(1) Ha Mim
(2) 'Ayn Sin Qaf
(3) Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu na Mwenye hekima anavyokuletea Wahyi wewe na walio kabla yako.
(4) Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu.
(5) Zinakaribia mbingu kupasuka juu huko, na Malaika wakimtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi, na wakiwaombea maghfira waliomo kwenye ardhi. Ama hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mno, Mwenye kurehemu sana.
(6) Na wale waliowafanya walinzi wengine badala yake Yeye, Mwenyezi Mungu ni Mwangalizi bora juu yao. Wala wewe si wakili juu yao.
(7) Na namna hivi tumekufunulia Qur-ani kwa Kiarabu ili uwaonye watu wa Mama wa Miji na wale walio pembezoni mwake. Na uhadharishe na Siku ya Mkutano, haina shaka hiyo. Kundi moja litakuwa Peponi na kundi jengine katika Moto wenye mwako mkali.
(8) Na Mwenyezi Mungu angelipenda, angewafanya wote umma mmoja, lakini anamwingiza katika rehema yake amtakaye. Na wenye kudhulumu hawana mlinzi wala msaidizi.
(9) Au wamechukua walinzi wengine badala yake! Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi hasa. Na Yeye ndiye anayehuisha wafu. Na Yeye ndiye Muweza zaidi wa kila kitu.
(10) Na mkihitalifiana katika jambo lolote, basi hukumu yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Huyo Mwenyezi Mungu ndiye Mola wangu Mlezi ninayemtegemea, na kwake Yeye narejea.
(11) Yeye ndiye Muumba mbingu na ardhi. Amekujaalieni mke na mume katika nafsi zenu, na katika nyama hoa dume na jike, anakuzidishieni namna hii. Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia mno, Mwenye kuona sana.
(12) Yeye ndiye Mwenye funguo za mbingu na ardhi. Humkunjulia riziki amtakaye na humpimia amtakaye. Hakika Yeye ni Mjuzi zaidi wa kila kitu.
(13) Amekuamrisheni Dini ile ile aliyomuusia Nuhu na tuliyokufunulia wewe, na tuliyowausia Ibrahim na Musa na Isa, kwamba shikeni Dini wala msifarikiane kwayo. Ni magumu kwa washirikina hayo unayowaitia. Mwenyezi Mungu humteua kwake amtakaye, na humwongoa kwake aelekeaye.
(14) Na hawakufarikiana ila baada ya kuwajia elimu kwa sababu ya husuda iliyokuwa baina yao. Na lau kuwa haikwisha tangulia kauli kutoka kwa Mola wako Mlezi ya kuahirisha mpaka muda maalumu, basi bila ya shaka pangelihukumiwa baina yao. Na hakika wale waliorithishwa Kitabu baada yao wanakitilia shaka inayowahangaisha.
(15) Basi kwa haya waite! Nawe simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa, wala usiyafuate matamanio yao. Na sema: 'Ninaamini aliyoteremsha Mwenyezi Mungu katika Vitabu. Na nimeamrishwa nifanye uadilifu baina yenu. Mwenyezi Mungu ni Mola wetu Mlezi, na Mola wenu Mlezi. Sisi tuna jukumu kwa vitendo vyetu, na nyinyi mna jukumu kwa vitendo vyenu. Hapana kuhojiana baina yetu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu atatukusanya pamoja, na marejeo ni kwake.'
(16) Na wale wanaohojiana juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kukubaliwa, hoja za hawa ni batili mbele ya Mola wao Mlezi, na juu yao ipo ghadhabu, na itakuwa kwao adhabu kali.
(17) Mwenyezi Mungu ndiye aliyeteremsha Kitabu kwa Haki na Mizani. Na ni nini kitakachokujulisha ya kwamba pengine Saa ya Kiyama ipo karibu?
(18) Wale wasioiamini huihimiza hiyo Saa ifike upesi, lakini wale wanaoamini wanaiogopa na wanajua kwamba hakika hiyo ni kweli. Ama kwa hakika hao wanaobishana katika habari za hiyo Saa wamo katika upotofu wa mbali kabisa.
(19) Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake. Humruzuku amtakaye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mtukufu.
(20) Mwenye kutaka mavuno ya Akhera, tutamzidishia katika mavuno yake. Na mwenye kutaka mavuno ya duniani, tutampa katika hayo, lakini katika Akhera hana fungu lolote.
(21) Au hao wana miungu ya kishirikina waliowatungia dini asiyoitolea idhini Mwenyezi Mungu? Na lau lisingekuweko neno la kupambanua, basi wangelikatiwa hukumu baina yao. Na hakika wenye kudhulumu watapata adhabu chungu.
(22) Utawaona hao madhalimu wanavyokuwa na hofu kwa sababu ya waliyoyachuma, nayo yatawafika tu. Na wale walioamini na wakatenda mema watakuwemo katika mabustani ya Peponi. Humo watapata wayatakayo kwa Mola wao Mlezi. Hiyo ndiyo fadhila kubwa.
(23) Hayo ndiyo aliyowabashiria Mwenyezi Mungu waja wake walioamini na wakatenda mema. Sema: 'Sikuombeni malipo yoyote juu yake ila mapenzi katika kujikurubisha. Na anayefanya wema, tutamzidishia wema. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu mno, Mwenye shukrani sana.'
