90 - Surat Al-Balad ()

|

(1) Mwenyezi Mungu Anaapa kwa mji huu mtakatifu wa Makkah.

(2) Na wewe, ewe Nabii, ni mkazi wa mji huu mtakatifu.

(3) Na Anaapa kwa mzazi wa wanaadamu, ambaye ni Ādam, amani imshukie, na kilichozalikana na yeye.

(4) Hakika Tumemuumba binadamu katika usumbufu na shida za kilimwengu.

(5) Kwani anadhani kwa mali aliyoyakusanya kuwa Mwenyezi Mungu Hatakuwa na uwezo juu yake?

(6) Huwa akisema kwa kujigamba: «Nimetumia mali mengi.»

(7) Kwani anadhani, kwa kitendo chake hiko, kuwa Mwenyezi Mungu, Aliyetukuka na kushinda, Hamuoni wala hatamhesabu juu ya kubwa na dogo?

(8) Kwani hatukumpa macho mawili ya kuonea,

(9) ulimi na midomo miwili ya kusemea

(10) na kumfafanulia njia mbili: ya kheri na ya shari?

(11) Basi ajiepushe na janga la Akhera kwa kutoa mali yake ili aokoke.

(12) Ni kitu gani kilichojulisha ni lipi hilo janga la Akhera na ni mambo gani yenye kusaidia kujiepusha nalo?

(13) Ni kuacha huru shingo iliyoamini kuikomboa na utumwa.

(14) Au kulisha, wakati wa shida ya njaa,

(15) yatima mwenye ujamaa, ili ipatikane fadhila ya sadaka na ya kuunga kizazi,

(16) au masikini asiyekuwa na kitu.

(17) Kisha akawa, baada ya kufanya amali njema zilizotajwa, ni miongoni mwa waliotakasa Imani yao kwa Mwenyezi Mungu, wakausiana kusubiri juu ya kumtii Mwenyezi Mungu kwa kufuata maamrisho Yake na kujiepusha na vitendo vya kumuasi na wakausiana kuwahurumia viumbe.

(18) Wenye kufanya hayo ndiwo watu wa kulia ambao watapelekwa Siku ya Kiyama upande wa kulia kuelekea Peponi.

(19) Na wale waliokanusha Qur’ani ndio ambao watapelekwa, Siku ya Kiyama, upande wa kushoto kuelekea Motoni.

(20) Malipo yao ni Moto wa Jahanamu wenye kuwafinika na kuwaziba.