14 - Surat Ibrahim ()

|

(1) Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu tulichokiteremsha kwako ili uwatoe watu kwenye giza mbalimbali uwapeleke kwenye mwangaza, kwa idhini ya Mola wao Mlezi, uwafikishe kwenye Njia ya Mwenye nguvu, Msifika,

(2) Naye ni Mwenyezi Mungu ambaye ni vyake Yeye vyote vilivyo katika mbingu zote na ardhi. Na ole wao makafiri kwa adhabu kali!

(3) Wale wanaofadhilisha uhai wa dunia kuliko Akhera, na wanawazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka kuipotosha. Hao wako katika upotofu wa mbali.

(4) Na hatukumtuma Mtume yeyote isipokuwa kwa ulimi wa kaumu yake ili apate kuwabainishia. Basi Mwenyezi Mungu anampoteza amtakaye, na anamwongoa amtakaye. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(5) Na tulimtuma Musa na miujiza yetu, tukamwambia: Watoe kaumu yako kwenye giza mbalimbali uwapeleke kwenye nuru. Na uwakumbushe siku za Mwenyezi Mungu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kila mwenye kusubiri sawasawa, mwenye kushukuru sana.

(6) Na Musa alipowaambia kaumu yake, "Kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu pale alipowaokoa kutokana na watu wa Firauni waliokuwa wakiwatia adhabu mbaya kabisa, wakiwachinja wana wenu wanaume, na wakiwaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa unaotoka kwa Mola wenu Mlezi."

(7) Na alipotangaza Mola wenu Mlezi: Mkishukuru, nitawazidishia; na mkikufuru, basi adhabu yangu ni kali.

(8) Na Musa alisema: Mkikufuru nyinyi na wote walio katika dunia, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Msifika.

(9) Je, hazikuwafikia habari za wale waliokuwa kabla yenu? Kaumu ya Nuhu, na 'Aadi, na Thamud, na wale waliokuwa baada yao, ambao hakuna awajuaye isipokuwa Mwenyezi Mungu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi, na wao wakarudisha mikono yao kwenye vinywa vyao, wakasema: Hakika sisi tumeyakufuru hayo mliyotumwa nayo, na hakika sisi tuko katika shaka kubwa na hayo mnayotuitia.

(10) Mitume wao wakasema: Ati kuna shaka kuhusiana na Mwenyezi Mungu, Muumba mbingu na ardhi? Yeye anawaita ili awafutie madhambi yenu, na awape muhula mpaka muda uliowekwa. Wakasema: Nyinyi si chochote isipokuwa ni wanadamu tu kama sisi. Mnataka kutuzuilia na yale waliyokuwa wakiabudu baba zetu. Basi tujieni na hoja iliyo wazi.

(11) Mitume wao wakawaambia: Sisi kweli si chochote isipokuwa ni wanadamu kama nyinyi. Lakini Mwenyezi Mungu humneemesha amtakaye katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kuwaletea uthibitisho isipokuwa kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na juu ya Mwenyezi Mungu basi na wategemee Waumini.

(12) Na tuna nini hata tusimtegemee Mwenyezi Mungu, na hali Yeye ametuongoa kwenye Njia zetu. Na hakuna hakika tutayavumilia hayo maudhi mnayotuudhi nayo. Na juu ya Mwenyezi Mungu na wategemee wanaotegemea.

(13) Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume wao: Hakika, tutawatoa katika nchi yetu, au lazima mtarudi katika mila yetu. Basi Mola wao Mlezi aliwafunulia wahyi: Hakika tutawaangamiza madhalimu!

(14) Na tutawaweka katika ardhi baada yao. Haya ni kwa anayehofu kusimamishwa mbele yangu, na akahofu ahadi yangu ya adhabu.

(15) Na wakaomba ushindi, na akashindwa kila jabari mkaidi.

(16) Ambaye nyuma yake ipo Jahannamu, na atanyweshwa katika maji ya usaha.

(17) Awe anayagugumia, wala hawezi kuyameza. Na mauti yatamjia kutokea kila upande, naye wala hafi. Na zaidi ya hayo ipo adhabu nyengine kali vile vile.

(18) Mfano wa wale waliomkufuru Mola wao Mlezi, vitendo vyao ni kama jivu linalopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya upepo mkali. Hawawezi kupata chochote katika yale waliyoyachuma. Huko ndiko kupotea kwa mbali!

(19) Je, huoni kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi kwa Haki? Akitaka, anawaondoa na alete viumbe wapya!

(20) Na hilo kwa Mwenyezi Mungu si jambo gumu.

(21) Na wote watajitokeza mbele ya Mwenyezi Mungu. Wanyonge watawaambia wale waliotakabari: Hakika sisi tulikuwa wafwasi wenu; basi hebu hamtuondolei kidogo hivi katika adhabu ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Lau Mwenyezi Mungu angelituongoa, basi hakuna shaka nasi tungeliwaongoa. Ni mamoja kwetu tukipapatika au tukisubiri; hatuna popote pa kukimbilia.

(22) Na shetani atasema itakapokatwa hukumu: Hakika Mwenyezi Mungu aliwaahidi ahadi ya kweli. Nami niliwaahidi; lakini sikuwatimizia ahadi yangu. Na sikuwa na mamlaka yoyote juu yenu, isipokuwa niliwaita, nanyi mkaniitikia. Basi msinilaumu mimi, bali jilaumuni wenyewe. Mimi siwezi kuwa mtetezi wenu, wala nyinyi hamuwezi kuwa watetezi wangu. Hakika mimi niliyakufuru tangu zamani huko kunishirikisha kwenu na Mwenyezi Mungu. Hakika madhalimu wana adhabu chungu.

(23) Na wale walioamini na wakatenda mema wataingizwa katika Mabustani yapitayo mito kwa chini yake, wadumu humo kwa idhini ya Mola wao Mlezi. Maamkizi yao humo yatakuwa: Salaam!

(24) Je, hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri, mizizi yake ni imara, na matawi yake yako mbinguni.

(25) Hutoa matunda yake kila wakati kwa idhini ya Mola wake Mlezi. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ili wapate kukumbuka.

(26) Na mfano wa neno ovu ni kama mti muovu, uliong'olewa juu ya ardhi. Hauna uimara wowote.

(27) Mwenyezi Mungu huwaimarisha wale walioamini kwa kauli ya imara katika uhai wa dunia na katika Akhera. Na Mwenyezi Mungu huwapoteza madhalimu. Na Mwenyezi Mungu hufanya apendavyo.

(28) Je, hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyezi Mungu kwa kufuru, na wakawafikisha kaumu yao kwenye nyumba ya maangamizo?

(29) Nayo ni Jahannamu wataiingia! Na ni mabaya mno makazi hayo!"

(30) Na walimfanyia Mwenyezi Mungu wenza ili wapoteze watu kutoka kwenye Njia yake. Sema: Stareheni! Kwani maishio yenu ni Motoni!

(31) Waambie waja wangu walioamini, wasimamishe Swala, na watoe katika tulivyowaruzuku, kwa siri na dhahiri, kabla ya kufika kwa Siku isiyokuwa na biashara yoyote wala urafiki wa dhati.

(32) Mwenyezi Mungu ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi, na akateremsha maji kutoka mbinguni. Na kwa hayo akatoa matunda kuwa ni riziki yenu. Na akawatiishia majahazi yanayokwenda baharini kwa amri yake, na akawatiishia mito.

(33) Na akawatiishia jua na mwezi vinavyokwenda daima dawamu, na akawatiishia usiku na mchana.

(34) Na akawapa katika kila mlichomuomba. Na mkihesabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti. Hakika mwanadamu ni dhalimu mkubwa, mwenye kuzikufuru neema.

(35) Na Ibrahim aliposema: Ewe Mola wangu Mlezi! Ujaalie mji huu uwe wa amani, na uniepushe mimi na wanangu na kuabudu masanamu.

(36) Ewe Mola wangu Mlezi! Hakika hayo yamewapoteza wengi wa watu. Basi aliyenifuata mimi, huyo ni wangu, na aliyeniasi, hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.

(37) Mola wetu Mlezi! Hakika mimi nimewaweka baadhi ya dhuria yangu katika bonde lisilokuwa na mimea, kwenye Nyumba yako Takatifu, ewe Mola wetu Mlezi, ili wasimamishe Swala. Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao, na waruzuku matunda, ili wapate kushukuru.

(38) Ewe Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe unajua tunayoyaweka hadharani na tunayoyaficha. Na hakuna kitu kinachofichikana kwa Mwenyezi Mungu katika ardhi wala katika mbingu.

(39) Alhamdulillahi (Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyenitunuku pamoja na uzee wangu Ismail na Is-haq. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusikia sana maombi.

(40) Mola wangu Mlezi! Nijaalie niwe mwenye kusimamisha Swala, na katika dhuria yangu pia. Ewe Mola wetu Mlezi, na ipokee dua yangu.

(41) Mola wetu Mlezi! Nighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku itakaposimama hesabu.

(42) Wala usidhani Mwenyezi Mungu ameghafilika na wanayoyafanya madhalimu. Hakika Yeye anawaahirisha tu mpaka siku yatakapokodoka macho yao.

(43) Natakuwa mbioni, vichwa juu, huku macho yao hayapepesi, na nyoyo zao tupu.

(44) Na waonye watu siku itakapowajia adhabu, na wale waliodhulumu waseme, "Ewe Mola wetu Mlezi! Tuahirishe muda kidogo tuitikie wito wako na tuwafuate Mitume." Kwani nyinyi hamkuapa zamani kwamba hamuwezi kuondoka?

(45) Na mkakaa katika maskani zile zile za wale waliozidhulumu nafsi zao. Na ikawabainikia jinsi tulivyowatendea. Nasi tukawapigia mifano mingi.

(46) Na hakika walifanya vitimbi vyao, na vitimbi vyao anavijua Mwenyezi Mungu. Wala vitimbi vyao si vya kuondosha milima.

(47) Basi kamwe usimdhanie Mwenyezi Mungu kuwa ni mwenye kuwavunjia ahadi yake Mitume wake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye Nguvu, Mwenye kulipiza.

(48) Siku itakapogeuzwa ardhi iwe ardhi nyingine, na mbingu zote pia. Nao watahudhuria mbele ya Mwenyezi Mungu Mmoja, Mshindi.

(49) Na utaona wahalifu siku hiyo wamefungwa katika minyororo.

(50) Nguo zao zitakuwa za lami, na Moto utazigubika nyuso zao.

(51) Ili Mwenyezi Mungu ailipe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwepesi wa kuhesabu.

(52) Huu ni ufikishaji kwa watu, ili waonywe kwao, na wapate kujua kuwa hakika Yeye ni Mungu Mmoja, na wapate kukumbuka wenye akili.