(1) Amri ya Mwenyezi Mungu itafika tu. Basi msiiharakishe. Ametakasika na ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo.
(2) Huwateremsha Malaika na ufunuo kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake kwamba onyeni kuwa hakuna mungu yeyote isipokuwa Mimi, basi nicheni Mimi.
(3) Ameziumba mbingu na dunia kwa Haki. Ametukuka na hayo wanayomshirikisha nayo.
(4) Amemuumba mtu kwa tone la manii. Na tazama, akawa mshindani aliye dhahiri.
(5) Na aliwaumbia wanyama. Katika hao mna vifaa vya kutia joto, na manufaa mengineyo, na baadhi yao mnawala.
(6) Na katika hao mnapata furaha pale mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka malishoni asubuhi.
(7) Nao hubeba mizigo yenu kupeleka kwenye miji msiyoweza kuifikia isipokuwa kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu Mlezi ni Mpole mno, Mwingi wa kurehemu.
(8) Na farasi, nyumbu, na punda ili muwapande, na wawe ni pambo. Na anaumba msivyovijua.
(9) Na ni juu ya Mwenyezi Mungu kuelekeza Njia. Na zipo njia za upotovu. Na angelipenda, angeliwaongoa nyote.
(10) Yeye ndiye anayewateremshia maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa, na miti ya kulishia.
(11) Kwa hayo Yeye anawaoteshea mimea, na mizaituni, na mitende, na mizabibu, na kila aina ya matunda. Hakika katika hayo ipo ishara kwa kaumu wanaotafakari.
(12) Na amewatiishia usiku na mchana, na jua na mwezi, na nyota zimetiishwa kwa amri yake. Hakika katika hayo zipo ishara kwa kaumu watumiao akili.
(13) Na vile alivyowaenezea katika ardhi vya rangi mbalimbali. Hakika katika hayo ipo ishara kwa kaumu wanaokumbuka.
(14) Yeye ndiye aliyeitiisha bahari, ili kutokana na humo mpate kula nyama laini, na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na utaona marikebu zikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake, na mpate kushukuru.
(15) Na akaweka katika ardhi milima madhubuti ili ardhi isiyumbe yumbe nanyi. Na mito, na njia mbalimbali ili mpate kuongoka.
(16) Na alama nyingine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.
(17) Ati yule anayeumba ni kama asiyeumba? Basi hebu hamkumbuki?
(18) Na mkizihesabu neema za Mwenyezi Mungu, hamwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye maghfira mno, Mwingi wa kurehemu.
(19) Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyaficha na mnayoyaweka hadharani.
(20) Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.
(21) Ni wafu, si wahai, na wala hawajui watafufuliwa lini.
(22) Mungu wenu ni Mungu Mmoja. Lakini wale wasioiamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wanatakabari.
(23) Hakuna shaka kuwa hakika Mwenyezi Mungu anayajua yale wanayoyaficha na wanayoyaweka hadharani. Hakika, Yeye hawapendi wanaotakabari.
(24) Na wanapoambiwa, "Ni nini alichoteremsha Mola wenu Mlezi?" Husema: Hadithi za kubuni za wa mwanzo!
(25) Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu Siku ya Qiyama, na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Angalia, ni mabaya mno hayo wanayoyabeba!
(26) Walipanga njama wale waliokuwa kabla yao, naye Mwenyezi Mungu akayasukua majengo yao kwenye misingi, kwa hivyo dari zake zikawaporomoka juu yao, na adhabu ikawajia kutokea wasipohisi.
(27) Kisha Siku ya Qiyama atawahizi na atasema: Wako wapi hao washirika wangu ambao kwao mlikuwa mkipinga (Manabii)? Watasema wale waliopewa elimu: Hakika leo ndiyo hizaya na ubaya vitawashukia makafiri.
(28) Wale ambao Malaika huwafisha huku wamejidhulumu nafsi zao! Basi wanasalimu amri, waseme: Hatukuwa tukifanya ubaya wowote. (Wataambiwa). Hasha! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkiyatenda.
(29) Basi ingieni milango ya Jahannamu, humo mdumu. Ni mabaya mno makazi ya wafanyao kiburi!
(30) Na wataambiwa wale waliomcha Mungu: Mola wenu Mlezi aliteremsha nini? Watasema: Heri. Kwa wale waliofanya mazuri katika dunia hii watapata mazuri. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi, na ni njema mno nyumba hiyo ya wachamungu.
(31) Bustani za milele wataziingia; iwe inapita kwa chini yake mito. Humo watapata watakacho. Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye kumcha.
(32) Wale ambao Malaika huwafisha katika hali nzuri, wanawaambia: Salama iwe juu yenu! Ingieni Peponi kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.
(33) Wanangojea jingine hawa isipokuwa Malaika wawafikie, au iwafikie amri ya Mola wako Mlezi? Kama hivyo, walitenda wale waliokuwa kabla yao. Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, lakini walijidhulumu wenyewe.
