(1) Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi ambaye aliwaumba kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka kwayo. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume wengi na wanawake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaomba, na jamaa zenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalia.
(2) Na wapeni mayatima mali zao. Wala msibadilishe kibaya kwa kizuri. Wala msile mali zao pamoja na mali zenu. Hakika, yote hayo ni dhambi kubwa.
(3) Na ikiwa mnaogopa kuwa hamtowafanyia mayatima uadilifu, basi oeni mnaowapenda katika wanawake, wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi mmoja tu, au wale ambao mikono yenu ya kulia imewamiliki. Kufanya hivi ndiko kutapelekea msidhulumu.
(4) Na wapeni wanawake mahari yao hali ya kuwa ni kipawa. Lakini wakiwatunuku kitu kwayo kwa roho safi yao, basi kileni kiwashuke kwa raha.
(5) Wala msiwape wasio na akili mali zenu ambazo Mwenyezi Mungu amezifanya kuwa za kuwakimu. Na walisheni kutoka kwayo, na wavisheni, na waambieni kauli njema.[1]
[1] Na katika aya hii kuna ishara ya kuisifu mali. Na watangulizi wema walikuwa wakisema: Mali ni silaha ya Muumini. Ni bora zaidi kwangu niache mali (nikifa) ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu ataniuliza juu yake kuliko niwahitaji watu.(Tafsir Al-Alusi)
(6) Na wajaribuni mayatima mpaka wanapofikia umri wa kuoa. Mkiona uamuzi wa busara ndani yao, basi wapeni mali zao. Wala msizile kwa kupitiliza na mapema mapema kwa kuwa watakuja kuwa watu wazima. Na yule ambaye ni tajiri, basi na ajizuilie. Na yule ambaye ni fakiri, basi na ale kwa wema. Na mtakapowapa mali zao, basi washuhudisheni mashahidi juu yao. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu.
(7) Wanaume wana fungu katika yale wanayoyaacha wazazi na jamaa wa karibu. Na wanawake wanalo fungu katika yale waliyoyaacha wazazi na jamaa wa karibu. Kwa kile kilicho kidogo chake au kingi. Ni mafungu yaliyofaradhiwa.[1]
[1] Waarabu wakati wa Jahiliyya kwa sababu ya ukatili wao na ugumu wao walikuwa hawawarithishi wanyonge kama vile wanawake na watoto. Na walikuwa wakiwagawia urithi wanaume wenye nguvu tu. Kwa sababu walikuwa wakidai kuwa wao tu ndio wanaoweza vita, na kunyang’anya, na kupora.
(8) Na wakihudhuria ugawi jamaa wa karibu, na mayatima, na masikini, basi wapeni kwayo (yani mali ya urithi), na waambieni kauli njema.
(9) Na wachelee wale ambao lau kuwa na wao wangeliacha nyuma yao dhuria wanyonge, wangeliwahofia. Basi nao wamche Mwenyezi Mungu, na waseme kauli iliyo sawa.
(10) Hakika, wale wanaokula mali za mayatima kwa dhuluma, hapana shaka yoyote wanakula matumboni mwao moto. Na wataingia Moto wenye Mwako mkali.
(11) Mwenyezi Mungu anawausia juu ya watoto wenu: Fungu la mwanamume ni kama fungu la wanawake wawili. Na wakiwa ni wanawake zaidi ya wawili, basi wana theluthi mbili za alichokiacha maiti. Lakini akiwa mtoto mwanamke ni mmoja, basi fungu lake ni nusu. Na kwa wazazi wake wawili, kila mmoja wao apate sudusi moja katika kile alichokiacha, ikiwa ana mtoto. Na akiwa hana mtoto, na wazazi wake wawili wakawa wanamrithi, basi mama yake atapata theluthi moja. Na akiwa ana ndugu, basi mama yake atapata sudusi. Haya ni baada ya kutolewa alichousia au kulipa deni. Baba zenu na watoto wenu, nyinyi hamjui ni nani kati yao aliyekaribu zaidi kwenu kwa manufaa. Hiyo ni Sharia iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu. Bila ya shaka, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.[1]
[1] Kiliekwa kiwango cha mwanamke kuwa ni nusu ya kiwango anachokirithi mwanamume kwa sababu mwanamke hutoshelezwa na jamii, au mumewe. Naye mwanamume huwa amejukumishwa kumlea mwanamke katika maisha. (Uadilifu wa Mirathi ndani ya Usilamu cha Mnaswab Abdulrahman)
(12) Nanyi mna nusu ya walichoacha wake zenu ikiwa hawana mtoto. Lakini ikiwa wana mtoto, basi mna robo katika kile walichokiacha, baada ya wasia waliyousia au kulipa deni. Na wake zenu wana robo katika kile mlichokiacha, ikiwa hamna mtoto. Lakini ikiwa mna mtoto, basi wana thumuni katika kile mlichokiacha, baada ya wasia mliousia au kulipa deni. Na ikiwa mwanamume au mwanamke anayerithiwa hana mtoto wala wazazi, lakini anaye kaka au dada, basi kila mmoja wao ana sudusi. Na wakiwa zaidi kuliko hivyo, basi watashirikiana katika theluthi, baada ya wasia iliyousiwa au kulipa deni, pasi na kuleta madhara. Huu ndio wasia uliotoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mpole.
(13) Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito chini yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
(14) Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, naye ana adhabu ya kudhalilisha.
(15) Na wale ambao wanafanya uchafu miongoni mwa wanawake wenu, washuhudisheni watu wanne katika nyinyi. Watakaposhuhudia, basi wazuieni majumbani mpaka wafishwe na mauti au Mwenyezi Mungu awafanyie njia nyengine.
(16) Na wawili kati yenu wafanyao hayo miongoni mwenu, waudhini. Na wakitubia wakatengenea, basi waacheni. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kupokea toba, Mwenye kurehemu.
