(1) Enyi mlioamini! Timizeni mapatano. Mmehalalishiwa wanyama wa kufugwa, isipokuwa wale mnaosomewa. Lakini msihalalishe kuwinda hali ya kuwa mko katika Ihram. Hakika, Mwenyezi Mungu anahukumu apendavyo.
(2) Enyi mlioamini! Msivunje alama za Dini, za Mwenyezi Mungu wala mwezi mtakatifu, wala wanyama wanaopelekwa Makka kama zawadi kuchinjwa, wala wale wanaotiwa vigwe, wala wale wanaoelekea kuiendea Nyumba Takatifu, wakitafuta fadhila kutoka kwa Mola wao Mlezi na radhi. Na mkishatoka katika Ihram, basi windeni. Wala kuwachukia watu kwa kuwa waliwazuia kuufikia Msikiti mtakatifu kusiwapelekeeni kuwafanyia uadui. Na saidianeni katika wema na uchamungu. Wala msisaidiane katika dhambi na kupita mipaka. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
(3) Mmeharimishiwa nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na kile kilichochinjwa kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na yule aliyekufa kwa kunyongeka koo. Na yule aliyekufa kwa kupigwa, na yule aliyekufa kwa kuanguka, na yule aliyekufa kwa kupigwa pembe, na yule aliyeliwa na mnyama, isipokuwa mkimdiriki kumchinja, na yule aliyechinjiwa masanamu, na ni haramu kupiga ramli. Hayo yote ni kupita mipaka. Leo wale waliokufuru wamekata tamaa na Dini yenu; basi msiwaogope, bali niogopeni Mimi. Leo nimewakamiliishia Dini yenu, na nimewatimizia neema yangu, na nimeridhia Uislamu uwe ndiyo Dini yenu. Na mwenye kulazimishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(4) Wanakuuliza ni nini wamehalalishiwa? Sema: Mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri na mlichowafundisha wanyama kukiwinda. Mnawafundisha alivyowafunzeni Mwenyezi Mungu. Basi kuleni katika kile walichowakamatia, na mkisomee jina la Mwenyezi Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.
(5) Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha wale waliopewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu, mtakapowapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya zinaa na kila mtu, wala na mpenzi asiyekuwa katika ndoa. Na mwenye kuikufuru Imani, bila shaka matendo yake yameharibika, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye hasara.
(6) Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Sala, basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake katika vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba, basi jisafisheni. Na mkiwa wagonjwa au katika safari, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi likusudieni vumbi lililo nzuri, na pakeni nyuso zenu na mikono yenu katika hilo. Hapendi Mwenyezi Mungu kuwatia katika uzito, bali anataka kuwatakasa na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru.
(7) Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu, na agano lake alilofungamana nanyi, mliposema: Tumesikia na tumetii. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua sana yaliyomo ndani ya vifua.
(8) Enyi mlioamini! Kuweni wasimamao madhubuti kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, wenye kushuhudia kwa haki. Na wala kamwe kusiwapelekee kuchukiana na watu kutofanya uadilifu. Fanyeni uadilifu. Hivyo ndivyo kuwa karibu mno na uchamungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.
(9) Mwenyezi Mungu amewaahidi wale walioamini na wakatenda mema kwamba wana kufutiwa dhambi na malipo makubwa.
(10) Na wale waliokufuru na wakazikadhibisha Ishara zetu, hao ndio wenza wa Jahiim.
(11) Enyi mlioamini! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, walipotaka watu kuwanyooshea mikono yao, naye akaizuia mikono yao kuwafikia. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu, basi na wategemee Waumini.
(12) Na hakika Mwenyezi Mungu alichukua agano la Wana wa Israili. Na tukawatumia kutokana nao wakuu kumi na wawili. Na Mwenyezi Mungu akasema: Kwa yakini Mimi niko pamoja nanyi. Mkisimamisha Swala, na mkatoa Zaka, na mkawaamini Mitume wangu, na mkawasaidia, na mkamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, hapana shaka nitawafutia mabaya yenu na nitawaingiza katika mabustani yapitayo mito chini yake. Kwa hivyo mwenye kukufuru miongoni mwenu baada ya hayo, basi bila ya shaka atakuwa amepotea njia iliyo sawa.
(13) Basi kwa sababu ya kuvunja kwao agano lao, tuliwalaani, na tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu. Wanayabadilisha maneno kutoka pahali pake, na walisahau sehemu katika yale waliyokumbushwa kwayo. Na huachi kutambua hiyana kutoka kwao, isipokuwa wachache miongoni mwao. Basi wasamehe na uwaache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.
(14) Na kutoka kwa wale waliosema: Sisi ni Manasara, tulichukua agano lao, lakini wakasahau sehemu katika yale waliyokumbushwa kwayo. Kwa hivyo tukaweka kati yao uadui na chuki mpaka Siku ya Qiyama. Na hapo Mwenyezi Mungu atawaambia yale waliyokuwa wakiyafanya.
(15) Enyi Watu wa Kitabu! Hakika amekwisha wajia Mtume wetu anayewabainishia mengi katika yale mliyokuwa mkiyaficha katika Kitabu, na anayaacha mengi. Bila shaka imekwisha wajia kutoka kwa Mwenyezi Mungu nuru na Kitabu kilicho wazi.
(16) Mwenyezi Mungu huwaongoa kwacho wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza mbalimbali na kuwapeleka kwenye nuru kwa idhini yake, na huwaongoa kwenye Njia iliyonyooka.
(17) Hakika wamekufuru wale waliosema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryam. Sema: Basi ni nani mwenye kumiliki chochote mbele ya Mwenyezi Mungu ikiwa Yeye angetaka kumwangamiza Masihi mwana wa Maryamu, na mama yake, na wote waliomo katika ardhi? Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu. Huumba apendavyo. Na Mwenyezi Mungu anao uweza juu ya kila kitu.
(18) Na Mayahudi na Wakristo walisema: Sisi ni wana wa Mwenyezi Mungu na vipenzi vyake. Sema: Basi kwa nini anawaadhibu kwa sababu ya dhambi zenu? Bali nyinyi ni wanadamu tu kama wale wengine aliowaumba. Humfutia dhambi amtakaye na humuadhibu amtakaye. Na ni wa Mwenyezi Mungu tu ufalme wa mbingu na ardhi. Na marejeo ni kwake Yeye.[1]
[1] Hii ni hoja ya nguvu zaidi katika kubatilisha yale wanayosema Wakristo na Wayahudi kwamba wao ni wana wa Mwenyezi Mungu. Nayo ni kwamba mwana wa Mwenyezi Mungu hana dhambi hata moja; mbali na kuadhibiwa kwayo; kwa sababu mwana huwa wa aina moja na baba yake. Na kwa sababu wao huadhibiwa kwa madhambi yao, basi wao si wana wa Mwenyezi Mungu. (Nadhm Addurar, cha Albaqaaii)
(19) Enyi Watu wa Kitabu! Bila ya shaka amewajia Mtume wetu akiwabainishia katika wakati usiokuwa na Mitume, ili msije mkasema: Hakutujia mbashiri wala mwonyaji. Basi kwa hakika amekwisha wajia mbashiri na mwonyaji. Na Mwenyezi Mungu ana uweza juu ya kila kitu.
(20) Na pale Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu, alipowateua Manabii kati yenu, na akawafanya watawala, na akawapa yale ambayo hakuwapa wowote katika walimwengu.
(21) Enyi watu wangu! Ingieni katika nchi takatifu ambayo Mwenyezi Mungu amewaandikia. Wala msirudi nyuma, mkawa wenye kuhasirika.
(22) Wakasema: Ewe Musa! Hakika, huko wako watu majabari. Nasi kamwe hatutaingia humo mpaka wao watoke humo. Wakitoka humo, hapo hakika tutaingia.
(23) Wanaume wawili miongoni mwa wale wanaohofu ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha, wakasema: Waingilieni mlangoni. Na mtakapowaingilia, basi kwa yakini nyinyi mtashinda. Na mtegemeeni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
(24) Wakasema: Ewe Musa! Hakika Sisi hatutaingia humo kamwe maadamu wao wamo humo. Basi nenda wewe na Mola wako Mlezi mkapigane. Sisi hakika tutakaa papa hapa.
(25) Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika mimi similiki isipokuwa nafsi yangu na kaka yangu. Basi tutenge na hawa watu wapotovu.
(26) (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika nchi hiyo wameharimishiwa, kwa muda wa miaka arobaini watakuwa wakitangatanga katika ardhi. Basi wewe usiwasikitikie watu wapotovu.
(27) Na wasomee habari za wana wawili wa Adam kwa haki. Walipotoa mhanga, basi ukakubaliwa wa mmoja wao, na wa mwingine haukukubaliwa. Akasema: Lazima nitakuua. Akasema mwingine: Hakika Mwenyezi Mungu hupokea tu kutoka kwa wachamungu.
(28) Ukininyooshea mkono wako ili uniue, mimi sitakunyooshea mkono wangu ili nikuue. Hakika mimi namhofu Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(29) Hakika Mimi ninataka ubebe dhambi zangu na dhambi zako, ili wewe uwe miongoni mwa wenza wa Moto. Na hayo ndiyo malipo ya wenye kudhulumu.
(30) Basi nafsi yake ikampelekea kumuua kaka yake, na akamuua. Kwa hivyo akawa miongoni mwa waliohasirika.
(31) Hapo Mwenyezi Mungu akamtuma kunguru anayefukua katika ardhi ili amwonyeshe jinsi ya kuuzika mwili wa kaka yake. Akasema: Ole wangu! Nimeshindwa kuwa kama kunguru huyu nikauzika mwili wa kaka yangu? Basi akawa miongoni mwa wenye kujuta.
(32) Kwa sababu ya hayo, tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba mwenye kuiua nafsi bila ya nafsi hiyo kuiua nyingine, au kufanya uharibifu katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kuiweka hai, basi ni kama amewaoka watu wote. Na hakika walikwishawajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha hakika wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.
(33) Basi malipo ya wale wanaompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakawania kufanya uharibifu katika nchi, ni kuuawa, au kusulibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchini. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera wana adhabu kubwa.
(34) Isipokuwa wale waliotubia kabla hamjawatia nguvuni. Basi jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(35) Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na tafuteni njia ya kumfikia. Na wanieni kwa juhudi katika njia yake ili mfaulu.
(36) Hakika wale waliokufuru lau yangelikuwa yao ni yote yaliyo katika dunia, na mfano wake pamoja na hayo, ili watoe kwayo fidia ya kuepukana na adhabu ya Siku ya Qiyama, yasingelikubaliwa kutoka kwao; na wana adhabu chungu.
(37) Wanataka kwamba watoke Motoni, lakini hawawezi kutoka humo, na wana adhabu inayodumu.
(38) Na mwizi mwanamume na mwizi mwanamke, ikateni mikono yao, yakiwa ni malipo ya waliyoyachuma, ndiyo adhabu ya mfano itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(39) Lakini mwenye kutubia baada ya dhuluma yake, na akatengenea, basi Mwenyezi Mungu ataipokea toba yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(40) Je hukujua ya kwamba Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu na ardhi? Humuadhibu amtakaye, na humsamehe amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(41) Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wale wanaokimbilia kukufuru, miongoni mwa wale waliosema kwa vinywa vyao, "Tumeamini", na hali nyoyo zao hazikuamini, na miongoni mwa wale waliotubia na kurudi kwa Mwenyezi Mungu (Mayahudi), wanaosikiliza sana uongo, wanaowasikiliza sana kaumu wengine ambao hawajakujia. Wao huyabadilisha maneno baada ya kuwekwa pahali pake. Wanasema, "Mkipewa haya, basi yachukueni, na msipopewa haya, tahadharini." Na yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumfitini, basi huwezi kuwa na uwezo kwa ajili yake mbele ya Mwenyezi Mungu. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu hataki kuzisafisha nyoyo zao. Wana hizaya katika dunia, na Akhera wana adhabu kubwa.
(42) Hao ni wasikilizaji sana wa uwongo, na ni walaji mno vya haramu! Basi wakikujia, wahukumu baina yao au wapuuze. Na ukiwapuuza, basi wao hawatakudhuru kitu. Na ukiwahukumu, basi hukumu baina yao kwa uadilifu. Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda waadilifu.
(43) Na vipi wanakufanya kuwa hakimu wao ilhali wanayo Taurati yenye hukumu za Mwenyezi Mungu ndani yake? Kisha baada ya hayo wanageuka. Na hao si Waumini.
(44) Hakika Sisi tuliiteremsha Taurati yenye uwongofu na nuru, ambayo kwayo Manabii walionyenyekea kiislamu, na wachamngu, na wanachuoni, waliwahukumu Mayahudi; kwani walikabidhiwa kukihifadhi Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Nao wakawa ni mashahidi juu yake. Basi msiwaogope watu, bali niogopeni Mimi. Wala msibadilishe Aya zangu kwa thamani chache. Na wasiohukumu kwa aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio makafiri.
(45) Na humo tuliwaandikia ya kwamba nafsi kwa nafsi, na jicho kwa jicho, na pua kwa pua, na sikio kwa sikio, na jino kwa jino, na kwa majeraha ni kisasi. Lakini kuitoa kama sadaka, basi hiyo ni kafara kwake. Na yule asiyehukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.
(46) Na tukawafuatishia nyuma yao, Isa bin Maryam akiyasadikisha yale yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na tukampa Injili iliyomo ndani yake uwongofu, na ni nuru, na inayosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake katika Taurati, na ni uwongofu na mawaidha kwa wachamungu.
(47) Basi na wahukumu Watu wa Injili kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu ndani yake. Na mwenye kutohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio waliopita mipaka.
(48) Na tulikuteremshia wewe Kitabu hiki kwa haki, kinachosadikisha yale yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda. Basi hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao ukaacha haki iliyokujia. Kila mmoja katika nyinyi tumemwekea sheria yake na njia yake. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelitaka, angeliwafanya nyote umma mmoja, lakini ni ili awajaribu kwa yale aliyowapa. Basi yakimbilieni mambo ya heri. Kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo yenu nyote, kisha atawaambia yale mliyokuwa mkihitalifiana juu yake.
(49) Na hukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao. Na watahadhari wasije wakakufitini ukaacha baadhi ya yale aliyokuteremshia Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi jua kwamba hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwasibu kwa baadhi ya dhambi zao. Na hakika wengi miongoni mwa watu ni wenye kupita mipaka.
(50) Je, wanataka hukumu za Kijahiliya? Na ni nani aliye mzuri zaidi katika kuhukumu kuliko Mwenyezi Mungu kwa watu wenye yakini?
(51) Enyi mlioamini! Msiwafanye Mayahudi na Wakristo kuwa ni marafiki wandani. Wao kwa wao ni marafiki wandani. Na mwenye kuwafanya marafiki wandani miongoni mwenu, basi huyo hakika ni miongoni mwao. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu wenye kudhulumu.
(52) Utawaona wale wenye maradhi katika nyoyo zao wanakimbilia kwao wakisema: Tunahofu kusibiwa na mabadiliko. Basi huenda Mwenyezi Mungu akaleta ushindi au jambo jingine kutoka kwake, na wakawa kwa yale waliyoyaficha katika nafsi zao ni wenye kujuta.
(53) Na wale walioamini wanasema: Je, hawa ndio wale walioapa kwa Mwenyezi Mungu viapo vyao vikali mno kuwa wao hakika wako pamoja nanyi? Vitendo vyao viliharibika, na wakawa wamehasirika.
(54) Enyi mlioamini! Atakayeiacha Dini yake miongoni mwenu, basi Mwenyezi Mungu atakuja leta watu anaowapenda nao wanampenda, wanyenyekevu kwa Waumini na wenye nguvu juu ya makafiri, wanapigania Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawaogopi lawama ya mwenye kulaumu. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua vyema.
(55) Hakika rafiki yenu mwandani ni Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, ambao husimamisha Swala na hutoa Zaka, nao wanarukuu.
(56) Na mwenye kumfanya rafiki wandani Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wale walioamini, basi hakika kundi la Mwenyezi Mungu ndio wenye kushinda.
(57) Enyi mlioamini! Msiwafanye marafiki wandani wale walioifanyia kejeli na mchezo Dini yenu miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu, na makafiri wengine. Na mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
(58) Na mnapoiadhinia Swala, wao wanaifanyia masihara na mchezo. Hayo ni kwa sababu wao ni kaumu wasiokuwa na akili.
(59) Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Je, mnatuchukia isipokuwa tu kwamba tulimuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa na yale yaliyoteremshwa kabla, na kwa kuwa wengi wenu ni wapotofu?
(60) Sema: Je, niwaambie lililo baya zaidi kuliko hilo katika malipo mbele ya Mwenyezi Mungu? Ni yule ambaye Mwenyezi Mungu alimlaani na akamkasirikia, na akawafanya miongoni mwao manyani na nguruwe, na wakamuabudu Shetani. Hao ndio wenye mahali pabaya zaidi na waliopotea zaidi njia iliyo sawa.
(61) Na wanapowajia, husema, "Tumeamini." na ilhali hakika waliingia na ukafiri wao, nao wameshatoka nao pia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema yale wanayoyaficha.
(62) Na utawaona wengi miongoni mwao wanakimbilia kwenye dhambi, na kupita mipaka, na ulaji wao vya haramu. Ni maovu mno hayo wayatendayo!
(63) Mbona hao wanachuoni wa Kiyahudi na makuhani wao hawawakatazi kusema kwao dhambi, na kula kwao vya haramu? Ni maovu mno hayo wayafanyayo!
(64) Na Mayahudi walisema: Mkono wa Mwenyezi Mungu umefumba. Mikono yao ndiyo iliyofumba, na wamelaaniwa kwa sababu ya waliyoyasema. Bali mikono yake iko wazi. Hutoa apendavyo. Kwa yakini yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na kufuru. Na Sisi tumewatilia uadui na chuki baina yao mpaka Siku ya Qiyama. Kila mara wanapowasha moto wa vita, Mwenyezi Mungu anauzima. Na wanajitahidi kuleta uharibifu katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu hawapendi waharibifu.
(65) Na lau kuwa Watu wa Kitabu wangeliamini na wakamcha Mungu, hapana shaka tungeliwafutia mabaya yao, na tungeliwaingiza katika Mabustani yenye neema.
(66) Na lau kuwa wangeliisimamisha Taurati na Injili na yote waliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wao Mlezi, basi hapana shaka wangelikula vya juu yao na vya chini ya miguu yao. Wapo watu miongoni mwao walio sawa, lakini wengi wao wanayoyafanya ni mabaya mno.
(67) Ewe Mtume! Fikisha uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi. Na ikiwa hufanyi, basi hutakuwa umefikisha ujumbe wake. Na Mwenyezi Mungu atakulinda na watu. Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu ya makafiri.
(68) Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Hamna lenu jambo mpaka muisimamishe Taurati na Injili na yote mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na hakika uliyoteremshiwa wewe kutoka kwa Mola wako Mlezi yatawazidishia wengi katika wao uasi na ukafiri. Basi usiwasikitikie kaumu ya makafiri.
(69) Hakika wale walioamini, na wale waliotubia (yani Mayahudi) na Masabii na Wakristo, mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na akatenda mema, basi hawatakuwa na hofu juu yao wala hawatahuzunika.
(70) Hakika, tulichukua agano la Wana wa Israili, na tukawatumia Mitume. Kila alipowajia Mtume kwa yale zisiyoyapenda nafsi zao, wengine wao waliwakanusha, na wengine wao wakawaua.
(71) Na wakadhani kuwa hapatakuwa majaribio; basi wakawa vipofu na viziwi. Kisha Mwenyezi Mungu akawapokelea toba zao. Kisha tena wengi katika wao wakawa vipofu na viziwi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona vyema hayo wayatendayo.
(72) Hakika, wamekufuru wale waliosema: Hakika, Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryam! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani, mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu amemharimishia Pepo, na pahali pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wowote wa kuwanusuru.
(73) Hakika, wamekufuru wale waliosema: Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa watatu. Hali hakuna mungu isipokuwa Mungu Mmoja tu. Na ikiwa hawayaachi hayo wanayoyasema, basi kwa yakini itawagusa wale waliokufuru miongoni mwao adhabu chungu.
(74) Je, hawatubii kwa Mwenyezi Mungu na wakamwomba awafutie dhambi? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(75) Masihi mwana wa Maryam si chochote isipokuwa ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyowabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyogeuzwa.
(76) Sema: Je, mnawaabudu, badala ya Mwenyezi Mungu, wale ambao hawawamilikii kudhuru wala kunufaisha? Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua vyema.
(77) Sema: Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu bila ya haki. Wala msifuate matamanio ya kaumu waliokwisha potea tangu zamani, na wakawapoteza wengi, na wenyewe wakapotea njia iliyo sawa.
(78) Walilaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa Wana wa Israili kwa ulimi wa Daud na Isa mwana wa Maryamu. Hayo ni kwa sababu waliasi na wakawa wanapita mipaka.
(79) Walikuwa hawakatazani maovu waliyokuwa wakiyafanya. Hakika ni maovu mno waliyokuwa wakiyafanya!
(80) Utawaona wengi miongoni mwao wanafanya urafiki wandani na wale waliokufuru. Hakika ni maovu mno ziliyozitanguliza nafsi zao hata Mwenyezi Mungu akawakasirikia, nao watadumu katika adhabu.
(81) Na lau wangelikuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu, na Nabii huyu, na yale yaliyoteremshwa kwake, wasingeliwafanya hao kuwa marafiki wandani. Lakini wengi miongoni mwao ni wapitao mipaka.
(82) Hakika utawakuta walio na uadui mkubwa mno kuliko watu wote juu ya wale walioamini ni Mayahudi na wale walioshirikisha. Na hakika utawakuta wale wao walio karibu mno kwa mapenzi kwa wale walioamini ni wale waliosema: Hakika Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwamba wao hawafanyi kiburi.
(83) Na wanaposikia yale yaliyoteremshwa kwa Mtume, utayaona macho yao yanamiminika machozi kwa sababu ya haki waliyoitambua. Wanasema: Mola wetu Mlezi! Tumeamini. Basi tuandike pamoja na wanaoshuhudia.
(84) Na kwa nini tusimwamini Mwenyezi Mungu na haki iliyotujia, na hali tunatumai Mola wetu Mlezi atuingize pamoja na kaumu ya walio wema?
(85) Basi Mwenyezi Mungu akawalipa kwa yale waliyoyasema, Mabustani yapitayo mito kwa chini yake, wadumu humo. Na hayo ndiyo malipo ya wafanyao wema.
(86) Na wale waliokufuru na wakazikadhibisha ishara zetu, hao ndio wenza wa Jahiim.
(87) Enyi mlioamini! Msiviharimishe vizuri alivyowahalalishia Mwenyezi Mungu, wala msivuke mipaka. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wavukao mipaka.
(88) Na kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu, vya halali na vizuri. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye nyinyi mnamwamini.
(89) Mwenyezi Mungu hawachukulii dhambi kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atawachukulia dhambi kwa mnavyoapa kweli kweli kwa makusudio. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha wastani mnachowalisha ahali zenu, au kuwavisha, au kumkomboa mtumwa. Na asiyepata, basi na afunge siku tatu. Hii ndiyo kafara ya viapo vyenu mnapoapa. Na hifadhini viapo vyenu. Namna hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kushukuru.
(90) Enyi mlioamini! Bila ya shaka mvinyo, na kamari, na masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya Shetani. Basi jiepusheni navyo, ili mfaulu.
(91) Hakika Shetani anataka kutia kati yenu uadui na chuki katika mvinyo na kamari, na awazuie kumkumbuka Mwenyezi Mungu na kuswali. Basi je, mmeacha?
(92) Na mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume, na tahadharini. Na ikiwa mtageuka, basi hakika jueni ya kuwa juu ya Mtume wetu ni kufikisha ujumbe kuliko wazi.
(93) Hakuna ubaya juu ya wale walioamini na wakatenda mema kwa vile walivyovila (zamani) maadamu wakimcha Mungu na wakiamini na wakitenda mema, kisha wakamcha Mungu, na wakaamini, kisha wakamcha Mungu na wakafanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao mazuri.
(94) Enyi mlioamini! Hakika Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa kitu kidogo katika mawindo inayowafikia mikono yenu na mikuki yenu, ili Mwenyezi Mungu amjue mwenye kumhofu katika ghaibu. Kwa hivyo, mwenye kuvuka mipaka baada ya hayo, basi ana adhabu chungu.
(95) Enyi mlioamini! Msiwaue mawindo hali ya kuwa mko katika Ihram (ya Hijja au 'Umra). Na miongoni mwenu atakayemuua makusudi, basi malipo yake yatakuwa ni kuchinja kilicho sawa na alichokiua, katika mifugo, kama wanavyohukumu hivyo waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al-Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga, ili aonje ubaya wa jambo lake hili. Mwenyezi Mungu amekwisha yafuta yaliyopita. Lakini atakayefanya tena, Mwenyezi Mungu atamwadhibu vikali. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye nguvu, na Mwenye kuadhibu vikali.
(96) Mmehalalishiwa mawindo ya baharini na kuyala, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharimishiwa mawindo barani maadamu mko katika Ihram. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye mtakusanywa kwake.
(97) Mwenyezi Mungu ameifanya Al-Kaaba, hii Nyumba Tukufu, kuwa ya kuwakimu watu, na Miezi Mitakatifu, na dhabihu walioletwa Makka kama zawadi, na dhabihu waliofungwa vigwe. Hayo ni ili mjue ya kwamba hakika Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika mbingu na yaliyo katika ardhi, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
(98) Jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(99) Hakuna kilicho juu ya Mtume isipokuwa kufikisha ujumbe tu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnachokidhihirisha na mnachokificha.
(100) Sema: Haviwi sawa viovu na vizuri hata kama utapendezwa na wingi wa viovu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, enyi wenye akili, ili mfaulu.
(101) Enyi mlioamini! Msiulize kuhusu mambo ambayo mkidhihirishiwa, yatawachukiza. Na mkiuliza juu yake wakati inateremshwa Qur-ani, mtadhihirishiwa hayo. Mwenyezi Mungu amesamehe hayo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mpole.
(102) Hakika, walikwisha yauliza kaumu ya kabla yenu, kisha wakawa wenye kuyakufuru.
(103) Mwenyezi Mungu hakuweka uharamu wowote juu ya "Bahira" wala "Saiba" wala "Wasila" wala "Hami". Lakini wale waliokufuru ndio humzulia uongo Mwenyezi Mungu, na wengi wao hawatumii akili.
(104) Na wanapoambiwa: Njooni kwenye yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, na kwa Mtume, wanasema: Yanatutosha tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawajui kitu wala hawakuongoka?
(105) Enyi mlioamini! Kilicho lazima juu yenu ni nafsi zenu. Hatawadhuru mwenye kupotoka ikiwa nyinyi mmeongoka. Ni kwa Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo yenu nyote; kisha atawaambia yale mliyokuwa mkiyatenda.
(106) Enyi mlioamini! Yanapomfikia mauti mmoja wenu na akataka kutoa wasia, basi wawepo mashahidi wawili miongoni mwenu ambao ni waadilifu. Na mnapokuwa katika safari, na msiba wa mauti ukawasibu, basi washuhudie wengineo wawili wasiokuwa katika nyinyi. Mtawazuia wawili hao baada ya Swala na waape kwa Mwenyezi Mungu, mkitilia shaka, wakisema: Hatutopokea thamani yoyote kwa haya hata kwa ajili ya jamaa; na wala hatutaficha ushahidi wa Mwenyezi Mungu; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa wenye dhambi.
(107) Lakini ikigundulika kuwa wawili hao wamestahiki dhambi, basi wawili wengineo kutokana na warithi wenye kudai haki washike mahali pa wale wa mwanzo. Nao waape kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hakika ushahidi wetu ni wa haki zaidi kuliko ushahidi wa wale. Na sisi hatujafanya dhambi; hakika hapo tutakuwa miongoni mwa waliodhulumu.
(108) Hivyo ni karibu zaidi na kwamba watatoa ushahidi ulio sawa au wataogopa visije vikaletwa viapo vingine baada ya viapo vyao. Na mcheni Mwenyezi Mungu na msikie. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu ya wavukao mipaka.
(109) Siku ambayo Mwenyezi Mungu atawakusanya Mitume na awaambie: Mlijibiwa nini? Watasema: Hatujui; hakika Wewe ndiwe Mwenye kujua yote yaliyofichikana
(110) Na pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa bin Maryamu! Kumbuka neema yangu juu yako, na juu ya mama yako, nilipokutia nguvu kwa Roho Mtakatifu, ukazungumza na watu katika utoto na utu uzimani. Na nilivyokufunza kuandika na hekima na Taurati na Injili. Na ulipokuwa unatengeneza kutoka katika udongo kama umbo la ndege, kwa idhini yangu, kisha ukapuliza ndani yake na likawa ndege kwa idhini yangu; na ulipowaponya vipofu na wakoma kwa idhini yangu; na ulipowafufua wafu kwa idhini yangu; na nilipokukinga na Wana wa Israili ulipowajia na hoja zilizo wazi, na wakasema wale waliokufuru miongoni mwao: Haya si lolote isipokuwa uchawi ulio wazi!
(111) Na nilipowafunulia wahyi Wanafunzi kwamba: "Niaminini Mimi na Mtume wangu." Wakasema: "Tumeamini, na shuhudia kuwa sisi hakika ni Waislamu."
(112) Wanafunzi waliposema: Ewe Isa bin Maryam! Je, Mola wako Mlezi anaweza kututeremshia meza yenye chakula kutoka mbinguni? Akasema: Mcheni Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni Waumini.
(113) Wakasema: Tunataka kula kwayo, na nyoyo zetu zitue, na tujue kwamba umetuambia ukweli, na tuwe miongoni mwa wanaoshuhudia juu ya hilo.
(114) Akasema Isa bin Maryam: Ewe Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wetu! Tuteremshie meza yenye chakula kutoka mbinguni ili kiwe kwetu Sikukuu kwa ajili ya wa mwanzo wetu na wa mwisho wetu, na kiwe ni ishara itokayo kwako. Basi turuzuku, kwani Wewe ndiye mbora zaidi wa wanaoruzuku.
(115) Mwenyezi Mungu akasema: Hakika Mimi nitawateremshia hicho. Lakini yeyote katika nyinyi atakayekufuru baadaye, basi hakika Mimi nitamuadhibu adhabu nisiyomuadhibu yeyote katika walimwengu.
(116) Na pale Mwenyezi Mungu aliposema: Ewe Isa bin Maryamu! Je, wewe ndiye uliwaambia watu: Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa ni miungu wawili badala ya Mwenyezi Mungu? (Isa) akasema: Subhanaka (Wewe umetakasika)! Hainifailii mimi kusema ambayo si haki yangu. Ikiwa nilisema, basi bila ya shaka umekwisha yajua. Wewe unayajua yaliyo ndani ya nafsi yangu, lakini mimi siyajui yaliyo katika nafsi yako. Hakika Wewe ndiye Mwenye kujua vyema yale yaliyofichikana.
(117) Sikuwaambia lolote isipokuwa yale uliyoniamrisha, kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Na mimi nilikuwa shahidi juu yao nilipokuwa miongoni mwao. Na uliponifisha, ukawa Wewe ndiye Muangalizi juu yao. Na Wewe ni shahidi juu ya kila kitu.
(118) Ukiwaadhibu, basi hao ni waja wako. Na ukiwafutia dhambi, basi Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(119) Mwenyezi Mungu akasema: Hii ndiyo Siku ambayo wasemao ukweli utawafaa ukweli wao. Wao wana Mabustani yapitayo mito chini yake. Humo watadumu milele. Mwenyezi Mungu amewawia radhi, nao walimridhia. Huku ndiko kufuzu kukubwa.
(120) Ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi na vilivyo ndani yake. Naye ni Muweza wa kila kitu.