UBORA WA UISLAMU

Mwandishi : Muhammad bin Abdul-Wahhab

Tafsiri:

Maelezo

Kitabu hiki kilicho tafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, kinazungumzia: Maana ya uislamu, ubora wa uislamu na uwajibu wa kuingia katika uislamu.

Download
Tuma maoni kuhusu ukurasa huu kwa msimamizi

Maelezo ya Kina

ora Wa ﷻ‬

Ubora Wa Uislamu

Mwandishi:

Imaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab

Tarjama:

Abu Bakr Khatwiyb al-Atrush

1. Utukufu wa Uislamu

Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

"Leo Nimekukamilishieni Dini yenu na Nime kutimizieni neema Yangu na Nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe [ndio] Dini yenu." (05:03)

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي شَكٍّ مِّن دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّـهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ

"Sema: “Enyi watu! Ikiwa mna shaka kutokana na Dini yangu, basi [mimi] siabudu ambavyo mnaviabudu badala ya Allaah; lakini namwabudu Allaah Ambaye [siku moja] Atakufisheni." (10:104)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

"Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na muaminini Mtume Wake! Hapo Atakupeni sehemu mbili kati ya Rahmah Zake na Atakujaalieni Nuru mnatembea nayo na Akusameheeni - Allaah ni Ghafuwrur-Rahiym, Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu." (57:28)

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Mfano wenu nyinyi na watu wa Kitabu ni kama mfano mtu mwenye kukodisha wafanyakazi na akasema: "Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyiakazi kuanzia asubuhi mpaka mchana kwa senti moja?" Mayahudi wakafanya hivo. Halafu akasema: "Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyia kazi kuanzia mchana mpaka ´Aswr kwa senti moja?" Manaswara wakafanya hivo. Kisha akasema: "Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyiakazi kuanzia ´Aswr mpaka jua kuzama kwa senti mbili?" Ndio nyinyi. Mayahudi na manaswara wakakasirika na kusema: "Ni kwa nini sisi ndio tufanye kazi sana na kupata ujira mdogo?" Akasema: "Nimepunguza kitu katika haki yenu?" Wakasema: "Hapana." Ndipo akasema: "Hiyo ni fadhila yangu ninampa yule ninayemtaka."[1]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Allaah amewapoteza waliokuwa kabla yetu siku ya ijumaa. Mayahudi wakapata jumamosi na manaswara jumapili. Allaah akatuleta na akatuongoza siku ya ijumaa. Kadhalika watatufuata siku ya Qiyaamah. Sisi ndio wa mwisho katika dunia hii, wa kwanza siku ya Qiyaamah."[2]

al-Bukhaariy amepokea kwa mlolongo wa wapokezi wenye kupungua kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Dini yenye kupendwa zaidi na Allaah ni ule upwekeshaji mwepesi."[3]

Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Shikamaneni na Njia na Sunnah. Hakuna mja mwenye kushikamana na Njia na Sunnah akamfikiria Allaah mpaka macho yake yakatiririka machozi kwa kumwogopa Allaah kisha aunguzwe na Moto. Hakuna mja mwenye kushikamana na Njia na Sunnah akamfikiria Allaah mpaka mwili wake ukasisimka kwa kumwogopa Allaah isipokuwa mfano wake ni kama mfano wa jani kavu kwenye mti lenye kuruka hewani; hali kadhalika yanamtoka madhambi yake. Ni bora kuwa mwenye kujizuia katika Njia na Sunnah kuliko kuwa na bidii katika yanayokwenda kinyume na Njia na Sunnah."[4]

Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Kule wale wenye busara wakawa ni wenye kulala na kuacha kufunga ni bora kuliko wajinga kuswali usiku na kufunga. Chembe kidogo ya wema ilio pamoja na uchaMungu na yakini, ni bora na ni yenye uzito kuliko ´ibaadah za waliodanganyika zilizo kubwa sawa na mlima."[5]

2. Uwajibu wa kuingia katika Uislamu

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

"Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika." (03:85)

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

"Hakika Dini mbele ya Allaah ni Uislamu." (03:19)

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu, [njia] iliyonyooka; basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!" (06:153)

Mujaahid amesema:

"Vichochoro ni Bid´ah na utata."

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenye kuzusha katika amri yetu hii yasiyokuwemo yatarudishwa."[6]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi mwingine imekuja:

"Mwenye kufanya tendo lisiloafikiana na amri yetu litarudishwa."[7]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Ummah wangu wote utaingia Peponi isipokuwa yule asiyetaka." Wakasema: "Ee Mtume wa Allaah! Ni nani atayekataa?" Akasema: "Mwenye kunitii ataingia Peponi na mwenye kuniasi amekataa."[8]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Watu wanaochukiwa zaidi na Allaah ni watatu; mtenda dhambi Haram, mwenye kutaka katika Uislamu kitu cha Jaahiliyyah na mwenye kuomba damu ya mtu muislamu pasina haki ili amwage damu yake."[9]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

"Kitu cha Jaahiliyyah inahusu kila kitu cha Jaahiliyyah, isiyofungwa [mutlaq] au iliyofungwa [muqayyad] kwa mtu kama myahudi, mnaswara, mwabudu sanamu au mwingine mwenye kwenda kinyume na yale waliyokuja nayo Mitume."

al-Bukhaariy amepokea kutoka kwa Hudhayfah ambaye amesema:

"Enyi wanazuoni! Bakieni katika njia iliyonyooka! Mkifanya hivo basi mmetangulia mbele. Na mkienda kuliani na kushotoni basi mmepotea upotevu wa mbali kabisa."[10]

Muhammad bin Wadhdhwaah ameeleza jinsi Hudhayfah alivyokuwa akiingia msikitini na kusema haya. Akasema:

"Sufyaan bin ´Uyaynah ametueleza, kutoka kwa Mujaalid bin Sa´iyd, kutoka kwa ´Aamir ash-Sha´biy, kutoka kwa Masruuq ambaye ameeleza kuwa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Hakuna mwaka unaokuja isipokuwa ulio baada yake ni mbaya zaidi. Simaanishi kuwa kuna mwaka wenye kunyesha zaidi kuliko mwingine au wenye rutuba zaidi kuliko mwingine wala kiongozi ambaye ni bora kuliko mwingine. Ninachomaanisha ni kwenda kwa wanazuoni wenu na watu wenu bora. Kisha kutajitokeza watu ambao watayakisia mambo kwa matamanio yao ambapo watauharibu Uislamu na uangamie."[11]

3. Maana ya Uislamu

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِنْ حَاجُّوكَ فَقُلْ أَسْلَمْتُ وَجْهِيَ لِلَّـهِ وَمَنِ اتَّبَعَنِ

"Na wakikuhoji, basi sema: “Nimejisalimisha kwa Allaah kikamilifu na wale walionifuata." (03:20)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Uislamu ni kushuhudia ya kwamba hapana mola mwenye haki ya kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, kusimamisha swalah, kutoa zakaah, kufunga Ramadhaan na kuhiji kwenye Nyumba ukiweza kuiendea."[12]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Muislamu ni yule mwenye kuwasalimisha waislamu kwa ulimi na mkono wake."[13]

Bahz bin Hakiym amepokea kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake ambaye ameeleza kuwa alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya Uislamu ambapo akajibu:

"Ni kuusalimisha moyo wako kwa Allaah (Ta´ala), kuuelekeza uso wako kwa Allaah (Ta´ala), kuswali swalah za faradhi na kutoa zakaah iliyofaradhishwa."[14]

Ameipokea Ahmad.

Abu Qilaabah amepokea kutoka kwa mtu miongoni mwa watu wa Shaam ambaye amepokea kutoka kwa baba yake ambaye alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu Uislamu ambapo akajibu:

"Ni kuusalimisha moyo wako kwa Allaah (Ta´ala) na waislamu wasalimike na ulimi na mkono wako." Akasema: "Ni Uislamu upi bora?" Akajibu: "Imani." Akauliza: "Ni nini imani?" Akajibu: "Ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Wake na kufufuliwa baada ya kufa." [15]

4. Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Matendo yatakuja siku ya Qiyaamah. Swalah itakuja na kusema: "Ee Mola! Mimi ndio swalah." Aseme: "Uko katika kheri." Kisha ije swadaqah na kusema: "Ee Mola! Mimi ndio swadaqah." Aseme: "Uko katika kheri." Kisha ije swawm na kusema: "Ee Mola! Mimi ndio swawm." Aseme: "Uko katika kheri." Halafu yaje matendo mengine yote na Aseme: "Uko katika kheri." Kusha kuje Uislamu na kusema: "Ee Mola! Wewe ni as-Salaam na mimi ndio Uislamu." Aseme: "Uko katika kheri." Leo hii Nitachukua na Kupeana kutokana na wewe." Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

"Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake, naye katika Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika." (03:85)

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume wa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenye kufanya tendo lisiloafikiana na amri yetu litarudishwa."

Ameipokea Ahmad.

5. Ni wajibu kufuata Qur-aan peke yake

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ

"Na Tumekuteremshia Kitabu kikiwa ni kielezo bayana cha kila kitu." (16:89)

an-Nasaa´iy na wengine wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliona kwenye mikono ya ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) karatasi ya Tawrat akasema:

"Ee mwana wa al-Khattwaab! Una shaka? Nimekufikishieni wazi wazi kabisa. Lau Muusa angelikuwa hai hii leo mkamfuata badala ya kunifuata mimi basi mgelikuwa mmepotea." ´Umar akasema: "Nimeridhia Allaah kuwa Mola Wangu, Uislamu kuwa dini yangu na Muhammad kuwa Mtume wangu."[16]

Katika upokezi mwingine imekuja:

"Lau Muusa angelikuwa hai hii leo asingelikuwa na namna isipokuwa kunifuata."

6. Hakuna manasibisho yasiyokuwa ya Kiislamu

Allaah (Ta´ala) amesema:

هُوَ سَمَّاكُمُ الْمُسْلِمِينَ مِن قَبْلُ وَفِي هَـٰذَا

"Yeye Ndiye hapo kabla [katika Vitabu vya awali] na katika [Kitabu] hiki Aliyekuiteni "Waislamu"." (22:78)

al-Haarith al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Ninakuamrisheni mambo matano ambayo Allaah ameniamrisha kwayo; usikivu, utiifu, Jihaad, Hijrah na mkusanyiko, Jamaa´ah. Hakika mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri basi amevua kamba ya Uislamu katika shingo yake isipokuwa ikiwa kama atajirudi. Mwenye kuita wito wa Jaahiliyyah ataadhibiwa Motoni." Mtu mmoja akasema: "Ee Mtume wa Allaah! Hata kama ataswali na kufunga?" Akajibu: "Hata kama ataswali na kufunga. Enyi waja wa Allaah! Iteni kwa wito wa Allaah; Yeye ndiye kakwiteni "waislamu" na "waumini"."[17]

Ameipokea Ahmad na at-Tirmidhiy ambaye amesema:

"Hadiyth ni Hasan na Swahiyh."

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Mwenye kuacha mkusanyiko kiasi cha shibri na akafa, amekufa kifo cha Jaahiliyyah."

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema pia:

"Mnaita wito wa Jaahiliyyah ilihali niko kati yenu?"

Abul-´Abbaas amesema:

"Kila jina lenye kwenda kinyume na Uislamu na Qur-aan na manasibisho ya nasabu, miji, makabila, madhehebu au mifumo ni katika sifa za Jaahiliyyah. Pindi mtu wa Muhaajiruun alipozozana na mtu wa Answaar na kila mmoja akawaita watu wake, ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

"Mnaita wito wa Jaahiliyyah ilihali niko kati yenu?"

Akaghadhibika sana kutokana na hilo."[18]

7. Uwajibu wa kujisalimisha kikamilifu na kuacha mengine yote

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا ادْخُلُوا فِي السِّلْمِ كَافَّةً وَلَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ ۚ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ

"Enyi mlioamini! Jisalimisheni kikamilifu na wala msifuate hatua za Shaytwaan - hakika yeye kwenu ni adui wa wazi." (02:208)

أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ يَزْعُمُونَ أَنَّهُمْ آمَنُوا بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ وَمَا أُنزِلَ مِن قَبْلِكَ يُرِيدُونَ أَن يَتَحَاكَمُوا إِلَى الطَّاغُوتِ وَقَدْ أُمِرُوا أَن يَكْفُرُوا بِهِ وَيُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُضِلَّهُمْ ضَلَالًا بَعِيدًا

"Je, huoni wale wanaodai kwamba wao wameamini yaliyoteremshwa kwako na yale yaliyoteremshwa kabla yako, jinsi wanataka wahukumiane kwa hukumu za kufuru na hali wameamrishwa wazikanushe? Na Shaytwaan anataka awapoteze upotofu wa mbali." (04.60)

إِنَّ الَّذِينَ فَرَّقُوا دِينَهُمْ وَكَانُوا شِيَعًا لَّسْتَ مِنْهُمْ فِي شَيْءٍ ۚ إِنَّمَا أَمْرُهُمْ إِلَى اللَّـهِ ثُمَّ يُنَبِّئُهُم بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

"Hakika wale waliofarikisha dini yao na wakawa makundi makundi huna lolote kuhusiana na wao. Hakika amri yao iko kwa Allaah, kisha Atawajulisha kwa yale waliyokuwa wakifanya." (06:159)

يَوْمَ تَبْيَضُّ وُجُوهٌ وَتَسْوَدُّ وُجُوهٌ ۚ فَأَمَّا الَّذِينَ اسْوَدَّتْ وُجُوهُهُمْ أَكَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ

"Siku [baadhi ya] nyuso zitang´ara na [nyingine] zitafifia. Basi wale ambao nyuso zao zitafifia [wataambiwa:] “Je, mlikufuru baada ya kuamini kwenu? Basi onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru." (03:106)

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

"Wale walioshikamana na Sunnah na mshikamano ndio nyuso zao zitang´ara na wale walioshikamana na Bid´ah na tofauti ndio nyuso zao zitafifia."[19]

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Ummah wangu utafikwa na yale yaliyowafika wana wa Israaiyl kiasi cha kwamba, ikiwa kuna katika wao aliyemwingilia mama yake hadharani basi kutapatikana katika Ummah wangu ambaye atafanya vivyo hivyo. Wana wa Israaiyl walifarikiana katika makundi sabini na mbili na Ummah wangu utafarikiana katika makundi sabini na tatu; yote yataingia Motoni isipokuwa moja tu." Wakasema: "Ee Mtume wa Allaah! Ni lipi hilo?" Akasema: "Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata."[20]

Muumini ambaye anataraji kukutana na Allaah azingatie maneno ya mkweli na msadikishwaji na khaswa pale aliposema:

"Ni lile linalofuata yale mimi na Maswahabah zangu tunayofuata."

Ni mawaidha yaliyoje lau yatazifikia nyoyo zilizo hai!"

Ameipokea at-Tirmidhiy.

at-Tirmidhiy ameipokea tena kupitia kwa Abu Hurayrah na akaisahihisha. Lakini hata hivyo ndani yake hakukutajwa Moto, kama ilivyo katika Hadiyth ya Mu´aawiyah inayopatikana kwa Ahmad na Abu Daawuud. Humo mna:

"Kutajitokeza watu katika Ummah wangu ambao watachukua matamanio hayo kama jinsi mbwa kichaa inavyomuathiri muathirikaji; haitoacha mshipa wala kiungo isipokuwa itaingia ndani yake."[21]

Tafsiri ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) "mwenye kutaka katika Uislamu kitu cha Jaahiliyyah" imeshatangulia.

8. Bid´ah ni mbaya zaidi kuliko madhambi makubwa

Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚوَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا بَعِيدًا

"Hakika Allaah Hasamehi kushirikishwa; lakini Anasamehe yasiyokuwa hayo kwa Amtakae; na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amepotoka upotofu wa mbali." (04:116)

فَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا لِّيُضِلَّ النَّاسَ بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ

"Ni nani dhalimu zaidi kuliko yute anayemtungia Allaah uongo ili apoteze watu bila elimu? Hakika Allaah Hawaongozi watu madhalimu." (06:144)

لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۙ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ ۗ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ

"Ili wabebe mizigo [ya madhambi] yao kamili Siku ya Qiyaamah na mizigo ya wale waliowapoteza bila ya elimu. Tanabahi! Uovu ulioje wanayoyabeba." (16:25)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Khawaarij:

"Popote mnapokutana nao waueni. Ikiwa nitakutana nao basi nitawaua kama walivyouawa kina ´Aad."[22]

Kumepokelewa [Hadiyth] Swahiyh ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kupambana na viongozi madhalimu maadamu wanaswali[23].

Jariyr bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa kuna mtu aliyetoa swadaqah na watu wakawa wamemuiga. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

"Yule mwenye kuanzisha katika Uislamu msingi mzuri basi ana ujira wake na ujira wa yule atakayeifanya baada yake pasina kupungua chochote katika ujira wao. Na yule mwenye kuanzisha katika Uislamu msingi mbaya basi ana madhambi yake na madhambi na yule atakayeifanya pasina kupungua chochote katika madhambi yao."[24]

Ameipokea Muslim ambaye amepokea tena mfano wa Hadiyth kama hiyo kupitia kwa Abu Hurayrah:

"Yule mwenye kuita katika uongofu..." na "Yule mwenye kuita katika upotevu..."[25]

9. Allaah ameizuia tawbah kwa mtu wa Bid´ah

Yamepokelewa katika Hadiyth ya Anas bin Maalik pamoja na al-Hasan al-Baswriy kwa mfuatano wa wasimulizi uliokatika kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ibn Wadhdhwaah ameeleza kuwa Ayyuub amesema:

"Kuna mtu katika sisi aliyekuwa na I´tiqaad mbovu na baadae akaiacha. Nikamwendea Muhammad bin Siriyn na kumwambia: "Je, unajua kuwa fulani ameacha I´tiqaad yake?" Akasema: "Tazama amegeuka kuwa nini. Sehemu ya mwisho ya Hadiyth ni kipigo kwao kuliko sehemu yake ya mwanzo:

"Wanatoka katika Uislamu na kisha hawarudi tena."[26]

Ahmad bin Hanbal aliulizwa maana yake akajibu:

"Hawawafikishwi tawbah."

10. Watu wa Kitabu ni kwanini mnahojiana kuhusu Ibraahiym?

Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَهْلَ الْكِتَابِ لِمَ تُحَاجُّونَ فِي إِبْرَاهِيمَ وَمَا أُنزِلَتِ التَّوْرَاةُ وَالْإِنجِيلُ إِلَّا مِن بَعْدِهِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ هَا أَنتُمْ هَـٰؤُلَاءِ حَاجَجْتُمْ فِيمَا لَكُم بِهِ عِلْمٌ فَلِمَ تُحَاجُّونَ فِيمَا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

"Enyi watu wa Kitabu! Kwanini mnahojiana kuhusu Ibraahiym na hali haikuteremshwa Tawraat na Injiyl isipokuwa baada yake? Je, hamtii akilini? Nyinyi ndio hawa mliohojiana katika yale ambayo mnayo elimu nayo, basi kwa nini [sasa] mnahojiana katika yale msiyokuwa na elimu nayo? Na Allaah Anajua, na nyinyi hamjui. Hakuwa Ibraahiym yahudi wala naswara - lakini alikuwa ni mwenye imani iliyo safi na kutakasika na alikuwa ni Muislamu; na hakuwa miongoni mwa washirikna." (03:65-67)

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ

"Na nani atakayejitenga na imani ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu? Na kwa yakini Tumemchagua duniani, naye Aakhirah ni miongoni mwa [waja] wema." (02:130)

Hadiyth kuhusu Khawaarij imeshatangulia. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Kizazi cha baba fulani sio mawalii wangu. Mawalii wangu ni wale wachaMungu."[27]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Anas ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipata khabari kuwa kuna Maswahabah waliosema: "Mimi sintokula nyama." Mwingine akasema: "Nitaswali tu na sintolala." Mwingine akasema: "Mimi sintooa." Mwingine akasema: "Nitafunga tu." Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

"Mimi ninaswali na kulala, ninafunga na kuacha, ninaoa na kula nyama. Atakayeipa mgongo Sunnah yangu basi huyo si katika mimi."[28]

Tafakari ni ukali namna gani Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivyowakemea baadhi ya Maswahabah pindi walipotaka kuishi maisha ya kuipa nyongo dunia kwa kupitiliza ili kumuabudu Allaah na akaita matendo yao kuwa ni kuipa mgongo Sunnah yake. Unafikiriaje inapokuja katika Bid´ah nyinginezo? Unafikiriaje inapokuja kwa wengine wasiokuwa Maswahabah?

