54 - Surat Qamar ()

|

(1) Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!

(2) Na wakiona Ishara, hugeuka upande na husema: 'Huu uchawi tu unazidi kuendelea.'

(3) Na wamekanusha na wamefuata matamanio yao. Na kila jambo ni lenye kuthibiti.

(4) Na bila ya shaka zimewajia habari zenye makaripio.

(5) Hekima kaamili; lakini maonyo hayafai kitu!

(6) Basi jiepushe nao. Siku atakapoita mwitaji kuliendea jambo linalochusha.

(7) Macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika.

(8) Wanamkimbilia mwitaji, na makafiri wanasema: 'Hii ni siku ngumu.'

(9) Kabla yao kaumu ya Nuhu walikanusha; wakamkanusha mja wetu, na wakasema ni mwendawazimu, na akakaripiwa.

(10) Basi akamwomba Mola wake Mlezi akasema: 'Kwa hakika mimi nimeshindwa, basi ninusuru!'

(11) Basi tukaifungua milango ya mbingu kwa maji yanayomiminika.

(12) Na tukazipasua ardhi kwa chemichemi, yakakutana maji kwa jambo lililokwisha pangwa.

(13) Na tukambeba kwenye safina ya mbao na kamba.

(14) Ikawa inakwenda kwa macho yetu, kuwa ni malipo kwa alivyokuwa amekanushwa.

(15) Na bila ya shaka tuliiacha iwe ni Ishara. Lakini je, yupo anayekumbuka?

(16) Basi ilikuwaje adhabu yangu, na maonyo yangu.

(17) Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani iwe nyepesi kufahamika. Lakini yupo anayekumbuka?

(18) Kina 'Adi walikanusha. Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?

(19) Hakika Sisi tuliwatumia upepo wa kimbunga katika siku korofi mfululizo.

(20) Ukiwang'oa watu kama vigogo vya mitende vilivyong'olewa.

(21) Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu?

(22) Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani nyepesi kufahamika; lakini yupo anayekumbuka?

(23) Thamudi waliwakanusha Waonyaji.

(24) Wakasema: 'Ati tumfuate binadamu mmoja katika sisi? Basi hivyo sisi tutakuwa katika upotofu na kichaa!

(25) Ni yeye tu aliyeteremshiwa huo ukumbusho kati yetu sote? Bali huyu ni mwongo mno mwenye mshari mkubwa!

(26) Kesho watajua ni nani huyo mwongo mwenye kiburi.

(27) Hakika Sisi tutawatumia ngamia jike ili kuwajaribu, basi watazame vyema tu na ustahamili.

(28) Na waambie kwamba hakika maji yatagawanywa baina yao; kila sehemu ya maji itahudhuriwa na aliyehusika.

(29) Basi wakamwita mtu wao akaja akamchinja.

(30) Basi ilikuwaje adhabu yangu na maonyo yangu!

(31) Hakika Sisi tuliwatumia ukelele mmoja tu, wakawa kama mabuwa ya kujengea ua.

(32) Na bila ya shaka Sisi tumeifanya Qur-ani iwe nyepesi kwa kukumbuka, lakini yupo akumbukaye?

(33) Kaumu Lut'i nao waliwakadhibisha Waonyaji.

(34) Hakika Sisi tukawatumia kimbunga cha vijiwe, isipokuwa wafuasi wa Lut'i. Hao tuliwaokoa karibu na alfajiri.

(35) Kwa neema inayotoka kwetu. Hivyo ndivyo tumlipavyo anayeshukuru.

(36) Na hakika yeye aliwaonya adhabu yetu; lakini wao waliyatilia shaka hayo maonyo.

(37) Na walimtaka awape wageni wake. Tukayapofua macho yao, na tukawaambia: 'Onjeni basi adhabu na maonyo yangu!'

(38) Na iliwafikia wakati wa asubuhi adhabu yangu ya kuendelea.

(39) Basi onjeni adhabu na maonyo yangu!

(40) Na hakika tumeisahilisha Qur-ani kuikumbuka. Lakini yupo anayekumbuka?

(41) Na Waonyaji waliwajia watu wa Firauni.

(42) Walizikadhibisha Ishara zetu zote, nasi tukawashika mshiko wa Mwenye nguvu, Mwenye uwezo.

(43) Je, makafiri wenu ni bora kuliko hao, au yameandikwa vitabuni kuwa nyinyi hamtiwi makosani?

(44) Au ndiyo wanasema: 'Sisi ni wengi tutashinda tu.'

(45) Wingi wao huu utashindwa, na wao watasukumwa nyuma.

(46) Bali Saa ya Kiyama ndiyo miadi yao, na Saa hiyo ni nzito zaidi na chungu zaidi.

(47) Hakika wakosefu wamo katika upotofu na wazimu.

(48) Siku watakapokokotwa Motoni kifudifudi waambiwe: 'Onjeni mguso wa Saqar!'

(49) Kwa hakika Sisi tumekiumba kila kitu kwa kipimo.

(50) Na amri yetu haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.

(51) Na bila ya shaka tumekwisha waangamiza wenzenu. Lakini yupo anayekumbuka?

(52) Na kila jambo walilolifanya limo vitabuni.

(53) Na kila kidogo na kikubwa kimeandikwa.

(54) Hakika wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na mito.

(55) Katika mahali pa kukalia pa haki kwa Mfalme Mwenye uweza.