66 - Surat At-Tahrim ()

|

(1) Ewe Nabii! Kwa nini unaharamisha alichokuhalilishia Mwenyezi Mungu? Unatafuta kuwaridhi wake zako. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mno, Mwingi wa kurehemu.

(2) Hakika Mwenyezi Mungu kakupeni Sheria ya kufungua viapo vyenu, na Mwenyezi Mungu ni Mola wenu. Na Yeye ni Mwenye kujua mno, Mwenye hekima.

(3) Na Nabii alipomwambia mmoja wa wake zake jambo la siri. Basi alipolitangaza yule mke, na Mwenyezi Mungu akamdhihirishia Mtume, alimjuvya sehemu na akaacha sehemu nyingine. Alipomwambia hayo, huyo mke akasema: 'Ni nani aliyekwambia haya?' Mtume akasema: 'Kaniambia Yule ajuaye zaidi, Mwenye habari zote!'

(4) Kama nyinyi wawili hamtatubia kwa Mwenyezi Mungu, basi nyoyo zenu zimekwishaelekea huko. Na mkisaidiana dhidi yake (Mtume), basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye kipenzi chake, na Jibrili, na Waumini wema, na zaidi ya hayo Malaika pia watasaidia.

(5) Asaa Mola wake Mlezi, akikupeni talaka, akampa wake wengine badala yenu nyinyi, walio bora kuliko nyinyi, wanyenyekevu, Waumini, watawa, waliotubu, wenye kushika ibada, wafanyao heri, waliowahi kuoleka na wale ambao hawajawahi kuoleka.

(6) Enyi mlioamini! Jilindeni nafsi zenu na ahali zenu kutokana na Moto ambao kuni zake ni watu na mawe. Wanausimamia Malaika wakali, wenye nguvu, hawamuasi Mwenyezi Mungu kwa anayowaamrisha, na wanatenda wanayoamrishwa.

(7) Enyi mliokufuru! Msilete udhuru leo. Hakika mnalipwa mliyokuwa mkiyatenda.

(8) Enyi mlioamini! Tubuni kwa Mwenyezi Mungu toba iliyo ya kweli! Asaa Mola wenu Mlezi akakufutieni maovu yenu na akakuingizeni katika Pepo zipitazo mito kati yake, siku ambayo Mwenyezi Mungu hatamdhalilisha Nabii na wale walioamini pamoja naye. Nuru yao inakwenda mbele yao na pande zao za kulia, na huku wanasema: 'Mola wetu Mlezi! Tutimilizie nuru yetu, na utughufirie! Hakika Wewe ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.'

(9) Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanafiki, na kuwa mgumu kwao! Na makazi yao ni Jahannamu. Na hayo ni marejeo mabaya.

(10) Mwenyezi Mungu amewapigia mfano wale waliokufuru: mke wa Nuhu na mke wa Lut'i. Walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu. Lakini wakawafanyia uhaini waume zao, nao wasiwafae kitu kutokana na Mwenyezi Mungu. Na ikasemwa: 'Ingieni Motoni pamoja na wanaoingia!'

(11) Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano wale walioamini - mkewe Firauni, aliposema: Mola wangu Mlezi! Nijengee kwako nyumba Peponi, na uniokoe na Firauni na vitendo vyake, na uniokoe na watu madhalimu.

(12) Na Mariamu binti wa Imrani, aliyelinda ubikira wake, na tukampulizia humo kutoka roho yetu, na akayasadiki maneno ya Mola wake Mlezi na Vitabu vyake, na alikuwa miongoni mwa watiifu.