(1) Alif Lam Mim.[1]
[1] Ama herufi za mkato mwanzoni mwa sura mbalimbali. Lililo salama zaidi kuhusiana nazo ni kukaa kimya na kutoziingilia maana zake bila ya dalili ya Kisheria, pamoja na kuwa na yakini kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuziteremsha bure, bali kwa hekima tusiyoijua. (Tafsir As-Sa'dii)
(2) Hiki ni Kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake; ni uwongofu kwa wachamungu.[1]
[1] Na kwa sababu shaka ni kusitasita kati ya mambo, basi kitu chenye shaka hakiwezi kumuongoa mtu. Na kwa sababu sifa ya Qur-aani ni kwamba haina shaka yoyote, basi ikalazimu kwamba ni yenye kuongoa. Ndiyo maana Mwenyezi Mungu akasema: "Ni uwongofu kwa wachamungu" peke yao. Kwa sababu, wasiokuwa wachamungu na wakaidi hawakosi kuwa na shaka katika jambo hata kama halina shaka yoyote. (Tafsir Al-Baqa'ii)
(3) Ambao huyaamini ya ghaibu na hushika Sala, na hutoa katika[1] tuliyowapa (tuliyowaruzuku).
[1] Na alitumia neno “min (katika)” linalomaanisha baadhi (ya kitu), ili awatanabahishe kuwa yeye kwa hakika hakuta kutoka kwao isipokuwa sehemu ndogo kutoka kwa mali zao, ambayo haina madhara kwao wala uzito wowote, bali wao wanafaidika kwa kuitoa, na pia ndugu zao wanafaidika kwayo.
(4) Na ambao wanayaamini yaliyoteremshwa kwako, na yaliyoteremshwa kabla yako; na Akhera wana yakini nayo.
(5) Hao wapo juu ya uwongofu utokao kwa Mola wao Mlezi, na hao ndio waliofaulu.[1]
[1] Kwa sababu Qur-ani ndio uwongofu wao, limetumika neno "juu" ili kuifananisha hali ya kuimarika kwa Waumini katika uwongofu na uthabiti wao juu yake; na kujaribu kwao kuuongeza na kutembea katika njia za heri. Na mwonekano wa (mtu) aliyepanda kipando (kama farasi) katika kuwa kwake juu ya kipando hicho, na uwezo wake wa kukiendesha na kukifanya kuwa kitiifu. (Tafsir At-Tahrir Wat-tanwiir cha Ibn 'Aashuur)
(6) Hakika, wale waliokufuru[1] ni sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawaamini.[2]
[1] Maana ya 'ukafiri' katika lugha ya Kiarabu ni kufunika kitu. Kwa hivyo, mtu kafiri ameitwa kwa hilo jina kwa sababu yeye huifunika haki. (Zaad Al-Masiir fii 'ilm At-Tafsiir, cha Ibn Al-Jawzii).
[2] Alipowataja Waumini na hali zao (katika aya ya pili hadi ya tano), akawataja makafiri na hatima yao (katika aya ya sita na saba) (Tafsir Al-Qurtubii).
(7) Mwenyezi Mungu ameziziba nyoyo zao na masikio yao, na juu ya macho yao pana pazia. Nao wana adhabu kubwa.[1]
[1] Na kauli yake "wana" inaashiria kwamba hali yao inaitisha sana adhabu hii, na kwamba wanaistahiki, na kwamba nafsi zao zinaelekea kwenye adhabu hiyo mpaka waione waziwazi. Na kauli yake "kubwa" ni kwa sababu itaiadhibu miili yao kiujumla bila kuacha chochote, kwa sababu miili yao na nafsi zao na roho zao havikugusa chochote cha kuwazuia kutokana na adhabu. (Tafsir Al-Baqa'ii)
(8) Na katika watu, wapo wasemao: Tumemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, wala wao si wenye kuamini.[1]
[1] Alipowaeleza Waumini mwanzoni mwa sura hii kwa aya nne (kuanzia aya ya pili hadi ya tano), kisha akabainisha hali ya makafiri kwa aya mbili (ya sita na saba). Mwenyezi Mungu Mtukufu akaanza kueleza hali ya wanafiki wanaodhihirisha imani na kuficha ukafiri. Na kwa kuwa jambo lao huwa linawachanganya watu wengi, akarefusha mno katika kuwataja kwa sifa zao nyingi (katika aya kumi na tatu). (Tafsir Ibn Kathir)
(9) Wanamhadaa Mwenyezi Mungu na wale walioamini, lakini hawahadai ila nafsi zao; nao hawatambui.[1]
[1] Wanaitakidi kwa ujinga wao kuwa wao wanamhadaa Mwenyezi Mungu na Waumini kwa kudhihirisha kwao Imani na kuficha kwao ukafiri. Nao hawamhadai yoyote isipokuwa wao wenyewe, kwa kuwa, madhara ya kuhadaa kwao yanawarudia wao. Na kwa sababu ujinga wao umekolea na nyoyo zao zimeharibika, huwa hawana hisia ya hilo. (Tafsir Muyasar cha jopo la wanachuoni)
(10) Nyoyoni mwao mna maradhi[1], na Mwenyezi Mungu amewazidishia maradhi. Basi watakuwa na adhabu chungu kwa sababu ya kusema kwao uongo.[2]
[1] Kilichokusudiwa na maradhi hapa ni maradhi ya shaka, dhana potovu na unafiki. (Tafsir Assa'dii).
[2] Al-Junayd alisema: Ugonjwa wa nyoyo ni kufuata matamanio, kama vile ugonjwa wa viungo ni yale maradhi ya kiwiliwili. (Tafsir Al-Qurtubii).
(11) Na wanapoambiwa: Msifanye uharibifu katika ardhi. Husema: Bali sisi ni watengenezaji.[1]
[1] Na kujengeka kwa kitendo hiki (wanapoambiwa) katika hali ya kutomtaja anayewaambia, kunaashiria kwamba wao humuasi yeyote yule anayewaambia hata awe ni nani. (Tafsir Nidhaam Addurar fii Tanasub Al-Aayat Wassuwar cha Al-Baqaa'ii)
(12) Tambueni! Kwa hakika, wao ndio waharibifu, lakini hawatambui.
(13) Na wanapoambiwa: Aminini kama walivyoamini watu. Husema: Tuamini kama walivyoamini wapumbavu? Hakika wao ndio wapumbavu, lakini hawajui tu.[1]
(14) Na wanapokutana na walioamini husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao na mashet'ani wao, husema: Hakika sisi tu pamoja nanyi. Hakika sisi tunawadhihaki tu.
(15) Mwenyezi Mungu atawadhihaki wao na atawaacha katika upotovu wao wakitangatanga ovyo.
(16) Hao ndio walioununua upotovu kwa uwongofu; lakini biashara yao haikupata faida, wala hawakuwa wenye kuongoka.[1]
[1] Na huu ni katika mifano mizuri kabisa. Kwani (mnafiki) aliufanya upotovu ambao ndio shari kubwa zaidi kuwa bidhaa, na akaufanya uwongofu ambao ndio kutengenea kukubwa zaidi pahali pa bei. Kwa hivyo, wakautoa uwongofu (ambayo ndiyo bei) kwa kuukataa na kuutaka upotovu (ambayo ndiyo bidhaa). (Tafsir Assa'dii) Lakini biashara hiyo yao haikupata faida, pamoja na kudai kwao kwamba wao ndio wajuzi zaidi katika hilo la kutengeneza. Na wala hawakuongoka, yaani walipoteza mpaka mtaji wao, yani uwongofu wa Qur-aani. (Tafsir Nidhaam Addurar fii Tanasub Al-Aayat Wassuwar cha Al-Baqaa'ii)
(17) Mfano wao ni kama mfano wa aliyekoka moto, na ulipoangaza vile vilivyoko kandokando yake, Mwenyezi Mungu aliiondoa nuru yao na akawaacha katika viza mbalimbali, hawaoni.[1]
[1] Huu ni mfano wa yule aliyekuwa katika giza kubwa, kwa hivyo akauwasha moto kutoka kwa mtu mwingine. (Tafsir Assa'dii) Na nuru ya moto huo ilitoka kwa Waislamu ambao wao (wanafiki) wanaishi pamoja nao. Na hakusema: Mwenyezi Mungu aliuondoa 'mwangaza wao'. Kwa sababu mwangaza ni ziada juu ya nuru. Kwa hivyo, aliondoa asili (nuru) na ziada yake (mwangaza). (Tafsir Ibn Al-Qayyim)
(18) Ni viziwi, mabubu, vipofu; kwa hivyo hawatarejea.[1]
[1] Ni viziwi kwa sababu hawaisikii heri. Ni mabubu kwa sababu hawaitamki heri. Na ni vipofu kwa sababu hawaioni haki. Kwa hivyo, hawatarejea kwa haki kwa kuwa waliiacha baada ya kuijua. Tofauti na mwenye kuiacha haki kwa ujinga na upotovu, yeye yuko karibu zaidi na kurudi katika haki. (Tafsir Assa'dii)
(19) Au ni kama mvua kubwa itokayo mbinguni, ina viza mbalimbali, na radi, na umeme; wakawa wanatia vidole vyao katika masikio yao kwa sababu ya mapigo ya radi, kwa kuogopa kufa. Na Mwenyezi Mungu amewazunguka makafiri.[1]
[1] Hapa Mwenyezi Mugnu aliufananisha uwongofu aliowaongoza kwao waja wake, na mvua. Kwa sababu, nyoyo huhuishwa kwa uwongofu, kama vile ardhi huhuishwa na mvua. Na fungu la wanafiki katika uwongofu huo ni kama fungu la yule ambaye hakupata katika mvua isipokuwa giza, radi na umeme, wala hana fungu zaidi ya hayo katika yale yaliyokusudiwa kutoka kwa mvua hiyo kama vile uhai wa nchi, watu, miti na wanyama. (Tafsir Ibn Al-Qayyim)
(20) Unakaribia umeme kunyakua macho yao. Kila ukiwatolea mwangaza, wanatembea ndani yake. Na linapowawia giza, wanasimama. Na angelitaka Mwenyezi Mungu angeliondoa kusikia kwao na kuona kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.[1]
[1] Aya imemalizika kwa kusema: "Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu." Kwa sababu aliwaonya wanafiki juu ya adhabu yake na uwezo wake, na akawaambia kwamba amewazunguka, na kwamba ana uwezo wa kuondoa kusikia na kuona kwao. (Tafsir Ibn Kathir)
(21) Enyi watu! Muabuduni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni nyinyi na wale wa kabla yenu, ili mpate Kumcha Mwenyezi Mungu.[1]
[1] "Enyi watu" inawaamrisha wanadamu wote. (Tafsir Ibn Al-Qayyim)
(22) (Mwenyezi Mungu) ambaye amekufanyieni ardhi hii kuwa kama tandiko, na mbingu kama paa. Na akateremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo akatoa mazao yawe riziki zenu.[1] Basi msimfanyizie Mwenyezi Mungu washirika, na hali nyinyi mnajua.[2]
[1] Unaonaje mtu ambaye atazinduka kutoka usingizini au katika hali ya kughafilika, (yani kuumbwa) na akakuta ametandikiwa zulia zuri (yani ardhi) na ameekewa hema (yani mbingu) hapo; na kuwekewa chakula na kinywaji. Je hapaswi kumshukuru aliyetenda haya? Basi hii ndiyo maana ya aya hii. (Tafsir Al-Baqqaa'ii)
[2] "Na hali nyinyi mnajua" kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye aliyefanya vitendo hivyo vyote. Basi ni vipi mnamfanyia washirika? (Tafsir Ibn Al-Qayyim)
(23) Na ikiwa mna shaka kwa hayo tuliyomteremshia mja wetu, basi leteni sura moja ya mfano wake, na muwaite mashahidi wenu badala ya Mwenyezi Mungu, ikiwa mnasema kweli.
(24) Na ikiwa hamtofanya - na wala hamtofanya kamwe - basi uogopeni moto ambao kuni zake ni watu na mawe, umeandaliwa makafiri.
(25) Na wabashirie walioamini na wakatenda mema kwamba watapata mabustani yapitayo mito kati yake; kila watakapopewa matunda humo, watasema: Haya ndiyo kama tuliyopewa mbele. Na wataletewa matunda yaliyofanana; na humo watakuwa na wake waliotakasika; na wao humo watadumu.
(26) Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walioamini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyotoka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale waliokufuru husema: Ni nini analokusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu.
(27) Wanaovunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kwisha ifunga, na wakayakata aliyoamrisha Mwenyezi Mungu kuungwa, na wakafanya uharibifu katika nchi; hao ndio wenye hasara.
(28) Vipi mnamkanusha Mwenyezi Mungu na hali mlikuwa wafu, akakufufueni! Kisha atakufisheni, tena atakufufueni, kisha kwake mtarejeshwa?
(29) Yeye ndiye aliyekuumbieni vyote vilivyo katika ardhi, kisha akaelekea kuziumba mbingu, na akazifanya mbingu saba, naye ndiye ajuaye mno kila kitu.
(30) Na pale Mola wako Mlezi alipowaambia Malaika: Mimi nitamweka katika ardhi Khalifa (mfwatizi), wakasema: Utaweka humo atakayefanya uharibifu humo na kumwaga damu, hali sisi tunakutakasa kwa sifa zako na tunakutaja kwa utakatifu wako? Akasema: Hakika Mimi nayajua msiyoyajua.
(31) Na akamfundisha Adam majina ya vitu vyote, kisha akaviweka mbele ya Malaika, na akasema: Niambieni majina ya hivi ikiwa mnasema kweli.
(32) Wakasema: Subhanaka (Wewe umetakasika!) Hatuna ujuzi isipokuwa kwa uliyotufunza Wewe. Hakika Wewe ndiye Mjuzi Mwenye hekima.
(33) Akasema: Ewe Adam! Waambie majina yake. Basi alipowaambia majina yake alisema: Sikukwambieni kwamba Mimi ninajua siri za mbinguni na za duniani, na ninayajua mnayoyadhihirisha na mliyokuwa mnayaficha?
(34) Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam, wakamsujudia wote isipokuwa Iblis, alikataa na akajivuna na akawa katika makafiri.
(35) Na tulisema: Ewe Adam! Kaa wewe na mkeo katika Bustani, na kuleni humo maridhawa popote mpendapo, lakini msiukaribie mti huu tu; mkawa katika wale waliodhulumu.
(36) Lakini Shet'ani aliwatelezesha hao wawili na akawatoa katika waliyokuwamo, na tukasema: Shukeni, nanyi ni maadui nyinyi kwa nyinyi. Katika ardhi yatakuwa makaazi yenu na starehe kwa muda.
(37) Kisha Adam akapokea maneno kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Mola wake Mlezi alimkubalia toba yake; hakika Yeye ndiye Mwingi wa kukubali toba na Mwenye kurehemu.
(38) Tukasema: Shukeni nyote; na kama ukikufikieni uwongofu utokao kwangu, basi watakaofuata uwongofu wangu huo, haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
(39) Na wenye kukufuru na kuzikanusha ishara zetu, hao ndio wenza wa Moto, wao watadumu humo.[1]
[1] Na maana wenza ni yule anayekaa na kuandamana nawe na hamuachani. (Tafsir Al-Alusii) Hao pia wataandamana na Moto bila ya kuachana kama wenza.
(40) Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyokuneemesheni, na timizeni ahadi yangu, na Mimi nitatimiza ahadi yenu, na niogopeni Mimi tu.[1]
[1] “Enyi Wana wa Israili!” Anayekusudiwa na Israili hapa ni (Nabii) Yaaqub, amani iwe juu yake. (Tafsir Assa'dii)
(41) Na aminini niliyoyateremsha ambayo yanasadikisha mliyo nayo, wala msiwe wa kwanza kuyakataa. Wala msiuze Ishara zangu kwa thamani ndogo. Na niogopeni Mimi tu.[1]
[1] Aya hii inawaonya wana wa Israili dhidi ya kuyauza mafundisho ya Mwenyezi Mungu kwa kuficha maelezo ya Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake - yaliyopo katika vitabu vyao. Na kuchukua "thamani ndogo" ya duniani kama vile yale wanayopata kutoka kwa wafuasi wao kama vile chakula, uongozi n.k. (Tafsir Al-Wajiiz cha Al-Waahidii)
(42) Wala msichanganye kweli na uwongo, na mkaificha kweli nanyi mnajua.
(43) Na shikeni Sala, na toeni Zaka, na inameni pamoja na wanaoinama.
(44) Je, mnawaamrisha watu mema na mnazisahau nafsi zenu, na hali nyinyi mnasoma Kitabu? Basi je, hamzingatii?
(45) Na tafuteni msaada kwa kusubiri na kwa kusali; na kwa hakika jambo hilo ni gumu isipokuwa kwa wanyenyekevu.[1]
[1] Na alipowakataza kufuata matamanio yao, akawaongoza kwenye dawa ya hilo, ambayo ni maadili makubwa zaidi ya kinafsi na matendo bora ya kimwili, ambayo ni kuwa na "subira" katika kudhihirisha haki na kutotii matamanio ya nafsi zao katika hilo. Na "swala" ambayo inafikisha katika vyeo vikubwa zaidi kuliko hivyo vya kidunia. (Tafsir Al-Baqaa'ii)
(46) Ambao wana yakini kuwa hakika watakutana na Mola wao Mlezi na ya kuwa hakika watarejea kwake.
(47) Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni zile neema zangu nilizokuneemesheni, na nikakuteueni kuliko wote wengineo.
(48) Na icheni Siku ambayo mtu hatomfaa mtu kwa lolote, wala hayatakubaliwa kwake maombezi, wala hakitapokewa kikomboleo kwake; wala hawatanusuriwa.[1]
[1] Aya hii imekanusha (huko Akhera) mambo ambayo wanadamu wamezoea kuyafanya katika dunia hii wanapopatwa na shida. (Tafsir Assa'dii). Nayo ni kufanyiwa uombezi, au kutoa fidiya, au kunusuriwa. (Tafsir Al-Muharrar Al-Wajiiz cha Ibn Atwiyya)
(49) Na (kumbukeni) tulipowaokoa kutoka kwa watu wa Firauni, waliokuwa wakiwapa adhabu mbaya, wakiwachinja wana wenu wa kiume, na wakiwawacha hai wanawake wenu. Na katika hayo kulikuwa na mtihani mkubwa kutoka kwa Mola wenu Mlezi.
(50) Na tulipoipasua bahari kwa ajili yenu na tukakuokoeni, tukawazamisha watu wa Firauni, na huku mnatazama.
(51) Na tulipomuahidi Musa masiku arubaini, kisha mkamchukua ndama (mkamuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
(52) Kisha tukakusameheni baada ya hayo, ili mpate kushukuru.
(53) Na tulipompa Musa Kitabu na pambanuo ili mpate kuongoka.
(54) Na Musa alipowaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmezidhulumu nafsi zenu kwa kuchukua kwenu ndama (kumuabudu). Basi tubuni kwa Muumba wenu na ziueni nafsi zenu. Haya ni bora kwenu mbele ya Muumba wenu. Naye akapokea toba yenu. Hakika Yeye ndiye apokeaye toba na Mwenye kurehemu.
(55) Na mliposema: Ewe Musa! Hatutakuamini mpaka tumwone Mwenyezi Mungu waziwazi. Ukakunyakueni mpigo wa radi nanyi mnaangalia.
(56) Kisha tukakufufueni baada ya kufa kwenu, ili mpate kushukuru.
(57) Na tukakutilieni kivuli kwa mawingu na tukakuteremshieni Manna na Salwa; tukakwambieni: Kuleni vitu vizuri hivi tulivyokuruzukuni. Nao hawakutudhulumu Sisi lakini walikuwa wanazidhulumu nafsi zao.
(58) Na tuliposema: Ingieni mji huu, na humo mle mpendapo maridhawa, na ingieni katika mlango wake kwa unyenyekevu, na semeni: Tusamehe! Tutakusameheni makosa yenu, na tutawazidishia wema wafanyao wema.
(59) Lakini waliodhulumu waliibadili kauli isiyo kuwa waliyoambiwa. Kwa hivyo tukaiteremsha juu ya wale waliodhulumu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya walivyokuwa wamepotoka.
(60) Na Musa alipoomba maji kwa ajili ya watu wake, tulimwambia: Lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikatimbuka chemichemi kumi na mbili; kila kabila likajua mahali pake pa kunywea. Tukawaambia: Kuleni na mnywe riziki ya Mwenyezi Mungu, wala msiasi katika nchi mkafanya uharibifu.
(61) a mliposema: Ewe Musa! Hatuwezi kuvumilia chakula cha namna moja tu, basi tuombee kwa Mola wako Mlezi atutolee vile vinavyomea katika Ardhi, kama mboga zake, na matango yake, na thom zake, na adesi zake, na vitunguu vyake. Akasema: Mnabadili kilicho duni kwa kilicho bora? Shukeni mjini, huko mtapata mlivyoviomba. Na wakapigwa na unyonge,na umasikini, na wakastahili ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na haya ni kwa sababu walikuwa wakiyakataa maneno ya Mwenyezi Mungu, na wakiwauwa Manabii pasipo haki. Hayo ni kwa walivyoasi na wakapindukia mipaka.[1]
[1] Hapa kuna tishio kwa umma huu kwa wale wanaoitaka dunia sana ambao huchagua vilivyo chini, yani vilivyo haramu, na kuacha vile vilivyo juu, yani halali, ili wasije wakawa kama hao wana wa Israil . (Tafsir Al-Biqaa'ii)
(62) Hakika Walioamini, na Mayahudi na Wakristo, na Wasabai; yeyote atakayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na akatenda mema basi watapata malipo yao kwa Mola wao Mlezi, wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.[1]
[1] Hii ilikuwa hukumu yao kabla ya utume wa Muhammad - rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake. Na aya hii ilitajwa hapa kwa sababu Mwenyezi Mungu alipowakashifu wana wa Israil kwa dhambi zao, na maovu yao, huenda iliingia katika nafsi za baadhi yao kwamba sio wote waliyafanya hayo. Kwa hivyo, aya hii ikawaondoa wale ambao hawakuhusika katika kashfa hiyo. (Tafsir Assa'dii)
(63) Na tulipochukua ahadi yenu, na tukaunyanyua mlima juu yenu (tukakwambieni): Shikeni kwa nguvu haya tuliyokupeni, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kuokoka.
(64) Kisha mligeuka baada ya haya. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema zake, mngelikuwa miongoni mwa wenye kupata hasara.
(65) Na hakika mlikwisha yajua ya wale miongoni mwenu waliopindukia mipaka kuhusu Sabato, (siku ya mapumziko, Jumamosi) na tukawaambia: Kuweni manyani mliodhalilika.
(66) Kwa hivyo tukayafanya hayo kuwa onyo kwa wale waliokuwa katika zama zao na waliokuja baada yao, na mawaidha kwa wachamungu.