(24) Ati wanasema Amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo? Mwenyezi Mungu akipenda ataziba moyo wako. Na Mwenyezi Mungu anaufuta upotofu na anaithibitisha Haki kwa maneno yake. Hakika Yeye anayajua yaliyomo vifuani.
(25) Naye ndiye anayepokea toba kwa waja wake, na anasamehe mabaya, na anayajua mnayoyatenda.
(26) Na anawaitikia wanaoamini na wakatenda mema, na anawazidishia fadhila zake. Na makafiri watakuwa na adhabu chungu.
(27) Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeliwakunjulia riziki waja wake, basi bila ya shaka wangelipanda kiburi katika dunia. Lakini anaiteremsha kwa kipimo akitakacho. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
(28) Naye ndiye anayeiteremsha mvua baada ya wao kwisha kata tamaa, na hueneza rehema yake. Naye ndiye Mlinzi, Mwenye kusifiwa sana.
(29) Na katika Ishara zake ni kuumba mbingu na ardhi, na wanyama aliowaeneza ndani yake. Naye ni Mwenye uweza mkubwa wa kuwakusanya apendapo.
(30) Na misiba inayowasibu ni kwa sababu ya vitendo vya mikono yenu. Naye anasamehe mengi.
(31) Na nyinyi hamwezi kushinda katika ardhi. Na wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi badala ya Mwenyezi Mungu.
(32) Na katika Ishara zake ni vyombo vinavyokwenda na kurejea baharini kama vilima.
(33) Akitaka, huutuliza upepo navyo hivyo vyombo husimama tutwe juu ya bahari. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa kila mwenye subira kubwa na akashukuru sana.
(34) Au huviangamiza hivyo vyombo kwa sababu ya waliyoyatenda hao watu. Naye husamehe mengi.
(35) Na ili wajue wanaojadiliana katika Ishara zetu kwamba hawana pahali popote pa kukimbilia.
(36) Basi vyote mlivyopewa ni starehe ya maisha ya dunia tu, lakini kilichoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora na cha kudumu zaidi kwa ajili ya walioamini na wakawa wanamtegemea Mola wao Mlezi.
(37) Na wanayoyaepuka madhambi makubwa na mambo machafu, na wanapokasirika wao husamehe.
(38) a wanaomwitikia Mola wao Mlezi, na wakashika Sala, na mambo yao yakawa ni kwa kushauriana baina yao, na kutokana na tulichowaruzuku wakawa wanatoa.
(39) Na ambao wanapofanyiwa jeuri hujitetea.
(40) Na malipo ya uovu ni uovu mfano wa huo. Lakini mwenye kusamehe na akasuluhisha, basi huyo malipo yake yapo kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye hawapendi wenye kudhulumu.
(41) Na wanaojitetea baada ya kudhulumiwa, hao hapana njia ya kuwalaumu.
(42) Bali lawama ipo kwa wale wanaowadhulumu watu, na wanafanya jeuri katika nchi bila ya haki. Hao watapata adhabu iliyo chungu.
(43) Na anayekuwa na subira, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa.
(44) Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana mlinzi baada yake. Na utawaona wenye kudhulumu watakapoiona adhabu wanasema: 'Je! Ipo njia ya kurudi?'
(45) Na utawaona wanapelekwa kwenye Moto, nao wamenyenyekea kwa unyonge, wanatazama kwa mtazamo wa kificho. Na walioamini watasema: 'Hakika wapatao hasara ni hao waliohasiri nafsi zao na ahali zao Siku ya Kiyama.' Ama hakika wenye kudhulumu watakuwa katika adhabu ya daima.
(46) Wala hawatakuwa na walinzi wa kuwanusuru mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, hana njia yoyote.
(47) Muitikieni Mola wenu Mlezi kabla haijafika siku isiyoepukika, itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Siku hiyo hamtakuwa na pa kukimbilia wala hamtakuwa na cha kukingia.
(48) Na wakipuuza, basi Sisi hatukukupeleka ili uwe mwangalizi wao. Si juu yako ila kufikisha Ujumbe tu. Na hakika Sisi tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, huifurahia. Na akisibiwa na ovu kwa sababu ya iliyoyatanguliza mikono yao, basi hakika mtu huyu anakufuru.
(49) Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; anaumba apendavyo, anamtunukia amtakaye watoto wa kike, na anamtunukia amtakaye watoto wa kiume.
(50) Au huwachanganya wanaume na wanawake, na akamfanya amtakaye tasa. Hakika Yeye ni Mjuzi, Mwenye uweza.
(51) Na haikuwa kwa mwanadamu kwamba Mwenyezi Mungu amsemeze ila kwa Wahyi (Ufunuo), au kwa nyuma ya kizuizi, au kumtuma Mjumbe. Naye humfunulia ayatakayo kwa idhini yake. Hakika Yeye ni Mtukufu, Mwenye hekima.
(52) Na namna hivi tumekufunulia Qur-ani kwa amri yetu. Ulikuwa hujui Kitabu ni nini, wala Imani. Lakini tumekifanya kuwa ni Nuru ambayo kwayo tunamwongoa tumtakaye katika waja wetu. Na hakika wewe unaongoa kwenye Njia Iliyonyooka.
(53) Njia ya Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye tu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Jueni kuwa mambo yote yanarudi kwa Mwenyezi Mungu.