81 - Surat At-Takwir ()

|

(1) Pindi jua litakapokunjwa, na mwangaza wake ukaondoka.

(2) Na pindi nyota zitakapopuputika na nuru yake ikafutika.

(3) Na pindi majabali yatakapoondoshawa kwenye uso wa ardhi yakawa ni vumbi linaloenea.

(4) Na pindi ngamia wenye mimba watakapoachwa na kupuuzwa.

(5) Na pindi wanyama mwitu watakapokusanywa na kutangamanishwa, ili Mwenyezi Mungu Awape nafasi ya kulipizana wao kwa wao.

(6) Na pindi bahari zitakapowashwa moto zikawa ni moto unaowaka.

(7) Na pindi nafsi zitakapokutanishwa na mfano wake na sampuli yake.

(8) Na pindi mtoto wa kike aliyezikwa akiwa hai atakapoulizwa, Siku ya Kiyama, suala la kumbembeleza na kumkejeli aliyemzika:

(9) ni kwa dhambi gani ilikuwa kuzikwa kwake?

(10) Na pindi kurasa za matendo zitakapoonyeshwa.

(11) Na pindi mbingu zitakapong’olewa na kuondoshwa zilipokuwa.

(12) Na pindi Moto utakapowashwa na ukawaka.

(13) Na pindi Pepo , Nyumba ya Neema, itakaposongezewa watu wake wachamungu.

(14) Litakapotokea hilo, itayakinisha kila nafsi na kujua kile ilichokitanguliza cha kheri au shari.

(15) Anaapa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa nyota zinazofichika nuru yake mchana,

(16) zinazotembea na zinazoghibu katika anga zake.

(17) Na Anaapa kwa usiku unapojitokeza na giza lake.

(18) Na kwa asubuhi unapojitokeza mwangaza wake.

(19) Hakika Qur’ani ni ujumbe wa mjumbe mtukufu , naye ni Jibrili, amani imshukike.

(20) Mwenye nguvu katika kuyapitisha yale anayoamrishwa. Mwenye cheo cha juu kwa Mwenyezi Mungu. Anayesikilizwa na Malaika.

(21) Anayeaminiwa juu ya Wahyi anaoteremka nao.

(22) Hakuwa Muhammad mnayemjua ni mwendawazimu.

(23) Na kwa hakika Muhammad alimuona Jibrili anayemjia na utume katika pambizo kubwa.

(24) Wala yeye hafanyi ubakhili katika kufikisha Wahyi.

(25) Wala haikuwa hii Qur’ani ni neno la Shetani aliyefukuzwa na kutolewa kwenye rehema ya Mwenyezi Mungu. Lakini Qur’ani hii ni maneno ya Mwenyezi Mungu na ni Wahyi wake.

(26) Akili zenu zawapeleka wapi katika kukanusha baada ya hoja hizi zilizo wazi na zenye nguvu?

(27) Hayakuwa haya isipokuwa ni mawaidha kutoka kwa Mwenyezi Mungu yanapewa watu wote.

(28) Kwa atakaye, kati yenu, kulingana juu ya haki na Imani.

(29) Wala nyinyi hamtotaka isipokuwa kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote.