(1) Alif Lam Ra. Hizo ni Aya za Kitabu chenye hekima.
(2) Je, imekuwa ajabu kwa watu kwamba tumemfunulia mwanamume kutokana nao kuwa, “Waonye watu, na wabashirie wale walioamini ya kuwa wana cheo cha juu kwa Mola wao Mlezi?” Wakasema makafiri, “Hakika huyu ni mchawi aliye dhahiri!”
(3) Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu, ambaye ameziumba mbingu na ardhi kwa siku sita, kisha akaimarika juu ya Kiti cha Enzi, anaendesha mambo yote. Hakuna mwombezi yeyote isipokuwa baada ya idhini yake. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi. Basi muabuduni Yeye. Je, hamkumbuki?
(4) Kwake Yeye tu ndiyo marejeo yenu nyote. Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo ya kweli. Hakika Yeye ndiye anayeanzisha uumbaji, kisha ataurejesha ili awalipe kwa uadilifu wale walioamini na wakatenda mema. Na wale waliokufuru, wana vinywaji vya maji ya moto, na adhabu chungu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyakufuru.
(5) Yeye ndiye aliyelijaalia jua kuwa na mwangaza, na mwezi ukawa na nuru, na akaupimia vituo ili mjue idadi ya miaka na hesabu. Mwenyezi Mungu hakuviumba hivyo isipokuwa kwa haki. Anazipambanua Ishara kwa kaumu wanaojua.
(6) Hakika katika kuhitalifiana usiku na mchana, na katika vile alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika mbingu na ardhi, zipo Ishara kwa kaumu wamchao.
(7) Hakika wale wasiotaraji kukutana nasi, na wakaridhia uhai wa dunia hii na wakatua nao, na wale walioghafilika na Ishara zetu.
(8) Hao, makazi yao ni Motoni kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
(9) Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao Mlezi atawaongoa kwa sababu ya Imani yao. Itapita mito kwa chini yao katika Mabustani yenye neema.
(10) Wito wao humo utakuwa, “Subhanaka Allahumma (Umetakasika Ee Mwenyezi Mungu!)." Na maamkizi yao humo ni "Salama." Na mwisho wa wito wao ni, “Alhamdulillahi Rabbil 'aalamiin (Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote)."
(11) Na lau kama Mwenyezi Mungu angeliwafanyia watu haraka kuwaletea maovu kama wanavyojiharakishia kuletewa heri, basi bila ya shaka wangelikwisha timiziwa muda wao. Lakini tunawaacha wale wasiotaraji kukutana nasi wakihangaika katika upotovu wao.
(12) Na mtu akiguswa na shida, hutuomba naye kaegesha ubavu, au kakaa, au kasimama. Lakini tunapomwondoshea shida yake hiyo, huendelea kama kwamba hakuwahi kutuomba tumwondoshee shida iliyomgusa. Hivyo ndivyo walivyopambiwa wapitilizao viwango yale waliyokuwa wakiyatenda.
(13) Na hakika tuliviangamiza vizazi vya kabla yenu walipo dhulumu, na waliwajia Mitume wao kwa Ishara zilizo wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini. Hivyo ndivyo tunavyowalipa kaumu wahalifu.
(14) Kisha tukawafanya nyinyi ndio wenye kushika pahala pao katika ardhi baada yao ili tuone jinsi mtakavyotenda.
(15) Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, wale wasiotaraji kukutana na Sisi husema, “Leta Qur-aani isiyokuwa hii, au ibadilishe.” Sema, “Haiwi kwangu niibadilishe nitakavyo mimi mwenyewe. Mimi sifuati isipokuwa yale ninayofunuliwa kwa Wahyi. Hakika mimi ninahofu, nikimuasi Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku iliyo kuu.
(16) Sema, “Mwenyezi Mungu angelitaka, nisingeliwasomea, wala nisingelikuwa mwenye kukijua zaidi yenu. Kwani nalikwisha kaa miongoni mwenu umri mzima kabla yake! Kwani, hamtii akilini?”
(17) Basi ni nani aliye dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu na akazikadhibisha Ishara zake? Hakika hawafaulu wahalifu.
(18) Nao, wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu wale wasiowadhuru wala kuwanufaisha, na wanasema, “Hawa ndio waombezi wetu kwa Mwenyezi Mungu!” Sema, “Je, mnamwambia Mwenyezi Mungu yale asiyoyajua ya katika mbingu wala katika ardhi? Ametakasika na ametukuka na hao wanaomshirikisha naye.”
(19) Na watu hawakuwa isipokuwa Umma mmoja tu, kisha wakahitalifiana. Na lau kuwa si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, hapana shaka hukumu ingelikwisha katwa baina yao katika yale wanayohitalifiana.
(20) Na wanasema, “Kwa nini hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi?” Sema, “Hakika mambo ya ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu tu. Basi nyinyi ngojeni, na mimi niko pamoja nanyi katika wanaongojea.”
(21) Na tunapowaonjesha watu rehema baada ya shida iliyowagusa, tazama, wanafanya njama katika Ishara zetu. Sema, “Mwenyezi Mungu ni Mwepesi zaidi wa kupanga njama. Hakika wajumbe wetu wanayaandika hayo mnayoyapangia njama.”
(22) Yeye ndiye anayewaendesha katika nchi kavu na baharini. Mpaka mnapokuwa katika majahazi na yakawa yanakwenda nao kwa upepo mzuri na wakaufurahia, upepo mkali ukayajia, na yakawajia mawimbi kutoka kila mahali, na wakaona kwamba wameshazungukwa, basi hapo wanamwomba Mwenyezi Mungu kwa kumpwekeshea yeye tu dini, “Ukituokoa na haya, bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.”
(23) Lakini anapowaokoa, tazama, wanafanya jeuri tena katika ardhi bila ya haki. Enyi watu! Hakika jeuri zenu zitawadhuru nyinyi wenyewe. Hii ni starehe ya maisha ya dunia tu. Kisha marejeo yenu ni kwetu, na hapo tutawaambia yale mliyokuwa mkiyatenda.
(24) Hakika mfano wa uhai wa dunia hii ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, kisha mimea ya ardhi ikachanganyika nayo miongoni mwa vile wanayvovila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipokamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani kwamba wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, kwa hivyo tukaifanya kama iliyofyekwa, kama kwamba haikuwapo jana. Hivyo ndivyo tunavyozipambanua Ishara zetu kwa kaumu wanaotafakari.
(25) Na Mwenyezi Mungu anaita kwenye Nyumba ya amani, na anamwongoa amtakaye kwenye Njia iliyonyooka.
(26) Kwa wafanyao uzuri ni uzuri na zaidi. Wala vumbi halitawafunika nyuso zao, wala madhila. Hao ndio wenza wa Pepo. Wao, humo watadumu.
(27) Na wale waliochuma mabaya, malipo ya baya ni kwa mfano wake, na watafunikwa na madhila. Hawatakuwa na wa kuwalinda na Mwenyezi Mungu. Nyuso zao ni kama kwamba zimefunikwa na vipande vya usiku wa giza. Hao ndio wenza wa Moto. Wao, humo watadumu.
(28) Na siku tutakapowakusanya wote, kisha tutawaambia wale walioshirikisha, "Simameni pahali penu nyinyi na washirika wenu." Kisha tutatenganisha baina yao. Na hao washirika wao watasema, "Nyinyi hamkuwa mkituabudu sisi."
(29) Basi Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni shahidi baina yetu na nyinyi. Hakika sisi tulikuwa hatuna habari na ibada yenu.
(30) Huko kila nafsi itayajua iliyoyatanguliza. Na watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa haki, na yote ya uongo waliyokuwa wakiyazua yatawapotea.
(31) Sema, "Ni nani anayewaruzuku kutoka mbinguni na ardhi? Au ni nani anayemiliki kusikia na kuona? Na ni nani atoaye kilicho hai kutoka kwa maiti, na atoaye maiti kutoka kwa kilicho hai? Na ni nani anayeyaendesha mambo yote?" Basi watasema, "Mwenyezi Mungu." Basi sema, "Je, hamchi?"
(32) Basi huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi wa haki. Na kipo kitu gani baada ya haki, isipokuwa upotovu tu? Basi ni vipi mnageuzwa?
(33) Ndivyo hivyo kauli ya Mola wako Mlezi ilivyowathibitikia wale waliovuka mipaka ya kwamba hawataamini.
(34) Sema: Je, yupo katika washirika wenu mwenye kuanzisha kuumba viumbe, kisha akavirejesha? Sema: Mwenyezi Mungu anaazisha kuumba viumbe, kisha anavirejesha. Basi ni vipi mnadanganywa?
(35) Sema, "Je, yupo yeyote katika washirika wenu mwenye kuongoa kwenye haki?" Sema, "Mwenyezi Mungu anaongoa kwenya haki." Basi, je, yule anayeongoa kwenye haki anastahiki zaidi kufuatwa au yule asiyeongoka isipokuwa akiongozwa? Basi nyinyi mna nini, mnahukumu namna gani?
(36) Na wengi wao hawafuati isipokuwa dhana tu. Na hakika, dhana haifai kitu mbele ya haki. Hakika Mwenyezi Mungu anajua zaidi yote wanayoyatenda.
(37) Na haikuwa Qur-ani hii ni ya kuzuliwa kutoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini ni usadikisho wa yale yaliyoitangulia, na ni maelezo ya kina ya Kitabu kisicho na shaka yoyote ndani yake, kutoka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(38) Ama ndiyo wanasema ameizua? Sema, "Hebu leteni sura moja mfano wake na muwaite muwawezao, kando na Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli."
(39) Bali waliyakadhibisha yale wasiyoyaelewa elimu yake vyema kabla hayajawajia maelezo yake. Hivyo ndivyo walivyokadhibisha wale waliokuwa kabla yao. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa madhalimu hao.
(40) Na miongoni mwao kuna anayeiamini, na miongoni mwao kuna asiyeiamini. Na Mola wako Mlezi ndiye anawajua vyema waharibifu.
(41) Na wakikukadhibisha, basi sema, "Mimi nina matendo yangu, na nyinyi mna matendo yenu. Nyinyi mko mbali sana na yale ninayoyatenda, nami niko mbali sana na mnayoyatenda."
(42) Na miongoni mwao kuna wale wanaokusikiliza. Je, wewe unaweza wasikizisha viziwi hata kama hawatumii akili?
(43) Na miongoni mwao kuna yule anayekutazama. Je, wewe unaweza kuwaongoa vipofu hata kama hawaoni?
(44) Hakika Mwenyezi Mungu hawadhulumu watu kitu chochote, lakini watu wenyewe wanazidhulumu nafsi zao.
(45) Na Siku atakapowakusanya, itakuwa kama kwamba hawakukaa isipokuwa saa moja tu katika mchana! Watatambuana. Hakika wamehasirika wale waliokadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu, wala hawakuongoka.
(46) Na ima tutakuonyesha baadhi ya yale tunayowaahidi, au tukufishe kabla yake, basi marejeo yao ni kwetu. Kisha Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa wanayoyafanya.
(47) Na kila umma una Mtume. Alipowajia Mtume wao walihukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawadhulumiwi.
(48) Na wanasema, “Ni lini ahadi hii, ikiwa nyinyi ni wakweli?
(49) Sema: Sijimilikii nafsi yangu shari wala kheri ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Kila umma una muda wao waliowekewa. Ukifika muda wao hawakawii hata saa moja wala hawatangulii.
(50) Sema, “Mnaonaje ikiwajia adhabu yake hiyo usiku au mchana. Basi wahalifu wanaharakisha nini?”
(51) Tena je, ikishatokea ndiyo mtaiamini? Je, sasa? Na ilhali mlikuwa mkiifanyia haraka?
(52) Kisha wale waliodhulumu wataambiwa, "Ionjeni adhabu ya kudumu. Kwani mtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyachuma?"
(53) Na wanakuuliza, "Je, ni kweli hayo?" Sema, "Ehe! Ninaapa kwa Mola wangu Mlezi! Hakika hayo ni kweli, na wala nyinyi hamtashinda."
(54) Na lau kuwa kila nafsi iliyodhulumu inamiliki kila kilichomo katika ardhi, basi bila ya shaka ingejikomboa kwavyo. Na watakapoiona adhabu, wataficha majuto. Na itahukumiwa baina yao kwa uadilifu, nao hawatadhulumiwa.
(55) Jueni kuwa hakika ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyo katika mbingu na katika ardhi. Jueni kuwa hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya haki. Lakini wengi wao hawajui.
(56) Yeye ndiye anayehuisha na anayefisha. Na kwake mtarejeshwa.
(57) Enyi watu! Yamekwisha wajia mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza ya yale yaliyo katika vifua, na uwongofu, na rehema kwa Waumini.
(58) Sema, "Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi na wafurahi kwa hayo. Hayo ndiyo bora kuliko hayo wanayoyakusanya.
(59) Sema: Je, munaonaje yale aliyowateremshia Mwenyezi Mungu katika zile riziki, basi mkafanya katika hizo nyingine haramu na nyingine halali. Sema, "Je, Mwenyezi Mungu aliwaruhusu, au mnamzulia Mwenyezi Mungu tu?"
(60) Na ni nini dhana ya wale wanaomzulia Mwenyezi Mungu uongo Siku ya Qiyama? Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wao hawashukuru.
(61) Na huwi katika jambo lolote, wala husomi sehemu yoyote katika Qur-ani, wala hamtendi kitendo chochote isipokuwa Sisi huwa ni mashahidi juu yenu mnaposhughulika nayo. Na hakifichikani kwa Mola wako Mlezi chenye uzito hata wa chembe katika ardhi na katika mbingu, wala kidogo kuliko hicho wala kikubwa isipokuwa kimo katika Kitabu kilicho wazi.
(62) Jueni kuwa vipenzi wa Mwenyezi Mungu hawana hofu yoyote juu yao wala hawatahuzunika.
(63) Wale walioamini na wakawa wachaji.
(64) Wao wana bishara njema katika uhai wa dunia na katika Akhera. Hakuna mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(65) Wala yasikuhuzunishe maneno yao. Hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mwenye kusikia vyema Mwenye kujua yote.
(66) Jueni kuwa ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyo katika mbingu na katika ardhi. Na wala hawawafuati washirika wowote hao wanaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu. Wao hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawasemi isipokuwa uongo.
(67) Yeye ndiye aliyewajaalia usiku ili mtulie humo, na mchana wa kuonea. Hakika katika haya zipo Ishara kwa kaumu wanaosikia.
(68) Walisema, "Mwenyezi Mungu alijifanyia mwana." Ametakasika! Yeye ndiye asiyehitajia kitu. Ni vyake vilivyo katika mbingu na katika ardhi. Nyinyi hamna uthibitisho wowote wa haya! Je, mnamzulia Mwenyezi Mungu msiyoyajua?
(69) Sema, "Hakika wale wanaomzulia uongo Mwenyezi Mungu hawatafanikiwa."
(70) Hiyo ni starehe ya katika dunia tu, kisha marejeo yao ni kwetu. Kisha tutawaonjesha adhabu kali kwa sababu ya yale waliyokuwa wakikufuru.
