81 - Surat At-Takwir ()

|

(1) Jua litakapokunjwa,

(2) Na nyota zikazimwa,

(3) Na milima ikaondolewa,

(4) Na ngamia wenye mimba pevu watakapoachwa wasishughulikiwe,

(5) Na wanyama wa mwituni wakakusanywa,

(6) Na bahari zikawaka moto,

(7) Na nafsi zikaunganishwa,

(8) Na msichana aliyezikwa hai atakapoulizwa,

(9) Kwa kosa gani aliuliwa?

(10) Na madaftari yatakapoenezwa,

(11) Na mbingu itakapotanduliwa,

(12) Na Jahannamu itakapochochewa,

(13) Na Pepo ikasogezwa,

(14) Kila nafsi itajua ilichokihudhurisha.

(15) Ninaapa kwa nyota zinaporejea nyuma.

(16) Zinazokwenda, kisha zikajificha.

(17) Na kwa usiku unapopungua.

(18) Na kwa asubuhi inapopambazuka.

(19) Kwamba hakika bila ya shaka hii ni kauli ya Mjumbe mtukufu.

(20) Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi.

(21) Anayetiiwa, tena muaminifu.

(22) Na wala huyu mwenzenu hana wazimu.

(23) Na hakika yeye alimwona kwenye upeo wa macho ulio safi.

(24) Wala yeye si bahili kwa mambo ya ghaibu.

(25) Wala hii si kauli ya Shetani aliyelaaniwa.

(26) Basi mnakwenda wapi?

(27) Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

(28) Kwa yule miongoni mwenu anayetaka kwenda sawa.

(29) Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote.