22 - Surat Al-Hajj ()

|

(1) Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi. Hakika mtetemeko wa Saa (ya Qiyama) ni jambo kuu.

(2) Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshaye, na kila mwenye mimba ataharibu mimba yake. Na utaona watu wamelewa, na kumbe hawakulewa. Lakini adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kali.

(3) Na miongoni mwa watu wapo wanaobishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya ilimu, na wanamfuata kila shetani aliyeasi.

(4) meandikiwa kwamba anayemfanya kuwa rafiki, basi huyo hakika atampoteza na atamwongoza kwenye adhabu ya Moto mkali.

(5) "Enyi watu! Ikiwa nyinyi mna shaka juu ya kufufuliwa basi kwa hakika Sisi tulikuumbeni kutokana na udongo, kisha kutokana na manii, kisha kutokana na kipande cha damu iliyogandana, kisha kutokana na kipande cha nyama chenye umbo na kisichokuwa na umbo, ili tuwabainishie. Nasi tunakiweka katika matumbo ya uzazi tunachokitaka mpaka muda uliowekwa. Kisha tunawatoe kwa hali ya mtoto mchanga, kisha mfikie kutimia akili. Na wapo katika nyinyi wanaokufa, na wapo katika nyinyi wanaorudishwa kwenye umri wa unyonge kabisa, hata mtu awe hajui kitu baada ya kuwa anakijua. Na unaiona ardhi imetulia kimya, lakini tunapoyateremsha maji juu yake husisimka na kututumka, na kumea kila namna ya mimea mizuri.

(6) Hayo ni kwa sababu hakika Mwenyezi Mungu ndiye Haki, na kwamba hakika Yeye ndiye mwenye kuhuisha wafu, na kwamba hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.

(7) Na kwamba hakika Saa (ya Qiyama) itakuja hapana shaka kwa hilo, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu atawafufua walio makaburini."

(8) Na katika watu wapo wanaobishana juu ya Mwenyezi Mungu bila ya elimu, wala uwongofu, wala Kitabu chenye nuru.

(9) Anayegeuza shingo yake ili kupoteza watu waiache Njia ya Mwenyezi Mungu. Duniani atapata hizaya, na Siku ya Kiyama tutamwonjesha adhabu ya kuunguza.

(10) (Ataambiwa): Hayo ni kwa sababu ya iliyoitanguliza mikono yako. Na hakika Mwenyezi Mungu si dhalimu kwa waja.

(11) Na katika watu wapo wanaomuabudu Mwenyezi Mungu kwa ukingoni. Ikimfikia kheri hutulia kwayo, na ukimfikia msukosuko hugeuza uso wake. Amekhasiri dunia na Akhera; hiyo ndiyo hasara iliyo wazi.

(12) Badala ya Mwenyezi Mungu, yeye huomba kisichomdhuru wala kumnufaisha. Huko ndiko kupotolea mbali!

(13) Humuomba yule ambaye bila ya shaka dhara yake ipo karibu zaidi kuliko nafuu yake. Kwa hakika huyo ni mlinzi muovu, na rafiki muovu.

(14) Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza wale walioamini na wakatenda mema katika Bustani zipitazo mito kwa chini yake. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda atakayo.

(15) Anayedhani kwamba Mwenyezi Mungu hatamnusuru (Mtume) katika dunia na Akhera, basi na afunge kamba kwenye dari kisha na aikate, na atazame je hila yake itayaondoa hayo yaliyomkasirisha?

(16) Na namna hivyo tumeiteremsha (Qur-ani) kuwa ni Aya zilizo wazi, na hakika Mwenyezi Mungu humwongoa amtakaye.

(17) Hakika walioamini, na ambao ni Mayahudi na Wasabai na Wakristo na Majusi na wale walioshiriki - hakika Mwenyezi Mungu atawapambanua baina yao Siku ya Kiyama. Hakika Mwenyezi Mungu ni Shahidi wa kila kitu.

(18) Je! Huoni kwamba vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, na jua, na mwezi, na nyota, na milima, na miti, na wanyama, na wengi miongoni mwa watu. Na wengi imewastahiki adhabu. Na anayefedheheshwa na Mwenyezi Mungu hana wa kumheshimu. Hakika Mwenyezi Mungu hutenda ayapendayo.

(19) Hawa ni wagomvi wawili waliogombana kwa ajili ya Mola wao Mlezi. Basi waliokufuru watakatiwa nguo za moto, na yatamiminwa juu ya vichwa vyao maji yanayochemka.

(20) Kwa maji hayo vitayeyushwa vilivyomo matumboni mwao, na ngozi zao pia.

(21) Na kwa ajili yao yatakuwapo marungu ya chuma.

(22) Kila wakitaka kutoka humo kwa sababu ya uchungu watarudishwa humo humo, na wataambiwa: Onjeni adhabu ya kuunguza!

(23) Hakika Mwenyezi Mungu atawaingiza walioamini na wakatenda mema katika Bustani zipitiwazo na mito kati yake. Watapambwa humo kwa mapambo ya mikononi ya dhahabu na lulu. Na mavazi yao humo ni hariri.