(71) Na wasomee habari za Nuhu alipowaambia kaumu yake: Enyi kaumu yangu! Ikiwa ni kukubwa kwenu kukaa kwangu nanyi na kuwakumbusha kwangu kwa Ishara za Mwenyezi Mungu, basi mimi namtegemea Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, nyinyi likusanyeni jambo lenu pamoja na washirika wenu, kisha jambo lenu hilo lisiwe la kufichikana kwenu, kisha nihukumuni, wala msinipe muhula.
(72) Na mkigeuka, basi mimi sikuwaomba ujira wowote. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Na nimeamrishwa kwamba niwe miongoni mwa Waislamu.
(73) Lakini wakamkadhibisha. Kwa hivyo tukamwokoa, pamoja na wale waliokuwa naye, katika jahazi. Na tukawafanya wao ndio waliobakia, na tukawazamisha wale waliozikadhibisha Ishara zetu. Basi angalia vipi ulikuwa mwisho wa walioonywa.
(74) Kisha baada yake tukawatuma Mitume kwa kaumu zao. Nao wakawajia kwa Ishara zilizo wazi. Lakini hawakuwa wenye kuyaamini wale waliyoyakanusha kabla yake. Hivyo ndivyo tunavyoziziba nyoyo za wavukao mipaka.
(75) Kisha baada yao tukamtuma Musa na Haruni kwa Firauni na waheshimiwa wake, kwa Ishara zetu. Wakatakabari, na wakawa kaumu wahalifu.
(76) Basi ilipowajia haki kutoka kwetu, walisema: Hakika huu ni uchawi ulio dhahiri.
(77) Akasema Musa, "Je, mnasema hivi juu ya haki ilipowajia? Je, huu ni uchawi? Na wachawi hawafanikiwi!"
(78) Wakasema: Je, umetujia ili utuachishe tuliyowakuta nayo baba zetu, na mpate nyinyi wawili ukubwa katika ardhi? Wala sisi hatuwaamini nyinyi.
(79) Na Firauni akasema: Nileteeni kila mchawi ajuaye zaidi!
(80) Basi walipokuja wachawi hao, Musa akawaambia: Vitupeni mnavyovitupa!
(81) Basi walipotupa, Musa akasema, "Mliyoleta ndiyo uchawi. Hakika Mwenyezi Mungu ataubatilisha. Hakika Mwenyezi Mungu hayatengenezi matendo ya waharibifu.
(82) Na Mwenyezi Mungu huihakikisha haki kwa maneno yake, hata wakichukia wahalifu.
(83) Basi hawakumwamini Musa isipokuwa baadhi ya vijana kutoka kwa kaumu yake, kwa kumwogopa Firauni na wakuu wao wasiwatese. Kwani hakika Firauni alikuwa jeuri katika ardhi. Na kwa yakini alikuwa miongoni mwa waliopita kiasi.
(84) Na Musa alisema: Enyi kaumu yangu! Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu, basi mtegemeeni Yeye, ikiwa nyinyi ni Waislamu.
(85) Wakasema: Tunamtegemea Mwenyezi Mungu. Ewe Mola wetu Mlezi! Usitufanye wenye kutiwa majaribio na hao kaumu madhalimu.
(86) Na utuokoe kwa rehema yako kutokana na kaumu hawa makafiri.
(87) Na tukamteremshia wahyi Musa na ndugu yake kuwa: Watengenezeeni majumba kaumu yenu katika Misri na zifanyeni nyumba zenu ndimo mahali mwa ibada, na msimamishe Swala, na wabashirie Waumini.
(88) Na Musa akasema: Mola wetu Mlezi! Hakika wewe umempa Firauni na wakuu wake mapambo na mali katika uhai wa dunia. Hivyo wanapoteza watu kutoka kwa njia yako. Mola wetu Mlezi! Zifutilie mbali mali hizo na zifunge nyoyo zao, wasiamini mpaka waione adhabu chungu.
(89) Mwenyezi Mungu akasema: Hakika maombi yenu yamekubaliwa. Basi nyookeni, wala msifuate njia ya wale wasiojua.
