(1) Alif Lam Mim Ra. Hizi ni Ishara za Kitabu. Na yale uliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki. Lakini wengi wa watu hawaamini.
(2) Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziinua mbingu bila ya nguzo mnazoziona, kisha akainuka juu ya Kiti cha Enzi, na akatiisha jua na mwezi, kila kimoja kinakwenda kwa muda maalumu. Anaendesha mambo, na anazipambanua Ishara kwa kina ili mpate kuwa na yakini ya kukutana na Mola wenu Mlezi.
(3) Naye ndiye aliyeikunjua ardhi na akaweka humo milima mathubuti na mito. Na katika kila matunda akafanya jozi mbili la kiume na la kike. Huufunika usiku juu ya mchana. Hakika katika hayo zimo Ishara kwa kaumu wanaotafakari.
(4) Na katika ardhi vimo vipande vilivyokaribiana, na zipo bustani za mizabibu, na mimea mingine, na mitende yenye kuchipua kwenye shina moja na isiyochipua kwenye shina moja, nayo inanyweshwa katika maji yale yale. Na tunaifanya baadhi yao kuwa bora kuliko mengine katika kula. Hakika katika hayo zimo ishara kwa kaumu wanaotia mambo akilini.
(5) Na kama ukistaajabu, basi cha ajabu zaidi ni huo usemi wao: Je, tukishakuwa mchanga, kweli tutakuwa katika umbo jipya? Hao ndio waliomkufuru Mola wao Mlezi. Na hao ndio watakaokuwa na makongwa shingoni mwao, na hao ndio watu wa Motoni. Humo watadumu.
(6) Na wanakuhimiza ulete mabaya kabla ya mazuri, hali ya kuwa zimekwisha pita kabla yao adhabu za kupigiwa mfano. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye msamaha kwa watu juu ya udhalimu wao. Na hakika Mola wako Mlezi ni Mkali wa kuadhibu.
(7) Na wale waliokufuru wanasema: Mbona hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Hakika wewe ni Mwonyaji tu, na kila kaumu ina wa kuwaongoza.
(8) Mwenyezi Mungu anajua mimba abebayo kila cha kike, na kinachopunguka na kuzidi matumboni mwa uzazi. Na kila kitu kwake ni kwa kipimo.
(9) Yeye ndiye Mwenye kujua ya ghaibu na yanayoonekana, Mkubwa, Mtukufu.
(10) Ni sawa anayeficha kauli yake miongoni mwenu na anayeidhihirisha, na anayejibanza usiku na anayetembea jahara mchana.
(11) Kila mtu analo kundi la malaika mbele yake na nyuma yake linamlinda kwa amri ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu habadili yaliyoko kwa kaumu mpaka wabadili wao yaliyomo katika nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anapowatakia kaumu ubaya, basi hakuna cha kuyazuia wala hawana mlinzi yeyote asiyekuwa Yeye.
(12) Yeye ndiye anayewaonyesha umeme kwa hofu na matumaini, na huyaanzisha mawingu mazito.
(13) Na radi inamtakasa Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia, kwa kumhofu. Naye hutuma mapigo ya radi na kumsibu kwayo amtakaye. Nao wanabishana kuhusiana na Mwenyezi Mungu, na Yeye ndiye Mwenye adhabu kali!
(14) Wa kuombwa kweli ni Yeye tu. Na hao wanaowaomba badala yake hawawajibu chochote; bali ni kama mwenye kunyoosha viganja vyake kwenye maji ili yafike kinywani mwake, lakini hayakifikii. Na maombi ya makafiri hayako isipokuwa katika upotovu.
(15) Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi kwa kutii na kwa lazima. Na pia vivuli vyao asubuhi na jioni.
(16) Sema: Ni nani Mola Mlezi wa mbingu na ardhi? Sema: Mwenyezi Mungu. Sema: Basi je, mnawafanya wenginewe badala yake kuwa ni walinzi, nao hawajimilikii manufaa yoyote wala madhara? Sema: Je, kipofu na mwenye kuona huwa sawa? Au je, huwa sawa giza na mwangaza? Au wamemfanyia Mwenyezi Mungu washirika walioumba kama alivyoumba Yeye, na viumbe hivyo vikawachanganyikia? Sema: Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa kila kitu. Na Yeye ni Mmoja, Mwenye kushinda!
(17) Ameteremsha maji kutoka mbinguni. Na mabonde yakamiminika maji kwa kiasi chake. Na mafuriko yakabeba mapovu yaliyokusanyika juu yake. Na kutokana na wanavyoyeyusha katika moto kwa kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Namna hivyo Mwenyezi Mungu ndivyo anavyopiga mifano ya haki na batili. Basi lile povu linapita kama takataka tu. Na ama kinachowafaa watu hubakia kwenye ardhi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyopiga mifano.
(18) Wale waliomuitikia Mola wao Mlezi watapata mazuri. Na wale ambao hawakumuitikia, hata wangelikuwa na vyote vilivyomo katika ardhi na mfano wa hivyo, bila ya shaka wangelivitoa kujikombolea! Hao wana hesabu mbaya kabisa, na makao yao ni Jahannamu. Na hapo ni pahali pabaya mno pa kupumzikia!
(19) Je, anayejua ya kwamba yale yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi ni Haki ni sawa na aliye kipofu? Hakika wenye akili tu ndio wanaokumbuka.
(20) Wale ambao wanatimiza ahadi ya Mwenyezi Mungu, wala hawavunji agano.
(21) Na wale ambao huyaunga yale aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanamhofu Mola wao Mlezi, na wanaiogopa hesabu mbaya.
(22) Na ambao husubiri kwa kuutaka uso wa Mola wao Mlezi, na wakasimamisha Swala, na wakatoa, kwa siri na kwa uwazi, katika vile tulivyowapa; na wakayaondoa mabaya kwa mazuri. Hao ndio wana malipo ya Nyumba ya Akhera.
(23) Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na wale waliotengenea miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika watawaingilia katika kila mlango.
(24) (Wakiwaambia) Assalamu Alaikum (Amani iwe juu yenu), kwa sababu ya vile mlivyosubiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.
(25) Na wale wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata yale aliyoamrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya uharibifu katika ardhi, hao wana laana, na wana Nyumba mbaya.
(26) Mwenyezi Mungu humkunjulia riziki amtakaye, na humkunjia kwa kipimo. Na waliufurahia uhai wa dunia. Na uhai wa dunia kwa kulinganisha na Akhera si kitu isipokuwa ni starehe ndogo.
(27) Na wanasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye, na humwongoa anayerudi kwake.
(28) Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Sikilizeni! Kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu ndiyo nyoyo hutua!
(29) Wale walioamini na wakatenda mema watakuwa na raha na marejeo mazuri.
(30) Ndivyo hivyo tulivyokutuma kwa umma ambao wamekwsiha pita kabla yao umma nyingine, ili uwasomee yale tuliyokufunulia, na wao wanamkufuru Rahmani (Mwingi wa Rehema)! Sema: Yeye ndiye Mola wangu Mlezi. Hakuna mungu isipokuwa Yeye. Juu yake nimetegemea, na kwake ndiyo marejeo!
(31) Na kama ingelikuwako Qur-ani inayoendeshewa milima, na kupasuliwa kwayo ardhi, na kusemeshwa kwayo wafu, (basi ingelikuwa Qur-ani hii). Bali mambo yote ni ya Mwenyezi Mungu. Je, hawajajua wale walioamini kwamba lau kuwa Mwenyezi Mungu angependa bila ya shaka angeliwaongoa watu wote? Na wale waliokufuru hawaachi kusibiwa na balaa kwa yale waliyoyatenda, au ikawateremkia karibu na nyumbani kwao, mpaka ije ahadi ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu havunji miadi yake.
(32) Na hakika walifanyiwa kejeli Mitume waliokuwa kabla yako. Na nikawapururia wale waliokufuru, kisha nikawashika! Basi ilikuwaje adhabu yangu!
(33) Je, anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma...? Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu kuwa na washirika! Sema watajeni. Au ndiyo mnampa habari ya yale asiyoyajua katika ardhi, au ni maneno matupu tu? Bali wale waliokufuru wamepambiwa njama zao na wamezuiliwa njia ya sawasawa. Na yule ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza, basi hana wa kumwongoa yeyote.
(34) Wana adhabu katika uhai wa dunia, na adhabu ya Akhera hakuna shaka ndiyo ngumu zaidi. Na wala hawatakuwa na wa kuwalinda kutokana na Mwenyezi Mungu.
(35) Mfano wa Bustani waliyoahidiwa wachamungu, kwa chini yake inapita mito, chakula chake ni cha daima, na pia kivuli chake. Huu ndio mwisho wa wale waliomcha Mungu. Na mwisho wa makafiri ni Moto.
(36) Na wale tuliowapa Kitabu wanayafurahia yale yaliyoteremshwa kwako. Na katika makundi mengine wapo wanaoyakataa baadhi yake. Sema: Hakika nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu tu, na wala nisimshirikishe. Kwake Yeye ndiko ninaitia na kwake Yeye ndiko marejeo.
(37) Na ndivyo hivyo tumeiteremsha (Qur-ani hii kuwa ni) hukumu kwa lugha ya Kiarabu. Na ukifuata matamanio yao baada ya elimu hii iliyokujia, hutakuwa na rafiki yeyote wala mlinzi kando na Mwenyezi Mungu.
(38) Na hakika Sisi tulikwisha watuma Mitume kabla yako, na tukawafanya wawe na wake na dhuria. Na haikuwa kwa Mtume yeyote kuleta ishara isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Kila kipindi kina hukumu yake iliyoandikwa.
(39) Mwenyezi Mungu hufuta na huthibitisha ayatakayo. Na asili ya hukumu zote zilizoandikwa iko kwake.
(40) Na ikiwa tutakuonyesha baadhi ya yale tuliyowaahidi au tukakufisha kabla yake, juu yako wewe ni kufikisha ujumbe tu na juu yetu ni hesabu.
(41) Je, hawakuona kwamba tunaijia ardhi tukiipunguza kutokea nchani mwake? Na Mwenyezi Mungu huhukumu, na hakuna wa kurekebisha hukumu yake, naye ni Mwepesi wa kuhesabu.
(42) Na walipanga njama wale waliokuwa kabla yao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye njama zote. Yeye anajua kile inachochuma kila nafsi. Na makafiri watakuja jua ni ya nani nyumba ya mwisho Akhera!
(43) Na wale waliokufuru wanasema: Wewe hukutumwa. Sema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi baina yangu na nyinyi, na pia yule mwenye elimu ya Kitabu.