29 - Surat Al-Ankabut ()

|

(1) Alif Lam Mim

(2) Je, watu wanadhani kwamba wataachwa kwa kuwa wanasema, "Tumeamini." Nao wasijaribiwe?

(3) Hakika tuliwajaribu waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawajua wale walio wakweli na atawajua waongo.

(4) Au wale wanaotenda maovu wanadhani kwamba watatushinda? Ni hukumu mbaya mno hiyo wanayohukumu.

(5) Mwenye kutaraji kukutana na Mwenyezi Mungu, basi hakika miadi ya Mwenyezi Mungu itafika bila ya shaka. Naye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua zaidi.

(6) Na anayefanya juhudi, basi bila ya shaka anafanya juhudi kwa ajili ya nafsi yake. Hakika Mwenyezi Mungu si mhitaji wa walimwengu.

(7) Na wale walioamini na wakatenda mema, kwa yakini tutawafutia makosa yao, na bila shaka tutawalipa bora ya waliyokuwa wakiyatenda.

(8) Na tumemuusia mwanadamu kuwafanyia wema wazazi wake. Na ikiwa watapambana nawe ili unishirikishe Mimi na yale usiyokuwa na elimu nayo, basi usiwatii. Kwangu Mimi ndiyo marejeo yenu, na nitawaambia yale mliyokuwa mkiyatenda.

(9) Na wale walioamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawatia miongoni mwa watu wema.

(10) Na katika watu yupo yule anayesema, "Tumemuamini Mwenyezi Mungu." Lakini anapopewa maudhi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, anayafanya mateso ya watu kama ni adhabu ya Mwenyezi Mungu. Na inapokuja nusura kutoka kwa Mola wako Mlezi, kwa yakini husema, "Hakika sisi tulikuwa pamoja nanyi." Kwani Mwenyezi Mungu hayajui zaidi yaliyomo vifuani mwa walimwengu?

(11) Na hapana shaka Mwenyezi Mungu atawajua wale walioamini, na atawajua wanafiki.

(12) Na wale waliokufuru waliwaambia wale walioamini, "Fuateni njia yetu, nasi tutayabeba makosa yenu." Wala wao hawatabeba katika makosa yao chochote kile. Hakika hao ni waongo.

(13) Na hapana shaka wataibeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa Siku ya Qiyama juu ya yale waliyokuwa wakiyazua.

(14) Na hakika tulimtuma Nuhu kwa watu wake, na akakaa nao miaka elfu kasoro miaka hamsini. Basi tufani ikawachukua, nao ni madhalimu.

(15) Nasi tukamwokoa yeye na wenziwe wa katika safina, na tukaifanya kuwa ni Ishara kwa walimwengu wote.

(16) Na Ibrahim pale alipowaambia watu wake, "Muabuduni Mwenyezi Mungu, na mcheni Yeye. Hiyo ndiyo heri yenu, ikiwa nyinyi mnajua."

(17) Hakika nyinyi mnaabudu tu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu, na mnazua uzushi. Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu hawawamilikii riziki yoyote. Basi tafuteni riziki kutoka kwa Mwenyezi Mungu, na mumuabudu Yeye, na mumshukuru Yeye. Kwake Yeye ndiko mtarudishwa.

(18) Na mkikadhibisha, basi kaumu kadhaa wa kadhaa za kabla yenu zilikwisha kadhibisha. Na si juu ya Mtume isipokuwa kufikisha Ujumbe waziwazi."

(19) Je, wao hawaoni jinsi Mwenyezi Mungu anavyoanzisha uumbaji, na kisha akaurudisha tena. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

(20) Sema, "Tembeeni katika ardhi na tazameni jinsi alivyoanzisha uumbaji; kisha Mwenyezi Mungu ndiye anayeumba umbo la baadaye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

(21) Humuadhibu amtakaye, na humrehemu amtakaye. Na kwake Yeye mtapelekwa.

(22) Na nyinyi si wenye kushinda katika ardhi wala katika mbingu. Wala nyinyi hamna mlinzi wala msaidizi isipokuwa Mwenyezi Mungu.

(23) Na wale waliozikanusha Ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye, hao ndio waliokata tamaa na rehema yangu, na hao ndio wana adhabu chungu.

(24) Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipokuwa walisema, "Muueni au mchomeni moto!" Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu akamwokoa kutokana na moto huo. Hakika katika hayo zipo Ishara kwa watu wanaoamini.