(24) Na wataongozwa kwenye maneno mazuri, na wataongozwa kwenye Njia ya Msifiwa.

(25) Hakika wale waliokufuru na wakazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu na Msikiti Mtakatifu, ambao tumeufanya kwa ajili ya watu wote sawasawa, kwa wakaao humo na wageni. Na kila atakayetaka kufanya upotofu humo kwa dhuluma, basi tutamwonjesha adhabu chungu.

(26) Na pale tulipomweka Ibrahim pahala penye ile Nyumba tukamwambia: Usinishirikishe na chochote; na isafishe Nyumba yangu kwa ajili ya wanaoizunguka kwa kut'ufu, na wanaokaa hapo kwa ibada, na wanaorukuu, na wanaosujudu.

(27) Na watangazie watu Hija; watakujia kwa miguu na juu ya kila ngamia aliyekonda, wakija kutoka katika kila njia ya mbali.

(28) Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa aliowaruzuku. Basi kuleni katika hao na mlisheni mwenye shida aliye fakiri.

(29) Kisha wajisafishe taka zao, na waondoe nadhiri zao, na waizunguke Nyumba ya Kale.

(30) Ni hivyo! Na anayevitukuza vitakatifu vya Mwenyezi Mungu basi hayo ndiyo kheri yake mbele ya Mola wake Mlezi. Na mmehalalishiwa nyama hoa ila wale mliosomewa. Basi jiepusheni na uchafu wa masanamu, na jiepusheni na usemi wa uongo.

(31) Kwa kumtakasikia Imani Mwenyezi Mungu, bila ya kumshirikisha. Na anayemshirikisha Mwenyezi Mungu ni kama kwamba ameporomoka kutoka mbinguni, kisha ndege wakamnyakua au upepo ukamtupa pahali mbali.

(32) Ndiyo hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.

(33) Katika hao nyinyi mna manufaa mpaka muda maalumu. Kisha pahali pa kuchinjiwa kwake ni kwenye Nyumba ya Kale.

(34) Na kila umma tumewafanyia mahali pa kuchinjia mihanga ya ibada ili walitaje jina la Mwenyezi Mungu juu ya vile walivyoruzukiwa katika wanyama wa mifugo. Basi Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Jisalimishieni kwake tu, na wabashirie wanyenyekevu.

(35) Wale ambao, anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hutetemeka, na wanaovumilia kwa yanayowasibu, na wanaoshika Sala, na wanatoa katika tulivyowaruzuku.

(36) Na ngamia wa sadaka tumewafanyia kuwa ni kudhihirisha matukuzo kwa Mwenyezi Mungu; kwa hao mna kheri nyingi. Basi litajeni jina la Mwenyezi Mungu juu yao wanaposimama kwa safu. Na waangukapo ubavu kuleni katika hao na walisheni waliokinai na wanaolazimika kuomba. Ndiyo kama hivi tumewafanya hawa wanyama dhalili kwenu ili mpate kushukuru.

(37) Nyama zao hazimfikii Mwenyezi Mungu wala damu zao, lakini unamfikia uchamungu wenu. Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo waongoa. Na wabashirie wafanyao mema.

(38) Hakika Mwenyezi Mungu huwakinga walioamini. Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila haini mwingi wa kukanya mema.

(39) Wameruhusiwa kupigana wale wanaopigwa vita kwa sababu wamedhulumiwa - na kwa yakini Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuwasaidia.

(40) Wale ambao wametolewa majumbani mwao pasipo haki, ila kwa kuwa wanasema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingelivunjwa nyumba za watawa, na makanisa, na masinagogi, na misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anayemsaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mtukufu.

(41) Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndiyo marejeo ya mambo yote.

(42) Na wakikukanusha basi walikwisha kanusha kabla yao watu wa Nuhu, na kina A'ad na kina Thamud.

(43) Na watu wa Ibrahim na watu wa Luti.

(44) Na watu wa Madiana. Na Musa pia alikanushwa. Nikawapa muda makafiri, kisha nikawatia mkononi. Basi ilikuwaje adhabu yangu!

(45) Basi ni miji mingapi iliyokuwa ikidhulumu tuliiangamiza, ikawa imebaki magofu, na visima vilivyoachwa, na majumba yaliyokuwa madhubuti?

(46) Je, hawatembei katika ardhi ili wapate kuwa na nyoyo zao za kuzingatia, au masikio ya kusikilia? Kwani hakika si macho yanayopofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo zilizomo vifuani.

(47) Na wanakuhimiza ulete adhabu, lakini Mwenyezi Mungu hatakwenda kinyume na ahadi yake kabisa. Na hakika siku moja kwa Mola wako Mlezi ni kama miaka elfu mnavyohesabu nyinyi.

(48) Na ni miji mingapi niliipa muda na hali ilikuwa imedhulumu, na kisha nikaitia mkononi? Na kwangu Mimi ndiyo marejeo yote.

(49) Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni mwonyaji kwenu niliye dhahiri.

(50) Basi walioamini na wakatenda mema watapata kusitiriwa dhambi na riziki za ukarimu.

(51) Na wanaojitahidi kuzipinga Aya zetu hao ndio watu wa Motoni.

(52) Na hatukumtuma kabla yako Mtume wala Nabii ila anaposoma, Shetani hutumbukiza katika masomo yake. Lakini Mwenyezi Mungu huyaondoa anayoyatia Shetani; kisha Mwenyezi Mungu huzithibitisha Aya zake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.

(53) Hayo ni ili alifanye lile analolitia Shetani liwe ni fitna kwa wale wenye maradhi ndani ya nyoyo zao, na wale ambao nyoyo zao ni ngumu. Na hakika madhalimu wamo katika mfarakano wa mbali.

(54) Na ili waliopewa elimu wajue kuwa hayo ni Haki itokayo kwa Mola wako Mlezi na waamini, na zipate kutua nyoyo zao. Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayewaongoa wenye kuamini kwenye Njia Iliyonyooka.

(55) Na waliokufuru hawatoacha kuwa katika wasiwasi kwa hilo mpaka Saa ya Kiyama iwafikie ghafla, au iwafikie adhabu ya Siku Tasa.

(56) Ufalme wote siku hiyo utakuwa wa Mwenyezi Mungu. Atahukumu baina yao. Basi walioamini na wakatenda mema watakuwa katika Bustani zenye neema.

(57) Na waliokufuru na kuzikanusha Ishara zetu, basi hao watapata adhabu ya kufedhehesha.

(58) Na waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kisha wakauwawa au wakafa, bila ya shaka Mwenyezi Mungu atawaruzuku riziki njema. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mbora wa wanaoruzuku.

(59) BIla ya shaka atawaingiza pahala watakapoparidhia. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mpole.

(60) Ndio namna hivi. Na anayelipiza mfano wa alivyoadhibiwa, kisha akadhulumiwa, basi hapana shaka Mwenyezi Mungu atamsaidia. Hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwenye maghfira.

(61) Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu huingiza usiku katika mchana, na huuingiza mchana katika usiku, na ya kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia Mwenye kuona.

(62) Hayo ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye wa kweli, na kwamba wale wanaowaomba badala yake, ni batili, na hakika Mwenyezi Mungu ndiye aliye juu na ndiye mkubwa.

(63) Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huteremsha maji kutoka mbinguni, na mara ardhi inakuwa chanikiwiti? Hakika Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kujua.

(64) Ni vyake vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujitosha, Mwenye kusifiwa.

(65) Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu amevidhalilisha kwenu vilivyomo katika ardhi, na marikebu zipitazo baharini kwa amri yake, na amezishika mbingu zisianguke juu ya ardhi, ila kwa idhini yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye huruma kwa watu, Mwenye kurehemu.

(66) Na Yeye ndiye aliyewahuisha kisha atawafisha, na kisha atawafufua. Hakika mwanaadamu hana fadhila.

(67) Kila umma tumewajaalia na ibada zao wanazozishika. Basi wasizozane nawe katika jambo hili. Na waite watu kwendea kwa Mola wako Mlezi. Hakika wewe uko kwenye uwongofu ulionyooka.

(68) Na wakikujadili basi sema: Mwenyezi Mungu anajua zaidi mnayoyatenda.

(69) Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu Siku ya Kiyama katika hayo mnayokhitalifiana.

(70) Je, hujui kwamba Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo mbinguni na katika ardhi? Hakika hayo yamo Kitabuni. Hakika hayo kwa Mwenyezi Mungu ni mepesi.

(71) Na wanaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ambavyo hakuviteremshia ushahidi, na ambavyo hawana ujuzi navyo. Na madhalimu hawatakuwa na wa kuwasaidia.

(72) Na wanaposomewa Aya zetu zilizo wazi, utaona chuki katika nyuso za waliokufuru. Hukaribia kuwavamia wale wanaowasomea hizo Aya zetu. Sema: Je, nikwambieni yaliyo mabaya zaidi kuliko haya? Ni Moto. Mwenyezi Mungu amewaahidi waliokufuru, na ni marudio mabaya hayo.

(73) Enyi watu! Unapigwa mfano, basi usikilizeni. Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawawezi kuumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo. Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake. Amedhoofika kweli huyo mwenye kutaka na mwenye kutakiwa.

(74) Hawakumuadhimisha Mwenyezi Mungu anavyostahiki kuadhimishwa. Hakika Mwenyezi Mungu bila ya shaka ni Mwenye kushinda.

(75) Mwenyezi Mungu huteua Wajumbe miongoni mwa Malaika na miongoni mwa watu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

(76) Anayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Na kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote.

(77) Enyi mlioamini! Rukuuni na sujuduni, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe.

(78) Na fanyeni juhudi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kama inavyostahiki jihadi yake. Yeye amewateua. Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini. Nayo ni mila ya baba yenu Ibrahim. Yeye (Mwenyezi Mungu) aliwaita Waislamu tangu zamani, na katika hii (Qur'ani) pia, ili awe Mtume shahidi juu yenu, na nyinyi muwe mashahidi kwa watu. Basi shikeni Swala na toeni Zaka na shikamaneni na Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mlinzi wenu, na mlinzi bora kabisa, na msaidizi bora kabisa.