(67) Na Musa alipowaambia watu wake: Hakika Mwenyezi Mungu anakuamrisheni mchinje Ng'ombe. Wakasema: Je! Unatufanyia mzaha? Akasema: "Audhu billahi!" Najikinga kwa Mwenyezi Mungu nisiwe miongoni mwa wajinga.
(68) akasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni Ng'ombe gani? Akasema: Hakika Yeye anasema kwamba Ng'ombe huyo si mpevu, wala si kinda, bali ni wa katikati baina ya hao. Basi fanyeni mnavyoamrishwa.
(69) Wakasema: Tuombee kwa Mola wako atupambanulie ipi rangi yake? Akasema: Yeye anasema, kuwa Ng'ombe huyo ni wa manjano, na rangi yake imekoza, huwapendeza wanaomtazama.
(70) Wakasema: Tuombee kwa Mola wako Mlezi atupambanulie ni yupi? Hakika tunaona ng'ombe wamefanana. Na kwa yakini, Inshaallah, Mwenyezi Mungu akipenda, tutaongoka.
(71) Akasema: Yeye anasema: Kuwa huyo ni Ng'ombe asiyetiwa kazini kulima Ardhi wala kumwagia maji mimea, mzima, hana baka. Wakasema: Sasa umeleta (jambo la) haki. Basi wakamchinja, na walikaribia kuwa wasifanye hayo.
(72) Na mlipo muua mtu, kisha mkakhitalifiana kwayo, na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuyatoa hayo mliyokuwa mkiyaficha.
(73) Tukasema: Mpigeni kwa kipande chake (huyo Ng'ombe). Ndivyo hivi Mwenyezi Mungu huwahuisha wafu; na anakuonyesheni Ishara zake ili mpate kufahamu.
(74) Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, hata zikawa kama mawe au ngumu zaidi; kwani kuna mawe yanayotimbuka mito, na kuna mengine yanayopasuka yakatoka maji ndani yake, na kuna mengine huanguka kwa sababu ya kumhofu Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.
(75) Mnatumai watakuaminini na hali baadhi yao walikuwa wakisikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha wanayabadili baada ya kuwa wameyafahamu, na hali wanajua?
(76) Na wanapokutana na wale walioamini, husema: Tumeamini. Na wanapokuwa peke yao, wao kwa wao, husema: Mnawaambia aliyokufunulieni Mwenyezi Mungu ili wapate kukuhojieni mbele ya Mola wenu Mlezi? Basi hamfahamu nyinyi?
(77) Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyaficha na wanayoyatangaza?
(78) Na wamo miongoni mwao wasiojua kusoma; hawakijui Kitabu isipokuwa uongo wanaoutamani, nao hawana ila ni kudhania tu.
(79) Basi ole wao wanaoandika kitabu kwa mikono yao, kisha wakasema: Hiki kimetoka kwa Mwenyezi Mungu, ili wanunue kwacho thamani ndogo. Basi ole wao kwa yale iliyoyaandika mikono yao, na ole wao kwa yale wanayoyachuma.
(80) Na walisema: Hautatugusa Moto ila kwa siku chache tu. Sema: Mmechukua ahadi kwa Mwenyezi Mungu? Kweli Mwenyezi Mungu hatokwenda kinyume na ahadi yake. Au mnamsingizia Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua?
(81) Ndiyo, anayechuma ubaya - na makosa yake yakamzunguka, hao ndio wenzi wa Moto; humo watadumu.
(82) Na wale walioamini na wakatenda mema, hao ndio wenzi wa Pepo, humo watadumu.
(83) Na tulipofunga agano na Wana wa Israili: Hamtamuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu; na muwafanyie wema wazazi na jamaa na mayatima na masikini, na semeni na watu kwa wema, na shikeni Swala, na toeni Zaka. Kisha mkageuka isipokuwa wachache tu katika nyinyi; na nyinyi mnapuuza.[1]
[1] Mwenyezi Mungu aliwaamrisha kuwafanyia wema wazazi, na akaunganisha katika Aya hii haki ya wazazi na tawhidi, kwa sababu malezi ya kwanza yalitoka kwa Mwenyezi Mungu, na malezi ya pili yanatoka kwa wazazi. (Tafsir Al-Qurtubii)
(84) Na tulipochukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali, nanyi mnashuhudia.
(85) Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauwana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani mwao, mkisaidiana (na adui zao) dhidi yao kwa dhambi na uadui. Na wakikujieni mateka, mnawakomboa, na hali kuwatoa mmekatazwa. Je, mnaamini baadhi ya Kitabu na mnakataa baadhi yake? Basi ni yapi malipo ya mwenye kutenda hayo miongoni mwenu ila aibu katika maisha ya duniani, na Siku ya Kiyama watapelekwa kwenye adhabu kali kabisa. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda.
(86) Hao ndio walionunua uhai wa dunia kwa (uhai wa) Akhera. Kwa hivyo, hawatapunguziwa adhabu, wala hawatanusuriwa.
(87) Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukafuatisha baada yake Mitume wengine. Na tukampa Isa, mwana wa Mariamu hoja waziwazi, na tukamtia nguvu kwa Roho Takatifu. Basi kila walipokufikieni Mitume kwa yale ambayo hayapendwi na nafsi zenu, mlijivuna; wengine mkawakanusha, na wengine mkawauwa.
(88) Na walisema: Nyoyo zetu zimefunikwa. Bali Mwenyezi Mungu amewalaani kwa kufuru zao; kwa hivyo ni kidogo tu wanayoyaamini.
(89) Na kilipowajia Kitabu kitokacho kwa Mwenyezi Mungu kinacho thibitisha waliyo nayo - na wao walikuwa wakitafutia ushindi kuwashinda makafiri - yalipowajia yale waliyokuwa wakiyajua, waliyakanusha. Basi laana ya Mwenyezi Mungu juu ya wakanushao!
(90) Kiovu kweli walichoziuzia nafsi zao, nacho ni kule kukataa kwao aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya kuona haya kwa kuwa Mwenyezi Mungu humteremshia fadhila yake amtakaye miongoni mwa waja wake. Basi wamejiletea wenyewe ghadhabu juu ya ghadhabu. Na makafiri watapata mateso ya kudhalilisha.
(91) Na wanapoambiwa: Yaaminini aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu. Wao husema: Tunaamini tuliyoteremshiwa sisi. Na huyakataa yasiyokuwa hayo. Na hali ya kuwa hii ndiyo haki inayothibitisha yale waliyo nayo wao. Sema: Mbona mliwauwa Manabii wa Mwenyezi Mungu hapo zamani ikiwa kweli mlikuwa Waumini?
(92) Na alikujieni Musa na hoja zilizo wazi, kisha mkamchukua ndama (kumuabudu) baada yake, na mkawa wenye kudhulumu.
(93) Na tulipochukua ahadi yenu na tukauinua mlima juu yenu (tukakwambieni): Kamateni kwa nguvu haya tuliyokupeni na sikieni. Wakasema: Tumesikia na tumekataa! Na wakanyweshwa nyoyoni mwao (imani ya) ndama kwa kufuru yao. Sema: Ni uovu mno iliyokuamrisheni imani yenu ikiwa ni wenye kuamini.
(94) Sema: Ikiwa ile nyumba ya Akhera iliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni yenu tu bila ya watu wengine, basi tamanini mauti kama nyinyi mnasema kweli.
(95) Wala hawatayatamani kamwe; kwa sababu ya yale mikono yao ilitanguliza. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua vyema wanaodhulumu.
(96) Na hakika utawapata ni wenye pupa ya kuishi kuwashinda watu wote, na kuliko washirikina. Mmoja wao anatamani lau angelipewa umri wa miaka elfu. Wala hilo (la kuzidishiwa umri) haliwezi kumweka mbali na adhabu, ili apewe umri mrefu. Na Mwenyezi Mungu anayaona wanayoyatenda.
(97) Sema: Aliyekuwa ni adui wa Jibril, basi huyo ndiye aliyeiteremsha Qur'ani moyoni mwako kwa idhini ya Mwenyezi Mungu inayothibitisha yaliyokuwa kabla yake, na ni uwongofu na bishara njema kwa Waumini.
(98) Aliyekuwa adui wa Mwenyezi Mungu na Malaika wake na Mitume wake na Jibril na Mikail, basi hakika Mwenyezi Mungu ni adui wa makafiri.
(99) Hakika tumekuteremshia Ishara zilizo wazi na hapana anayezikufuru isipokuwa wenye kupindukia mipaka (wapotovu).
(100) Je, ati ndio kila wanapofunga ahadi, huwapo kikundi miongoni mwao kikaivunja? Bali wengi wao hawaamini.
(101) Na alipowajia Mtume kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mwenye kuthibitisha yale waliyo nayo, kundi moja miongoni mwa wale waliopewa Kitabu lilitupa Kitabu cha Mwenyezi Mungu hicho nyuma ya migongo yao kama kwamba hawajui.
(102) Na wakafuata yale waliyosoma mashetani katika ufalme wa Suleiman. Na wala Suleiman hakukufuru, bali mashetani ndio waliokufuru, wakiwafundisha watu uchawi, na yaliyoteremshwa kwa wale Malaika wawili, Haarut na Maarut huko Baabil. Wala hao hawakumfundisha yeyote mpaka wamwambie: Hakika sisi ni mtihani; basi usikufuru. Wakajifunza kwa hao wawili yale ya kumfarikisha mtu na mkewe. Wala hawawezi kumdhuru mtu ila kwa kutaka kwa Mwenyezi Mungu. Na wanajifunza yenye kuwadhuru wala hayawanufaishi. Na hakika, walikwishajua kwamba mwenye kuununua (uchawi), hatakuwa na fungu lolote katika Akhera. Na hakika ni kiovu mno walichouza kwacho nafsi zao, laiti wangelikuwa wanajua.[1]
[1] Na Suleiman amani iwe juu yake alipokufa, mashetani waliandika aina za uchawi katika kitabu, kisha wakakipiga kwa muhuri wa Suleiman. Kisha wakakizika chini ya kiti chake. Baadaye Wana wa Israili wakakikuta na wakasema: Ufalme wa Suleiman haukuwa isipokuwa kwa haya. Kwa hivyo, wakaeneza uchawi katika watu. (Tafsir Al-Baqaa'ii)
(103) Na lau kuwa wangeamini na wakamcha Mungu, bila ya shaka malipo yatokayo kwa Mwenyezi Mungu yangekuwa bora. Laiti wangelikuwa wanajua!
(104) Enyi mlioamini! Msiseme: "Raa'ina", na semeni: "Ndhurna". Na sikieni! Na makafiri watapata adhabu chungu.
(105) Waliokufuru miongoni mwa watu wa Kitabu na washirikina hawapendi mteremshiwe heri yoyote kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na Mwenyezi Mungu humkusudia kumpa rehema yake ampendaye. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kubwa.
(106) Ishara yoyote tunayoifuta au tunayoisahaulisha, tunaileta iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu?
(107) Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa Mbingu na Ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.
(108) Au mnataka kumuuliza Mtume wenu kama alivyoulizwa Musa zamani? Na anayebadilisha Imani kwa ukafiri bila ya shaka, huyo ameipotea njia iliyo sawa.
(109) Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wangekurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwisha wapambanukia haki. Basi sameheni na tupilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atakapoleta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(110) Na simamisheni Swala na toeni Zaka; na heri mtakazozitangulizia nafsi zenu, mtazikuta kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyafanya.
(111) Na walisema: Hataingia Peponi ila aliyekuwa Myahudi au Mkristo. Hayo ni matamanio yao. Sema: Leteni ushahidi wenu kama nyinyi ni wasema kweli.
(112) Sivyo hivyo! Yeyote anayeelekeza uso wake kwa Mwenyezi Mungu, naye ni mtenda mema, basi ana malipo yake kwa Mola wake Mlezi; wala haitakuwa hofu juu yao wala hawatahuzunika.
(113) Na Mayahudi husema: Wakristo hawana lao jambo (wanalolifuata). Na Wakristo husema: Mayahudi hawana lao jambo (wanalolifuata). Na ilhali wote wanasoma Kitabu kicho hicho (Biblia). Na kadhaalika walisema wale wasiojua kitu mfano wa kauli yao hii. Basi Mwenyezi Mungu atahukumu baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakikhitilafiana.
(114) Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayezuia misikiti ya Mwenyezi Mungu kutajwa ndani yake jina lake, na akajitahidi kuiharibu? (Watu) hao haitawafalia kuingia humo isipokuwa kwa hofu. Duniani watapata hizaya (aibu kubwa maishani), na Akhera watapata adhabu kubwa.[1]
[1] Kuiharibu ni kwa aina mbili: kihisia na kimaana. Ama kuiharibu kwa kihisia ni kuibomoa, kuiharibu, na kuichafua. Nako kuharibu kwa kimaana ni kuwazuia wale wanaolitaja jina la Mwenyezi Mungu ndani yake (Tafsir Assa'dii).
(115) Na mashariki na magharibi ni za Mwenyezi Mungu. Basi kokote mnakoelekea, huko Mwenyezi Mungu yupo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye elimu.
(116) Na ati wanasema: Mwenyezi Mungu ana mwana. Subhanahu (ametakasika na hayo!) Bali vyote vilivyomo mbinguni na duniani ni vyake. Vyote vinamdhalilikia Yeye kwa hofu.[1]
[1] Katika Aya hii, kuna kukanusha Mwenyezi Mungu kuwa na mwana. Kwa sababu, Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake bila ya mfano wa awali. Basi hakuna hata mmoja katika viumbe hao anayestahiki kuwa mwanawe, bali kila kitu humo ni waja (viumbe) wa Mwenyezi Mungu Mtukufu. (Tafsir Attahrir wa Attanwir cha Ibn 'Aashur)
(117) Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi pasina mfano wa awali; na anapotaka jambo, basi Yeye kwa hakika huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa.[1]
[1] Na kauli yake, "Na anapotaka jambo, basi Yeye kwa hakika huliambia tu: Kuwa! Nalo huwa," ni jawabu kwa dhana potofu ya Wakristo kwamba Mwenyezi Mungu ana mwana; ati kwa sababu kupatikana kwa Masihi bila ya baba ni dalili ya kuwa yeye ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu akaweka wazi kwamba kuunda vitu bila ya kutokana na kitu ni ajabu zaidi kuliko hilo la Masihi (kuwa na mama bila baba). (Tafsir Attahrir wa Attanwir cha Ibn 'Aashur)
(118) Na walisema wale wasiojua kitu: Mbona Mwenyezi Mungu hasemi nasi au zikatufikia Ishara. Kama hivyo walisema wale waliokuwa kabla yao mfano wa kauli yao hii. Nyoyo zao zimefanana. Hakika Sisi tumeziweka wazi Ishara kwa watu wenye yakini.
(119) Hakika Sisi tumekutuma kwa haki uwe mbashiri, na mwonyaji. Na wala hutaulizwa juu ya watu wa Motoni.
(120) Na Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao. Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio uwongofu. Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yaliyokujia katika elimu, hutapata mlinzi wala msaidizi kando na Mwenyezi Mungu.[1]
[1] Mayahudi na Manaswara hawawaridhii Waislamu kwa chochote isipokuwa kwamba wawafuate katika dini yao. Lakini hayo waliyo nayo ni matamanio tu, siyo dini ya haki, kwa dalili ya kauli yake. "Na kama ukifuata matamanio yao baada ya yale yaliyokujia katika elimu, basi hutapata mlinzi wala msaidizi yeyote kando na Mwenyezi Mungu." (Tafsir Assa'dii)
(121) Wale tuliowapa Kitabu, wanakisoma kama ipasavyo kusomwa. Hao ndio kweli wanakiamini. Na wanaokikataa, basi hao ndio wenye kukhasiri.
(122) Enyi Wana wa Israili! Kumbukeni neema yangu niliyokuneemesheni, na hakika Mimi nikakufadhilisheni kuliko wengineo wote.
(123) Na icheni siku ambayo hatamfaa mtu mwenziwe kwa lolote, wala hakitakubaliwa kwake kikomboleo, wala maombezi hayatamfaa, wala hawatanusuriwa.
(124) Na Mola wake Mlezi alipomjaribu Ibrahim kwa kumpa amri fulani, naye akazitimiza. Akamwambia: Hakika Mimi nitakufanya uwe mwongozi wa watu. Akasema: Je, na katika kizazi changu pia? Akasema: Ahadi yangu haitawafikia wenye kudhulumu.
(125) Na kumbukeni tulipoifanya ile Nyumba (ya Alkaaba) iwe pahali pa kukusanyikia watu na pahali pa amani. Na alipokuwa akisimama Ibrahim pafanyeni pawe pa kusalia. Na tuliagana na Ibrahim na Ismail: Itakaseni Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kutufu na wanaojitenga huko kwa ibada, na wanaoinama na kusujudu.
(126) Na aliposema Ibrahim: Ee Mola wangu Mlezi! Ufanye huu uwe mji wa amani, na uwaruzuku watu wake matunda, wale wanaomuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Akasema: Na mwenye kukufuru pia nitamstarehesha kidogo, kisha nitamsukumiza kwenye adhabu ya Moto, napo ni pahali pabaya mno pa kurejea.
(127) Na kumbukeni Ibrahim na Ismail walipo inyanyua misingi ya ile Nyumba wakaomba: Ewe Mola Mlezi wetu! Tukubalie! Hakika Wewe ndiye Msikizi Mwenye elimu.
(128) Ewe Mola Mlezi wetu! Tujaalie tuwe ni wenye kusilimu kwako, na pia miongoni mwa vizazi vyetu wawe umma uliosilimu kwako. Na utuonyeshe njia za ibada yetu na utusamehe. Bila shaka Wewe ndiye Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(129) Ewe Mola Mlezi wetu! Waletee Mtume anayetokana na wao, awasomee Aya zako, na awafundishe Kitabu na hekima na awatakase. Hakika Wewe ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(130) Na nani atajitenga na mila ya Ibrahim isipokuwa anayeitia nafsi yake katika upumbavu? Na kwa yakini, Sisi tulimteua yeye katika dunia. Na hakika yeye katika Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
(131) Na Mola wake Mlezi alipomwambia: Silimu! Alinena: Nimesilimu kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(132) Na Ibrahim akawausia wanawe hilo, na pia Yaaqub: Enyi wanangu! Hakika Mwenyezi Mungu amekuteulieni Dini hii. Basi msife ila nanyi ni Waislamu.[1]
[1] Yani iliichagua na akawateulia kama rehema na wema. Basi inapasa kusimama nayo na kusifika kwa sheria zake, na kujipaka maadili yake na kudumu namna hiyo hadi kifo. Kwa sababu, mwenye kuishi juu ya kitu, atakufa juu yake. Na mwenye kufa juu ya kitu, atafufuliwa juu yake. (Tafsir Assa'dii)
(133) Je, mlikuwapo yalipomfikia Yaaqub mauti, akawaambia wanawe: Mtamuabudu nani baada yangu? Wakasema: Tutamuabudu Mungu wako na Mungu wa baba zako, Ibrahim na Ismail na Is-hak, Mungu Mmoja tu. Na sisi tunasilimu kwake.[1]
[1] Hii ni hoja dhidi ya Mayahudi (na mfano wao) wanaodai kuwa wanaifuata mila (dini) ya Ibrahim na (Manabii wa) baada yake (kama vile) Yaaqub. Mwenyezi Mungu Mtukufu akawauliza ikiwa waliushuhudia wasia wa mwisho wa Yaqub kwa wana wake. "Je, mtamuabudu nani baada yangu?" Wakasema kuwa watamuabudu Mungu wake, Mungu wa baba zake, ambaye ni Mungu Mmoja tu, na kwamba wao ni wenye kujisilimisha kwake (yani Waislamu)." (Tafsir Assa'dii)
(134) Hao ni watu waliokwisha pita. Watapata waliyoyachuma, nanyi mtapata mtakayoyachuma; wala hamtaulizwa nyinyi waliyokuwa wakiyafanya wao.
(135) Na wakasema: Kuweni Mayahudi au Wakristo ndio mtaongoka. Sema: Bali tunashika mila ya Ibrahim mwongofu, wala hakuwa katika washirikina.[1]
[1] Mayahudi na Wakristo huwaita Waislamu kuingia katika Dini zao wakidai kuwa huo ndio uongofu. Lakini Mwenyezi Mungu akakanusha hilo, na kwamba mila (dini) ya Ibrahim ndiyo uwongofu. " Na katika kuipa mgongo mila yake ni ukafiri na kupotea. (Tafsir Assa'dii)
(136) Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoteremshiwa sisi, na yaliyoteremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wake, na waliyopewa Musa na Isa, na pia waliyopewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi kwake tumesilimu.
(137) Basi wakiamini kama mnavyoamini nyinyi, itakuwa kweli wameongoka. Na wakikengeuka, basi wao wamo katika upinzani tu. Na Mwenyezi Mungu atakutosheni kukukingeni na shari yao, na Yeye ndiye Msikizi, Mwenye elimu.
(138) Huko ndiko kupaka rangi kwa Mwenyezi Mungu. Na nani aliye mbora wa kupaka rangi kuliko Mwenyezi Mungu? Na sisi ni wenye kumuabudu Yeye tu.
(139) Sema: Mnahojiana nasi juu ya Mwenyezi Mungu, naye ni Mola wetu Mlezi na Mola wenu Mlezi, na sisi tuna vitendo vyetu na nyinyi mna vitendo vyenu? Nasi tunamsafia Yeye tu.
(140) Au mnasema kuwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na watoto wake walikuwa Mayahudi au Wakristo? Sema: Je, nyinyi mnajua zaidi au Mwenyezi Mungu? Na ni nani mwenye kudhulumu zaidi kuliko yule aliyeficha ushahidi alio nao utokao kwa Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na hayo myafanyayo.
(141) Hao ni watu waliokwisha pita. Wao watapata waliyoyachuma, na nyinyi mtapata mliyoyachuma, wala hamtaulizwa nyinyi yale waliyokuwa wakiyafanya wao.
(142) Wapumbavu miongoni mwa watu watasema: ‘Ni nini kilichowageuza kutoka kibla chao walichokuwa wakikielekea?’ Sema: ‘Mashariki na Magharibi ni ya Mwenyezi Mungu; Yeye humwongoa amtakaye kwenye njia iliyonyooka.’
(143) Na vivyo hivyo tumewafanya muwe Umma wa wastani, ili muwe mashahidi juu ya watu, na Mtume awe shahidi juu yenu. Na hatukukifanya kibla ulichokuwa juu yake isipokuwa ili tupate kumjua yule anayemfuata Mtume, na yule anayegeuka akarejea kwa visigino vyake. Na kwa yakini, hilo lilikuwa jambo kubwa isipokuwa kwa wale aliowaongoa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuipoteza Imani yenu. Kwa hakika, Mwenyezi Mungu kwa watu ni Mpole, Mwenye kuwarehemu.