(25) Na alisema, "Hakika nyinyi mmeyashika masanamu badala ya Mwenyezi Mungu kwa mapenzi yaliyo baina yenu katika uhai wa duniani. Kisha Siku ya Qiyama mtakataana nyinyi kwa nyinyi, na mtalaaniana nyinyi kwa nyinyi. Na makazi yenu ni Motoni. Wala hamtapata wa kukunusuru wowote."

(26) Luti akamuamini, na akasema, "Hakika mimi nahamia kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima."

(27) Na tulimtunukia (Ibrahim) Is-haq na Yaa'qub. Na tukajaalia katika dhuria zake Unabii na Kitabu, na tukampa ujira wake katika dunia; naye hakika katika Akhera bila ya shaka ni katika watu wema.

(28) Na pale Luti alipowaambia watu wake, "Hakika nyinyi mnafanya uchafu, ambao hapana mmoja katika walimwengu aliyewatangulia kwa hayo.

(29) Je, nyinyi mnawaingilia wanaume, na mnaikata njia? Na katika mikutano yenu mnafanya maovu?" Basi haikuwa jawabu ya watu wake isipokuwa walisema, "Tuletee hiyo adhabu ya Mwenyezi Mungu ikiwa wewe ni katika wakweli."

(30) Akasema, "Ewe Mola wangu Mlezi, ninusuru kutokana na watu waharibifu hawa!"

(31) Na wajumbe wetu walipomjia Ibrahim na bishara, walisema, "Hakika sisi hapana shaka tutawaangamiza watu wa mji huu, kwani watu wake hakika wamekuwa madhalimu."

(32) Akasema, "Hakika humo yumo Luti." Wao wakasema, "Sisi tunajua zaidi ni nani yumo humo. Hapana shaka tutamwokoa yeye na ahali zake, isipokuwa mkewe aliye miongoni mwa watakaokaa nyuma."

(33) Na wajumbe wetu walipomfikia Luti, alihuzunika kwa sababu yao, na moyo ukaona dhiki kubwa kwa sababu yao. Wakasema, "Usihofu, wala usihuzunike. Hakika sisi tutakuokoa wewe na ahali zako, isipokuwa mkeo aliye miongoni mwa watakaokaa nyuma.

(34) Kwa yakini sisi tutawateremshia watu wa mji huu adhabu kutoka mbinguni kwa sababu ya uchafu wanaoufanya.

(35) Na hakika tumeacha katika mji huo Ishara iliyo wazi kwa watu wanaotumia akili zao.

(36) Na kwa Madyana tulimtuma ndugu yao Shuaibu, naye akasema, "Enyi watu wangu, muabuduni Mwenyezi Mungu na iogopeni Siku ya Akhera, wala msiende katika ardhi mkifanya uharibifu."

(37) Lakini walimkadhibisha, basi ukawatwaa mtikiso wa ardhi, wakapambazukiwa ndani ya nyumba zao nao wameanguka kifudifudi.

(38) Na pia kina A'di na Thamud. Nanyi yamekwisha wabainikia kutokana na maskani zao. Na Shetani aliwapambia vitendo vyao, na akawazuilia Njia, na hali walikuwa wenye kuona.

(39) Na pia Qaruni na Firauni na Hamana! Na Musa aliwajia kwa Ishara waziwazi, lakini walijivuna katika nchi, wala hawakuweza kushinda.

(40) Basi kila mmoja tulimtesa kwa mujibu wa makosa yake. Kati yao wapo tuliowapelekea kimbunga cha changarawe; na kati yao wapo walionyakuliwa na ukelele; na kati yao wapo ambao tuliwadidimiza katika ardhi; na kati yao wapo tuliowazamisha. Wala Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini walikuwa wenyewe wakijidhulumu nafsi zao.

(41) Mfano wa wale waliowafanya walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, ni mfano wa buibui alivyojitandia nyumba. Na hakika nyumba dhaifu mno kuliko zote ni jumba la buibui, laiti kuwa wanajua.

(42) Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua kila kitu wanachokiomba badala yake Yeye. Na Yeye ndiye Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(43) Na hiyo ni mifano tunawapigia watu, na hawaifahamu isipokuwa wenye elimu.

(44) Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi kwa Haki. Kwa hakika katika hayo ipo Ishara kwa Waumini.

(45) Soma yale uliyofunuliwa katika Kitabu, na ushike Swala. Hakika Swala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Mwenyezi Mungu ndilo jambo kubwa kabisa. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyatenda.

(46) Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu isipokuwa kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipokuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni, "Tumeyaamini yaliyoteremshwa kwetu na yaliyoteremshwa kwenu. Na mungu wetu na mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake."

(47) Na namna hivyo tumekuteremshia Kitabu hiki (Qur-ani). Basi wale tuliowapa Kitabu (cha Biblia) wataiamini (Qur-ani), na miongoni mwa hawa (washirikina) wapo watakaoiamini. Na hawazikatai Ishara zetu isipokuwa makafiri.

(48) Na wewe hukuwa kabla yake unasoma kitabu chochote, wala hukukiandika kwa mkono wako wa kulia. Ingelikuwa hivyo, wana batili wangelifanya shaka.

(49) Bali hii (Qur-ani) ni Ishara zilizo wazi katika vifua vya wale waliopewa elimu. Na hawazikatai Ishara zetu isipokuwa madhalimu.

(50) Na walisema, "Mbona hakuteremshiwa Ishara kutoka kwa Mola wake Mlezi?" Sema, "Hakika Ishara ziko tu kwake Mwenyezi Mungu; ama mimi kwa hakika ni mwonyaji mwenye kubainisha tu."

(51) Je, kwani hayakuwatosha ya kwamba tumekuteremshia Kitabu hiki wanachosomewa? Hakika katika hayo, zipo rehema na mawaidha kwa watu wanaoamini.

(52) Sema, "Mwenyezi Mungu anatosha kuwa ni Shahidi kati yangu na nyinyi. Anayajua yaliyomo katika mbingu na ardhi. Na wale wanaoiamini batili na wakamkufuru Mwenyezi Mungu, hao ndio waliohasiri."

(53) Na wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka. Na lau kuwa hapana wakati maalumu uliowekwa, basi adhabu ingeliwajia, na ingeliwatokea kwa ghafla ilhali wao hawana habari.

(54) Wanakuhimiza waletewe adhabu kwa haraka, na hali Jahannamu kwa hakika imewazunguka makafiri!

(55) Siku itakapowafunika adhabu hiyo kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema, "Onjeni hayo mliyokuwa mkiyatenda!"

(56) Enyi waja wangu mlioamini! Kwa hakika ardhi yangu ina wasaa. Basi niabuduni Mimi peke yangu.

(57) Kila nafsi itaonja mauti. Kisha mtarudishwa kwetu.

(58) Na ambao wameamini na wakatenda mema, bila ya shaka tutawaweka katika maghorofa ya Peponi yenye kupitiwa chini yake mito, wakidumu humo. Ni mzuri ulioje huo ujira wa watendao.

(59) Ambao walisubiri, na wakamtegemea Mola wao Mlezi.

(60) Na ni wanyama wangapi hawawezi kujimilikia riziki zao! Mwenyezi Mungu anawaruzuku hao na nyinyi pia. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia Mwenye kujua zaidi.

(61) Na ukiwauliza; ni nani aliyeumba mbingu na ardhi na akafanya jua na mwezi kutiii amri yake? Bila ya shaka, watasema: Mwenyezi Mungu. Wapi basi wanakogeuzwa?

(62) Mwenyezi Mungu humkunjulia, na humkunjia riziki amtakaye katika waja wake. Kwa hakika Mwenyezi Mungu anajua zaidi kila kitu.

(63) Na ukiwauliza: Ni nani anayeteremsha maji kutoka mbinguni, na akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Sema: Alhamdu Lillahi (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu). Bali wengi katika wao hawatumii akili.

(64) Na haya maisha ya dunia si chochote isipokuwa ni pumbao na mchezo. Na hakika nyumba ya Akhera ndiyo maisha hasa; laiti wangelikuwa wanajua!

(65) Na wanapopanda katika marikebu, humwomba Mwenyezi Mungu kwa kumkusudia yeye tu dini yake. Lakini anapowavua wakafika nchi kavu, mara wanamshirikisha.

(66) Wapate kuyakufuru yale tuliyowapa, na wajistareheshe. Lakini watakuja jua!

(67) Je, hawaoni ya kwamba tumeifanya nchi takatifu ina amani, na hali watu wengine wananyakuliwa kote kwa majirani zao? Je, wanaamini batili, na neema za Mwenyezi Mungu wanazikufuru?

(68) Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu au anayekadhibisha Haki inapomjia? Je, si katika Jahannamu ndiyo yatakuwa makazi ya makafiri?

(69) Na wale wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi hakika tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema.