

Sitra ni kizuizi ambacho kinacho mzuia mpitaji kukata swala ya mwenye kuswali, inaweza kuwa nguzo ya msikiti au ukuta wa msikiti kwa upande wa mbele ao kuweka kitu chochote mbele yake.

Katika mambo yenye kuleta unyenyekevu katika swala, nikuweka sitra kwa mtu ambae anaswali akiwa peke yake au kuweka mbele ya imamu.

Kuswali nyuma ya sitra kuna faida nyingi miongoni mwa faida hizo:

A. Kuyazuiya macho kuangalia yalio mbele yako.

B. Kumzuiya mpitaji kukata swala yako.

C. Kumpa nafasi mwenye kupita.

D. Kumzuiya shetani kukukatia swala yako, au kuiharibu swala yako.

عَنْ سَهْلِ بْنِ أَبِى حَثْمَةَ يَبْلُغُ بِهِ النَّبِىَّ -صلى الله عليه وسلم- قَالَ « إِذَا صَلَّى أَحَدُكُمْ إِلَى سُتْرَةٍ فَلْيَدْنُ مِنْهَا لاَ يَقْطَعُ الشَّيْطَانُ عَلَيْهِ صَلاَتَهُ » رواه أبوداود

Kutoka kwa Sahli Bin Abii Hathamah radhi za Allah ziwe juu yake alisema: Alisema Mtume rehma na amani ziwe juu yake alisema: (Atakapo swali mmoja wenu akiwa ameweka sitra mbele yake basi aisogelee ili shetani asiikate swala yake). Hadithi hii kaipokea Abuu Daudi.

 9. NIKUWEKA MKONO WA KULIA JUU YA MKONO WA KUSHOTO JUU YA KIFUA.

Alikuwa Mtume Rehma na amani ziwe juu yake, anapo simama ili kuswali anaweka mkono wake wakulia juu ya mkono wakoshoto juu ya kifua chake.

Kufanya hivyo kuna hekima nyingi, miongoni mwa hekima hizo:

A. Nikutekeleza Sunna ya Mtume rehma na amani ziwe juu yake.

B. Kufanya hivyo nikujipamba na sifa ya unyenyekevu na sifa ya muombaji ambae anatakiwa kuwa dhalili mbele ya Allah.

 10. NIKUTIZAMA MWENYE KUSWALI MAHALA PAKUSUJUDU.

Muislamu pindi anapo swali anatakiwa macho yake yaangalie sehemu mbili:

1. Akiwa amesimama anatakiwa angalie sehemu anayosujudu.

2. Akiwa katika tahiyatu anatakiwa angalie kwenye kidole cha shahada huku akisema (atahiyatu).

عن عائشة-رضي الله عنها- أن رسول الله -صلى الله عليه وسلم -كان إذا صلى طأطأ رأسه و رمى ببصره نحو الأرض .

رواه البيهقي في السنن الكبرى، 2/ 283.

قال الشيخ الألباني-رحمه الله- : صحيح وله شواهد .

Kuto kwa Mama wa waislam Bi Aisha radhi za Allah ziwe juu yake, hakika Mtume rehma na amani ziwe juu yake alikuwa anapo swali anainamisha kichwa chake, na anaangalia chini).

Hadidhi hii ameipokea imamu Albayhaqy katika kitabu chake (Sunanul kubra 2/283).

Amesema Imamu Albany: Hadithi hii ni sahihi kwasababu ina hadithi zingine zinazo itia nguvu.

 11. NIKUTIKISA KIDOLE WAKATI AKISOMA TAHIYATU.

Kutikisa kidole wakati wa kusoma tahiyatu nikatika mambo ambayo yanayo leta unyenyekevu katika swala, pia nikatika mambo yanayo muumiza shetani mchafu ambae ndie aduwi mkubwa wa mwanadamu.

Anasema Mmtume rehma na amani ziwe juu yake: (Kutikisa kidole wakati wa kusoma tahiyatu nikali kwa shetani kuliko kumpiga kwa chuma) hadithi hii ameipokea Imamu Ahmad.

FAIDA ZA KUNYOSHA KIDOLE WAKATI WA SHAHADA:

A. Kuna mkumbusha mja kuwa Allah mtukufu ni mmoja.

B. Kunamfanya mja awe na ikhlas katika ibada yake.

C. Kunamchukiza shetani, Allah atukinge na shetani.

 12. KUSOMA SURA NA AYA TOFAUTI NA DHIKRI NA DUA TOFAUTI KATIKA SWALA.

Nakufanya hivyo kunamfanya mwenye kuswali awe nimwenye kupata hisia mpya na itamfaidisha kwa kujua madhumuni tofauti ya Ayah na Adhkari.

Kusoma ayah tofauti katika swala nikatika sunnah, na kunasaidia kuleta unyenyekevu katika swala.

 13. NIKULETA SIJDAH PINDI UNAPO SOMA AYAH INAYOZUNGUMZIA KUSUJUDU.

Anasema Allah mtukufu:

{وَيَخِرُّونَ لِلأَذْقَانِ يَبْكُونَ وَيَزِيدُهُمْ خُشُوعاً}(الإسراء:109).

Maana ya Ayah ii nikwamba:

(Na huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu)

 14. NIKUOMBA HIFADHI KWA ALLAH KUTOKANA NA SHETANI.

عن أبي العاص رضي الله عنه قال: يا رسول الله إن الشيطان قد حال بيني وبين صلاتي وقراءتي يلبسها علي، فقال الرسول عليه الصلاة والسلام: «ذاك شيطان يقال له خنزب فإذا أحسسته فتعوذ بالله منه واتفل على يسارك ثلاثاً». قال: ففعلت ذلك فأذهبه الله عني.

Kutoka kwa Abil Asi radhi za Allah ziwe juu yake alisema: Ewe Mtume wa Allah hakika shetani amezuia baina yangu na baina ya swala yangu na kisomo changu ananivuruga na kunichanganya wakati nikisoma ndani ya swala, akasema Mmtume (swala allah alaihi wasalam): huyo ni shetani anayeitwa (KHUNZUBU) ukihisi anakushawishi basi omba hifadhi kwa Allah kutokana naye, na uteme mate kushotoni kwako mara tatu.

Akasema Swahaba Abul aswi: Nikafanya kama alivyo niambia Mtume -swala allah alaihi wasalam-akaniondoshea Allah huyo shetani.

Kwahiyo katika mambo ambayo yanaleta unyenyekevu katika swala nikumuomba Allah akukinge na vishawishi vya shetani katika utekelezaji wa swala au ibada yoyote.

 15-NIKUZINGATIYA HALI YA WATU WEMA WALIO TANGULIA KATIKA SWALA ZAO.

Watu wema walio tangulia nimfano wa kuigwa kwetu hasa katika utekelezaji wao wa ibada tukianzia kwa Mtume - swala Allah alaihi wasalam- na maswahaba zake na wale walio kuja baada ya maswahaba.

Kwamfano tukiwaangalia watu wema:

1-Alikuwa Ibn Zubair anapo simama kwaajili ya kuswali kanakwamba ni kijiti cha mti kilicho kauka kutokana na unyenyekevu alio kuwa nao.

2.Alikuwa Maslamah bin Bshaar anaswali msikitini ukabomoka sehemu ya msikiti wakasimama watu waliokuwa wakiswali nayeye alikuwa anaswali hakuamka kutoka katika swala yake kwakuwa hakujuwa kama msikiti umebomoka kwa wingi wa unyenyekevu.

3. Na zimepokelewa katika baadhi ya riwaya kwamba baadhi ya watu walio tangulia katika watu wema walikuwa wakiswali walikua kama nguo ilio tupwa kwa wingi wa kunyenyekeya.

4. Na wengine walikuwa wakiswali rangi zao zina badilika kwa kisimamo kirefu na chenye unyenyekevu mbele ya Allah.

5.Nawengine walikuwa wakiwa kwenye swala zao hawa wafahamu watu ambao wanaswali nao kuliani na kushotoni mwao kwenye safu moja.

 16-NIKUJUWA FAIDA ZA UNYENYEKEVU KATIKA SWALA.

Na miongoni mwa faida za unyenyekevu katika swala ni hii kauli ya Mtume - swala allah alaihi wasalam –inayo sema:

عن عثمان بن عفان رضي الله عنه قال: سمعت رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول: (ما من إمرئ مسلم تحضره صلاة مكتوبه فيحسن وضوءها وخشوعها وركوعها إلا كانت كفارة لما قبلها من الذنوب ما لم تؤت كبيرة، وذلك الدهر كله). رواه مسلم في (الطهارة) برقم (335).

Kutoka kwa Othman Bin Afan radhi za Allah ziwe juu yake alisema: nilimsikia Mjumbe wa Allah rehma na amani ziwe juu yake akisema: Hakuna mtu yoyote muislam anae fikiwa na swala ya faradhi akatawadha vizuri kwa ajili ya swala kisha akaswali kwa unyenyekevu katika rukuu na kusujudu ispokuwa inakuwa nikafara ya madhambi ya kabla yake kwa muda hajafanya mja huyo madhambi makubwa, na kwamuda wa mwaka mzima.

Imepokelewa na Imamu Muslim katika kitabu Twahara (335).

 17.NI KUJITAHIDI KATIKA DUA KATIKA SEHEMU ZA KUOMBA DUA KATIKA SWALA, HASA KATIKA SIJDA.

Alisema Allah Mtukufu:

}ادْعُواْ رَبَّكُمْ تَضَرُّعاً وَخُفْيَةً{

Maana ya Ayah hii.

(Muombeni Allah kwa unyenyekevu na kwa siri)

Al Araaf 55.

)أقرب ما يكون العبد من ربه وهو ساجد فأكثروا الدعاء (رواه مسلم.

Na alisema Mtume rehma na amani ziwe juu yake :(Sehemu ambayo mja anakuwa karibu na Mola wake ni wakati anapokuwa katika Sijda basi zidisheni kumuomba Allah ) Imepokelewa na Imamu Muslim.

 18. NI KUDUMU NA NYIRADI ZA BAADA YA SWALA.

Kudumu katika kusoma nyiradi za baada ya swala ni sababu ya kupata unyenyekevu katika swala, pia inasaidia kuimarisha athari ya unyenyekevu katika moyo na yaliyo patikana miongoni mwa baraka za swala.

2.Nikuondoa vitu vinavyo ziwiya unyenyekevu kama kujishughulisha na mambo yasiyo takiwa katika swala,na yanayo ondoa unyenyekevu katika swala.

 19. KUONDOA MAMBO YANAYO MSHUGHULISHA MWENYE KUSWALI SEHEMU YA KUSWALIA.

Miongoni mwa mambo yanayo leta unyenyekevu kwenye swala nikuondoa mambo yanayo sababisha ushawishi katika swala.

عن أنس  قال: كان قِرام ( ستر فيه نقش وقيل ثوب ملوّن ) لعائشة سترت به جانب بيتها، فقال لها النبي :أميطي - أزيلي - عني فإنه لا تزال تصاويره تعرض لي في صلاتي (رواه البخاري.

Kutoka kwa Anas Ibn Maliki Radhi za Allah ziwe juu yake alisema:ilikuwa paziya ya Aisha radhi za Allah ziwe juu yake ni yenye mistari mistari alikuwa ameweka stara kwenye chumba chake, akamwambia Mtume rehma na amani ziwe juu yake :(Ondoa hiyo pazia kwasababu hiyo michoro inanijia katika swala yangu).Imepokelewa na Imamu Bukhari.

Hadithi hii inaonyesha kuwa mtu anapo swali kukawa na kitu chenye michoro au namba au maandishi basi vinamshawishi katika swala nakufanya asiwe na unyenyekevu, tunatakiwa katika vyumba vya kuswalia kusiwe na rangi tofauti zeye kuvutia kutizama ili zisimshughulishe mwenye kuswali.

 20. ASISWALI MUISLAM NA NGUO YENYE MICHORO, AU MAANDISHI.

Nguo zenye maandishi au michoro au namba zinamshawishi mweye kuswali,

Kutoka kwa Aisha radhi za Allah ziwe juu yake alisema:Aliswali Mtume Rehma na amani ziwe juu yake katika nguo yenye michoro na yenye mfano wa Drafti kasha akatizama kwenye ramani za nguo hiyo na alama zake akiwa anaswali,alipo maliza swala yake alisema :(Ipelekeni nguo hii kwa Abuu Jahmi Bin Hudhaifah na muniletee nguo ambayo haina Mistarii,na isiyokuwa na Alama wala michoro, kwasababu nguo yenye mistari imenishughulisha hivi punde katika swala yangu.

Imepokelewa na Imamu Muslim.

 21. ASISWALI WAKATI CHAKULA KIKIWA TAYARI NA YEYE ANAKITAMANI.

Kuswali wakati chakula kikiwa tayari na yeye akiwa anakitamani ima kwa njaa au ni chakula adimu kwake nisababu ya kukosekana unyenyekevu katika swala.

Inatakiwa kuandaa chakula baada ya swala au kabla haujafika muda wa swala na ikibidi basi aanze kula kwanza kisha ndio aswali.

قال):   لا صلاة بحضرة طعام (رواه مسلم.

Alisema Mtume Rehma na aman ziwe juu yake :(Hana swala mtu alie swali wakati wa chakula).

 22.NI KUSWALI WAKATI MTU ANAHISI HAJA KUBWA AU NDOGO:

Hakuna shaka kuwa miongoni mwa mambo yanayo ziwiya unyenyekevu katika swala nikuswali haliyakua umeshikwa na haja kubwa au ndogo, hilo limekatazwa na Mtume Rehma na amani ziwe juu yake, mtu kuswali haliyakuwa ameshikwa na haja kubwa au ndogo kwasababu hawezi kuwa na Unyenyekevu katika swala yake.

Alisema Mtume Rehma na amani ziwe juu yake: (Hana swala alie swali chakula kikiwa tayari wala mtu alie swali akiwa ameshikwa na haja kubwa au ndogo).

Imepokelewa na Imamu Muslim.

Na huku kusukumana na haja kubwa au ndogo kwa mtu alie shikwa na haja kunaondowa unyenyekevu katika swala, pia inaingia katika hukumu hii kusukumana na Upepo (Kujamba au Mashuzi).

 23.ASISWALI AKIWA AMEZIDIWA NA USINGIZI:

Mtu anapo swali akiwa na usingizi kisha akaswali basi anakosa unyenyekevu katika swala.

Kutoka kwa Anasi Radhi za Allah ziwe juu yake aliselima: alisema Mtume Rehma na amani ziwe juu yake: (Atakapo sinzia mmoja wenu katika swala basi alale mpaka atakapo juwa anacho sema) Imepokelewa na Imamu Bukhary.

Hadithi hii inamaanisha kuwa mtu akiswali akiwa hajuwi anachosema kwa sababu ya usingizi anakuwa hafanyi chochote, anapohisi usingizi akawa hajuwi anacho kisema basi anatakiwa asiswali alale mpaka usingizi uishe.

 24.ASISWALI NYUMA YA MWENYE KUONGEA AU ALIE LALA.

Miongoni mwa mambo ambayo yanaondosha unyenyekevu katika swala ni mtu kuswali nyuma ya mtu alie lala au mtu anae ongea, kwasababu Mtume (s.a.w) alikataza kufanya hivyo.

Kutoka kwa Ibn Abas (Radhi za Allah ziwe juu yake ) alisema : Alisema Mtume (Rehma na amani za Allah ziwe juu yake ): (Msiswali nyuma ya mtu alie lala au nyuma ya mtu anae zungumza).

Kwasababu Yule mzungumzaji anampumbaza mwenye kumsikiliza kwa mazungumzo yake, na anamshughulisha mwenye kuswali kwa maneno yake,

Ama mtu alie lala linaweza kutokea jambo ambalo sio la kawaida kama kupiga makelele au kutokwa na haja au kulia ikawa nisababu ya kumshawishi anae swali.

Na ikiwa hakuna uwezekano wa kutokea hayo basi inafaa kuswali nyuma ya alie lala.Allah ndie mjuzi.

Alisema Ibn Bazi Allah amrehemu katika hadithi hii :Hadithi hii nidhaifu katika njia zake zote, kama alivyo kumbusha Imamu Al-Khatwabi na wanachuoni wengine na kinacho onyesha juu ya Udhaifu wa hadithi hii nihadithi ya mama wa waumini Bi Aisha (Radhi za Allah ziwe juu yake ) kwamba Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake alikuwa anaswali usiku Mama Aisha akiwa amelala mbele yake) Imepokelewa na Imamu Bukharin a Imamu Muslim.

Tunajifunza latika Hadithi hizi mbili kwamba Inajuzu kuswali mbele ya mtu alie lala na hakuna Athari yoyote unacho takiwa nikuangakia mahala pakusujudia wakati ukiswali.

  25. MWENYE KUSWALI ASIJISHUGHULISHE NA KUSAFISHA MAHALA PA KUSUJUDU.

Katika mambo yenye kupunguza unyenyekevu katika swala nimtu kujishughulisha na kusafisha mahala pa kusujudu akiwa tayari ndani ya swala kitendo kama hicho kinaondowa unyenyekevu katika swala,

Kutoka kwa Muayqib Radhi za Allah ziwe juu yake hakika Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake alisema kumwambia mtu mmoja alie kuwa akiweka sawa mchanga ili apate sehemu nzuri ya kusujudia : Ikiwa hakuna budi kufanya hivyo basi fanya mara moja). Hadithi hii imepokelewa na Imamu Bukhari.

Na Sababu ya makatazo hayo nikuhifadhi unyenyekevu katika swala ili asikithirishe kufanya matendo ambayo yatamkosesha unyenyekevu wakati wa kuswali,na iliwa sehemu ya kusujudu kunahitaji usafi basi anatakiwa asafishe kabla ya kuingia katika swala.

 26.NIKUJIEPUSHA NA KUWASHAWISHI WENGINE KWA KUSOMA QURAAN.

Kusoma quraan nijambo zuri na lenye ibada kubwa na ndio dhikri yenye malipo makubwa lakini pamoja na ujira huo muislam hautakiwi kuisoma kwa sauti kubwa wakati ukiwa na wenzako katika ibada kwa kuepuka kuwa changanya katika ibada zao bali unatakiwa kusoma taratibu na kwasauti ya chini kwa kulinda haki za ndugu zako katika Imani,

Katika mambo yenye kuleta Unyenyekevu katika swala nikusoma Qur’an kwa sauti ya chini bila kuwashawishi wengine.

Alisema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake:

(Tanbueni hakika kila mmoja wenu anamuomba Mola wake basi msiudhiane na asinyanyue sauti katika kusoma juu ya mwenzake). Imepokelewa na Abuu Daudi.

 27. NIKUACHA KUGEUKA GEUKA KATIKA SWALA.

Katika mambo yanayo leya Unyenyekevu katika swala nikuhifadhi macho yako au kichwa chako kutokana na kugeuka geuka katika swala.

Kutoka kwa Abuu Dhari Radhi za Allah ziwe juu yake alisema: Alisema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake (Haachi Allah kumuelekea mja wake akiwa katika swala kwamuda haja geuka geuka katika swala, anapo geuka na Allah hamuelekei tena).

Aliulizwa Mtume Rehma na amani ziwe juu yake kuhusu kugeuka katika swala, akasema :(Huo niwizi anao iba shetani kutokana na swala ya mja).

Imepokelewa na Imamu Bukhari.

AINA ZA MIGEUKO KATIKA SWALA:

Wana wa chuoni wametaja aina tatu za migeuko katika swala:

1.Kugeuka kwa kifuwa kizima kikawa hakielekei upande wa Qibla, kugeuka huku kunaifanya swala kuwa batili kwasababu kuelekea Qibla nisharti ya kuswihi kwa swala.

2.Kugeuka kwa macho au kichwa na kubaki mwili mzima ukiwa umeelekea Qibla, huku kugeuka kwa namna hii ni Makruhu (Kunachukiza sana) muislam akipata dharura akageuka kwa kutumia macho au kichwa kwadharura kama kupatwa na khofu ya jambo lolote au kuangalia mali yake isiibiwe nk.

Basi hapo hakuna tatizo

Na ikiwa atageuka bila sababu yoyote basi zinapunguwa thawabu za swala yake, pamoja nakuwa swala yake haibatiliki, na ikiwa atazidisha kugeuka katika swala bila ya dharura ikawa kama mchezo basi inaweza kupelekea kubatilika kwa swala yake.

Rejea (Mausuatu Alfiqhiyyah vl 27/109).

Anasema Imamu Ibn Bazi Allah amrehemu katika fatawa (11/130): kugeuka katika swala kwa kujilinda na Shetani wakati anapo kupa wasiwasi hakuna tatizo, bali ni Sunnah wakati anapo hitaji mwenye kuswali na iwe kwa kichwa.

3.Kugeuka katika swala kwamoyo, kwakuwaza mambo tofauti katika maisha yake na yakasababisha asiwe na mazingatiyo katika swala yake.

Alisema Imamu Ibn Othaymiin katika kitabu (Sherhu Almumtii 3/70) :”Fahamu yakwamba kugeuka katika swala kuko aina mbili:

1.Kugeuka kwa mwili nako nikugeuka kwa kichwa.

2.Kugeuka kwa moyo,nako kunakuwa kwa sababu ya wasiwasi unao tokea moyoni.

 28.NIKUTO NYANYUA MACHO MBINGUNI.

Katika mambo yanayo ondoa unyenyekevu katika swala nikunyanyua macho nakuangalia mbinguni wakati wa kuswali, na imepokelewa kutoka kwa Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake, makatazo ya jambo hilo na yakaja makemeo katika jambo hilo na kwa mwenye kufanya hivyo.

Alisema Mtume :(Pindi atakapo kuwa mmoja wenu anaswali basi asiinuwe macho yake mbinguni) Imepokelewa na Imamu Ahmad.

Na yakazidi makatazo ya jambo hilo pale alipo sema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake (Nawakome watu na kuangalia mbinguni wakiwa wana swali au yatanyofolewa macho yao).Imepokelewa na Imamu Bukhari.

 29. KUTEMA MATE MBELE YAKE.

Mtu kutema mate mbele yake akiwa anaswali imekatazwa kwasababu inapingana na Unyenyekevu katika swala, na nikukosa adabu na Allah, Alisema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake (Atakapo kuwa mmoja wenu anaswali basi asiteme mate mbele yake kwasababu Allah anakua mbele ya swala ).

 30. NIKUJITAHIDI KUTOKUPIGA MIAYO KATIKA SWALA .

Alisema Mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake : (Atakapo piga miayo mmoja wenu katika swala basi afiche kadri ya uwezo wake hakika shetani anaingia mdomoni). Imepokelewa na Imamu Muslim.

 31. NIKUTO KUWEKA MIKONO KIUNONI KATIKA SWALA.

Kutoka kwa Abuu Huraira Radhi za Allah ziwe juu yake alisema:(Alikataza Mtume Rehma na amani ziwe juu yake kuweka mikono kiunoni wakati mtu akiwa katika swala).

 32. NIKUVAA NGUO INAYO BURUZIKA KWA MWANAUME.

Alikataza mtume Rehma na amani ziwe juu yake kuburuza nguo kwa mwanaume katika swala na azuie mwanaume mdomo wake akitoa miayo.

 33.NIKUACHA KUJIFANANISHA NA WANYAMA.

Alikataza mtume Rehma na amani za Allah ziwe juu yake mambo matatu:

1.Kudonoa swala kama anavyo donoa kunguru wakati wa kula.

2.Na kulaza mikono katika swala kama anavyo laza mbwa.

3.Na kujiwekea mtu sehemu yake maalumu ya kuswali katika msikiti.

Haya ndiyo tulio wezeshwa na Allah kuyasema katika kuzungumzia sababu zinazo leta unyenyekevu katika swala pia na sababu zinazo mshughulisha mtu katika swala ili aepukane nazo.

Swala na salam ziwe juu ya Mtume Muhamad Rehma na amani ziwe juu yake na ahali zake na watu wake na umma wake na wote watakao mfuata kwa wema mpaka siku ya Qiyama.

Imeandikwa na Shekh Muhammad Bin Swaleh Almunajid.

Imetafsiriwa na : Abubakari Shabani Rukonkwa.

Imepitiwa na: Yunus Kanuni Ngenda.

Imepitiwa na Saada Haruna Yunus