33 - Surat Al-Ahzab ()

|

(1) Ewe Nabii, mche Mwenyezi Mungu wala usiwatii makafiri na wanafiki. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.

(2) Na fuata uliyofunuliwa kwa wahyi kutokana na Mola wako Mlezi. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari ya mnayoyatenda.

(3) Na mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni wa kutegemewa.

(4) Mwenyezi Mungu hakumwekea mtu yeyote kuwa ana nyoyo mbili ndani ya mwili wake. Wala hakuwafanya wake zenu - ambao mnawalinganisha migongo yao na migongo ya mama zenu - kuwa ni mama zenu. Wala hakuwafanya watoto wenu wa kupanga kuwa ni wana wenu khasa. Hayo ni maneno ya vinywa vyenu tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayesema kweli, naye ndiye anayeongoa Njia.

(5) Waiteni kwa baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamuwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyokosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

(6) Nabii ni bora zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. Na jamaa ni karibu wao kwa wao katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu kuliko Waumini wengine na Wahamiaji. Ila muwe mnawafanyia wema marafiki zenu. Haya yamekwisha andikwa Kitabuni.

(7) Na tulipochukua ahadi kwa Manabii na kwako wewe, na Nuhu na Ibrahim na Isa mwana wa Mariamu, na tulichukua kwao ahadi ngumu.

(8) Ili Mwenyezi Mungu awaulize wakweli juu ya ukweli wao. Na amewaandalia makafiri adhabu chungu.

(9) Enyi mlioamini, zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu zilizo juu yenu. Pale yalipokufikieni majeshi, nasi tukayapelekea upepo, na majeshi msiyoaona. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

(10) Walipowakujieni kutoka juu yenu, na kutoka chini yenu; na macho yalipokodoka, na nyoyo zikapanda kooni, nanyi mkamdhania Mwenyezi Mungu dhana mbalimbali.

(11) Hapo ndipo Waumini walipojaribiwa, na wakatikiswa mtikiso mkali.

(12) Na waliposema wanafiki na wale wenye maradhi katika nyoyo zao: "Mwenyezi Mungu na Mtume wake hawakutuahidi ila udanganyifu tu."

(13) Na kundi moja katika miongoni mwao liliposema: "Enyi watu wa Yathrib, hapana kukaa nyinyi! Rudini." Na kundi jingine miongoni mwao likaomba ruhusa kwa Nabii kwa kusema: "Hakika nyumba zetu ni tupu." Wala hazikuwa tupu; hawakutaka isipokuwa kukimbia tu.

(14) Na lau kuwa wangeliingiliwa kwa pande zote, kisha wakatakiwa kufanya hiana, wangelifanya, na wasingelisita isipokuwa kidogo tu.

(15) Na hakika walikwishamuahidi Mwenyezi Mungu kabla yake kwamba hawatageuza migongo yao. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu ni yenye kuulizwa.

(16) Sema: Kukimbia hakuwafai kitu ikiwa mnakimbia mauti au kuuawa, na hata hivyo hamtastareheshwa isipokuwa kidogo tu.

(17) Sema: Ni nani wa kuwalinda kutokana na Mwenyezi Mungu pindi akiwatakia uovu, au akiwatakia rehema? Wala hawatapata mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

(18) Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawajua hao wanaozuilia, na wanaowaambia ndugu zao: "Njooni kwetu!" Wala hawaingii vitani isipokuwa kidogo tu.

(19) Wana choyo juu yenu. Ikifika hofu, utawaona wanakutazama na macho yao yanazunguka, kama yule ambaye alizimia kwa kukaribia mauti. Na hofu ikiondoka, wanawaudhi kwa ndimi kali, nao ni mabahili kwa kila la heri. Hao hawakuamini, basi Mwenyezi Mungu amevibatilisha vitendo vyao. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

(20) Wanafikiri yale makundi ya maadui hayajaondoka. Na yakija hayo makundi, watatamani laiti wao wako majangwani pamoja na mabedui, wakiuliza habari zenu. Na lau wakiwa pamoja nanyi, hawapigani isipokuwa kidogo tu.

(21) Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Mwenyezi Mungu sana.

(22) Na Waumini walipoyaona makundi, walisema, "Haya ndiyo aliyotuahidi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamesema kweli." Na hayo hayakuwazidisha ila Imani na utiifu.

(23) Miongoni mwa Waumini wapo watu waliotimiza waliyoahidiana na Mwenyezi Mungu. Baadhi yao wamekwisha kufa, na baadhi wanangojea, wala hawakubadilisha ahadi hata kidogo.

(24) Ili Mwenyezi Mungu awalipe wakweli kwa sababu ya ukweli wao, na awaadhibu wanafiki pindi akitaka, au apokee toba yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

(25) Na Mwenyezi Mungu aliwarudisha nyuma makafiri juu ya ghadhabu yao; hawakupata heri yoyote. Na Mwenyezi Mungu amewatosheleza Waumini katika vita. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu na uweza.

(26) Na akawateremsha wale waliowasaidia maadui katika Watu wa Kitabu kutoka katika ngome zao, na akatia hofu katika nyoyo zao. Baadhi yao mkawa mnawaua, na wengine mnawateka.

(27) Na akawarithisha ardhi zao na nyumba zao na mali zao, na ardhi msiyopata kuikanyaga. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.

(28) Ewe Nabii! Waambie wake zako: Ikiwa mnataka maisha ya dunia na pambo lake, basi njooni, nitawapa kutoka nyumba, na kuwaacha mwachano mzuri.

(29) Na ikiwa mnamtaka Mwenyezi Mungu na Mtume wake na nyumba ya Akhera, basi Mwenyezi Mungu amewaandalia wafanyao mema, miongoni mwenu, malipo makubwa.

(30) Enyi wake wa Nabii, atakayefanya uchafu dhahiri miongoni mwenu, atazidishiwa adhabu mara mbili. Na hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

(31) Na miongoni mwenu atakayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akatenda mema, tutampa malipo yake mara mbili, na tutamwandalia riziki ya ukarimu.

(32) Enyi wake wa Nabii, nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu, basi msilegeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.

(33) Na kaeni majumbani kwenu, wala msijishauwe kwa majishauwo ya kijahilia ya kizamani. Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kuwasafisheni sawasawa.

(34) Na kumbukeni yasomwayo majumbani mwenu katika Aya za Mwenyezi Mungu na hekima. Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo ya siri, na Mwenye habari.

(35) Hakika Waislamu wanaume na Waislamu wanawake, na Waumini wanaume na Waumini wanawake, na wanaume watiifu na wanawake watiifu, na wanaume wakweli na wanawake wakweli, na wanaume wanaosubiri, na wanawake wanaosubiri, na wanaume wanyenyekevu na wanawake wanyenyekevu, na wanaume watoao sadaka na wanawake watoao sadaka, na wanaume wanaofunga saumu na wanawake wanaofunga saumu, na wanaume wanaojihifadhi tupu zao, na wanawake wanaojihifadhi tupu zao, na wanaume wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi na wanawake wanaomdhukuru Mwenyezi Mungu kwa wingi, Mwenyezi Mungu amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.

(36) Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na hiari katika jambo lao, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wanapokata shauri katika jambo. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.

(37) Na ulipomwambia yule ambaye Mwenyezi Mungu alimneemesha, nawe ukamneemesha: Shikamana na mkeo, na mche Mwenyezi Mungu. Na ukaficha nafsini mwako aliyotaka Mwenyezi Mungu kuyafichua, nawe ukawachelea watu, hali Mwenyezi Mungu ndiye mwenye haki zaidi kumchelea. Basi Zaid alipokwisha haja naye, tulikuoza wewe, ili isiwe taabu kwa Waumini kuwaoa wake wa watoto wao wa kupanga watapokuwa wamekwisha timiza nao shuruti za talaka. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni yenye kutekelezwa.

(38) Hapana ubaya kwa Nabii kufanya aliyomhalalishia Mwenyezi Mungu. Huo ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa wale waliopita zamani. Na amri ya Mwenyezi Mungu ni mipango iliyokwisha pangwa.

(39) Hao wa zamani, waliokuwa wakifikisha jumbe za Mwenyezi Mungu na wanamwogopa Yeye, na wala hawamwogopi yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mhasibu.

(40) Muhammad si baba wa yeyote katika wanaume wenu, bali ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na Mwisho wa Manabii, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.

(41) Enyi mlioamini! Mdhukuruni Mwenyezi Mungu kwa wingi wa kumdhukuru.

(42) Na mtakaseni asubuhi na jioni.

(43) Yeye ndiye anayekurehemuni na Malaika wake ili akutoeni gizani hadi kwenye nuru. Naye ni Mwenye kuwarehemu sana Waumini.

(44) Maamkizi yao siku ya kukutana naye yatakuwa Salama! Na amewaandalia malipo ya ukarimu.

(45) Ewe Nabii! Hakika Sisi tumekutuma uwe shahidi na mbashiri na mwonyaji.

(46) Na mwitaji kumwendea Mwenyezi Mungu kwa idhini yake, na taa yenye kutoa nuru.

(47) Na wabashirie Waumini ya kwamba wana fadhila kubwa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu.

(48) Wala usiwatii makafiri na wanafiki, na usijali udhia wao. Nawe mtegemee Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Mtegemewa.

(49) Enyi mlioamini, mkiwaoa wanawake, Waumini, kisha mkawapa talaka kabla ya kuwagusa, basi hamna eda juu yao mtakayohesabu. Basi wapeni cha kuwaliwaza, na muwaache kwa wema.

(50) Ewe Nabii, tumekuhalalishia wake zako uliowapa mahari yao, na uliowamiliki kwa mkono wako wa kulia katika wale aliokupa Mwenyezi Mungu, na mabinti wa ami zako, na mabinti wa shangazi zako, na mabinti wa wajomba zako, na mabinti wa dada za mama yako waliohama pamoja nawe; na mwanamke Muumini akijitoa mwenyewe kwa Nabii, kama mwenyewe Nabii akitaka kumuoa. Ni halali kwako wewe tu, si kwa Waumini wengine. Sisi tunajua tuliyowafaradhishia wao katika wake zao na wanawake iliyowamiliki mikono yao ya kulia, ili isiwe dhiki kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

(51) Unaweza kuakhirisha zamu kwa umtakaye katika wao, na umsogeze umtakaye. Na kama ukimtaka yule uliyemtenga, basi si vibaya kwako. Kufanya hivi kutapelekea yaburudike macho yao, wala wasihuzunike, na wawe radhi juu ya kile unachowapa wao wote. Na Mwenyezi Mungu anajua yaliyomo nyoyoni mwenu, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua, Mwenye hekima.

(52) Baada ya hawa hawakuhalalikii wewe wanawake wengine, wala kuwabadilisha kwa wake wengine, ingawa uzuri wao ukikupendeza, isipokuwa yule uliyemmiliki kwa mkono wako wa kulia. Na Mwenyezi Mungu anachunga kila kitu.

(53) Enyi mlioamini, msiingie nyumba za Nabii isipokuwa mpewe ruhusa kwenda kula, siyo kungojea kiive. Lakini mtakapoitwa, basi ingieni, na mkisha kula tawanyikeni, wala msiweke mazungumzo. Hakika hayo yanamuudhi Nabii, naye anawastahi, lakini Mwenyezi Mungu hastahi kwa jambo la haki. Na mnapowauliza wakeze haja, waulizeni kwa nyuma ya mapazia. Hivyo ndivyo usafi zaidi kwa nyoyo zenu na nyoyo zao. Wala haiwafaieni kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wala kuwaoa wake zake baada yake kabisa. Hakika jambo hilo ni kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

(54) Mkidhihirisha chochote kile, au mkikificha, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.

(55) Hapana ubaya kwao, wake za Mtume, kuonana na baba zao, wala watoto wao, wala kaka zao, wala watoto wa kiume wa kaka zao, wala watoto wa kiume wa dada zao, wala wanawake wenzao, wala wale waliomilikiwa na mikono yao ya kulia. Na enyi wanawake, mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kushuhudia kila kitu.

(56) Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Nabii. Enyi mlioamini, mswalieni na mumsalimu kwa salamu.

(57) Hakika wanaomuudhi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Mwenyezi Mungu amewalaani duniani na Akhera, na amewaandalia adhabu ya kufedhehesha.

(58) Na wale wanaowaudhi Waumini wanaume na wanawake pasi na wao kufanya kosa lolote, bila ya shaka wamebeba dhuluma kubwa na dhambi iliyodhahiri.

(59) Ewe Nabii, waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana kwa hivyo wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

(60) Kama wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao, na waenezao fitina katika Madina hawataacha, basi kwa yakini tutakupa mamlaka juu yao, kisha hawatakaa humo karibu yako isipokuwa muda mchache tu.

(61) Wamelaaniwa! Popote watakapoonekana, watakamatwa na watauliwa kabisa.

(62) Hii ni ada ya Mwenyezi Mungu iliyokuwa kwa wale waliopita zamani. Wala hutapata mabadiliko katika ada ya Mwenyezi Mungu.

(63) Watu wanakuuliza habari ya Saa ya Kiyama. Sema: "Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu." Na nini kitakujulisha, pengine hiyo Saa iko karibu?

(64) Hakika Mwenyezi Mungu amewalaani makafiri na amewaandalia Moto unaowaka kwa nguvu.

(65) Watadumu humo milele. Hawatampata mlinzi wala wa kuwanusuru.

(66) Siku ambayo nyuso zao zitapinduliwa pinduliwa katika Moto, watasema: "Laiti tungelimtii Mwenyezi Mungu, na tungelimtii Mtume!"

(67) Na watasema: "Mola wetu Mlezi, hakika sisi tuliwatii bwana zetu na wakubwa wetu; nao ndio waliotupoteza njia."

(68) Mola wetu Mlezi, wape wao adhabu mara mbili, na uwalaani laana kubwa.

(69) Enyi mlioamini, msiwe kama wale waliomtaabisha Musa, lakini Mwenyezi Mungu akamtakasa na hayo waliyoyasema, naye alikuwa mwenye heshima mbele ya Mwenyezi Mungu.

(70) Enyi mlioamini, mcheni Mwenyezi Mungu na semeni maneno ya sawasawa.

(71) Atawatengenezea vitendo vyenu na awasamehe madhambi yenu. Na anayemtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefuzu kufuzu kukubwa.

(72) Kwa hakika Sisi tulikadimisha amana kwa mbingu na ardhi na milima, na vyote hivyo vikakataa kuichukua na vikaogopa. Lakini mwanadamu akaichukua. Hakika yeye amekuwa dhalimu, mjinga.

(73) Ili Mwenyezi Mungu awaadhibu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake, na washirikina wanaume na washirikina wanawake. Na awapokelee toba Waumini wanaume, na Waumini wanawake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.