100 - Surat Al-Aadiyat ()

|

(1) Mwenyezi Mungu Anaapa kwa farasi wenye kwenda shoti katika njia Yake kumkabili adui, wakitoa sauti kwa kasi ya kukimbia. Haifai kwa kiumbe kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kuapa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni ushirikina.

(2) Na wenye kutoa cheche za moto kwa kwato zao ngumu wanapokimbia kwa kasi.

(3) Wenye kushambulia maadui kipindi cha asubuhi.

(4) Wakarusha vumbi kwa mbio zao.

(5) Wakautia kati, kwa kuuzunguka kwa vipando vyao, mkusanyiko wa maadui.

(6) Hakika binadamu ni mkanushaji sana neema za Mola wake.

(7) Na yeye anakubali ukanushaji wake.

(8) Na yeye ana pupa sana la mali.

(9) Kwani binadamu hajui linalomngojea mbele yake, pindi Mwenyezi Mungu Atakapowatoa wafu makaburini waende kuhesabiwa na kulipwa?

(10) Na (kwani yeye hajui) yakatolewa yaliyo ndani ya vifua: mema au maovu?.

(11) Hakika Mola wao kwao na kwa amali zao, Siku Hiyo, ni Mtambuzi; hakuna chenye kufichamana Kwake.