12 - Surat Yusuf ()

|

(1) Alif Lam Raa. Hizi ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

(2) Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-ani kwa Kiarabu ili mpate kuzingatia.

(3) Sisi tunasimulia simulizi nzuri zaidi kwa kukufunulia Qur-ani hii. Na ijapokuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa walioghafilika.

(4) Yusuf alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja, na jua, na mwezi. Nimeviota vikinisujudia.

(5) (Baba) akasema: Ewe mwanangu! Usiwasimulie nduguzo ndoto yako, wakaja kukufanyia njama. Hakika Shetani ni adui aliye dhahiri kwa mwanadamu.

(6) Na hivyo ndivyo Mola wako Mlezi atakuteua na atakufundisha katika tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema zake juu yako na juu ya ukoo wa Yaa'qub, kama alivyowatimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.

(7) Kwa yakini katika Yusuf na nduguze ziko ishara kwa wanaouliza.

(8) Pale waliposema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi, ilhali sisi ni kikundi chenye nguvu. Hakika baba yetu yumo katika upotovu wa dhahiri.

(9) Muueni Yusuf, au mtupeni nchi ya mbali ili uso wa baba yenu uwaelekee nyinyi tu. Na baada ya haya mtakuwa kaumu njema.

(10) Akasema msemaji miongoni mwao: Msimuue Yusuf. Lakini mtumbukizeni ndani ya kisima. Baadhi ya wasafiri watakuja mwokota; ikiwa kweli mnataka kufanya.

(11) Wakasema: Ewe baba yetu! Una nini hata hutuamini kwa Yusuf? Na hakika sisi ni wenye kumtakia heri!

(12) Muachilie kesho pamoja nasi, ale kwa furaha na acheze, na bila ya shaka sisi tutamhifadhi.

(13) Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninahofia aje mbwa mwitu akamla ilhali nyinyi mmeghafilika naye.

(14) Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na ilhali sisi ni kundi lenye nguvu kabisa, basi bila ya shaka sisi tutakuwa tumehasirika.

(15) Basi walipokwenda naye, na wakakubaliana kwamba wamtumbukize ndani ya kisima, tulimfunulia Yusuf: Hakika utakuja waambia jambo lao hili, na wala wao hawatambui.

(16) Wakamjia baba yao usiku wakilia.

(17) Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana na tukamwacha Yusuf penye vitu vyetu. Basi mbwa mwitu akamla. Lakini wewe hutuamini ijapokuwa sisi ni wakweli.

(18) Na walikuja na shati lake likiwa lina damu ya uongo. Akasema: Bali nafsi zenu zimewashawishi kutenda kitendo. Lakini subira ni njema; na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyaeleza.

(19) Na ukaja msafara, kisha wakamtuma mchota maji wao, naye akatumbukiza ndoo yake. Alisema: Hii ni bishara njema! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili kumfanya ni bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema hayo wanayoyatenda.

(20) Na wakamuuza kwa thamani duni, dirhamu za kuhesabika tu. Wala hawakuwa na haja naye.

(21) Na yule aliyemnunua huko Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makazi ya heshima huyu; huenda akatufaa au tukamfanya mwanetu. Basi hivyo ndivyo tulivyomuweka Yusuf imara katika ardhi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kushinda katika jambo lake, lakini wengi wa watu hawajui.

(22) Na alipofikia utu uzima wake, tukampa hukumu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mazuri.

(23) Na yule bibi wa nyumba aliyokuwamo Yusuf akamtamani kinyume cha nafsi yake, na akafungafunga milango. Akamwambia: Njoo! Yusuf akasema: Audhubillahi (Najikinga na Mwenyezi Mungu!). Hakika Yeye ni Bwana wangu, aliniweka maskani nzuri, na hakika madhalimu hawafaulu.

(24) Na hakika yule mwanamke alimtamani, na Yusuf angelimtamani lau kuwa hakuona ishara ya Mola wake Mlezi. Ilikuwa hivyo, ili tumuepushie mabaya na uchafu. Hakika yeye alikuwa katika waja wetu walioteuliwa.

(25) Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akalirarua shati lake Yusuf kwa nyuma. Na wakamkuta bwana wake mlangoni. Mwanamke akasema: Hakuna malipo ya mwenye kutaka kumfanyia mabaya mkeo isipokuwa afungwe au kupewa adhabu chungu.

(26) Yusuf akasema: Yeye ndiye aliyenitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi aliyekuwa katika jamaa za mwanamke akasema: Ikiwa shati lake limechanwa kwa mbele, basi mwanamke amesema kweli, naye Yusuf ni katika waongo.

(27) Na ikiwa shati lake limechanwa kwa nyuma, basi mwanamke amesema uongo, naye Yusuf ni katika wakweli.

(28) Basi yule bwana alipoona shati lake limechanwa kwa nyuma, akasema: Hakika haya ni katika vitimbi vyenu wanawake. Hakika vitimbi vyenu ni vikuu.

(29) Yusuf! Achilia mbali haya. Na wewe, mwanamke, omba msamaha kwa dhambi zako. Hakika wewe ni katika waliofanya makosa.

(30) Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa Mheshimiwa anamtamani mtumishi wake bila ya yeye kumtaka! Hakika mapenzi yamemuingia sana moyoni. Sisi hakika tunamwona yumo katika upotovu ulio dhahiri.

(31) Basi aliposikia yule bibi masengenyo yao, aliwaita, na akawawekea matakia ya kuegemea, na akampa kila mmoja wao kisu. Akamwambia Yusuf: Tokeza mbele yao. Basi walipomwona, waliona ni kitu kikubwa kabisa, na wakajikatakata mikono yao. Wakasema: Hasha Lillahi! Huyu si mwanadamu. Huyu si isipokuwa Malaika mtukufu.

(32) Yule bibi akasema: Huyu basi ndiye huyo mliyenilaumia! Na kweli mimi nilimtaka naye akakataa. Na asipofanya ninayomwamrisha, basi hapana shaka atafungwa gerezani, na atakuwa miongoni mwa walio duni kabisa.

(33) Yusuf akasema: Ee Mola wangu Mlezi! Ninapendelea kifungo kuliko haya anayoniitia. Na usiponiondoshea vitimbi vya wanawake, mimi nitaelekea kwao, na nitakuwa katika wajinga.

(34) Basi Mola wake Mlezi akamwitikia, na akamwondoshea vitimbi vyao. Hakika Yeye ni Msikizi, Mwenye kujua vyema.

(35) Kisha ikawadhihirikia baada ya kuona Ishara kuwa lazima wamfunge kwa muda.

(36) Na wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota kuwa ninakamua mvinyo. Na mwingine akasema: Hakika mimi nimeota kuwa nimebeba mikate juu ya kichwa changu, na ndege wanakula kwayo. Hebu tuambie tafsiri yake, kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wazuri.

(37) Akasema: hakitawajia chakula mtakachoruzukiwa isipokuwa nitawaambia hakika yake kabla ya kuwajia. Hayo ni katika yale aliyonifundisha Mola wangu Mlezi. Hakika mimi nimeacha mila ya kaumu wasiomuamini Mwenyezi Mungu, na wakawa wameikufuru Akhera.

(38) Na nimefuata mila ya baba zangu, Ibrahim, na Is-haq, na Yaa'qub. Haikutufailia sisi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu, lakini wengi wa watu hawashukuru.

(39) Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, mabwana wengi tofautitofauti ni bora au Mwenyezi Mungu Mmoja Mwenye nguvu?

(40) Hamuabudu badala yake isipokuwa majina tu mliyowaita nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote. Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Yeye ameamrisha msimuabudu yeyote isipokuwa Yeye tu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka. Lakini wengi wa watu hawajui.

(41) Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu, yeye atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwengine, yeye atasulubiwa, na ndege watakula katika kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilokuwa mkiuliza.

(42) Na akamwambia yule aliyejua kuwa ataokoka katika wawili hao: Nikumbuke kwa bwana wako. Lakini Shetani alimsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi Yusuf akakaa gerezani miaka kadhaa.

(43) Na siku moja mfalme alisema: Hakika mimi nimeota ng'ombe saba wanene wanaliwa na ng'ombe saba waliokonda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi waheshimiwa! Niambieni maana ya ndoto zangu, ikiwa nyinyi mnaweza kuagua ndoto.

(44) Wakasema: Hizi ni ndoto zilizoparaganyika, wala sisi sio wenye kujua tafsiri ya ndoto hizi.

(45) Hapo akasema yule aliyeokoka katika wale wawili na akakumbuka baada ya muda. Mimi nitawaambia tafsiri yake. Basi nitumeni.

(46) Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze ni nini maana ya ng'ombe saba wanene kuliwa na ng'ombe saba waliokonda. Na mashuke saba mabichi na mengine makavu, ili nirejee kwa watu ili wapate kujua.

(47) Akasema: Mtalima miaka saba kwa juhudi. Kwa hivyo mtakachovuna, kiwacheni katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtachokula kwacho.

(48) Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayokula kile mlichoiwekea isipokuwa kidogo katika kile mtakachokihifadhi.

(49) Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao katika mwaka huo watu watasaidiwa, na watakamua.

(50) Na mfalme akasema: Nijieni naye! Basi mjumbe huyo alipomjia, Yusuf akasema: Rudi kwa bwana wako na umuulize wana nini wale wanawake waliojikatakata mikono yao. Hakika Mola wangu Mlezi anazijua vyema njama zao.

(51) Mfalme alisema: Mlikuwa mna nini mlipomtaka Yusuf kinyume na nafsi yake? Wakasema: Hasha Lillahi (Mwenyezi Mungu apishe mbali!) Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa Mheshimiwa yule akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume na nafsi yake, na hakika yeye ni katika wakweli.

(52) Hayo ni ili ajue ya kwamba sikumfanyia hiyana alipokuwa hayupo, na ya kwamba Mwenyezi Mungu haziongoi njama za wahaini.

(53) Nami sijitoi lawamani. Kwa hakika nafsi ni yenye kuamrisha mno mabaya, isipokuwa kile alichorehemu Mola wangu Mlezi. Hakika Mola wangu Mlezi ni Msamehevu mno, Mwenye kurehemu sana.

(54) Basi mfalme akasema, "Nijieni naye, awe wangu mwenyewe hasa." Basi alipomsemesha, akasema, "Hakika wewe leo umekwisha kuwa imara kwetu na umeaminika."

(55) Yusuf akasema: Nifanye msimamizi wa hazina za nchi. Kwani hakika mimi ni mlinzi mzuri, mwenye elimu sana.

(56) Basi hivyo ndivyo tulivyomuimarisha Yusuf katika ardhi, akawa anakaa humo popote anapotaka. Tunamfikishia rehema zetu tumtakaye, wala hatupotezi malipo ya wafanyao mazuri.

(57) Na hakika malipo ya Akhera ni bora zaidi, kwa wale walioamini na wakawa wanamcha Mungu.

(58) Wakaja ndugu zake Yusuf, na wakaingia alimokuwa. Yeye akawajua, na wao hawakumjua.

(59) Na alipowatengenezea tayari haja yao, alisema: Nileteeni ndugu yenu wa kwa baba yenu. Je, hamuoni ya kwamba mimi hakika ninatimiza kipimo, nami ni mbora wa wanaokirimu?

(60) Na msiponijia naye, basi hamtapata kipimo chochote kwangu, wala msinikaribie.

(61) Wakasema: Sisi tutamrai baba yake juu yake, na bila ya shaka tutafanya hilo.

(62) Na Yusuf akawaambia watumishi wake: Tieni bidhaa zao katika mizigo yao, ili wazione watakaporudi kwa watu wao ili wapate kurejea tena.

(63) Basi waliporejea kwa baba yao, walisema: Ewe baba yetu! Tumenyimwa chakula zaidi. Basi muachilie ndugu yetu pamoja nasi ili tupate kupimiwa. Nasi hakika tutamlinda.

(64) Je, niwaamini juu yake isipokuwa kama nilivyowaamini kwa nduguye zamani? Lakini Mwenyezi Mungu ndiye Mbora zaidi wa kulinda, naye ndiye Mbora zaidi wa wanaorehemu.

(65) Na walipofungua mizigo yao, wakakuta bidhaa zao wamerudishiwa. Wakasema: Ewe baba yetu! Tutake nini zaidi? Hizi bidhaa zetu tumerudishiwa. Wacha tuwaletee watu wetu chakula, na tutamlinda ndugu yetu, na tutaongeza shehena ya ngamia. Na hicho ni kipimo kidogo.

(66) Akasema: Sitamuachilia pamoja nanyi mpaka mnipe agano kwa Mwenyezi Mungu kwamba lazima mtanijia naye isipokuwa ikiwa mtazungukwa. Basi walipompa agano yao, alisema: Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa tuyasemayo.

(67) Na akasema: Enyi wanangu! Msiingie kupitia mlango mmoja, bali ingieni kwa kupitia milango tofautitofauti. Wala mimi siwafai kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Hukumu haiko isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu tu. Juu yake Yeye mimi nimetegemea, na juu yake Yeye na wategemee wanaotegemea.

(68) Na walipoingilia pale alipowaamrisha baba yao, hakuwa wa kuwafaa kitu kwa Mwenyezi Mungu, isipokuwa ni haja tu iliyokuwa katika nafsi ya Yaa'qub aliyoitimiza. Na hakika yeye alikuwa na elimu kwa sababu tulimfundisha, lakini wengi wa watu hawajui.

(69) Na walipoingia alimokuwa Yusuf, alimkumbatia nduguye na akasema: Mimi hakika ndiye yule nduguyo. Basi usihuzunike kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

(70) Na alipokwisha watayarishia mahitaji yao, akakitia kikopo cha kunywea maji katika mzigo wa nduguye huyo, kisha mwenye kunadi akanadi: Enyi msafara! Hakika nyinyi ni wezi!

(71) Wakasema huku wamegeuka kuwaelekea, “Kwani mmepoteza nini?”

(72) Wakasema: Tumepoteza kopo la mfalme. Na atakayenijia nalo, atapewa shehena nzima abebayo ngamia. Nami ni mdhamini juu ya hilo.

(73) Wakasema: Tallahi! Hakika mlikwisha jua vyema kwamba sisi hatukuja kufanya uharibifu katika nchi hii, wala sisi si wezi.

(74) Wakasema: Basi malipo yake ni nini ikiwa nyinyi ni waongo?

(75) Wakasema: Malipo yake ni kwamba yule ambaye litapatikana katika shehena naye, basi huyo ndiye malipo yake. Hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.

(76) Basi akaanza na mizigo yao kabla ya mzigo wa nduguye. Kisha akalitoa katika mzigo wa nduguye. Hivyo ndivyo tulivyompangia njama Yusuf. Hakuwa ni wa kumzuia nduguye kwa sheria ya mfalme huyo isipokuwa Mwenyezi Mungu akitaka. Tunamuinua daraja tumtakaye. Na juu ya kila ajuaye yupo ajuaye zaidi.

(77) Wakasema: Akiwa ameiba huyu, basi hakika nduguye vile vile aliiba hapo zamani. Lakini Yusuf akaliweka hilo kisiri katika moyo wake wala hakulionyesha kwao. Akasema: Nyinyi ndio mko katika pahali paovu zaidi, na Mwenyezi Mungu anajua zaidi hayo mnayosingizia.

(78) Wakasema: Ewe Mheshimiwa! Hakika huyu anaye baba mzee sana. Kwa hivyo mchukue mmoja wetu badala yake. Hakika sisi tunakuona wewe ni katika watu wazuri.

(79) Akasema: Mwenyezi Mungu apishe mbali kumshika yeyote yule isipokuwa yule tuliyemkuta naye kitu chetu. Hakika, basi tutakuwa ni wenye kudhulumu.

(80) Basi walipokata tamaa naye, wakenda kando kunong'ona. Mkubwa wao akasema: Je! Hamjui ya kwamba baba yenu amechukua ahadi kutoka kwenu kwa Mwenyezi Mungu, na kabla ya hapo namna mlivyokosa katika agano lenu juu ya Yusuf? Basi mimi sitatoka nchi hii mpaka baba yangu anipe ruhusa au Mwenyezi Mungu anihukumie. Na Yeye ndiye Mbora wa mahakimu.

(81) Rudini kwa baba yenu, na mwambieni: Ee baba yetu! Hakika mwanao ameiba. Na sisi hatutoi ushahidi isipokuwa kwa tunayoyajua. Wala sisi hatukuwa wenye kuhifadhi mambo ya ghaibu.

(82) Na uliza mji tuliokuwamo, na msafara tuliokuja nao. Na hakika sisi ni wakweli.

(83) Akasema: Bali nafsi zenu zimewashawishi kwenye jambo fulani. Basi subira ni nzuri! Huenda Mwenyezi Mungu akaniletea wote pamoja. Hakika Yeye ndiye Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.

(84) Naye akajitenga nao, na akasema: Ah! Huzuni wangu kubwa juu ya Yusuf! Na macho yake yakawa meupe kutokana na huzuni, na aliizuia bila ya kuidhirisha.

(85) Wakasema: Tallahi! Huachi kumkumbuka Yusuf mpaka uwe mgonjwa sana au uwe katika walioangamia.

(86) Akasema: Hakika mimi namshitakia Mwenyezi Mungu tu sikitiko langu na huzuni wangu. Na ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua nyinyi.

(87) Enyi wanangu! Nendeni mumtafute Yusuf na nduguye, wala msikate tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu. Hakika hawakati tamaa na faraja ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kaumu makafiri.

(88) Basi walipoingia alimokuwa Yusuf, wakasema: Ewe Mheshimiwa! Imetupata shida kubwa, sisi na ahali zetu. Na tumekujia na mali kidogo. Basi tutimizie tu kipimo na tupe sadaka. Hakika Mwenyezi Mungu huwalipa watoao sadaka.

(89) Akasema: Je, mnajua yale mliyomfanyia Yusuf na nduguye mlipokuwa wajinga?

(90) Wakasema: Kumbe hakika wewe ndiye Yusuf? Akasema: Mimi ndiye Yusuf, na huyu ni ndugu yangu. Mwenyezi Mungu ametufanyia hisani. Hakika anayemcha Mungu na akasubiri, basi Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wafanyao mazuri.

(91) Wakasema: Tallahi! Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi, na hakika sisi tulikuwa wenye kukosa.

(92) Akasema: Leo hakuna lawama yoyote juu yenu. Mwenyezi Mungu atawasamehe, naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanaorehemu.

(93) Nendeni na shati langu hili na mlitupe usoni mwa baba yangu, atakuwa mwenye kuona. Na mnijie na ahali zenu wote.

(94) Na ulipoondoka tu msafara, baba yao akasema: Hakika mimi ninaipata harufu ya Yusuf, lau kuwa hamtanituhumu.

(95) Wakasema: Tallahi! Hakika wewe bado ungali katika upotovu wako wa zamani.

(96) Basi alipofika tu mbashiri huyo, akalitupa shati hilo usoni pake, basi akarejea kuona. Akasema: Je, sikuwaambia kuwa mimi ninajua kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua nyinyi?

(97) Wakasema: Ewe baba yetu! Tuombee msamaha kwa dhambi zetu. Hakika sisi tulikuwa katika waliokosa.

(98) Akasema: Nitakuja waombea msamaha kwa Mola wangu Mlezi. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusamehe mno, Mwenye kurehemu sana.

(99) Na wakati walipoingia alimokuwa Yusuf, aliwakumbatia wazazi wake na akasema: Ingieni Misri, Inshallah kwa amani.

(100) Na akawapandisha wazazi wake kwenye kiti cha enzi. Na wote wakaporomoka kumsujudia. Na akasema: Ewe baba yangu! Hii ndiyo tafsiri ya ile ndoto yangu ya zamani. Na Mola wangu Mlezi ameifanya kuwa kweli. Na Mwenyezi Mungu amenifanyia uzuri kunitoa gerezani, na akawaleta kutoka jangwani baada ya Shetani kuchochea baina yangu na ndugu zangu. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mpole kwa alitakalo. Hakika Yeye ndiye Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.

(101) Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika umenipa katika ufalme, na umenifunza katika tafsiri ya mambo. Ewe Muumba wa mbingu na ardhi! Wewe ndiye Mlinzi wangu katika dunia na Akhera. Nifishe hali ya kuwa ni Muislamu na niunganishe na walio wema.

(102) Hizo ni katika habari za ghaibu tulizokufunulia. Na hukuwa pamoja nao walipoazimia jambo lao hilo walipokuwa wanafanya njama zao.

(103) Na wengi wa watu si wenye kuamini hata ukijitahidi vipi.

(104) Wala wewe huwaombi ujira kwa haya. Hayakuwa haya isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

(105) Na ni ishara ngapi katika mbingu na ardhi wanazozipitia, lakini wao wanazipuuza.

(106) Na wengi wao hawamuamini Mwenyezi Mungu pasina kuwa ni washirikina.

(107) Je, wana amani kuwa iwajie adhabu ya Mwenyezi Mungu ya kuwagubika, au iwajie Saa ya Qiyama kwa ghafla, na hali hawatambui?

(108) Sema: Hii ndiyo Njia yangu - ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa ufahamu mzuri - mimi na wale wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.

(109) Na hatukuwatuma Mitume kabla yako isipokuwa wanaume tuliowafunulia wahyi miongoni mwa watu wa mijini. Je, hawakutembea katika ardhi wakaona jinsi ulivyokuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Na hakika nyumba ya Akhera ndiyo bora kwa wamchao Mungu. Basi hamtumii akili?

(110) Hata Mitume walipokata tamaa (ya watu wao kuamini) na wakaona kuwa wamekadhibishwa, hapo ikawajia nusura yetu, kwa hivyo wakaokolewa sawasawa tuwatakao. Na adhabu yetu haiwezi kurudishwa dhidi ya kaumu wahalifu.

(111) Kwa hakika katika hadithi zao limo zingatio kwa wenye akili. Hazikuwa hadithi tu zilizozuliwa, bali ni za kusadikisha yale yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kina wa kila kitu, na ni uwongofu na rehema kwa kaumu inayoamini.