(90) Tukawavusha bahari Wana wa Israili, naye Firauni na askari wake wakawafuata kwa dhulma na uadui. Mpaka kuzama kulipomfikia, akasema: Nimeamini kuwa hakuna mungu isipokuwa yule ambaye walimwamini Wana wa Israili, na mimi ni miongoni mwa Waislamu.
(91) Je, sasa? Na ilhali uliasi kabla yake na ukawa miongoni mwa waharibifu?
(92) Leo basi, tutakuokoa kwa mwili wako, ili uwe Ishara kwa wale walio nyuma yako. Na hakika watu wengi wameghafilika na Ishara zetu.
(93) Na hakika tuliwaandalia Wana wa Israili makao mema, na tukawaruzuku katika vitu vizuri. Nao hawakuhitalifiana mpaka ilipowafikia elimu. Hakika Mola wako Mlezi atahukumu baina yao Siku ya Qiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.
(94) Na ikiwa uko katika shaka juu yale tuliyokuteremshia, basi waulize wale wasomao Kitabu kabla yako. Kwa yakini imekwisha kujia haki kutoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe kabisa miongoni mwa wenye shaka.
(95) Na kabisa usiwe miongoni mwa wale waliozikadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, ukawa katika waliohasiri.
(96) Hakika wale ambao neno la Mola wako Mlezi limekwisha thibitika juu yao, hawataamini.
(97) Hata kama itawajia kila Ishara, mpaka waione adhabu iliyo chungu.
(98) Basi kwa nini hakikuwepo kijiji kilichoamini, kwa hivyo Imani yake ikakifaa, isipokuwa kaumu ya Yunus? Walipoamini, tukawaondolea adhabu ya hizaya katika uhai wa dunia, na tukawastarehesha kwa muda.
(99) Na angelitaka Mola wako Mlezi, wangeliamini walio katika ardhi wote kwa pamoja. Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?
(100) Na haiwi kwa nafsi kuamini isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Naye hujaalia adhabu juu ya wale wasiotumia akili zao.
(101) Sema: Angalieni yaliyo katika mbingu na ardhi! Na Ishara zote na maonyo hayawafai kitu kaumu wasioamini.
(102) Basi, je, wanangojea jingine isipokuwa kama yale yaliyotokea siku za watu waliopita kabla yao? Sema: Ngojeni! Nami ni pamoja nanyi katika wanaongoja.
(103) Kisha Sisi huwaokoa Mitume wetu na wale walioamini. Ndio kama hivyo, inatustahiki kuwaokoa Waumini.
(104) Sema: Enyi watu! Ikiwa nyinyi mko katika shaka juu ya Dini yangu, basi mimi siwaabudu mnaowaabudu nyinyi badala ya Mwenyezi Mungu. Lakini mimi namwabudu Mwenyezi Mungu anayewafisha. Na nimeamrishwa kwamba niwe miongoni mwa Waumini.
(105) Na kwamba uuelekeze uso wako kwenye Dini ya kweli, kwa unyoofu wala kamwe usiwe katika washirikina.
(106) Na wala usiombe badala ya Mwenyezi Mungu wale ambao hawakufai kitu wala hawakudhuru. Na ukifanya hivyo, basi wewe hakika ni miongoni mwa madhalimu.
(107) Na Mwenyezi Mungu akikugusa kwa madhara, basi hakuna wa kukuondolea isipokuwa Yeye. Na akikutakia heri, basi hakuna wa kurudisha fadhila yake. Humsibu kwayo amtakaye katika waja wake, na Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(108) Sema: Enyi watu! Haki imekwisha wajia kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo, anayeongoka, basi anaongoka kwa faida ya nafsi yake, na anayepotea, basi anapotea kwa hasara ya nafsi yake. Na mimi si mwakilishi juu yenu.
(109) Na wewe fuata yale yanayofunuliwa kwako kwa wahyi. Na vumilia mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu, na Yeye ndiye mbora wa mahakimu.