(17) Hakika, toba inayokubaliwa na Mwenyezi Mungu ni ya wale wafanyao uovu kwa ujinga, kisha wakatubia kwa haraka. Hao ndio Mwenyezi Mungu huwakubalia toba yao, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua, Mwenye hekima.
(18) Wala hawana toba wale wafanyao maovu mpaka yakamfikia mmoja wao mauti, kisha hapo akasema: Hakika, mimi sasa nimetubia. Wala wale wanaokufa hali ya kuwa wao ni makafiri. Hao tumewaandalia adhabu chungu.
(19) Enyi mlioamini! Si halali kwenu kuwarithi wanawake kwa nguvu. Wala msiwadhikishe ili muwapokonye baadhi ya mlivyowapa, isipokuwa wakifanya uchafu ulio wazi. Na kaeni nao kwa wema. Na ikiwa mmewachukia, basi huenda mkakichukia kitu, na Mwenyezi Mungu ametia heri nyingi ndani yake.
(20) Na mkitaka kubadilisha mke pahali pa mke hali ya kuwa mmempa mmoja wao chungu ya mali, basi msichukue katika hayo kitu chochote. Je, mnaichukua kwa dhuluma na kosa lililo wazi?
(21) Na vipi mnaichukua ilhali mmekwisha ingiliana nyinyi kwa nyinyi, nao (wanawake) walikwisha chukua kutoka kwenu agano lililo madhubuti?
(22) Wala msiwaoe wale waliowaoa baba zenu, isipokuwa yale yaliyokwisha pita. Hakika, huo ni uchafu, na uchukizo, na ni njia mbaya.
(23) Mmeharimishiwa mama zenu, na binti zenu, na dada zenu, na shangazi zenu, na khaalati zenu, na binti wa kaka, na binti wa dada, na mama zenu waliowanyonyesha, na dada zenu kwa kunyonya, na mama wa wake zenu, na watoto wenu wa kambo walio katika ulinzi wenu waliozaliwa na wake zenu mliowaingilia. Ikiwa hamkuwaingilia, basi hakuna ubaya juu yenu. (Pia mmeharimishwa) wake wa watoto wenu waliotoka katika migongo yenu. Na kuwaoa pamoja dada wawili isipokuwa yale yaliyokwisha pita. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(24) Na wanawake wenye waume, isipokuwa waliomilikiwa na mikono yenu ya kulia. Ndiyo Sheria ya Mwenyezi Mungu juu yenu. Na mmehalilishiwa wasiokuwa hao, mtafute kwa mali zenu kwa kuoa pasi na kuzini. Kama mnavyostarehe nao, basi wapeni mahari yao kwa kuwa ni wajibu. Wala hakuna ubaya juu yenu kwa mtakachokubaliana baada ya kutimiza wajibu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
(25) Na asiyeweza kati yenu kupata mali ya kuolea wanawake wa kiungwana Waumini, basi na aoe katika vijakazi Waumini iliyowamiliki mikono yenu ya kulia. Na Mwenyezi Mungu anajua vyema imani yenu. Nyinyi mmetokana wenyewe kwa wenyewe. Basi waoeni kwa idhini ya watu wao, na wapeni mahari yao kulingana na ada, wawe wanawake wema, si makahaba wala si mahawara. Na wanapoolewa kisha wakafanya uchafu basi adhabu yao itakuwa ni nusu ya adhabu waliyowekewa waungwana. Hayo ni kwa yule miongoni mwenu anayeogopa kuingia katika zinaa. Na mkisubiri ndio bora kwenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(26) Mwenyezi Mungu anataka kwamba awabainishie, na awaongoze nyendo za wale waliokuwa kabla yenu, na akubali toba zenu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
(27) Na Mwenyezi Mungu anataka kuwakubalia toba zenu, na wale wanaofuata matamanio wanataka kwamba mjipinde kujipinda kukubwa.
(28) Na Mwenyezi Mungu anataka kwamba awahafifishie, na mwanadamu ameumbwa dhaifu.
(29) Enyi mlioamini! Msizile mali zenu baina yenu kwa batili, isipokuwa ikiwa ni biashara kwa kuridhiana wenyewe. Wala msijiue. Hakika, Mwenyezi Mungu kwenu ni Mrehemevu.
(30) Na mwenye kufanya hayo kwa kupita mipaka na udhalimu, basi tutamwingiza motoni. Na hilo ni jepesi kwa Mwenyezi Mungu.
(31) Mkiyaepuka makubwa ya yale mnayokatazwa, tutawafutia makosa yenu madogo, na tutawaingiza pahali pa kuingia patukufu.
(32) Wala msitamani alichowafadhilisha kwacho Mwenyezi Mungu baadhi yenu kuliko wengine. Wanaume wana fungu katika walivyovichuma, na wanawake wana fungu katika walivyovichuma. Na mwombeni Mwenyezi Mungu katika fadhila zake. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.
(33) Na kila mmoja tumemfanyia warithi katika yale waliyoyaacha wazazi wawili na jamaa. Na wale mliofungamana nao kwa viapo, wapeni fungu lao. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Shahidi juu ya kila kitu.
(34) Wanaume ni wasimamizi imara wa wanawake, kwa yale aliyowafadhilisha kwayo Mwenyezi Mungu baadhi yao juu ya baadhi, na kwa yale wanayoyatoa katika mali zao. Basi wanawake wema ni wale wenye kutii na wanaojilinda hata katika siri kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameamrisha wajilinde. Na wale mnaochelea kutoka kwao katika utiifu, waaidhini, na wahameni katika malazi, na wapigeni. Basi wakiwatii, msitafute njia yoyote dhidi yao. Hakika, Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu, Mkubwa.[1]
[1] Na kinachomaanishwa na kuboreshwa katika kauli yake hii ni kuboreshwa kwa jinsia juu ya jinsia, na sio kumboresha kila mmoja wao juu ya mwengine. Kwa maana, kunaweza kuwa na wanawake ambao wana akili na elimu zaidi kuliko wanaume wengine. (Tafsir Tantawii)
(35) Na mkihofia kuwepo mfarakano baina ya wawili hao, basi mtumeni mpatanishi kutoka kwa jamaa za mume, na mpatanishi kutoka kwa jamaa za mke. Ikiwa wanataka kutengeneza mambo, Mwenyezi Mungu atawawezesha kati yao. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye habari zote.
(36) Na mwabuduni Mwenyezi Mungu wala msimshirikishe na chochote. Na wafanyieni wema wazazi wawili, na jamaa, na mayatima, na masikini, na jirani wa karibu, na jirani wa ubavuni, na mwenza wa ubavuni, na mwana njia, na wale iliowamiliki mikono yenu ya kulia. Hakika, Mwenyezi Mungu hampendi mwenye kiburi anayejifahiri.
(37) Ambao wanafanya ubahili na wanaamrisha watu ubahili, na wanaficha yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila zake. Na tuliwaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.
(38) Na ambao hutoa mali zao ili kujionyesha kwa watu, wala hawamwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Na yule ambaye Shetani amekuwa ndiye mwenza wake, basi ana mwenza mbaya mno.
(39) Na ingeliwadhuru nini wao lau wangelimwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyowaruzuku Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema.
(40) Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu hata uzito wa chembe moja. Na ikiwa ni zuri, atalizidisha na atapeana kutoka kwake malipo makubwa.
(41) Basi itakuwa vipi tutakapoleta kutoka kwa kila umma shahidi, na tukakuleta wewe kuwa shahidi dhidi ya hawa?
(42) Siku hiyo watapenda wale waliokufuru na wakamuasi Mtume lau kuwa ardhi isawazishwe kwa wao. Wala hawataweza kumficha Mwenyezi Mungu neno lolote.[1]
[1] Walitamani hivyo kwa sababu ya kuhofia yatakayowafika ya kufedheheshwa na kulaumiwa, kisha kudunishwa nakuadhibiwa. (Tafsiir Al-Baqaa'ii)
(43) Enyi mlioamini! Msiikaribie Swala hali ya kuwa mmelewa, mpaka myajue mnayoyasema. Wala mkiwa na janaba (msikaribie swala wala msikiti), isipokuwa wanaopita njia (msikitini), mpaka muoge. Na mkiwa wagonjwa, au katika safari, au mmoja wenu akitoka chooni, au mkiwagusa wanawake, na msipate maji, basi ukusudieni mchanga safi. Basi upangusieni kwenye nyuso zenu na mikono yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kufuta dhambi.
(44) Je, hukuwaona wale waliopewa fungu katika Kitabu wanaununua upotovu na wanataka kwamba mpotee Njia?
(45) Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema maadui zenu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mlinzi, na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mwenye kunusuru.
(46) Miongoni mwa Mayahudi wamo wanaopotosha maneno kuyatoa pahali pake, na husema: Tumesikia na tumeasi, na sikia bila ya kusikizishwa. Na husema: "Raai'naa", kwa kuzipotoa ndimi zao na kuitukana Dini. Na lau kama wangelisema: Tumesikia na tumetii, na usikie na "Undhurna (Utuangalie)," ingelikuwa heri kwao na ya unyoofu zaidi. Lakini Mwenyezi Mungu aliwalaani kwa kufuru yao; basi hawaamini isipokuwa wachache tu.
(47) Enyi mliopewa Kitabu! Aminini tuliyoyateremsha yenye kusadikisha yale mliyo nayo, kabla hatujazifutilia mbali nyuso na kuzipeleka nyuma yake, au tuwalaani kama tulivyowalaani watu wa Sabato (Jumamosi). Na amri ya Mwenyezi Mungu ni lazima ifanyike.
(48) Hakika, Mwenyezi Mungu hafuti dhambi ya kushirikishwa, na hufuta dhambi ya yale yaliyo duni ya hilo kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, basi hakika amezua dhambi kubwa.
(49) Je, hukuwaona wale wanaojitakasa nafsi zao? Bali Mwenyezi Mungu humtakasa amtakaye. Na hawatadhulumiwa hata kiasi cha kijiuzi kilichomo ndani ya uwazi wa kokwa ya tende.
(50) Tazama namna wanavyomzulia uwongo Mwenyezi Mungu, na haya yanatosha kuwa dhambi iliyo wazi.
(51) Je, hukuwaona wale waliopewa fungu katika Kitabu? Wanaamini masanamu na Taghut! Na wanasema kuhusu wale waliokufuru kwamba hawa ndio walioongoka zaidi katika njia kuliko wale walioamini.
(52) Hao ndio Mwenyezi Mungu amewalaani. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemlaani, basi hutapata wa kumnusuru.
(53) Au wanalo fungu katika mamlaka? Basi hapo wasingewapa watu hata jicho la kokwa ya tende.
(54) Au wanawahusudu watu kwa yale aliyowapa Mwenyezi Mungu katika fadhila yake? Basi hakika tuliwapa ukoo wa Ibrahim Kitabu na hekima, na tukawapa ufalme mkubwa.
(55) Basi miongoni mwao kuna yule aliyemwamini, na miongoni mwao kuna yule aliyemkufuru. Na Jahannamu inatosha kuwa ndio moto wenye mwako mkali.
(56) Hakika wale waliozikufuru Ishara zetu, tutawaingiza motoni. Kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilishia ngozi nyingine ili waionje hiyo adhabu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(57) Na wale walioamini na wakatenda mema, tutawaingiza katika Pepo zipitazo mito chini yake wadumu humo milele. Humo watakuwa na wake waliotakaswa, na tutawaingiza katika vivuli vizuri kwelikweli.
(58) Hakika Mwenyezi Mungu anawaamrisha kwamba mzirudishe amana kwa wenyewe. Na mnapohukumu baina ya watu mhukumu kwa uadilifu. Hakika haya anayowawaidhi kwayo Mwenyezi Mungu ndiyo mazuri sana. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
(59) Enyi mlio amini! Mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume na wenye mamlaka katika nyinyi. Na mkizozana katika kitu, basi kirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.
(60) Je, hukuwaona wale wanaodai kwamba wameamini yale yaliyoteremshwa kwako na yale yaliyoteremshwa kabla yako? Wanataka kupeleka kesi yao kwa Twaghut, na ilhali kwa hakika waliamrishwa kwamba wazikufuru! Na anataka Shetani kwamba awapoteze kupotea kwa mbali.
(61) Na wanapoambiwa: Njooni kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu na kwa Mtume, utawaona wanafiki wanaepukana na wewe kuepuka kukubwa.
(62) Basi inakuwa vipi unapowasibu msiba kwa sababu ya yale iliyotanguliza mikono yao? Hapo, wanakujia wakiapa kwa Mwenyezi Mungu wakisema: Hatukutaka isipokuwa wema na mapatano.
(63) Hao ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nyoyo zao. Basi wapuuze, na uwawaidhi, na uwaambie maneno ya kuathiri na kuingia katika nafsi zao.
(64) Na hatukumtuma Mtume yeyote isipokuwa atiiwe kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na lau pale walipozidhulumu nafsi zao, wangelikujia, wakamwomba Mwenyezi Mungu kuwafutia dhambi, na Mtume akawaombea kufutiwa dhambi, basi bila ya shaka wangelimkuta Mwenyezi Mungu ni Mwenye kupokea toba, Mwenye kurehemu.
(65) Hapana! Ninaapa kwa Mola wako Mlezi! Hawataamini mpaka wakufanye wewe ndiye mwenye kuhukumu katika yale wanayohitalifiana, kisha wasipate uzito wowote katika nyoyo zao juu ya hukumu utakayotoa, na wajisalimishe kujusalimisha kukamilifu.
(66) Na lau kuwa tuliwaandikia kuwa: Jiueni, au tokeni majumbani mwenu, wasingeliyafanya hayo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Na lau kama wangeliyafanya yale wanayowaidhiwa kwayo, ingelikuwa bora kwao na uthibitisho wa nguvu zaidi.
(67) Na hapo tungewapa malipo makubwa kutoka kwetu.
(68) Na tungeliwaongoa njia iliyonyooka.
(69) Na mwenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, basi hao wako pamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Masiddiqi (Wakweli), na Mashahidi, na Watu wema. Na hao ndio wenza wazuri mno!
(70) Hiyo ndiyo fadhila itokayo kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kwamba ndiye Mwenye kujua.
(71) Enyi mlioamini! Chukueni tahadhari yenu! Na mtoke haraka kwa vikosi au tokeni nyote kwa pamoja!
(72) Na hakika yupo kati yenu anayejikokota sana. Na ukiwapata (nyinyi) msiba, husema: Hakika Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa vile sikuwa nimehudhuria pamoja nao.
(73) Na ikiwapata fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu, anasema, kana kwamba hapakuwa mapenzi baina yenu na yeye: Aa! Laiti ningelikuwa pamoja nao nikafuzu kufuzu kukubwa.
(74) Basi na wapigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu wale ambao wanauza uhai wa dunia kwa Akhera. Na mwenye kupigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha akauwawa au akashinda, basi tutampa ujira mkubwa.
(75) Na mna nini hampigani katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na ya wale wanaoonewa miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhalimu, na tufanyie mlinzi kutoka kwako, na tufanyie wa kutunusuru kutoka kwako.
(76) Wale walioamini wanapigana vita katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wale waliokufuru wanapiana vita katika njia ya Twaghut. Basi piganeni na marafiki wa Shetani. Hakika, hila ya Shetani ni dhaifu.
(77) Je, hukuwaona wale walioambiwa: ‘Izuieni mikono yenu, na mshike Swala na mtoe Zaka.’ Na pindi walipoamrishwa kupigana, mara kundi moja miongoni mwao likawaogopa watu kama kumwogopa Mwenyezi Mungu, au kwa hofu kubwa zaidi. Na wakasema: ‘Mola wetu Mlezi! Kwa nini umetuamrisha kupigana? Laiti ungetuahirishia kiasi ya muda kidogo hivi!’ Sema: ‘Starehe ya dunia ni ndogo, na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kuchamungu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende.’
(78) Popote mtakapokuwa, mauti yatawafikia, hata kama mtakuwa katika ngome zilizoimarishwa. Na likiwapata zuri, wanasema: Hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu. Na likiwapata ovu, wanasema: Hili limetoka kwako wewe. Sema: Yote hayo yanatokana na Mwenyezi Mungu. Basi wana nini watu hawa hata hawakaribii kufahamu maneno?
(79) Yaliyokupata katika mazuri, basi ni kutokana na Mwenyezi Mungu. Na yaliyokusibu katika maovu, basi ni kutokana na nafsi yako. Nasi tumekutuma kwa watu uwe ni Mtume. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.
(80) Mwenye kumtii Mtume, basi hakika amemtii Mwenyezi Mungu. Na mwenye kugeuka, basi Sisi hatukukutuma uwe mlinzi juu yao.
(81) Na wanasema: Tunatii. Lakini wanapotoka kule uliko, kundi moja miongoni mwao hupanga njama usiku kinyume na unayoyasema. Na Mwenyezi Mungu anayaandika yote hayo wanayoyapangia njama za usiku. Basi wape mgongo, na umtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa
(82) Kwani hawaizingatii hii Qur-ani? Na lau kuwa ingetoka kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka wangelikuta ndani yake hitilafu nyingi.
(83) Na linapowajia jambo lolote linalohusiana na amani au hofu, wao wanalitangaza. Na lau kuwa wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka kati yao, wale wanaochunguza miongoni mwao wangelijua. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, mngelimfuata Shetani isipokuwa wachache tu.
(84) Basi pigana vita katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Hutwikwi isipokuwa nafsi yako tu. Na wahimize Waumini. Huenda Mwenyezi Mungu akayazuia mashambulizi ya wale waliokufuru. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mkali zaidi wa kushambulia, na Mkali zaidi wa kutesa.
(85) Mwenye kufanya uombezi mzuri, ana fungu lake katika hayo. Na mwenye kufanya uombezi mbaya, naye ana sehemu yake katika hayo. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo na ujuzi juu ya kila kitu.
(86) Na mnapoamkiwa kwa maamkizi yoyote, basi itikieni kwa yaliyo mazuri zaidi kuliko hayo, au yarejesheni hayo hayo. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuhesabu kila kitu.
(87) Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipokuwa Yeye. Kwa yakini, atawakusanya Siku ya Qiyama. Halina shaka hilo. Na ni nani mkweli zaidi katika mazungumzo kuliko Mwenyezi Mungu?
(88) Basi mna nini mmekuwa makundi mawili kuhusiana na (habari ya) wanafiki, na ilhali Mwenyezi Mungu amewageuza kwa sababu ya yale waliyoyachuma? Je, mnataka kumwongoa yule ambaye Mwenyezi Mungu amempoteza? Na mwenye kupotezwa na Mwenyezi Mungu, basi wewe hutapata njia yoyote kwa ajili yake.
(89) Wanapenda lau kuwa mtakufuru kama walivyokufuru wao, ili muwe sawasawa. Basi, msifanye marafiki wandani miongoni mwao mpaka wahame katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na wakigeuka, basi wakamateni, na waueni popote mnapowapata. Wala msifanye miongoni mwao rafiki mwandani wala msaidizi.
(90) Isipokuwa wale waliofungamana na kaumu ambao kuna ahadi baina yenu na wao, au wanawajia hali ya kuwa vifua vyao vina dhiki juu ya kupigana nanyi, au kupigana na kaumu yao. Na lau angelipenda Mwenyezi Mungu, angeliwapa mamlaka juu yenu wangelipigana nanyi. Kwa hivyo, wakijitenga nanyi, na wasipigane nanyi, na wakawaletea amani, basi Mwenyezi Mungu hakuwapa nyinyi njia dhidi yao.
(91) Mtawakuta wengine wanataka wapate salama kwenu na salama kwa watu wao. Kila wakirudishwa kwenye fitina, hudidimizwa humo. Na ikiwa hawajitengi nanyi, na wakawaletea salama, na wakaizuia mikono yao, basi wakamateni na waueni popote mnapowakuta. Na hao, tumewapa nyinyi hoja zilizo wazi juu yao.
(92) Na haiwi Muumini kumuua Muumini isipokuwa kwa kukosea. Na mwenye kumuua Muumini kwa kukosea, basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa zake maiti, isipokuwa waiache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni wa kutoka kwa kaumu ambao ni maadui zenu, ilhali yeye ni Muumini, basi ni kwa kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa kaumu ambao kuna agano baina yenu na wao, basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiyepata, basi afunge miezi miwili mfululizo, iwe ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima kubwa.
(93) Na mwenye kumuua Muumini kwa kukusudia, basi malipo yake ni Jahannamu humo atadumu, na Mwenyezi Mungu amemkasirikia, na amemlaani, na amemwandalia adhabu kubwa.
(94) Enyi mlioamini! Mnaposafiri katika Njia ya Mwenyezi Mungu, basi chunguzeni sawasawa, wala msimwambie anayewatolea salamu: Wewe si Muumini; kwa kutaka manufaa ya maisha ya dunia hii, hali ya kuwa kwa Mwenyezi Mungu ndiko zipo ghanima nyingi. Hivyo ndivyo mlivyokuwa nyinyi zamani, na Mwenyezi Mungu akawaneemesha. Basi chunguzeni sawasawa. Hakika, Mwenyezi Mungu kwa yale mnayoyatenda anazo habari zote.
(95) Hawawi sawa wanaokaa tu miongoni mwa Waumini wasiokuwa na dharura, na wale wanaopigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Mwenyezi Mungu ameboresha kwa daraja wale wanaopigana kwa mali zao na nafsi zao juu ya wale wanaokaa tu. Na kila mmoja wao Mwenyezi Mungu amemuahidi mazuri. Lakini Mwenyezi Mungu amewaboresha kwa ujira mkubwa wale wanaopigana kuliko wale wanaokaa tu.
(96) Hivyo ni vyeo kutoka kwake, na kufutiwa dhambi, na rehema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi mno, na Mwenye kurehemu sana.
(97) Hakika, wale ambao Malaika wanawafisha hali ya kuwa wamezidhulumu nafsi zao, watawaambia: Mlikuwa katika nini? Watasema: Tulikuwa tumefanywa kuwa wanyoge katika ardhi. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa, mkahamie humo? Basi hao makazi yao ni Jahannam, nayo ni marejeo mabaya kabisa.
(98) Isipokuwa wale waliodhoofishwa miongoni mwa wanaume na wanawake na watoto wasioweza hila wala hawawezi kufuata sawasawa njia ya kuhama.
(99) Basi hao, huenda Mwenyezi Mungu akawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kufuta dhambi.
(100) Na mwenye kuhama katika Njia ya Mwenyezi Mungu, atapata pengi duniani pa kukimbilia, na atapata wasaa. Na mwenye kutoka katika nyumba yake akihamia kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kisha yakamfika mauti, basi hakika umekwisha wajibika ujira kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(101) Na mnaposafiri katika nchi, basi hakuna ubaya juu yenu mkifupisha katika Swala, iwapo mnachelea kwamba wale waliokufuru watawajaribu. Hakika, makafiri ni maadui zenu walio wazi wazi.