11. Elekeza uso wako katika Dini yenye imani safi na iliyotakasika

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚلَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

"Basi elekeza uso wako katika Dini yenye imani safi na iliyotakasika, imani hiyo ndio maumbile Allaah Aliyowaumbia watu [wote] - hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah! Hivyo ndio Dini iliyonyooka sawasawa, lakini watu wengi hawajui. (30:30)

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

"Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na [kadhalika] Ya'quwb [akawaambia]: “Enyi wanangu! Hakika Allaah Amekuchagulieni nyinyi Dini; basi msife isipokuwa nyinyi ni Waislamu." (02:132)

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

"Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani ya Ibraahim iliyo safi na kutakasika na hakuwa miongoni mwa washirikina." (16:123)

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Hakika kila Mtume ana msaidizi katika Mitume na mimi msaidizi wangu katika wao ni baba yangu na Khaliyl wa Allaah Ibraahiym." Halafu akasoma:

إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗوَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ

"Hakika watu waliokaribu zaidi kwa Ibraahiym ni wale waliomfuata, kama mfano wa Nabii huyu na wale walioamini. Na Allaah ni Mlinzi wa Waumini."[29] (03:68)

Ameipokea at-Tirmidhiy.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Allaah hatazami miili yenu wala mali zenu; Anatazama nyoyo zenu na matendo yenu."[30]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Nitasimama nikiwangoja kwenye hodhi. Wanaume katika Ummah wangu watanyanyuliwa kwangu na pindi ninapoenda kuwachukua, watawekwa mbali na mimi ambapo nitasema: "Ee Mola! Wafuasi wangu!" Kusemwe: "Hakika wewe hujui waliyozusha baada yako."[31]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Ninatamani lau tungeliwaona ndugu zetu." Waseme: "Ee Mtume wa Allaah! Kwani sisi sio ndugu zako?" Aseme: "Nyinyi ni Maswahabah zangu. Ndugu zangu ni wale ambao bado hawajaja." Wakasema: "Ee Mtume wa Allaah! Vipi utamjua ni katika Ummah wako ambaye bado hajaja?" Akajibu: "Mnaonaje lau mtu atakuwa na farasi aliye na doa kati ya farasi weusi, hatomjua farasi wake?" Wakasema: "Ndio, ee Mtume wa Allaah." Akasema: "Watakuja wakiwa na madoa [mwanga] kutokana na wudhuu. Nitawaongoja katika hodhi. Hata hivyo kuna wanaume wataofukuzwa na hodhi yangu siku ya Qiyaamah kama anavyofukuzwa ngamia aliyepotea. Ninawaita, lakini kutasemwa: "Walibadilisha baada yako", kisha niseme: "Tokomeeni! Tokomeeni!"[32]

Katika al-Bukhaariy imekuja:

"Nitakuwa nimesimama katika umati wa watu. Pindi nitapowajua atatoka mtu kati yetu na kusema: "Njooni!" Niseme: "Wapi?" Aseme: "Ninaapa kwa Allaah! Motoni." Niseme: "Wana nini?" Aseme: "Waliritadi baada yako." Halafu kuje umati mwingine", na useme hali kadhalika. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): "Wachache sawa na idadi ya ngamia waliohuru ndio wataifikia."[33]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Nitasema kama alivyosema mja mwema:

وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ

"Na nilikuwa juu yao shahidi wakati nilipokuwa nao, lakini uliponichukua juu [mbinguni] Ulikuwa Wewe ndiye Mwenye kuchunga juu yao; na Wewe juu ya kila kitu ni Shahiyd, Mwenye kushuhudia." (05:117)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Hakuna mtoto isipokuwa huzaliwa katika maumbile. Baada ya hapo wazazi wake ndio humfanya kuwa myahudi, mnaswara au mwabudu moto. Ni kama mfano mnyama mwenye pembe anavyomzaa mnyama mwenye pembe kama yeye. Je, mtahisi kuwa hana pembe? Kisha Abu Hurayrah akasoma:

فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا

"... imani hiyo ndio maumbile Allaah Aliyowaumbia watu [wote]..." (30:30)

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Watu walikuwa wakimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mambo ya kheri na mimi nikimuuliza kuhusu mambo ya shari kwa kuchelea yasije kunipata. Nikasema: "Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa katika Jaahiliyyah na shari na Allaah akatuletea kheri hii. Je, kuna shari baada ya kheri hii?" Akajibu: "Ndio." Nikasema: "Je, kuna kheri baada ya shari hiyo?" Akajibu: "Ndio, na itakuwa na moshi." Nikamuuliza: "Ni upi moshi wake?" Akajibu: "Ni watu wenye kufuata isiyokuwa njia yangu. Kuna mambo utayokubaliana nayo na mengine utayapinga." Nikasema: "Kuna shari baada ya kheri hiyo?" Akasema: "Ndio, fitina ya upofu na walinganizi katika milango ya Motoni. Yule mwenye kuwaitikia wanamtupa humo." Nikasema: "Ee Mtume wa Allaah! Tueleze nao." Akasema: "Ni watu wanaotokamana na sisi na wanazungumza lugha yetu." Nikauliza: "Unaniamrisha nini nikikutana na hilo?" Akasema: "Shikamana na mkusanyiko wa waislamu na kiongozi wao." Nikasema: "Vipi kukiwa hakuna mkusanyiko wala kiongozi?" Akasema: "Jiepushe na hayo makundi yote hata kama utahitajia kuuma mzizi wa mti mpaka yakufikie mauti."[34]

