(1) Mbingu itakapochanika.
(2) Na nyota zitakapotawanyika.
(3) Na bahari zitakapopasuliwa.
(4) Na makaburi yatakapofukuliwa.
(5) Hapo kila nafsi itajua ilichotanguliza, na ilichobakisha nyuma.
(6) Ewe mwanaadamu! Nini kilichokughuri ukamwacha Mola wako Mlezi Mtukufu?
(7) Aliyekuumba, akakuweka sawa, akakunyoosha.
(8) Katika sura yoyote aliyoipenda akakujenga.
(9) Sivyo hivyo! Bali nyinyi mnaikanusha Siku ya Malipo.
(10) Na hakika bila ya shaka wapo walinzi juu yenu.
(11) Waandishi wenye heshima.
(12) Wanayajua mnayoyatenda.
(13) Hakika wema bila ya shaka watakuwa katika neema.
(14) Na hakika waovu bila ya shaka watakuwa Motoni.
(15) Wataingia humo Siku ya Malipo.
(16) Na hawatoacha kuwamo humo.
(17) Na nini kitakachokujulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
(18) Tena nini kitakachokujulisha Siku ya Malipo ni siku gani?
(19) Siku ambayo nafsi haitakuwa na madaraka yoyote juu ya nafsi; na amri yote siku hiyo ni ya Mwenyezi Mungu tu.