(102) Na unapokuwa miongoni mwao, na ukawasimamishia Swala, basi kundi moja miongoni mwao lisimame pamoja nawe, na wachukue silaha zao. Na watakapomaliza kusujudu, basi na wawe nyuma yenu, na lije kundi lingine ambalo halijaswali, na waswali pamoja nawe, nao wachukue hadhari yao na silaha zao. Walipenda wale waliokufuru lau mghafilike na silaha zenu na mizigo yenu ili wawavamie mvamio wa mara moja. Wala hakuna ubaya juu yenu ikiwa mnaona udhia kwa sababu ya mvua au mkawa wagonjwa, mkaziweka silaha zenu. Na chukueni hadhari yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu amewaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.
(103) Na mkishamaliza Swala, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu hali ya kuwa mmesimama, na mkikaa, na kwa mbavu zenu. Na mtakapotulia, basi simamisheni Swala. Kwani, hakika Swala juu ya Waumini ni andiko lililowekewa nyakati maalum.
(104) Wala msilegee katika kuwafukuzia kaumu hawa (ya maadui). Ikiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyoumia. Nanyi mnataraji kwa Mwenyezi Mungu yale wasiyoyataraji. Na hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
(105) Hakika Sisi tumekuteremshia Kitabu hiki kwa haki ili uhukumu baina ya watu kwa kile alichokuonyesha Mwenyezi Mungu. Wala usiwe mtetezi wa mahaini.
(106) Na muombe Mwenyezi Mungu kufutiwa dhambi. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(107) Wala usimbishanie wale wanaozihini nafsi zao. Hakika, Mwenyezi Mungu hampendi yule ambaye ni haini mkubwa, mwenye dhambi nyingi.
(108) Wanawaficha watu, wala hawamfichi Mwenyezi Mungu, naye yu pamoja nao pale wanapopanga njama usiku kwa maneno asiyoyapenda. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka vyema wanayoyatenda.
(109) Hivi ni nyinyi hawa mmewabishania katika uhai huu wa duniani. Basi ni nani atakayewabishania dhidi ya Mwenyezi Mungu Siku ya Kiyama? Au ni nani atakuwa wakili wao wa kumtegemea?
(110) Na anayetenda uovu au akaidhulumu nafsi yake, kisha akaomba kufutiwa dhambi kwa Mwenyezi Mungu, atamkuta Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(111) Na mwenye kuchuma dhambi, basi ameichumia nafsi yake mwenyewe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
(112) Na mwenye kuchuma kosa au dhambi kisha akamsingizia asiye na kosa, basi amejitwika kashfa na dhambi iliyo wazi.
(113) Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yako na rehema yake, kundi moja kati yao lingedhamiria kukupoteza. Na hawapotezi isipokuwa nafsi zao, wala hawawezi kukudhuru kwa lolote. Na Mwenyezi Mungu amekuteremshia Kitabu na hekima, na akakufundisha yale uliyokuwa huyajui. Na fadhila za Mwenyezi Mungu zilizo juu yako ni kubwa.
(114) Hakuna heri katika mengi ya wanayoshauriana kwa siri, isipokuwa kwa yule anayeamrisha kutoa sadaka, au kutenda mema, au kupatanisha baina ya watu. Na mwenye kufanya hayo kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, basi tutampa ujira mkubwa.
(115) Na mwenye kumpinga Mtume baada ya kubainikiwa na uwongofu, na akafuata njia isiyokuwa ya Waumini, tutamuelekeza alikoelekea, na tutamuingiza katika Jahannam. Na hayo ni marejeo maovu zaidi.
(116) Hakika Mwenyezi Mungu hasamehi kushirikishwa na kitu. Lakini Yeye husamehe yasiyo kuwa hayo kwa amtakaye. Na mwenye kumshirikisha Mwenyezi Mungu, basi kwa hakika amepotea upotovu wa mbali.
(117) Wao hawawaombi badala yake Yeye isipokuwa vya kike, na wala hawamuombi isipokuwa Shetani aliyeasi.
(118) Mwenyezi Mungu amemlaani. Naye Shetani akasema: Hakika, nitawachukua sehemu maalum katika waja wako.
(119) Na hakika nitawapoteza, na nitawatia matamanio, na nitawaamrisha, basi watakata masikio ya wanyama, na nitawaamrisha, basi watabadili aliyoumba Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumfanya Shetani kuwa ni rafiki mwandani badala ya Mwenyezi Mungu, basi hakika amehasiri hasara ya dhahiri.
(120) Anawaahidi, na anawatia tamaa. Na Shetani hawaahidi isipokuwa udanganyifu.
(121) Hao makao yao ni Jahannam, na wala hawapati makimbilio kutoka humo.
(122) Na wale walioamini na wakatenda mema, tutawaingiza katika Bustani zipitazo mito kwa chini yake. Watadumu humo milele. Ndiyo ahadi ya Mwenyezi Mungu iliyo kweli. Na ni nani mkweli zaidi wa kauli kuliko Mwenyezi Mungu.
(123) Si kwa matamanio yenu, wala matamanio ya Watu wa Kitabu! Mwenye kufanya ubaya, atalipwa kwa huo, wala hatajipatia kando na Mwenyezi Mungu mlinzi wala wa kumnusuru.
(124) Na mwenye kufanya katika mema, akiwa wa kiume au wa kike, naye ni Muumini, basi hao wataingia Peponi wala hawatadhulumiwa kiasi cha jicho la kokwa ya tende.
(125) Na ni nani aliye bora zaidi kwa dini kuliko yule aliyeusilimisha uso wake kwa Mwenyezi Mungu hali ya kuwa ni mwema, na akafuata mila ya Ibrahim mnyoofu? Na Mwenyezi Mungu alimfanya Ibrahim kuwa ni rafiki mwandani.
(126) Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika dunia. Na Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu.
(127) Na wanakuuliza kuhusiana na wanawake. Sema: Mwenyezi Mungu anawatolea fatwa juu yao, na yale mnayosomewa katika Kitabu hiki kuhusu mayatima wanawake ambao hamuwapi kile walichoandikiwa, na mnapenda kwamba muwaoe, na kuhusu wanyonge katika watoto, na kwamba muwasimamie mayatima kwa uadilifu. Na chochote mnachofanya katika heri, basi hakika Mwenyezi Mungu anaijua vyema.
(128) Na mwanamke akihofia kutupwa au kutojaliwa na mumewe, basi si vibaya kwao wakisikizana kwa suluhu. Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa machoni mwake tamaa na uchoyo. Na mkifanya wema na mkamcha Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda.
(129) Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake, hata mkikakamia. Kwa hivyo, msiegemee moja kwa moja mkamwacha (mmojawapo) kama aliyetundikwa. Na mkisikizana na mkamcha Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(130) Na wakitengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kutoka katika wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye hekima.
(131) Na ni vya Mwenyezi Mungu tu vyote vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika dunia. Na kwa hakika tuliwausia wale waliopewa Kitabu kabla yenu, na nyinyi pia, kwamba mumche Mwenyezi Mungu. Na mkikufuru, basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika dunia. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosheleza, Msifiwa.
(132) Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
(133) Akitaka, atawaondoa, enyi watu! Na awalete wengineo. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa hayo.
(134) Mwenye kutaka malipo ya dunia, basi kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo ya dunia na Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kuona yote.
(135) Enyi mlioamini! Kuweni wenye kusimama imara katika kufanya uadilifu, wenye kushuhudia kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, hata kama ni juu ya nafsi zenu, au wazazi wawili na jamaa zenu. Akiwa tajiri au fukara, Mwenyezi Mungu ndiye anayewastahiki zaidi. Basi msifuate matamanio, mkaacha kufanya uadilifu. Na mkiupotoa au mkaupa mgongo, basi Mwenyezi Mungu anajua vyema mnayoyatenda.
(136) Enyi mlioamini! Muaminini Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha juu ya Mtume wake, na Kitabu alichokiteremsha kabla yake. Na anayemkufuru Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake, na Mitume wake, na Siku ya Akhera, basi hakika amekwisha potea kupotea kwa mbali.
(137) Hakika, wale walioamini, kisha wakakufuru, kisha wakaamini, kisha wakazidi ukafiri, Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwafutia dhambi wala wa kuwaongoa njia.
(138) Wabashirie wanafiki kwamba hakika wana adhabu chungu.
(139) Wale ambao huwafanya makafiri kuwa ndio marafiki wandani badala ya Waumini. Je, wanataka wapate kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.
(140) Naye amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki ya kwamba mnaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na zinafanyiwa kejeli, basi msikae pamoja nao, mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo mtakuwa nanyi mfano wao hao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote pamoja katika Jahannam.
(141) Wale ambao wanawangoja. Basi mkipata ushindi unaotoka kwa Mwenyezi Mungu wao husema: kwani hatukuwa pamoja nanyi? Na ikiwa ni sehemu ya makafiri kushinda, wao huwaambia: Hatukuwa ni waweza wa kuwashinda, nasi tukawakinga na hawa Waumini? Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Qiyama, wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini.
(142) Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali ni Yeye ndiye mwenye kuwahadaa wao. Na wanapoinuka kusali huinuka kwa unyong'onyo, wanajionyesha kwa watu tu, wala hawamdhukuru Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
(143) Wanayumba yumba baina ya huku na huko. Huku hawako na huko hawako. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea, kabisa hutompa njia.
(144) Enyi mlioamini! Msiwafanye makafiri kuwa ndio wasaidizi wandani badala ya Waumini. Je, mnataka kumfanyia Mwenyezi Mungu hoja iliyo wazi juu yenu?
(145) Hakika, wanafiki watakuwa katika tabaka la chini kabisa katika Moto, wala hutompata yeyote wa kuwanusuru.
(146) Isipokuwa wale waliotubu, na wakatengenea, na wakashikamana na Mwenyezi Mungu, na wakamfanyia Mwenyezi Mungu peke yake Dini yao, basi hao wako pamoja na Waumini. Na Mwenyezi Mungu atawapa Waumini ujira mkubwa.
(147) Mwenyezi Mungu atafanyia nini kuwaadhibu ikiwa mtashukuru na mkaamini? Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushukuru, Mwenye kujua.
(148) Mwenyezi Mungu hapendi kutajwa mabaya hadharani isipokuwa kwa aliyedhulumiwa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
(149) Mkidhihirisha wema au mkiuficha, au mkiyasamehe mabaya, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Muweza.
(150) Hakika, wale wanaomkufuru Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanataka kufarikisha baina ya Mwenyezi Mungu na Mitume wake, na wanasema: Wengine tunawaamini na wengine tunawakufuru. Na wanataka kushika njia iliyo kati ya hayo.
(151) Hao ndio makafiri wa hakika. Na tumewaandalia makafiri adhabu ya kudunisha.
(152) Na wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mitume wake, wala hawakumfarikisha yeyote kati yao, hao atawapa ujira wao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(153) Watu wa Kitabu wanakuuliza uwateremshie kitabu kutoka mbinguni. Na kwa hakika, walikwisha muuliza Musa makubwa zaidi ya hayo. Walisema: Tuonyeshe Mwenyezi Mungu wazi wazi. Kwa hivyo, radi ikawapiga kwa dhuluma yao hiyo. Kisha wakamchukua ndama kumwabudu, baada ya kwisha wajia hoja zilizo wazi. Nasi tukasamehe hayo, na tukampa Musa hoja zilizo dhahiri.
(154) Na tukanyanyua mlima juu yao kwa kufanya agano nao. Na tukawaambia: Ingieni mlangoni kwa kusujudu. Na tukawaambia: Msikiuke mipaka kuhusiana na Siku ya Sabato (Jumamosi). Na tukachukua kwao agano lililo madhubuti.
(155) Basi kwa sababu ya kuvunja kwao agano zao, na kuzikufuru kwao ishara za Mwenyezi Mungu, na kuwauwa kwao Manabii bila ya haki, na kusema kwao: Nyoyo zetu zimefumbwa; bali Mwenyezi Mungu ameziziba kwa kufuru zao, basi hawaamini isipokuwa kidogo tu.
(156) Na kwa kufuru zao na kusema kwao juu ya Maryam uongo mkubwa.
(157) Na kusema kwao: Hakika, sisi tulimuua Masihi Isa, mwana wa Maryam, Mtume wa Mwenyezi Mungu. Nao hawakumuua wala hawakumsulubisha, bali walifananishiwa tu. Na hakika wale waliohitalifiana katika haya wamo katika shaka nayo. Wao hawana elimu yoyote nayo isipokuwa ni kufuata dhana tu. Wala hawakumuua kwa yakini.
(158) Bali Mwenyezi Mungu alimwinua kwenda kwake, na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(159) Na hawi katika Watu wa Kitabu isipokuwa hakika atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Naye Siku ya Qiyama atakuwa shahidi juu yao.[1]
[1] Aya hii inamaanisha kwamba kila mtu miongoni mwa Watu waliopewa Kitabu kama vile Wayahudi na Wakristo kabla ya kufa kwake humwamini Isa (Yesu) kwamba ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kwamba ni Mungu wala mototo wa Mungu. Kwani wakati anapokufa, huonyeshwa uhakika wa jambo hili. Kisha Siku ya Kiyama, Isa (Yesu) atakuwa shahidi dhidi yao kwamba aliwafikishia wito wa Mola wao Mlezi, lakini wakaupuuza na kwamba Wakristo waliubadilisha. (Tafsir At-Tahriir wat-Tanwiir, cha Ibn 'Aashuur)
(160) Basi kwa sababu ya dhuluma ya wale waliotubu na kumrudia Mwenyezi Mungu (yani Mayahudi), tuliwaharimishia vitu vizuri walivyohalalishiwa. Na kwa sababu ya kuwazuilia kwao watu wengi na Njia ya Mwenyezi Mungu.
(161) Na kuchukua kwao riba, na ilhali walikwisha katazwa hilo, na kula kwao mali ya watu kwa batili. Basi tumewaandalia makafiri katika wao adhabu chungu.
(162) Lakini waliobobea katika elimu miongoni mwao, na Waumini, wanayaamini yale yaliyoteremshwa juu yako, na yale yaliyoteremshwa kabla yako. Na wanaosimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, hao tutawapa malipo makubwa.
(163) Hakika Sisi tumekufunulia wahyi wewe kama tulivyomfunulia wahyi Nuhu na Manabii waliokuwa baada yake. Na tulimfunulia wahyi Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wanawe, na Isa na Ayub na Yunus na Harun na Suleiman, naye Daud tukampa Zaburi.
(164) Na Mitume tuliokwisha kukuhadithia kabla yake, na Mitume wengine hatukukuhadithia. Na Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa kwa maneno.
(165) Mitume hao ni wabashiri na waonyaji, ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(166) Lakini Mwenyezi Mungu anayashuhudia yale aliyokuteremshia wewe. Aliyateremsha kwa elimu yake, na Malaika pia wanashuhudia. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa shahidi.
(167) Hakika, wale waliokufuru na wakaizuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, hakika wamekwisha potea kupotea kwa mbali.
(168) Hakika, wale waliokufuru na wakadhulumu, hakuwa Mwenyezi Mungu ni wa kuwafutia dhambi wala kuwaongoa njia.
(169) Isipokuwa njia ya Jahannam. Humo watadumu milele. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.
(170) Enyi Watu! Hakika, amekwisha wajia Mtume huyu kwa haki kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi aminini, ndiyo heri kwenu. Na mkikufuru, basi hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyo katika mbingu na duniani. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.
(171) Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki tu. Hakika, Masihi Isa mwana wa Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilomfikishia Maryam, na ni roho iliyotoka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komekeni! Itakuwa heri kwenu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametakasika Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote vilivyo katika mbingu na vilivyo katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.
(172) Masihi hatajiinua juu zaidi kuwa mja wa Mwenyezi Mungu, wala Malaika waliowekwa karibu. Na mwenye kujiinua juu zaidi ya kumuabudu Yeye Mwenyezi Mungu na akafanya kiburi, basi atawakusanya wote kwake.
(173) Basi wale walioamini na wakatenda mema, atawalipa ujira wao kikamilifu, na atawazidishia katika fadhila yake. Na ama wale waliojiinua juu, na wakafanya kiburi, basi atawaadhibu adhabu chungu. Wala hawajitapa kando na Mwenyezi Mungu rafiki mwandani wala wa kuwanusuru.
(174) Enyi watu! Hakika umekwisha wafikia ushahidi kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na tumewateremshia Nuru iliyo wazi.
(175) Ama wale waliomwamini Mwenyezi Mungu, na wakashikamana naye, basi atawaingiza katika rehema itokayo kwake, na fadhila, na atawaongoa kwenye Njia iliyonyooka.
(176) Wanakuuliza hukumu ya kisheria, sema: Mwenyezi Mungu anawapa hukumu ya kisheria juu ya kalala (mtu aliyekufa bila ya kuacha mzazi wala mwana. Ikiwa mtu amekufa, naye hana mwana, lakini anaye dada, basi huyo atapata nusu ya alichokiacha. Naye (mwanamume) atamrithi (dada yake) ikiwa hana mwana. Na ikiwa wao ni madada wawili, basi watapata theluthi mbili za alichokiacha. Na wakiwa ndugu wanaume na wanawake, basi wa kiume atapata sehemu iliyo sawa na ya wa kike wawili. Mwenyezi Mungu anawabainishia ili msipotee. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.