55 - Surat Ar-Rahman ()

|

(1) mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema

(2) Amemfundisha binadamu Qur’ani kwa kurahisisha kuisoma, kuihifadhi na kuelewa maana yake.

(3) Amemuumba binadamu,

(4) Amemfundisha ufasaha wa kujieleza ili kumtenganisha na wengine.

(5) Jua na mwezi zinatembea kwa kufuatana, moja baada ya nyingine, kwa hesabu madhubuti isiyotafautiana wala kugongana.

(6) Na nyota iliyo mbinguni na miti ya ardhini, vinamjua Mola wao, vinamsujudia na vinanyosha shingo zao kufuata vile ambavyo vimepangiwa vifuate vya maslahi ya waja Wake na manufaa yao.

(7) Na mbingu Ameiinua na kuifanya iwe juu ya ardhi, Na Ameweka kwenye ardhi uadilifu Aliouamrisha na kuulazimisha kwa waja Wake.

(8) Ili msipite mipaka na msimfanyie hiyana mnayempimia.

(9) Na simamisheni upimaji kwa usawa na msipunguze mizani mnapowapimia watu.

(10) Na ardhi Ameiweka na Ameitayarisha, ili viumbe vitulie juu yake.

(11) Humo mna matunda na mitende yenye makarara ya matunda. Na humo kuna nafaka zenye maganda, vikiwa ni chakula chenu na wanyama wenu.

(12) Na humo mna kila mmea wenye harufu nzuri.

(13) Bas ni neema gani za Mola wenu, za kidini na za kidunia, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha? Na ni jawabu nzuri ilioje ya majini alipowasomea wao Nabii, rehema ya Mwenyezi Mungu na amani zimshukie, sura hii, kila akipita kwenye aya hii walikuwa wakisema, «Hakuna chochote miongoni mwa neema zako, ewe Mola wetu, tunachokanusha. Sifa njema zote ni zako.» Na hivi ndivyo inavyotakiwa kwa mja anapoelezewa neema za Mwenyezi Mungu na mema Yake akubali na amshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizo.

(14) Amemuumba baba wa wanadamu, naye ni Ādam, kwa udongo mkavu kama vyungu.

(15) Na Amemuumba Iblisi, naye ni katika majini, kwa mroromo wa moto uliochanganyika.

(16) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(17) Mola wa pande mbili za Mashariki ya jua, katika kusi na kaskazi, na Mola wa pande mbili za Magharibi ya jua, katika kusi na kaskazi, kwani vyote viko chini ya uendeshaji Wake na ulezi Wake..

(18) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(19) Mwenyezi Mungu Ameyachanganya maji ya bahari mbili, tamu na chumvi, yanakutana, baina yake kuna kizuizi,

(20) mojawapo haiingii sehemu ya nyingine na kuiondoa sifa yake, bali ya tamu inasalia kuwa tamu na ya chumvi inasalia kuwa chumvi pamoja na kukutana kwake.

(21) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(22) Inatoka kwenye bahari mbili hizo, kwa uweza wa Mwenyezi Mungu, lulu na marjani.

(23) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(24) Ni Yake Yeye, Aliyetakasika na kutukuka, mamlaka ya kuyaendesha majahazi makubwa yanayotembea baharini kwa manufaa ya watu, yenye kusimamisha juu milongoti yake na matanga yake kama vile majabali.

(25) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu mnazikanusha?

(26) Kila aliye juu ya uso wa ardhi miongoni mwa viumbe ni mwenye kuangamia,

(27) na utasalia uso wa Mola wako Mwenye utukufu, ubora, kheri nyingi na upaji. Katika aya hii pana kuthibitisha sifa ya uso kwa Mwenyezi Mungu kwa namna inavyonasibiana na Yeye, kutakasika ni Kwake, bila kufananisha wala kueleza namna ulivyo.

(28) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(29) Wanamuomba Yeye walioko mbinguni na ardhini haja zao. Hakuna yoyote anayejitosheleza kutomhitajia Yeye, kutakasika ni Kwake. Kila siku Yeye Yuko kwenye jambo: Anatukuza na Anatweza, Anatoa na Anazuia.

(30) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(31) Nitawatengea kipindi cha kuwahesabu na kuwalipa kwa matendo yenu mliyoyafanya, enyi vizito viwili:-majini na binadamu-, tuwatese watu wa maasia na tuwape malipo mema watu wa utiifu.

(32) Ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(33) Enyi mkusanyiko wa majini na binadamu! Mkiweza kuihepa amri ya Mwenyezi Mungu na uamuzi Wake kwa kukimbia kwenye pambe za mbingu na ardhi basi fanyeni, na hamuwezi kufanya hivyo isipokuwa kwa nguvu na hoja na amri inayotoka kwa Mwenyezi Mungu Aliyetukuka. (Na vipi mtaweza kufanya hivyo na hali nyinyi hamzimilikii nafsi zenu manufaa yoyote wala madhara?).

(34) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(35) Mtatumiwa mroromo wa moto na shaba iliyoyayushwa, mmiminiwe juu ya vichwa vyenu msiweze kusaidiana.

(36) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazukanusha?

(37) Na pindi mbingu itakapopasuka na kuachana Siku ya Kiyama, ikawa nyekundu kama rangi ya waridi na kama mafuta yaliyochemshwa na risasi iliyoyayushwa, kutokana na mambo magumu na vituko vya Siku ya Kiyama.

(38) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(39) Katika Siku hiyo Malaika hawatawauliza wale wahalifu, miongoni mwa binadamu na majini, kuhusu dhambi zao.

(40) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(41) Malaika watawajua wahalifu kwa alama zao, hapo wawashike kwenye paa za vichwa vyao na nyayo zao wawarushe Motoni.

(42) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(43) Wataambiwa hao wahalifu kwa njia ya kulaumiwa na kudhalilishwa, «Huu ndio moto wa Jahanamu ambao wahalifu duniani walikuwa wakiukanusha:

(44) mara wanaadhibiwa kwenye Jaḥīm, na mara nyingine wananyweshwa Hāmīm, nacho ni kinywaji kilichofikia upeo wa ukali wa moto, kinakata tumbo na sehemu za ndani ya mbavu.

(45) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu mnazikanusha?

(46) Na anayemcha Mwenyezi Mungu, miongoni mwa waja Wake binadamu na majini, akaogopa kusimama kwake mbele Yake, akamtii na akaacha kumuasi atakuwa na mabustani mawili ya Pepo.

(47) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(48) Mabustani mawili hayo ya Pepo yana matawi yaliyostawi kwa matunda ya kila aina.

(49) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(50) Katika Pepo mbili hizo kuna chemchemi mbili za maji zinazopita katikati yake.

(51) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(52) Katika mabustani hayo mawili ya Pepo kuna sampuli mbili za kila aina ya matunda.

(53) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(54) Na wale wanaoogopa kusimama mbele ya Mola Wao watakuwa na mabustani mawili ya Pepo, ambayo ndani yake watastarehe, hali ya kutegemea juu ya matandiko yaliyojazwa dibaji nzito. Na matunda ya mabustani mawili hayo ya pepo yako karibu nao.

(55) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mtazikanusha?

(56) Katika matandiko hayo wapo wake macho yao yanawatazama waume zao tu, hawawatazami wengineo, wamefungamana na wao. Hakuna aliyewaingilia, kabla ya hao waume zao, binadamu yoyote wala jini.

(57) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadanu, mnazikanusha?

(58) Kama kwamba hawa wake wa kihurulaini ni yakuti na marijani katika sifa zao na uzuri wao.

(59) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa najini na binadamu , mnazikanusha?

(60) Je atakuwa na malipo yoyote, huyu aliyekuwa mwema wa matendo duniani, isipokuwa ni afanyiwe wema kwa kupewa Pepo huko Akhera?

(61) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(62) Na chini ya mabustani ya Pepo mawili yaliyotangulia kuna mabustani ya Pepo mawili mengine.

(63) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(64) Mabustani haya mawili ni rangi ya kijani. Ujani wake umeiva sana mapaka umeingia kwenye weusi.

(65) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(66) Ndani ya mabustani mawili hayo ya Peponi kuna chemchemi mbili zenye kububujika maji daima bila kukatika.

(67) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(68) Kwenye mabustani hayo mawili kuna aina za matunda, mitende na mikomamanga.

(69) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(70) Ndani ya mabustani haya manne ya Pepo kuna wake walio wema wa tabia na wazuri wa nyuso.

(71) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(72) Mahurulaini wakunjufu wa macho, waliositiriwa na kuhifadhiwa mahemani.

(73) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(74) Hawajaingiliwa Mahurulaini hawa na binadamu yoyote wala jini kabla ya waume zao.

(75) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(76) Hali ya kuwa wametegemea kwenye mito yenye mifuko rangi ya kijani na matandiko mazuri.

(77) Basi ni neema gani za Mola wenu, enyi mkusanyiko wa majini na binadamu, mnazikanusha?

(78) Zimekithiri mno baraka za Jina la Mola wako, na kheri Zake zimekuwa nyingi, Mwenye haiba kubwa, utukufu wenye kukamilika na takrima kwa wenye kumtegemea Yeye.