(144) Kwa yakini, tuliona unavyougeuza geuza uso wako mbinguni. Basi, tutakuelekeza kwenye Kibla unachokiridhia. Basi, elekeza uso wako upande wa Msikiti Mtakatifu. Na popote mnapokuwa, zielekezeni nyuso zenu upande wake. Na hakika, wale waliopewa Kitabu wanajua sana kwamba hiyo ndiyo haki itokayo kwa Mola wao Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.
(145) Na hata ukiwaletea hao waliopewa Kitabu hoja za kila namna, hawatafuata Kibla chako. Wala wewe hutafuata kibla chao. Wala baadhi yao hawatafuata kibla cha wengineo. Na kama ukiyafuata matamanio yao baada ya kile kilichokufikia katika elimu, wewe kwa hakika hapo utakuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.[1]
[1] Hili linabainisha kumakinika kwao katika kufuata matamanio ya nafsi, na kwamba kuwahalifu huku wanakowahalifu na ukaidi wao sio dhidi yenu tu, bali hata hali yao wao kwa wao ni hivyo. (Tafsir Al-Alusi)
(146) Wale tuliowapa Kitabu, wanayajua haya kama wanavyowajua watoto wao. Na kuna kikundi katika wao huificha haki na hali wanajua.[1]
[1] Wao kwa hakika walikuwa wanajua katika sifa zake kabla ya kumuona, ambazo ziliingiliana na yeye mwenyewe walipomuona. (Tafsir Ibn Al-Qayyim)
(147) Haki inatoka kwa Mola wako Mlezi. Basi usiwe kabisa miongoni mwa wenye shaka.
(148) Na kila mmoja anao mwelekeo anaoelekea. Basi shindanieni mema. Popote mlipo, Mwenyezi Mungu atawaleta nyote pamoja. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(149) Na kokote uendako, uelekeze uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na hiyo kwa hakika ndiyo haki itokayo kwa Mola wako Mlezi. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na mnayoyatenda.
(150) Na kokote uendako, uelekeza uso wako kwenye Msikiti Mtakatifu. Na popote mlipo, zielekezeni nyuso zenu upande wake, ili watu wasiwe na hoja juu yenu; isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Basi, msiwaogope wao, lakini niogopeni Mimi. Na ili niwatimizie neema yangu, na ili mpate kuongoka
(151) Kama tulivyomtuma Mtume kwenu anayetokana na nyinyi, anawasomea Aya zetu na kuwatakasa na kuwafundisha Kitabu na hekima, na anawafundisha ambayo hamkuwa mnayajua.
(152) Basi nikumbukeni, nitawakumbuka. Na nishukuruni, wala msinikufuru.
(153) Enyi mlioamini! Takeni msaada kwa subira na Swala. Hakika, Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.
(154) Wala msiseme kuwa wale waliouwawa katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni maiti. Bali hao ni hai. Lakini nyinyi hamtambui.[1]
[1] Inajulikana kuwa kipenzi hakiachiwi na wenye akili timamu, isipokuwa kwa ajili ya kipenzi kilicho juu zaidi na kikubwa kukiliko. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu akajulisha kwamba mwenye kuuawa katika njia yake akipigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, ili neno la Mwenyezi Mungu liwe ndilo la juu zaidi; na dini yake iwe iliyo dhahiri zaidi. Basi yeye kwa hakika hajakosa uhai alioupenda, bali (alipouawa) alipata uhai mkubwa na kamili zaidi kuliko mnavyofikiria nyinyi. (Tafsir Assa'dii)
(155) Hapana shaka, tutakujaribuni kwa chembe ya hofu, na njaa, na upungufu wa mali na watu na mazao. Na wabashirie wanaosubiri..
(156) Wale ambao ukiwapata msiba, husema: Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake Yeye hakika tutarejea.[1]
[1] Wao husema hivyo kwa sababu wanajua kwamba wanamilikiwa na Mwenyezi Mungu, wanasimamiwa chini ya amri yake na uendeshaji wake. Kwa hivyo, hatuna chochote katika nafsi zetu wala mali zetu. Na akitujaribu kwa kitu katika hayo, basi Yeye Mwingi wa Rehema atakuwa amewaendesha wamilikiwa wake na mali zake. Kwa hivyo haifai kuwa na pingamizi lolote dhidi yake. (Tafsir Assa'dii)
(157) Hao juu yao zitakuwa baraka zitokazo kwa Mola wao Mlezi na rehema. Na hao ndio walioongoka.
(158) Hakika, vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za Mwenyezi Mungu. Basi, anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akafanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka. Na anayejitendea mwenyewe kheri. Basi bila ya shaka Mwenyezi Mungu ni Mwenye shukrani na Mwenye elimu.
(159) Hakika, wale wanaoficha tuliyoyateremsha, nazo ni hoja zilizo wazi na uwongofu baada ya Sisi kuzibainisha kwa watu Kitabuni. Hao anawalaani Mwenyezi Mungu, na wanawalaani kila wenye kulaani.
(160) Isipokuwa wale waliotubu, wakatengeneza na wakabainisha. Basi hao nitapokea toba yao, na Mimi ni Mwenye kupokea toba na Mwenye kurehemu.
(161) Hakika, waliokufuru na wakafa hali ni makafiri, hao iko juu yao laana ya Mwenyezi Mungu na ya Malaika na ya watu wote.
(162) Watadumu humo. Hawatapunguziwa adhabu wala hawatapewa muda wa kupumzika.[1]
[1] Hawatapumzishwa, yani kupewa muhula, kwa sababu wakati wa muhula ambao ulikuwa duniani nao ulikwisha pita. (Tafsir Assa'dii)
(163) Na Mungu wenu ni Mungu mmoja tu, hapana mungu ila Yeye. Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
(164) Hakika, katika kuumbwa kwa mbingu na ardhi, na kukhitalifiana usiku na mchana. Na marikebu ambazo hupita baharini kwa viwafaavyo watu, na maji anayoyateremsha Mwenyezi Mungu kutoka mbinguni Na kwa hayo, akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake, na akaeneza humo kila aina ya wanyama; na katika mabadiliko ya pepo. Na mawingu yanayoamrishwa kupita baina ya mbingu na ardhi, bila shaka zimo Ishara kwa watu wanaozingatia.
(165) Na katika watu wapo wanaojifanyia waungu wasio kuwa Mwenyezi Mungu. Wanawapenda kama kumpenda Mwenyezi Mungu. Lakini walioamini wanampenda Mwenyezi Mungu zaidi sana. Na laiti waliodhulumu wakajua watakapoiona adhabu kuwa nguvu zote ni za Mwenyezi Mungu, na kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu!
(166) Waliofuatwa watakapowakataa wale waliowafuata, na hali ya kuwa wamekwishaiona adhabu; na yatakatika mafungamano yao.
(167) Na watasema wale waliofuata: Laiti tungeweza kurudi tukawakataa wao kama wanavyotukataa sisi! Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu atakavyowaonyesha vitendo vyao kuwa majuto yao; wala hawatakuwa wenye kutoka Motoni.[1]
[1] Basi matendo yao (ya kumwabudu asiyekuwa Mwenyezi Mungu Mmoja) yakapotelea mbali. Na hali zao zikaangamia, na ikawadhihirikia kuwa wao walikuwa ni waongo. Na kwamba matendo yao waliyoyatarajia yawanufaishe na wapate matokeo yake yaliwabadilikia yakawa masikitiko na majuto. (Tafsir Assa'dii)
(168) Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika yeye ni adui yenu aliye dhahiri.
(169) Yeye anakuamrisheni maovu na machafu, na mumsingizie Mwenyezi Mungu mambo msiyoyajua.
(170) Na wanapoambiwa: Fuateni aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu; wao husema: Bali tutafuata tuliyowakuta nayo baba zetu. Je, hata ikiwa baba zao walikuwa hawaelewi kitu, wala hawakuongoka?
(171) “Na mfano wa waliokufuru ni kama mfano wa anayempigia kelele asiyesikia isipokuwa wito na sauti tu. Ni viziwi, mabubu, vipofu, kwa hivyo hawaelewi”.
(172) Enyi mlio amini! Kuleni katika vizuri tulivyokuruzukuni, na mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
(173) Yeye amekuharimishieni mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichotajiwa, katika kuchinjwa kwake, jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini aliyefikiwa na dharura bila ya kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(174) Hakika, wale wanaoficha aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu katika Kitabu. Na wakanunua kwacho thamani ndogo, hao hawali katika tumbo zao isipokuwa moto. Wala Mwenyezi Mungu hatawaongelesha Siku ya Kiyama, wala hatawatakasa, nao wana adhabu chungu.
(175) Hao ndio walionunua upotofu kwa uwongofu, na adhabu kwa maghfira (msamaha). Ama wavumilivu wa Moto watu hawa!
(176) Hayo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu ameteremsha Kitabu kwa haki. Na hakika wale waliohitilafiana katika Kitabu wamo katika upinzani ulio mbali na haki.
(177) Siyo wema kuwa mnaelekeza nyuso zenu upande wa mashariki na magharibi. Bali wema ni wa anayemuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho na Malaika na Kitabu na Manabii. Na anawapa mali, licha ya kuipenda kwake, jamaa na mayatima na masikini na wasafiri, na waombao, na katika ukombozi. Na akawa anashika Swala, na akatoa Zaka, na wanaotimiza ahadi yao wanapoahidi, na wanaovumilia katika shida na dhara na wakati wa vita. Hao ndio walio sadikisha, na hao ndio wachamungu.
(178) Enyi mlio amini! Mmepewa ruhusa kulipa kisasi katika waliouawa - muungwana kwa muungwana, na mtumwa kwa mtumwa, na mwanamke kwa mwanamke. Na anayesamehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani. Huko ni kupunguziwa kulikotokana na Mola wenu Mlezi, na ni rehema. Na atakayevuka mipaka baada ya haya, basi yeye atapata adhabu chungu.
(179) Mtakuwa na uhai mzuri katika kulipiza kisasi enyi wenye akili, ili mpate kuwa wachamungu.
(180) Mmeandikiwa mmoja wenu anapofikwa na mauti, kama ataacha heri (yani mali), afanye wasia kwa wazazi wake wawili, na jamaa zake kwa wema. Ni haki juu ya wachamungu.
(181) Na atakayeibadilisha (wasia) baada ya kuusikia, basi dhambi yake ni juu ya wale watakaoibadilisha; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
[1] Basi mwenye kuibadilisha wasia, na akaupindua, na akaigeuza hukumu yake, na akaongeza kitu ndani yake. Au akapunguza, - na anaingia katika hilo (mwenye) kuificha njia ya ubora zaidi. - "Basi dhambi yake ni juu ya wale watakaoibadilisha." (Tafsir Ibn Kathir)
(182) Na mwenye kumhofia muusiaji kwenda kombo au kupata dhambi, na akasuluhisha baina yao, basi hakuna dhambi yoyote juu yake. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye kurehemu.
(183) Enyi mlioamini! Mmeandikiwa Saumu, kama walivyoandikiwa (watu) waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu.
(184) (Mfunge) siku zenye kuhesabika. Na atakayekuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Na wale wasioweza, watoe fidia kwa kumlisha masikini. Na atakayefanya wema kwa kujitolea, basi ni bora kwake. Na mkifunga ndiyo bora kwenu, ikiwa mnajua.
(185) Mwezi wa Ramadhani ndio ambao imeteremshwa Qur-ani ndani yake kuwa uwongofu kwa watu, na hoja zilizo wazi za uwongofu na upambanuzi. Kwa hivyo, atakayeushuhudia mwezi miongoni mwenu, basi na afunge. Na atakayekuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hesabu katika siku nyingine. Mwenyezi Mungu anawatakia yaliyo mepesi, wala hawatakii yaliyo mazito, na ili mkamilishe hesabu hiyo, na ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa yale aliyowaongoa ili mpate kushukuru.
(186) Na waja wangu watakapokuuliza kunihusu Mimi, basi Mimi kwa hakika nipo karibu. Ninaitikia maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka.
(187) Mmehalalishiwa usiku wa Saumu kuingiliana na wake zenu. Wao ni vazi kwenu, na nyinyi ni vazi kwao. Mwenyezi Mungu alikwisha jua kwamba mlikuwa mkizihini nafsi zenu. Kwa hivyo amewakubalia toba yenu na amewasamehe. Basi sasa changanyikeni nao na tafuteni kile alichowaandikia Mwenyezi Mungu. Na kuleni na kunyweni mpaka uwabainikie weupe wa alfajiri kutokana na weusi wa usiku. Kisha timizeni Saumu mpaka usiku. Wala msichanganyike nao hali ya kuwa mmekaa Itikafu msikitini. Hiyo ni mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi msiikaribie. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya (Ishara) zake watu ili wapate kumcha.
(188) Wala msiliane mali zenu kwa batili, na kuzipeleka kwa mahakimu ili mpate kula sehemu ya mali ya watu kwa dhambi, na hali mnajua.
(189) Wanakuuliza kuhusu miezi miandamo. Sema: Hiyo ni vipimo vya nyakati kwa ajili ya watu na Hija. Wala sio wema kwamba mziingie nyumba kwa nyuma yake. Bali mwema ni mwenye kumcha Mungu. Na ingieni majumbani kupitia milangoni mwake. Na mcheni Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu.
(190) Na piganeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaopigana nanyi, wala msianzishe uadui. Kwani Mwenyezi Mungu kwa hakika hawapendi waanzao uadui.
(191) Na waueni popote muwakutapo, na watoeni popote walipowatoa; kwani fitina ni mbaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao kwenye Msikiti Mtakatifu mpaka wawapigie huko. Wakikupigeni huko, basi nanyi pia wapigeni. Na hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri.
(192) Lakini wakiacha, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(193) Na piganeni nao mpaka pasiwepo fitina, na Dini iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha, basi usiwepo uadui isipokuwa kwa madhulumu (waliodhulumiwa).
(194) Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi. Basi, anayewashambulia, nanyi mshambulieni kwa sawa na alivyowashambulia. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu kwa hakika yu pamoja na wachamungu.
(195) Na toeni katika njia ya Mwenyezi Mungu, wala msijitupe katika maangamivu kwa mikono yenu. Na fanyeni wema. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaofanya wema.
(196) Na timizeni Hijja na Umra kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa mtazuiwa, basi (chinjeni) wanyama walio wepesi kupatikana. Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama hao wafike machinjoni mwao. Na atakayekuwa mgonjwa miongoni mwenu au ana vya kumuudhi kichwani mwake, basi atoe fidia kwa kufunga saumu au kwa kutoa sadaka au kuchinja wanyama. Na mtakapokuwa na amani, basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiyepata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakaporudi. Hizo ni kumi kamili. Hayo ni kwa yule ambaye jamaa zake hawako karibu na Msikiti Mtakatifu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
(197) Hijja ni miezi maalumu. Basi anayehirimia Hijja ndani yake (miezi hiyo), basi asijamiiane wala asipindukie mipaka wala asibishane katika Hijja. Na chochote mnachokifanya katika heri, Mwenyezi Mungu anaijua. Na chukueni masurufu. Na hakika, masurufu (yaliyo) bora zaidi ni uchamungu. Na nicheni Mimi, enyi wenye akili na busara!
(198) Hakuna ubaya wowote juu yenu kutafuta fadhila kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi mtakapomiminika kutoka 'Arafat, mtajeni Mwenyezi Mungu katika Mash'aril Haram (eneo takatifu). Na mtajeni kama alivyowaongoa, ijapo kabla ya hilo mlikuwa miongoni mwa waliopotea.
(199) Kisha miminikeni kutoka pale wanapomiminika watu, na muombeni Mwenyezi Mungu msamaha. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(200) Na mkishatimiza ibada zenu, basi mtajeni Mwenyezi Mungu kama mlivyokuwa mkiwataja baba zenu au utajo mkubwa zaidi. Na katika watu kuna wale wanaosema, “Mola wetu Mlezi, tupe duniani!” Naye katika Akhera hana fungu lolote.
(201) Na miongoni mwao kuna wale wanaosema, “Mola wetu Mlezi, tupe duniani mema, na Akhera mema, na utulinde kutokana na adhabu ya Moto!”
(202) Hao ndio walio na fungu kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhisabu.[1]
[1] Ali bin Abi Twalib - Mwenyezi Mungu awe radhi naye - aliambiwa: Vipi Mwenyezi Mungu atawafanyia watu hisabu pamoja na wingi wao? Akasema: (Atawafanyia hisabu) Kama anavyowaruzuku pamoja na wingi wao. (Tafsir Ibn Juzy)
(203) Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazohisabiwa. Lakini mwenye kufanya haraka (akarejea) katika siku mbili, basi hakuna dhambi juu yake. Na mwenye kukawia, pia hakuna dhambi juu yake, kwa mwenye kumcha Mungu. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba nyinyi mtakusanywa kwake.
(204) Na katika watu yupo yule ambaye maneno yake kwa maisha ya kidunia hukupendeza; naye humshuhudisha Mwenyezi Mungu kwa yaliyomo katika moyo wake, na hali yeye ndiye mgomvi mkubwa mno.
(205) Na akishageuka akaenda, anazunguka katika ardhi ili afanye humo ufisadi na anaharibu mimea na viumbe. Na Mwenyezi Mungu hapendi ufisadi.
(206) Na akiambiwa, “mche Mwenyezi Mungu,” hupandwa na mori wa kutenda madhambi. Basi huyo kinachomtosha ni Jahannam. Napo hakika ni pahali pabaya mno pa kupumzikia.[1]
[1] Vipi hali yako unapooambiwa kumcha Mwenyezi Mungu? Ilipokewa kwamba 'Umar Ibn Al-Khattwab - Mwenyezi Mungu amwiye radhi - aliambiwa, "Ittaqillah (mche Mwenyezi Mungu"). Kwa hivyo, akaliweka shavu lake juu ya ardhi kwa kumnyenyekea Mwenyezi Mungu.(Tafsir Assam'aanii)
(207) Na katika watu kuna yule anayeiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mpole kwa waja wake.[1]
[1] Mwenyezi Mungu alipoeleza katika Aya iliyotangulia hali ya mtu anayeitoa dini yake kwa ajili ya mambo ya kidunia. Akaitaja katika Aya hii hali ya mtu anayeyatoa maisha yake ya duniani, nafsi yake na mali yake ili kutafuta dini. (Tafsir Ar-Raazii)
(208) Enyi mlioamini! Ingieni katika Uislamu kwa ukamilifu, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika, yeye kwenu ni adui wa dhahiri.
(209) Na mkiteleza baada ya kufikiwa na hoja zilizo wazi, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(210) Je, wanangoja mpaka Mwenyezi Mungu awajie katika vivuli vya mawingu pamoja na Malaika, na hukumu iwe imekwisha tolewa? Na kwa Mwenyezi Mungu ndiyo hurejeshwa mambo yote.
(211) Waulize Wana wa Israili: Tumewapa ishara ngapi zilizo wazi? Na anayezibadili neema za Mwenyezi Mungu baada ya kumfikia, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.
(212) Waliokufuru wamepambiwa maisha ya duniani; na wanawafanyia masihara wale walioamini. Na wale wanaomcha Mwenyezi Mungu watakuwa juu yao Siku ya Kiyama. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
(213) Watu wote walikuwa umma mmoja. Kisha Mwenyezi Mungu akawatuma Manabii wenye kupeana habari njema na waonyaji. Na akateremsha pamoja nao Kitabu kwa haki, ili kihukumu baina ya watu katika yale waliyohitilafiana. Na wala hawakuhitilafiana ndani yake isipokuwa wale waliopewa Kitabu hicho baada ya kufikiwa na hoja zilizo wazi, kwa sababu ya uhasidi baina yao. Ndipo Mwenyezi Mungu kwa idhini yake akawaongoa walioamini kwendea haki katika yale waliyohitilafiana ndani yake. Na Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye kwenye Njia iliyonyooka.
(214) Ama mnadhani kuwa mtaingia Peponi, ilhali bado hamjajiwa na mfano wa (yaliyowajia) wale waliopita kabla yenu? Uliwapata ufukara (shida) na maradhi, na wakatikiswa mpaka Mtume na walioamini pamoja naye wakasema. “Ni lini nusura ya Mwenyezi Mungu (itakuja)?” Jueni kuwa hakika nusura ya Mwenyezi Mungu ipo karibu.
(215) Wanakuuliza watoe nini? Sema: Chochote mnachotoa katika heri ni kwa ajili ya wazazi na jamaa na mayatima na masikini na msafiri. Na chochote mnachofanya katika heri, basi Mwenyezi Mungu kwa hakika anaijua.
(216) Mmeandikiwa kupigana vita, navyo vinawachukiza. Lakini huenda mkachukia kitu, nacho ni heri kwenu. Na huenda mkapenda kitu, nacho ni shari kwenu. Na Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.[1]
[1] Kuchukia huku kunahusiana na maumbile, ambayo kawaida hayalipendi kwa sababu ya yale yaliyomo ndani yake kama vile kutoa mali, na ugumu juu ya nafsi, na kuhatarisha nafsi. Na siyo kwa sababu ya kuichukia amri ya Mwenyezi Mungu. (Tafsir Al-Baghawi)
(217) Wanakuuliza juu ya kupigana vita katika mwezi mtakatifu. Sema: Kupigana vita ndani yake ni dhambi kubwa. Lakini kuzuia watu wasiende katika Njia ya Mwenyezi Mungu na kumkufuru Yeye, na kuzuilia watu wasiende kwenye Msikiti Mtakatifu na kuwatoa watu wake humo, ni makubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na fitina ni jambo kubwa zaidi kuliko kuua. Wala hawataacha kupigana nanyi mpaka wawatoe katika Dini yenu kama wakiweza. Na yeyote katika nyinyi atakayeacha Dini yake, na akafa hali ya kuwa ni kafiri, basi hao ndio ambao matendo yao yameharibika katika dunia na Akhera. Na hao ndio wenza wa Moto. Wao humo watadumu.
(218) Hakika, wale walioamini, na wale waliohama na wakafanya juhudi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanaotarajia rehema za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(219) Wanakuuliza juu ya mvinyo na kamari. Sema: Katika hivyo zipo dhambi kubwa na manufaa kwa watu. Lakini dhambi zake ni kubwa zaidi kuliko manufaa yake. Na wanakuuliza watoe nini? Sema: Kilicho chepesi. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya zake ili mpate kutafakari.
(220) Katika dunia na Akhera na wanakuuliza juu ya mayatima. Sema: Kuwatengenezea ndio heri. Na mkichanganyika nao, basi ni ndugu zenu. Na Mwenyezi Mungu anamjua mharibifu, na mtengenezaji. Na Mwenyezi Mungu angelipenda, angeliwatia katika udhia. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(221) Wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mwanamke mshirikina hata akiwapendeza. Wala msiwaoze (binti zenu) wanaume washirikina mpaka waamini. Na mtumwa mwanamume Muumini ni bora kuliko mwanamume mshirikina hata akiwapendeza. Hao wanaitia kwenye Moto, naye Mwenyezi Mungu anaitia kwenye Pepo na maghfira kwa idhini yake. Naye huwabainishia Aya zake watu ili wapate kukumbuka.
(222) Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie: hayo ni madhara. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi, wala msiwakaribie mpaka wawe safi. Na wakishajisafisha, basi waendeeni namna alivyowaamrisha Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wanaotubu, na huwapenda wanaojisafisha.
(223) Wake zenu ni konde zenu. Basi ziendeeni konde zenu mpendavyo. Lakini zitangulizieni heri nafsi zenu, na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kuwa hakika nyinyi mtakutana naye. Na wape habari njema Waumini.
(224) Wala msifanye Mwenyezi Mungu katika viapo vyenu kuwa kisingizio cha kuacha kufanya wema, na kumcha Mungu, na kupatanisha baina ya watu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
(225) Mwenyezi Mungu hawachukulii ubaya katika viapo vyenu ambavyo hamkuvikusudia. Lakini anawachukulia ubaya kwa yale ambayo nyoyo zenu zinachuma. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
(226) Kwa wale wanaoapa kujitenga na wake zao, wangojee miezi minne. Na wakirejea, basi Mwenyezi Mungu hakika ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(227) Na wakiazimia kuwapa talaka, basi Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mweye kujua.
(228) Na wanawake waliopewa talaka, wazizuie nafsi zao tahara (au hedhi) tatu. Wala sio halali kwao kuficha alichoumba Mwenyezi Mungu katika matumbo yao ya uzazi, ikiwa wanamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Na waume wao wana haki zaidi ya kuwarejesha katika muda huo, kama wakitaka kufanya suluhu. Nao wanawake wanayo haki sawa na ile haki iliyo juu yao. Na wanaume wana daraja zaidi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(229) Talaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa uzuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote katika kile mlichowapa wake zenu, isipokuwa ikiwa wote wawili watahofia ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi mkihofia kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu, hapo hakuna ubaya juu yao katika kile ambacho mke atajikomboa kwacho. Hii ndiyo mipaka ya Mwenyezi Mungu. Basi msiikiuke. Na mwenye kukiuka mipaka ya Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.
(230) Na akimtaliki (talaka ya tatu), basi yeye si halali kwake baada ya hayo mpaka aolewe na mume asiyekuwa yeye. Na (huyo mwingine) akimtaliki, basi hakuna ubaya kwao kurejeana wakiona kuwa watashikamana na mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na hii ni mipaka ya Mwenyezi Mungu anayoibainisha kwa watu wanaojua.
(231) Na mtakapowataliki wanawake talaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakayefanya hivyo, ameidhulumu nafsi yake. Wala msizichukulie Aya za Mwenyezi Mungu kwa masikhara. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu, na aliyowateremshia katika Kitabu na hekima anachowaonya kwacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
(232) Na mtakapowataliki wanawake, nao wakamaliza muda wao (wa eda), basi msiwazuie kuoleka kwa waume zao endapo baina yao wamekubaliana kwa wema. Hayo anawaidhiwa kwayo yule miongoni mwenu anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ni bora zaidi kwenu na safi kabisa. Na Mwenyezi Mungu anajua, lakini nyinyi hamjui.
(233) Na wazazi wanawake wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili kwa anayetaka kutimiza kunyonyesha. Na ni juu ya aliyezaliwa mwana huyo chakula chao na kuwalisha mavazi yao kwa wema. Wala halazimishwi mtu isipokuwa kwa kiwango cha uwezo wake. Mama asitaabishwe kwa sababu ya mwanawe, wala yule aliyezaliwa mwana kwa sababu ya mwanawe. Na juu ya mrithi ni mfano wa hivyo. Na kama wote wawili wakitaka kumwachisha kunyonya kwa kuridhiana na kushauriana, basi hakuna ubaya juu yao. Na mkitaka kuwapa watoto wenu mama wa kuwanyonyesha, basi hakuna ubaya juu yenu ikiwa mtapeana mlichoahidi kwa wema. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.
(234) Na wale miongoni mwenu wanaofishwa, na wanaacha wake, hawa wake wazizuie nafsi zao miezi minne na siku kumi. Na wanapotimiza muda wao (wa eda), basi hakuna ubaya wowote juu yao katika yale wanayojifanyia kwa wema. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda.
(235) Wala hakuna ubaya juu yenu katika kupeleka posa kwa ishara tu kwa wanawake walio katika eda au mkalificha ndani ya nyoyo zenu. Mwenyezi Mungu alikwisha jua kwamba nyinyi mtawakumbuka. Lakini msiwaahidi kwa siri, isipokuwa mseme maneno mema. Wala msiazimie kufunga mkataba wa ndoa mpaka andiko (la amri ya eda) lifike muda wake. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu kwa hakika anajua yaliyomo katika nafsi zenu. Basi jitahadharini naye. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mpole.
(236) Hakuna ubaya wowote juu yenu mkiwataliki wanawake ambao hamjawagusa au kuwabainishia mahari yao. Lakini wapeni cha kuwaliwaza, mwenye wasaa kwa kiwango awezacho na mwenye dhiki kwa kiwango awezacho, maliwazo kwa wema, ni haki juu ya watendao mema.
(237) Na mkiwataliki kabla ya kuwagusa, na tayari mmeshawakatia mahari mahususi, basi wapeni nusu ya mahari mliyowakatia. Isipokuwa ikiwa wanawake wenyewe watasamehe, au amesamehe yule ambaye fundo la ndoa liko mkononi mwake. Na mkisamehe ndiyo kuwa karibu zaidi na uchamungu. Wala msisahau fadhila zilizo baina yenu. Hakika, Mwenyezi Mungu anayaona vyema mnayoyatenda.
(238) Zilindeni Swala, na hasa Swala ya katikati. Na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa unyenyekevu.
(239) Na mkiwa na hofu, basi (swalini) hali ya kuwa mnakwenda kwa miguu au mmepanda. Na mtakapokuwa katika amani, basi mkumbukeni Mwenyezi Mungu kama alivyowafunza yale ambayo hamkuwa mnayajua.
(240) Na wale miongoni mwenu wanaofishwa, na wanawaacha wake, na wausie kwa ajili ya wake zao kupata matumizi kwa mwaka mmoja bila ya kuwatoa nyumbani. Na wanawake wenyewe wakiondoka, basi hakuna ubaya wowote juu yenu katika yale waliyojifanyia wenyewe kwa wema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(241) Na wanawake waliotalikiwa wapewe cha kuwaliwaza kwa wema. Hii ni haki juu ya wachamungu.
(242) Namna hivi ndivyo anavyowabainishia Mwenyezi Mungu Aya zake ili mpate kufahamu.
(243) Je, hukuwaona wale waliotoka katika maboma yao kwa maelfu kwa kuogopa mauti? Na Mwenyezi Mungu akawaambia: Kufeni! Kisha akawahuisha. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.
(244) Na piganeni vita katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
(245) Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema; ili amzidishie mizidisho mingi. Na Mwenyezi Mungu hukunja na hukunjua. Na kwake Yeye mtarejeshwa.
(246) Je, hukuwaona watukufu katika Wana wa Israili baada ya Musa, walipomwambia Nabii wao: Tuwekee mfalme ili tupigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Akasema: Je, haielekei ikiwa mtaandikiwa vita kuwa msipigane? Wakasema: Itakuwaje tusipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu, ilhali tumeshatolewa katika maboma yetu na watoto wetu? Lakini walipoandikiwa kupigana vita, wakageuka, isipokuwa wachache miongoni mwao. Na Mwenyezi Mungu anawajua vyema madhalimu.
(247) Na Nabii wao akawaambia: Hakika, Mwenyezi Mungu ameshawateulia Taluti (Sauli) kuwa ndiye mfalme. Wakasema: Vipi atakuwa na ufalme juu yetu, ilhali sisi tuna haki zaidi kupata ufalme kuliko yeye, naye hakupewa wasaa wa mali? Akasema: Hakika, Mwenyezi Mungu amemteua yeye juu yenu na amemzidishia ukunjufu wa elimu na kiwiliwili. Na Mwenyezi Mungu humpa ufalme wake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
(248) Na Nabii wao akawaambia: Hakika, alama ya ufalme wake ni kwamba awaletee lile sanduku ambalo ndani yake mna kituliza nyoyo zenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Na mabaki ya waliyoyaacha watu wa Musa na watu wa Harun, linalobebwa na Malaika. Bila shaka, katika hayo zimo dalili kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.
(249) Basi Taluti alipoondoka na majeshi, alisema: Hakika, Mwenyezi Mungu atawajaribu kwa mto. Hivyo basi, atakayekunywa humo, si pamoja nami. Na yule asiyeyaonja, basi huyo atakuwa pamoja nami; ila atakayeteka humo kiasi ya kitanga cha mkono wake. Lakini walikunywa humo isipokuwa wachache tu miongoni mwao. Na alipovuka mto yeye na wale walioamini pamoja naye, walisema: Leo hatumwezi Jaluti (Goliati) na majeshi yake. Wakasema wale wenye yakini ya kukutana na Mwenyezi Mungu: Ni makundi mangapi madogo yameshinda makundi makubwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.[1]
[1] Baadhi ya wafasiri waliwagawanya wafuasi wa Taluti katika makundi matatu: Wale waliokunywa sana kinyume na amri ya Taluti. Na wale waliokunywa kiasi cha kitanga cha mkono wake kama walivyoruhusiwa na kamanda wao. Na wale ambao hawakunywa kabisa, si kwa uchache wala kwa wingi. (Tafsir Tantaawii)
(250) Na walipotoka ili kupambana na Jaluti na majeshi yake, walisema: Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira, na isimamishe imara miguu yetu, na utunusuru juu ya watu hawa Makafiri.
(251) Kwa hivyo, wakawashinda kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na Daudi akamuua Jaluti. Na Mwenyezi Mungu akampa Daudi ufalme na hekima, na akamfundisha katika aliyoyapenda. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawazuii watu kwa watu, basi dunia ingeliharibika. Lakini Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila juu ya walimwengu wote.
(252) Hizi ni Aya za Mwenyezi Mungu tunakusomea kwa haki. Na hakika wewe ni miongoni mwa Mitume.
(253) Mitume hao tumewaboresha baadhi yao juu ya wengineo. Miongoni mwao kuna wale ambao Mwenyezi Mungu alisema nao, na akawapandisha vyeo baadhi yao. Na tukampa Isa mwana wa Maryam hoja zilizo wazi, na tukamtia nguvu kwa Roho mtakatifu. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana wale waliokuwa baada yao, baada ya kujiwa na hoja zilizo wazi. Lakini walihitalifiana. Basi miongoni mwao kuna wale walioamini, na miongoni mwao kuna wale waliokufuru. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelipigana. Lakini Mwenyezi Mungu hufanya kile akitakacho.
(254) Enyi mlioamini! Toeni katika tulivyowaruzuku kabla haijakuja Siku ambayo hapatakuwapo biashara yoyote, wala urafiki, wala uombezi. Na makafiri ndio madhalimu.
(255) Mwenyezi Mungu - hapana mungu isipokuwa Yeye, Aliye hai, Msimamizi wa mambo yote milele. Hashikwi na kusinzia wala kulala. Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo duniani. Ni nani huyo awezaye kufanya uombezi mbele yake isipokuwa kwa idhini yake? Anayajua yaliyo mbele yao, na yaliyo nyuma yao, wala wao hawajui vyema chochote katika elimu yake isipokuwa kwa kile akitakacho. Kursi yake imeenea mbingu na dunia, na wala halemewi na kuvilinda vyote viwili. Na Yeye ndiye aliye juu zaidi, Mkuu.
(256) Hakuna kulazimisha katika Dini. Kwani uwongofu umekwishapambanuka kutokana na upotovu. Basi anayemkufuru Taaghuut[1] na akamwamini Mwenyezi Mungu, basi bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua vyema.[2]
[1] Taghut inamaanisha Shetani, mchawi, kuhani, sanamu, waovu katika watu na majini. Chochote kipitacho mipaka ya Mwenyezi Mungu na kinaabudiwa badala yake ima kwa kulazimisha hilo au kutiiwa tu sawa kiwe mwanadamu au sanamu (Tafsir ya Al-Mawardii).
[2] Na wala hakuna upinzani baina ya maana hii na Aya nyingi zinazolazimu kuwepo kwa Jihadi. Kwani, Mwenyezi Mungu ameamrisha kupigana vita ili Dini yote iwe ya Mwenyezi Mungu tu. Na kuzuia uadui wa wenye kufanya uadui dhidi ya dini. (Tafsir Assa'dii)
(257) Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa walioamini. Huwatoa hadi katika giza mbalimbali kwenda katika nuru.[1] Lakini wale waliokufuru, walinzi wao ni Taaghut. Huwatoa katika nuru kwenda hadi katika giza mbalimbali. Hao ndio wenza wa Moto, humo watadumu.
[1] Hapa neno 'nuru' liko katika hali ya umoja, ilhali 'giza' liko kwa wingi, kwa sababu haki ni moja tu, nao ukafiri ni aina mbalimbali. (Tafsir Ibn Kathir)
(258) Kwani hukumuona yule aliyehojiana na Ibrahim kuhusu Mola wake Mlezi kwa sababu Mwenyezi Mungu alimpa ufalme? Ibrahim aliposema: Mola wangu Mlezi ni yule ambaye huhuisha na kufisha. Yeye akasema: Mimi pia ninahuisha na ninafisha. Ibrahim akasema: Kwa hakika, Mwenyezi Mungu hulileta jua kutokea mashariki, basi wewe lilete kutokea magharibi. Kwa hivyo, akashindwa yule aliyekufuru.[1] Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu dhalimu.
[1] Alishindwa kwa hoja, kwa fikira, pia kwa ilimu na ufahamu.
(259) Au kama yule aliyepita karibu na mji hali ya kuwa umekwisha kuwa magofu tu. Akasema: Vipi Mwenyezi Mungu ataufufua mji huu baada ya kufa kwake? Basi Mwenyezi Mungu akamfisha yeye (muda wa) miaka mia moja, kisha akamfufua. Akasema: Je umekaa muda gani? Akasema: (Labda) nimekaa siku moja au sehemu ya siku. Akasema: Bali umekaa miaka mia moja. Hebu angalia chakula chako na vinywaji vyako, havikuharibika. Na mwangalie punda wako. Na ili tukufanye uwe ni ishara kwa watu. Na iangalie mifupa yake hii jinsi tunavyoinyanyua kisha tuivishe nyama. Basi yalipombainikia, alinena: Ninajua kwamba kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
(260) Na Ibrahim aliposema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe vipi unavyofufua wafu. Mwenyezi Mungu akasema: Kwani huamini? Akasema: Hasha! Lakini ili moyo wangu utue. Akasema: Basi wachukue wanne katika ndege na uwazoeshe kwako. Kisha weka juu ya kila kilima sehemu katika hao, kisha waite, watakujia mbio. Na ujue kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(261) Mfano wa wale wanaotoa mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje moja iliyochipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia moja. Na Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
(262) Wale wanaotoa mali zao kwa Njia ya Mwenyezi Mungu, kisha hawafuatishi kile walichotoa masimbulizi wala udhia, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Wala haitakuwa hofu juu yao wala wao hawatahuzunika.
(263) Kauli njema na msamaha ni bora kuliko sadaka inayofuatwa na maudhi. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosheleza, Mpole.
(264) Enyi mlioamini! Msiharibu sadaka zenu kwa masimbulizi na maudhi. Kama yule anayetoa mali yake ili kujionyesha kwa watu, wala hamuamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho. Basi mfano wake ni kama mfano wa jabali ambalo juu yake kuna udongo, kisha likapigwa na mvua kubwa, ikaliacha tupu. Basi hawatakuwa na uweza wowote kwa kile walichochuma. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu ya makafiri.
(265) Na mfano wa wale wanaotoa mali zao kwa kuitafuta radhi za Mwenyezi Mungu, na kuzipa nguvu roho zao ni kama mfano wa bustani iliyo mahali pa juu. Ikaifikia mvua kubwa na ikaleta mazao yake maradufu. Na hata kama haifikiwi na mvua kubwa, basi manyunyu tu yanatosha. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.
(266) Je, angependa mmoja wenu kwamba awe na bustani ya mitende na mizabibu ipitayo mito chini yake. Naye humo hupata katika mazao ya kila namna, na uzee ukamfikia ilhali ana watoto dhuria nyonge. Kisha ikapigwa na kimbunga chenye moto, kwa hivyo ikaungua? Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia ishara ili mtafakari.
(267) Enyi mlioamini! Toeni katika vile vizuri mlivyovichuma, na katika vile tulivyowatolea katika ardhi. Wala msikusudie kutoa vilivyo vibaya, ilhali nyinyi wenyewe msingevipokea isipokuwa kwa kuvifumbia macho. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifiwa.
(268) Shetani anawatia hofu ya ufakiri, na anawaamrisha machafu. Na Mwenyezi Mungu anawaahidi msamaha kutoka kwake na fadhila. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
(269) Yeye humpa hekima amtakaye. Na mwenye kupewa hekima, basi bila ya shaka amepewa heri nyingi. Na hawakumbuki isipokuwa wenye akili.
(270) Na chochote mnachotoa au nadhiri mnazoweka, basi hakika Mwenyezi Mungu anajua hayo. Na madhalimu hawana wowote wa kuwanusuru.
(271) Mkizidhihirisha sadaka, basi hilo ni vizuri. Na mkizificha na mkawapa mafakiri kwa siri, basi hilo ni heri kwenu, na yatawaondolea katika maovu yenu. Na Mwenyezi Mungu ana habari ya mnayoyatenda.
(272) Si juu yako wewe kuwaongoa, lakini Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye. Na chochote mnachotoa katika heri, basi ni cha nafsi zenu. Wala hamtoi isipokuwa kwa kutafuta uso wa Mwenyezi Mungu. Na chochote mnachotoa katika heri, mtalipwa kwa ukamilifu, nanyi hamtadhulumiwa.
(273) Na wapewe mafakiri waliozuilika katika njia za Mwenyezi Mungu, wasioweza kusafiri katika nchi kutafuta riziki. Asiyewajua hali zao huwadhania kuwa ni matajiri kwa sababu ya kujizuia kwao. Utawatambua kwa alama zao; hawawang'ang'anilii watu kwa kuwaomba. Na chochote mnachotoa katika heri, basi hakika Mwenyezi Mungu anaijua.
(274) Wale wanaotoa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa hofu juu yao, wala wao hawatahuzunika.
(275) Wale wanaokula riba, hawasimami isipokuwa kama anavyosimama aliyezugwa na Shetani kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa walisema: Hakika, biashara ni kama riba. Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba. Basi mwenye kujiwa na mawaidha kutoka kwa Mola wake Mlezi, kisha akakomeka, basi yake ni yaliyokwisha pita. Na mambo yake yako kwa Mwenyezi Mungu. Na wenye kurudia, basi hao ndio wenza wa Moto, wao watadumu humo.
(276) Mwenyezi Mungu huiondolea baraka riba, na huzibariki sadaka. Na Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye kukufuru na afanyae dhambi nyingi.
(277) Hakika, wale walioamini na wakatenda mema na wakashika Swala na wakatoa Zaka, wao watapata ujira wao kwa Mola wao Mlezi. Wala haitakuwa hofu juu yao, wala hawatahuzunika.
(278) Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na acheni riba zilizobaki, ikiwa nyinyi ni Waumini.
(279) Na msipofanya, basi jitangazieni vita kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilimali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe.
(280) Na (mdaiwa) akiwa ana ugumu, basi (mdai) angoje mpaka awe katika wepesi. Na mkiifanya deni kuwa ni sadaka, basi ni bora kwenu, ikiwa mnajua.
(281) Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilichochuma. Nao hawatadhulumiwa.
(282) Enyi mlioamini! Mnapodaiana deni hadi muda maalumu, basi liandikeni. Na mwandishi aandike baina yenu kwa uadilifu, wala mwandishi asikatae kuandika kama alivyomfunza Mwenyezi Mungu. Basi na aandike, na mwenye deni juu yake aandikishe; na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi, wala asipunguze chochote ndani yake. Na akiwa mwenye kudaiwa ni mtu aliye pumbaa au mnyonge au hawezi kuandikisha mwenyewe, basi aandikishe mlinzi wake kwa uadilifu. Na washuhudisheni mashahidi wawili katika wanaume wenu. Na ikiwa wanaume wawili hawapo, basi mwanamume mmoja na wanawake wawili katika wale mnaowaridhia miongoni mwa mashahidi. Ili ikiwa mmoja wao atapotea, basi mmoja wao amkumbushe huyo mwengine. Na mashahidi wasikatae pindi wanapoitwa. Wala msipuuze kuliandika deni likiwa dogo au kubwa mpaka muda wake. Hayo ndiyo ya uadilifu zaidi kwa Mwenyezi Mungu, na ndiyo sawa zaidi kwa ushahidi, na ya chini zaidi ili msiwe na shaka. Isipokuwa ikiwa ni biashara ya mkono kwa mkono mnayoifanya baina yenu, basi hapo hakuna ubaya juu yenu msipoiandika. Lakini wekeni mashahidi mnapouziana. Wala asitiwe matatani mwandishi wala shahidi. Na mkifanya hivyo, basi hakika huko ni kupita mipaka mlio nako. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anajua kila kitu.
(283) Na mkiwa katika safari, na hamkupata mwandishi, basi yatosha kukabidhiwa rehani. Na mmoja wenu akimwekea amana mwenziwe, basi aliyeaminiwa airudishe amana ya mwenzake, na amche Mwenyezi Mungu, Mola wake Mlezi. Wala msifiche ushahidi. Na atakayeuficha, basi hakika moyo wake ni wenye kutenda dhambi. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyatenda
(284) Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo katika mbingu na viliomo katika dunia. Na mkidhihirisha yaliyomo katika nafsi zenu au mkayaficha, Mwenyezi Mungu atawahesabu kwayo. Kisha atamsamehe amtakaye na amwadhibu amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu.
(285) Mtume ameamini yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na Waumini vile vile. Wote wamemwamini Mwenyezi Mungu, na Malaika wake, na Vitabu vyake na Mitume wake. Hatutofautishi baina ya yeyote katika Mitume wake, na (Waumini) husema: Tumesikia na tumetii. Tunakutaka maghfira Mola wetu Mlezi! Na marejeo ni kwako.
(286) Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kiwango cha iwezavyo. Faida ya iliyoyachuma ni yake, na hasara ya iliyoyachuma ni juu yake pia. (Semeni) Mola wetu Mlezi! Usituchukulie ubaya tukisahau au tukikosea. Mola wetu Mlezi! Usitubebeshe mzigo kama uliyowabebesha wale waliokuwa kabla yetu. Mola wetu Mlezi! Usitutwike tusiyoyaweza, na uyatupilie mbali mabaya yetu, na utusamehe na uturehemu. Wewe ndiye Mlinzi wetu. Basi tupe ushindi dhidi ya kaumu ya makafiri.