Ameipokea al-Bulkhaariy na Muslim ambaye amezidisha:

"Kuna nini baadaye?" Akasema: "Kisha atajitokeza ad-Dajjaal. Atakuwa na mto na moto. Atayetumbukia kwenye moto wake itamuwajibikia kulipwa ujira wake na madhambi yake kufutwa. Na yule mwenye kutumbukia kwenye pepo yake itamuwajibikia kuadhibiwa." Nikasema: "Kuna nini baadaye?" Akasema: "Halafu kunakuja Qiyaamah."[35]

Abul-´Aaliyah amesema:

"Jifunzeni Uislamu. Mtapojifunza, msiupe mgongo. Shikamaneni na njia iliyonyooka, kwani hakika ndio Uislamu. Msende kinyume na njia kuliani na kushotoni. Shikamaneni na Sunnah za Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tahadharini na matamanio haya."

Yazingatie maneno haya ya Abul-´Aaliyah - ni matukufu kiasi gani! Tambua zama zake ambapo akitahadharisha matamanio ambayo yule mwenye kuyafuata anakuwa ameupa Uislamu mgongo. Ameufasiri Uislamu kuwa ni Sunnah na khofu yake ilikuwa kwa Taabi´uun mabingwa wasiende kinyume na Qur-aan na Sunnah. Hapo ndipo itakubainikia maana ya Kauli ya Allaah:

إِذْ قَالَ لَهُ رَبُّهُ أَسْلِمْ ۖ قَالَ أَسْلَمْتُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ

"Pindi Mola Wake Alipomwambia: “Jisalimishe!" Akajibu: “Nimejisalimisha kwa [Allaah], Mola wa walimwengu." (02:131)

na:

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

"Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na [kadhalika] Ya'quwb [akawaambia]: “Enyi wanangu! Hakika Allaah Amekuchagulieni nyinyi Dini; basi msife isipokuwa nyinyi ni Waislamu." (02:132)

na:

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ

"Na nani atakayejitenga na imani ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu? Na kwa yakini Tumemchagua duniani, naye Aakhirah ni miongoni mwa [waja] wema." (02:130)

Izingatie misingi hii mikubwa ambayo ndio misingi ya misingi na ambayo watu wameghafilika nayo. Kwa kuielewa basi itabainika maana ya Hadiyth katika mlango huu na mingineyo.

Kuhusiana na yule mwenye kuisoma sawa hii na mingineyo na huku anajiaminisha kuwa hayawezi kumfika na anafikiria kuwa yanawahusu watu waliokuwepo hapo kale wakatokomea, basi Allaah yuwasema:

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ ۚ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ

"Je, wameaminisha mipango ya Allaah? Basi hawaaminishi mipango ya Allaah isipokuwa watu wenye kukhasirika." (07:99)

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitupigia msitari kwenye ardhi kisha akasema: "Hii ni njia ya Allaah." Halafu akapiga vimisitari kuliani na kushotoni kisha akasema: "Hivi ni vichochoro. Kuna Shaytwaan mwenye kuita kwenye kila kichochoro." Halafu akasoma:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ

“Hii ndio njia Yangu, [njia] iliyonyooka; basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vitakufarikisheni na njia Yake!" Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa."[36] (06:153)

12. Ugeni wa Uislamu na ubora wa wageni

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّنْ أَنجَيْنَا مِنْهُمْ ۗ وَاتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَا أُتْرِفُوا فِيهِ وَكَانُوا مُجْرِمِينَ

"Basi kwanini hawakuweko katika karne za kabla yenu, watu weledi wanakataza ufisadi katika ardhi isipokuwa wachache kati ya Tuliowaokoa miongoni mwao! Na wale waliodhulumu wakafuata [anasa] walizostareheshwa nazo na wakawa wahalifu." (11:116)

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Uislamu ulianza kama kitu kigeni na utarudi kuwa mgeni kama jinsi ulivyoanza - Twubaa kwa wageni!"[37]

Ameipokea Muslim.

Ahmad amepokea kupitia kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliulizwa:

"Ni kina nani wageni?" Akajibu: "Ni watu wachache katika makabila."[38]

Katika upokezi mwingine imekuja:

"Wageni ni wale wanaotengeneza pale wanapoharibika watu."[39]

Ahmad amepokea kupitia kwa Sa´d bin Abiy Waqqaas kwa muundo:

"Twuubaa kwa wageni siku ambayo watu wameharibika!"

at-Tirmidhiy amepokea kupitia kwa Kathiyr bin ´Abdillaah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake kwa muundo:

"Twuubaa kwa wageni wenye kutengeneza yale waliyoharibu watu katika Sunnah zangu!"[40]

Abu Umayyah amesema:

"Nilimuuliza Abu Tha´labah al-Khushaniy (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya Aayah:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا عَلَيْكُمْ أَنفُسَكُمْ ۖ لَا يَضُرُّكُم مَّن ضَلَّ إِذَا اهْتَدَيْتُمْ

"Enyi mlioamini! Ni juu yenu [majukumu ya] nafsi zenu. Hawakudhuruni waliopotoka, ikiwa mmeongoka." (05:105)

Akajibu: "Ninaapa kwa Allaah ya kwamba mimi mwenyewe nilimuuliza nayo mtu mjuzi; nilimuuliza Mtume wa Allaah na akasema: "Mtaamrishana mema na kukatazana maovu. Pindi mnapoona choyo inayotiiwa, matamanio yanayofuatwa, dunia inayopewa kipaumbele na jinsi kila mmoja anavyopendekeza maoni yake, shikamana na nafsi yako na uachane na ´Awwaam. Mbele yenu kunakuja masiku ambayo mwenye subira ni kama mfano wa aliyeshika kaa [la moto] na mtendaji mwenye kutenda kama nyinyi analipwa ujira wa wanaume khamsini." Tukasema: "Katika sisi au katika wao?" Akasema: "Katika wao."[41]

Ameipokea Abu Daawuud na at-Tirmidhiy.

Ibn Wadhdhwaah amepokea maana kama hiyo kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kwa muundo:

"Baada yenu kunakuja masiku ambayo yule aliyeshikamana na yale mnayofanya nyinyi hii leo analipwa ujira wa wanaume khamsini katika nyinyi."

Kisha akasema: "Muhammad bin Sa´iyd ametueleza: Asad ametueleza: Sufyaan bin ´Uyaynah ametueleza, kutoka kwa Aslam al-Baswriy, kutoka kwa Sa´iyd, ndugu wa al-Hasan, kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nikamwambia Sufyaan: "Haya yanatoka kwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?" Akasema: "Ndio." Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

"Hii leo mko katika ushahidi kutoka kwa Mola Wenu, mnaamrisha mema, mnakataza maovu na mnapigana Jihaad kwa ajili ya Allaah na hamjasibiwa na vilevi viwili ambacho ni kilevi cha ujinga na kilevi cha kupenda maisha. Hata hivyo mtakuja kubadilika muache kuamrisha mema, kukataza maovu, kupigana Jihaad kwa ajili ya Allaah na mtasibiwa na vilevi viwili. Siku hiyo yule mwenye kushikamana na Kitabu na Sunnah analipwa ujira khamsini." Wakasema: "Katika sisi?" Akasema: "Hapana. Katika nyinyi."[42]

Amepokea kwa mlolongo wa wapokezi kupitia kwa al-Mu´aafiriy ambaye ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

"Twuubaa kwa wageni wenye kushikamana na Kitabu pindi kinapoachwa na wanaitendea kazi Sunnah pindi inapozimwa!"[43]

13. Matahadharisho ya Bid´ah

al-´Irbaadhw bin Saariyah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitutolea mawaidha makali ambayo yalizitikisa nyoyo zetu na macho yetu yakatiririka machozi. Tukasema: "Ee Mtume wa Allaah! Ni kana kwamba ni mawaidha ya kutuaga; tuusie!" Akasema: "Ninakuusieni kumcha Allaah (´Azza wa Jall) na kusikiliza na kutii hata kama mtataliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi katika nyinyi basi atakuja kuona tofauti nyingi. Hivyo basi, shikamaneni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu watakasifu waongofu baada yangu. Ziumeni kwa magego. Tahadharini na mambo ya kuzua, kwani hakika kila Bid´ah ni upotevu."[44]

at-Tirmidhiy amesema:

"Hadiyth ni Hasan na Swahiyh."

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

"Kila ´ibaadah ambayo hawakuabudu kwayo Maswahabah wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi na nyinyi msiabudu kwayo. Wale wa kwanza hawakuwapa wa mwisho la kusema. Mcheni Allaah, enyi wanazuoni, na chukueni njia ya waliokuwa kabla yenu."[45]

Ameipokea Abu Daawuud.

ad-Daarimiy amesema: "al-Hakam bin Mubaarak ametueleza: ´Amr bin Yahyaa ametueleza: Nilimsikia baba yangu akieleza kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

"Tulikuwa tukikaa nje ya mlango wa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) kabla ya Fajr na anapotoka tunaenda naye mpaka msikitini. Siku moja akatujia Abu Muusa al-Ash´ariy (Radhiya Allaahu ´anh) na kusema: "Abu ´Abdir-Rahmaan ameshakujieni?" Tukasema: "Hapana." Akakaa na sisi mpaka alipotoka. Alipotoka sote tukasimama. Abu Muusa akamwambia: "Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hivi karibuni nimeona msikitini kitu nimechokipinga na ilikuwa ni kitu cha kheri tu." Akasema: "Ni kipi?" Akasema: "Ukiishi utakiona. Msikitini nimewaona watu wamekaa mzunguko wakisubiri swalah. Katika kila mzunguko kuna mtu na kwenye mikono yao wana vijiwe vidogo vidogo. Anasema: "Semeni: "Allaahu Akbar" mara mia", wanafanya hivo. Kisha anasema: "Semeni: "Laa ilaaha illa Allaah" mara mia", wanafanya hivo. Kisha anasema: "Semeni: "Subhaana Allaah" mara mia", wanafanya hivo." Akasema: "Uliwaambia nini?" Akasema: "Sikuwaambia kitu. Ninasubiri neno lako au amri yako." Akasema: "Ungeliwaamrisha wahesabu madhambi yao na kuwadhamini kuwa hakuna chochote katika mema yao kitachopotea." Halafu akaenda na tukafuatana naye. Alipofika katika mzunguko mmoja miongoni mwa mizunguko ile akasimama na kusema: "Nini haya ninayoona mnafanya?" Wakasema: "Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Ni vijiwe tu ambavyo tunafanya navyo Takbiyr, Tahliyl na Tasbiyh." Akasema: "Hesabuni madhambi yenu. Mimi ninakudhaminini hakuna chochote katika mema yenu kitachopotea. Ee Ummah wa Muhammad! Ole wenu! Ni haraka iliyoje mmeangamia! Hawa hapa Maswahabah wa Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) bado wamejaa, nguo zake hazijaharibika na chombo chake hakijapasuka. Ninaapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko Mkononi Mwake ima nyinyi mkono katika dini bora kuliko dini ya Muhammad au mmefungua mlango wa upotevu." Wakasema: "Ee Abu ´Abdir-Rahmaan! Hatukukusudia jengine isipokuwa kheri tu." Akasema: "Ni wangapi wenye kutaka kheri na hawaifikii! Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametueleza kuwa kutakuwepo watu wataoisoma Qur-aan bila ya kuvuka koo zao. Ninaapa kwa Allaah sijui pengine wengi wao ndio nyinyi wenyewe." Kisha akatoka pale akenda zake." ´Amr bin Salamah amesema: "Tuliona wengi katika wao wakishirikiana na Khawaarij siku ya Nahrawaan."[46]

Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada na Mwenye kutegemewa. Swalah na salaam zimwendee kiongozi wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake wote.[1] al-Bukhaariy (2268).

[2] al-Bukhaariy (876) na Muslim (855).

[3] al-Bukhaariy katika "al-Adab al-Mufrad" (1/108).

[4] Ibn-ul-Mubaarak katika "az-Zuhd" (1/21), Ahmad katika "az-Zuhd" (1/196) na Abu Nu´aym katika "Hilyat-ul-Awliyaa'" (1/252).

[5] Ahmad katika "az-Zuhd" (137) na Abu Nu´aym katika "Hilyat-ul-Awliyaa'" (1/211).

[6] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[7] Muslim (1718).

[8] al-Bukhaariy (7280).

[9] al-Bukhaariy (6882).

[10] al-Bukhaariy (7282).

[11] al-Bid´ah, uk. 61-62.

[12] al-Bukhaariy (4777) na Muslim (102).

[13] al-Bukhaariy (6484) na Muslim (41).

[14] Ahmad (3/5), Ibn Hibbaan (1/376) na al-Haakim (4/643).

[15] Ahmad (4/114)

[16] Ahmad (3/387), ad-Daarimiy (436), Abu Ya´laa (4/102) na wengineo.

[17] Ahmad (4/130), at-Tirmidhiy (2863), Ibn Hibbaan (14/125), Ibn Khuzaymah (3/195) na wengineo.

[18] as-Siyaasah ash-Shar´iyyah (1/82).

[19] Ibn Abiy Haatim (3/729), al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika "Taariykh Baghdaad" (7/379) na al-Laalakaa'iy katika "Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jama´ah" (1/72).

[20] at-Tirmidhiy (2641).

[21] Ahmad (4/102), Abu Daawuud (4597), al-Haakim (1/218) na at-Twabaraaniy (19/376). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika "Dhwilaal-ul-Jannah" (2).

[22] al-Bukhaariy (3611) na Muslim (1066).

[23] Muslim (1854).

[24] Muslim (1017).

[25] Muslim (2674).

[26] Muslim (1067).

[27] al-Bukhaariy (5990) na Muslim (215).

[28] al-Bukhaariy (5063) na Muslim (1401).

[29] at-Tirmidhiy (2995), al-Bazzaar (5/345) na al-Haakim (2/320).

[30] Muslim (2564).

[31] al-Bukhaariy (7049) na Muslim (2297).

[32] Muslim (249).

[33] al-Bukhaariy (6587).

[34] al-Bukhaariy (3606) na Muslim (1847).

[35] ´Abdur-Razzaaq katika "al-Muswannaf" (11/367), al-Marwaziy katika "as-Sunnah", uk. 13, al-Laalakaa'iy katika "Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (1/56) na Abu Nu´aym (2/218).

[36] an-Nasaa'iy (6/343), Ahmad (1/435), ad-Daarimiy (202) na al-Bazzaar (57113).

[37] Muslim (145).

[38] Ahmad (1/398).

[39] Zawaa'id-ul-Musnad (4/73).

[40] at-Tirmidhiy (2630) ambaye amesema: "Hadiyth ni Hasan na Swahiyh."

[41] Abu Daawuud (4341), at-Tirmidhiy (3058) na Ibn Maajah (4014).

[42] al-Bid´ah, uk. 133.

[43] al-Bid´ah, uk. 122.

[44] Abu Daawuud (4607), at-Tirmidhiy (2676) na Ibn Maajah (34). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika "al-Irwaa'" (2455).

[45] Ibn-ul-Mubaarak katika "az-Zuhd", uk. 16, al-Marwaziy katika "as-Sunnah" (1/30) na Ibn Abiy ´Aasim katika "as-Sunnah" (1/90).

[46] ad-Daarimiy (204), Bahshal katika "Taariykh Waaswit" na al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika "Taariykh Baghdaad" (12/162).

Utunzi wa kielimu: