25 - Surat Al-Furqan ()

|

(1) Ametukuka aliyeteremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.

(2) Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.

(3) Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka.

(4) Na wamesema waliokufuru: Haya si chochote ila ni uzushi aliouzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhuluma na uwongo.

(5) Na wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyoviandikisha, anavyosomewa asubuhi na jioni.

(6) Sema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

(7) Na wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?

(8) Au akaangushiwa hazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliyerogwa.

(9) Tazama jinsi wanavyokupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia.

(10) Ametukuka ambaye akitaka atakujalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fahari.

(11) Bali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa.

(12) Ule Moto ukiwaona tangu mahali mbali, wao watasikia hasira yake na mngurumo wake.

(13) Na watakapotupwa humo mahali penye dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe.

(14) Msiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!

(15) Sema: Je, haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamungu, iwe kwao malipo na marejeo?

(16) Watayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayoombwa.

(17) Na siku atakapowakusanya wao na hao wanaowaabudu, na akasema: Je, ni nyinyi mliowapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia?

(18) Watasema: Subhanaka! (Umetakasika na upungufu!) Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walioangamia.

(19) Basi waliwakanusheni kwa mliyoyasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa.

(20) Na hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakienda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine. Je, mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona.

(21) Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi, "Mbona sisi hatukuteremshiwa Malaika au tumwone nasi Mola wetu Mlezi?" Hakika, hawa wamejiona bora nafsi zao; na wamepanda kichwa, vikubwa mno!

(22) Siku watakapowaona Malaika, hakutakuwa na furaha yoyote siku hiyo kwa wahalifu. Na watasema, " Mwenyezi Mungu apishe mbali!" Na tutayajia yale waliyoyatenda katika vitendo vyao, na tuvifanye kuwa mavumbi yaliyotawanyika.

(23) Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo na tuyafanye kama mavumbi yaliyotawanywa.

(24) Wenza wa Pepo siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mahali penye starehe nzuri.

(25) Na siku zitakapopasuka mbingu zifunguke kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi.

(26) Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman (Mwingi wa rehema), na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

(27) Na siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!

(28) Ewe Ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki mwandani!

(29) Hakika alinipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwishanijia, na kweli Shetani ni haini mkubwa kwa mwanadamu.

(30) Na Mtume alikuwa akisema: Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika kaumu yangu wameifanya hii Qur-ani kuwa ni kihame.

(31) Na vivyo hivyo tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wahalifu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.

(32) Na wakasema wale waliokufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur-ani yote mara moja tu? Hayo ni hivyo ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndiyo tumeisoma kwa mafungu.

(33) Wala hawatakuletea mfano wowote, isipokuwa na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora zaidi.

(34) Wale ambao watakusanywa kwa nyuso zao hadi katika Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya mno, nao ndio wenye kuipotea zaidi njia.

(35) Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye kakaye, Harun, kuwa msaidizi.

(36) Tukawaambia: Nendeni kwa kaumu waliokanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa.

(37) Na kaumu ya Nuhu, walipowakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.

(38) Na (tuliwaangamiza) kina 'Adi na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyokuwa kati yao.

(39) Na wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

(40) Na kwa yakini wao walikwisha ujia mji ulioteremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiuona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.

(41) Na wanapokuona, hawakuchukulii isipokuwa ni mzaha tu, na (wanasema): Ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu alimtuma kuwa Mtume?

(42) Kwa hakika alikuwa karibu zaidi kutupoteza tuiache miungu yetu, lau kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapoiona adhabu, ni nani aliyepotea zaidi njia.

(43) Je, umemwona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndiyo mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?

(44) Au wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao sio isipokuwa ni kama wanyama tu, bali wao wamepotea zaidi njia.

(45) Je, huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyokitandaza kivuli. Na angelitaka, angelikifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake.

(46) Kisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.

(47) Naye ndiye aliyewafanyia usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akawafanyia mchana ni kufufuka.

(48) Naye ndiye anayezituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.

(49) Ili kwa hayo tuihuishe nchi iliyokufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tuliowaumba.

(50) Na kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini wengi wa watu wanakataa isipokuwa kukufuru tu.

(51) Na tungelitaka, tungelituma katika kila mji Mwonyaji.

(52) Basi usiwatii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa.

(53) Naye ndiye aliyezipeleka bahari mbili, hii ni tamu mno, na hii ni ya chumvi chungu. Na akaweka baina yake kinga na kizuizi kizuiacho.

(54) Naye ndiye aliyemuumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza mno.

(55) Na wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyowafaa wala yasiyowadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.

(56) Nasi hatukukutuma isipokuwa uwe Mbashiri na Mwonyaji.

(57) Sema: Sikuwaomba ujira wowote juu yake; isipokuwa atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.

(58) Na mtegemee aliye Hai, ambaye hafi. Na umtakase kwa sifa zake. Naye anatosha kuwa ndiye Mwenye habari zote za dhambi za waja wake.

(59) Ambaye aliziumba mbingu na ardhi, na vilivyo ndani yake kwa siku sita. Kisha akainuka juu ya 'Arshi, Arrahman (Mwingi wa rehema)! Uliza habari zake kwa wamjuaye.

(60) Na wanapoambiwa: Msujudieni Arrahman (Mwingi wa rehema!) Wao husema: Ni nani Arrahman (Mwingi wa rehema)? Je, tumsujudie unayetuamrisha wewe tu? Na huwazidishia kujitenga mbali.

(61) Ni Mwenye baraka nyingi yule aliyezijalia nyota mbinguni, na akajalia humo taa na mwezi unaong'ara.

(62) Naye ndiye aliyefanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya yule anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru.

(63) Na waja wa Arrahman (Mwingi wa rehema) ni wale wanaotembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza, hujibu: Salama!

(64) Na wale wanaokesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.

(65) Na wale wanaosema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.

(66) Hakika hiyo ni kituo na makao mabaya.

(67) Na wale ambao wanapotoa matumizi, hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubahili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.

(68) Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa haki, wala hawazini. Na atakayefanya hayo, atapata madhara.

(69) Atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyama, na atadumu humo kwa kufedheheshwa.

(70) Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda matendo mema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.

(71) Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.

(72) Na wale ambao hawatoi ushahidi wa uongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa heshima yao.

(73) Na wale ambao wanapokumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.

(74) a wale wanaosema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wana wetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamungu.

(75) Hao ndio watakaolipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkizi na salama.

(76) Wadumu humo, kituo na makao mazuri kabisa.

(77) Sema: Mola wangu Mlezi asingewajali lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.