58 - Surat Al-Mujadilah ()

|

(1) Hakika Mwenyezi Mungu amekwisha sikia usemi wa mwanamke anayejadiliana nawe juu ya mumewe, na anamshitakia Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anayasikia majibizano yenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia mno, Mwenye kuona zaidi.

(2) Wale miongoni mwenu wanaowasawazisha wake zao na mama zao, hao si mama zao. Hawakuwa mama zao ila wale waliowazaa. Na hakika hao wanasema neno ovu mno, na la uwongo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria mno, Mwenye kusamehe zaidi.

(3) Na wale wanaojitenga na wake zao, kisha wakarudia katika yale waliyoyasema, basi wamkomboe mtumwa kabla hawajagusana. Mnapewa maonyo kwa hayo. Na Mwenyezi Mungu anayajua yote mnayoyatenda.

(4) Na asiyepata mtumwa kumkomboa, basi na afunge saumu miezi miwili mfululizo kabla hawajagusana. Na asiyeweza hayo, basi awalishe masikini sitini. Hayo ni hivyo ili mumuamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na hiyo ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na makafiri watapata adhabu chungu.

(5) Hakika wanaopinzana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, watadhalilishwa kama walivyodhalilishwa wale waliokuwa kabla yao. Na tulikwisha teremsha Ishara zilizo wazi. Na makafiri watapata adhabu ya kufedhehesha.

(6) Siku atakapowafufua Mwenyezi Mungu, na awaambie yale waliyoyatenda. Mwenyezi Mungu ameyadhibiti, na wao wameyasahau! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu.

(7) Kwani huoni kwamba Mwenyezi Mungu anajua vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi? Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wanne wao, wala wa watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala wa wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yu pamoja nao popote pale walipo. Kisha Siku ya Kiyama atawaambia waliyoyatenda. Hakika Mwenyezi Mungu anajua zaidi kila kitu.

(8) Kwani huwaoni wale waliokatazwa kunong'onezana, kisha wakayarudia yale yale waliyokatazwa, na wakanong'ona juu ya mambo ya dhambi, na ya uadui, na ya kumuasi Mtume? Na wakikujia, hukuamkua sivyo anavyokuamkua Mwenyezi Mungu. Na husema katika nafsi zao: 'Mbona Mwenyezi hatuadhibu kwa haya tuyasemayo?' Basi Jahannamu itawatosha; wataingia humo! Na hayo ndiyo marejeo maovu yaliyoje!

(9) Enyi mlioamini! Mnaponong'ona, msinong'one kwa sababu ya mambo ya madhambi, na uadui, na kumuasi Mtume. Bali nong'onezane kwa kutenda mema na kuacha maovu. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwake mtakusanywa nyote.

(10) Kwa hakika minong'ono hiyo inatokana na Shetani ili awahuzunishe wale walioamini, na wala haitawadhuru chochote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu tu ndio wategemee Waumini.

(11) Enyi mlioamini! Mkiambiwa: Fanyeni nafasi katika mabaraza, basi fanyeni nafasi. Na Mwenyezi Mungu atakufanyieni nyinyi nafasi. Na mkiambiwa: Ondokeni, basi ondokeni. Mwenyezi Mungu atawainua wale walioamini miongoni mwenu, na wale waliopewa elimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

(12) Enyi mlioamini! Mnaposema siri na Mtume, basi tangulizeni sadaka kabla ya kusemezana kwenu. Hiyo ni heri kwenu na usafi zaidi. Na ikiwa hamkupata cha kutoa, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mno, Mwenye kurehemu zaidi.

(13) Mnachelea kutanguliza hiyo sadaka kabla ya kusemezana kwenu kwa siri? Ikiwa hamkufanya hayo, na Mwenyezi Mungu akapokea toba yenu, basi shikeni Sala, na toeni Zaka, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.

(14) Huwaoni wale waliofanya urafiki mwendani na watu ambao Mwenyezi Mungu amewakasirikia? Hao si katika nyinyi, wala si katika wao. Na huapa kwa uwongo hali ya kuwa wanajua.

(15) Mwenyezi Mungu amewaandalia adhabu kali. Kwa hakika waliyokuwa wakiyatenda ni maovu kabisa.

(16) Wamefanya viapo vyao ni ngao, na wakaipinga Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.

(17) Hayatawafaa kitu mali yao wala watoto wao mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu milele.

(18) Siku atakayowafufua Mwenyezi Mungu wote, wamuapie kama wanavyokuapieni nyinyi. Na watadhani kuwa wamepata kitu! Kwa hakika hao ndio waongo.

(19) Shetani amewatawala na akawasahaulisha kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Hao ndio kundi la Shetani. Sikilizeni, hakika kundi la Shetani ndilo lenye kuhasirika.

(20) Hakika wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hao ndio miongoni mwa madhalili wa mwisho.

(21) Mwenyezi Mungu ameandika: Hapana shaka Mimi na Mtume wangu tutashinda. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

(22) Huwakuti watu wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho kuwa wanawapenda wanaompinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hata wakiwa ni baba zao, au watoto wao, au ndugu zao, au jamaa zao. Hao ameandika katika nyoyo zao Imani, na amewapa nguvu kwa Roho itokayo kwake. Na atawaingiza katika Mabustani yapitayo mito kati yake. Humo watakaa daima. Mwenyezi Mungu awe radhi nao, na wao wawe radhi naye. Hao ndio (Hizbullahi) Kundi la Mwenyezi Mungu. Hakika Kundi la Mwenyezi Mungu ndilo lenye kufanikiwa.