57 - Surat Al-Hadid ()

|

(1) Kinamsabihi kumtakasa Mwenyezi Mungu kila kilichomo ndani ya mbingu na ardhi. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(2) Yeye ndiye Mwenye ufalme wa mbingu na ardhi. Anahuisha na anafisha. Na Yeye ni Mwenye uwezo mno wa kila kitu.

(3) Yeye ndiye wa Mwanzo na ndiye wa Mwisho, naye ndiye wa Dhahiri na wa Siri, naye ndiye ajuaye zaidi kila kitu.

(4) Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita; kisha akainuka juu ya Kitu cha enzi. Anayajua yanayoingia katika ardhi na yanayotoka humo, na yanayoteremka kutoka mbinguni, na yanayopanda humo. Naye yu pamoja nanyi popote mlipo. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyaona mno mnayoyatenda.

(5) Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake. Na mambo yote yanarejeshwa kwa Mwenyezi Mungu.

(6) Anaingiza usiku katika mchana, na anaingiza mchana katika usiku. Na Yeye ni Mwenye kuyajua mno yaliyomo vifuani.

(7) Muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake; na toeni katika alivyokufanyeni nyinyi kuwa ni waangalizi wake. Basi wale walioamini miongoni mwenu, na wakatoa, wana malipo makubwa.

(8) Na mna nini hata hamumuamini Mwenyezi Mungu na hali Mtume anakuiteni mumuamini Mola wenu Mlezi? Naye amekwisha chukua ahadi yenu, ikiwa nyinyi ni Waumini.

(9) Yeye ndiye anayemteremshia mja wake Aya zinazobainisha wazi ili akutoeni gizani hadi kwenye nuru. Na hakika Mwenyezi Mungu kwenu ni Mpole mno, Mwingi wa kurehemu.

(10) Na mna nini hata hamtoi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na hali urithi wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa miongoni waliotoa kabla ya Ushindi na wakapigana vita. Hao wana daraja kubwa zaidi kuliko wale ambao walitoa baadaye na wakapigana. Na wote hao Mwenyezi Mungu amewaahidia wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda.

(11) Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, ili amrudishie maradufu, na apate malipo ya ukarimu.

(12) Siku utakapowaona Waumini wanaume na Waumini wanawake, nuru yao iko mbele yao, na kuliani kwao: Furaha yenu leo - Bustani zipitazo mito kati yake, mtakaa humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.

(13) Siku wanafiki wanaume na wanafiki wanawake watakapowaambia wale walioamini: 'Tungojeni ili tupate mwangaza katika nuru yenu.' Waambiwe: 'Rejeeni nyuma yenu mkaitafute nuru!' Kisha itatiwa baina yao ukuta wenye mlango - ndani yake mna rehema, na nje upande wake wa mbele kuna adhabu.

(14) Watawaita wawaambie: 'Kwani hatukuwa pamoja nanyi?' Watawaambia: 'Ndiyo, lakini mlijifitini wenyewe, na mkatazamia mabaya (Waumini), na mkatia shaka, na matamanio ya nafsi zenu yakakudanganyeni mpaka ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu, na mdanganyifu yule akakudanganyeni msimfuate Mwenyezi Mungu.

(15) Basi leo haitachukuliwa kwenu fidia, wala kwa wale waliokufuru. Makazi yenu ni Motoni, ndio bora kwenu; na ni marejeo maovu yalioje!

(16) Je, wakati haujafika bado kwa wale walioamini zikanyenyekea nyoyo zao kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu na haki iliyoteremka? Wala wasiwe kama wale waliopewa Kitabu kabla yao, muda wao ukawa mrefu, kwa hivyo nyoyo zao zikawa ngumu, na wengi wao ni wapotovu.

(17) Jueni kwamba Mwenyezi Mungu huifufua ardhi baada ya kufa kwake. Hakika tumekubainishieni Ishara ili mpate kuzingatia.

(18) Kwa hakika wanaume wanaotoa sadaka, na wanawake wanaotoa sadaka, na wakamkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema, watazidishiwa maradufu na watapata malipo ya ukarimu.

(19) Na wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, hao ndio Masidiqi (wakweli zaidi) na Mashahidi mbele ya Mola wao Mlezi. Wao watapata malipo yao na nuru yao. Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ndio wana Motoni.

(20) Jueni ya kwamba maisha ya dunia ni mchezo, na pumbao, na pambo, na kujifahirisha baina yenu na kushindana kwa wingi wa mali na watoto. Mfano wake ni kama mvua ambayo huwafurahisha wakulima mimea yake, kisha hunyauka ukayaona yamepiga manjano kisha yakawa mabua. Na akhera kuna adhabu kali na maghfira kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi. Na maisha ya dunia si chochote ila ni starehe ya udanganyifu.

(21) Kimbilieni msamaha wa Mola wenu Mlezi, na Bustani ya mbinguni ambayo upana wake ni kama upana wa mbingu na ardhi, iliyoandaliwa kwa ajili ya wale waliomuamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Hiyo ndiyo fadhila ya Mwenyezi Mungu, humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kuu.

(22) Hautokei msiba katika ardhi wala katika nafsi zenu ila umekwisha andikwa katika Kitabu kabla hatujauumba. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

(23) Ili msihuzunike kwa kilichokupoteeni, wala msijitape kwa alichokupeni. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila anayejivuna akajifahirisha.

(24) Ambao wanafanya ubahili, na wanaamrisha watu wafanye ubahili. Na anayegeuka, basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa mno.

(25) Kwa hakika tuliwatuma Mitume wetu na ishara waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, na tumeteremsha chuma chenye nguvu nyingi na manufaa kwa watu, na ili Mwenyezi Mungu amjue anayemnusuru Yeye na Mitume wake kwa ghaibu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kushinda.

(26) Na bila ya shaka tulimtuma Nuhu na Ibrahim, na tukaweka katika dhuriya zao Unabii na Kitabu. Basi wapo miongoni mwao walioongoka, na wengi katika wao ni wavukao mipaka.

(27) Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na tukamfuatisha Isa bin Mariamu, na tukampa Injili. Na tukaweka katika nyoyo za wale waliomfuata upole na rehema. Na umonaki (utawa wa mapadri) wameuzua wao. Sisi hatukuwaandikia hayo, ila kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu. Lakini hawakuufuata inavyotakiwa kuufuata. Basi wale walioamini katika wao tuliwapa ujira wao. Na wengi wao ni wavukao mipaka.

(28) Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na muaminini Mtume wake, atakupeni sehemu mbili katika rehema yake, na atakufanyieni nuru ya kwenda nayo, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mno, Mwingi wa kurehemu.

(29) Ili watu wa Kitabu wajue kwamba wao hawana uwezo wowote juu ya fadhila za Mwenyezi Mungu. Na kwamba fadhila zote zimo mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Humpa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kuu.