(34) Basi yakawafikia mabaya ya yale waliyoyatenda, na yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai yakawazunguka.
(35) Na washirikina walisema: Mwenyezi Mungu angelitaka, tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharimisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo, walifanya wale waliokuwa kabla yao. Basi lipo lolote juu ya Mitume isipokuwa kufikisha tu kwa wazi?
(36) Na hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani. Basi kati yao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao uliwathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wale wanaokadhibisha.
(37) Hata ukiwa na pupa juu ya kuongoka kwao, basi hakika Mwenyezi Mungu hamwongoi yule anayeshikilia kupotea. Wala hawatapata yeyote wa kuwanusuru.
(38) Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa viapo vyao kwamba Mwenyezi Mungu hatamfufua aliyekufa. Kwani! Ni ahadi iliyo juu yake kikweli; lakini wengi wa watu hawajui.
(39) Ili awabainishie yale waliyohitalifiana ndani yake, na ili wajue wale waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.
(40) Hakika, kauli yetu kwa kitu tunapokitaka kiwe, ni kukiambia tu: Kuwa! Basi kinakuwa.
(41) Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, bila ya shaka tutawaweka katika maskani mazuri katika dunia; na katika ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi; lau wangekuwa wanajua!
(42) Wale waliosubiri na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
(43) Nasi hatukuwatuma kabla yako isipokuwa watu wanaume tuliowapa Wahyi (Ufunuo). Basi waulizeni wenye ukumbusho kama nyinyi hamjui.
(44) Kwa Ishara wazi na Vitabu. Nasi tumekuteremshia wewe Ukumbusho ili uwabainishie watu yale yaliyoteremshwa kwao, ili wapate kutafakari.
(45) Je wana amani wale wanaopanga njama mbaya kwamba Mwenyezi Mungu hatawadidimiza katika ardhi, na haitawafikia adhabu kutoka wasipohisi?
(46) Au hatawashika katika harakati zao, na wala hawatamshinda?
(47) Au hatawashika huku wana hofu? Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenye huruma kubwa, Mwingi wa kurehemu.
(48) Je, hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu, vivuli vyao vinaelekea kushotoni na kuliani, kumsujudia Mwenyezi Mungu na vikinyenyekea?
(49) Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vyote vilivyomo katika mbingu na katika ardhi, miongoni mwa wanyama mpaka Malaika na wala havitakabari.
(50) Vinamhofu Mola wao Mlezi aliye juu yao, na vinafanya vinavyoamrishwa.
(51) Na Mwenyezi Mungu amesema: Msijifanyie miungu wawili! Hakika Yeye ndiye Mungu Mmoja tu. Basi niogopeni Mimi tu!
(52) Na ni vyake Yeye vilivyomo katika mbingu na ardhi. Na Dini ni yake Yeye daima. Je, mnamcha mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?
(53) Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kisha yakiwagusa madhara, mnamyayatikia Yeye.
(54) Na anapowaondoshea madhara hayo, mara kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao Mlezi.
(55) Wakizikataa neema tulizowapa. Basi stareheni. Mtakuja jua!
(56) Na hao ambao hata hawawajui wanawawekea sehemu katika vile tunavyowaruzuku. Tallahi! Bila ya shaka mtaulizwa kwa hayo mliyokuwa mnayazua!
(57) Na wanamfanyia Mwenyezi Mungu ati ana mabinti, Subhanahu (ametakasika)! Na wao wenyewe, ati ndiyo wawe na hayo wanayoyatamani!
(58) Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasalia umesawijika na akawa na huzuni mno.
(59) Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa yule aliyebashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama, ni ubaya mno wanavyohukumu!
(60) Wale wasioiamini Akhera wana mfano mbaya mno, naye Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye mfano bora zaidi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(61) Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeliwaadhibu watu kwa mujibu wa dhuluma zao, basi asingelimwacha juu yake hata mnyama mmoja. Lakini anawaahirisha mpaka muda uliowekwa. Na unapofika muda wao, hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.
(62) Na wanampa Mwenyezi Mungu wanavyovichukia wao, na ndimi zao zinasema uongo kwamba wao watapata mazuri zaidi. Hakuna shaka kwamba hakika wana Moto, na kwamba kwa yakini wataachwa humo.
(63) Tallahi! Hakika tuliwatuma Mitume kwa umma zilizokuwa kabla yako, lakini Shetani akawapambia matendo yao. Kwa hivyo leo, yeye ndiye kipenzi chao msaidizi, nao wana adhabu chungu.
(64) Na hatukukuteremshia Kitabu hiki isipokuwa ili uwabainishie yale ambayo wanahitalifiana ndani yake, na kiwe Uwongofu na Rehema kwa kaumu wanaoamini.
(65) Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwa hayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Kwa hakika, katika hayo imo Ishara kwa kaumu wanaosikia.
(66) Na hakika katika nyama hoa, mna mazingatio. Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni mwao, vikatoka baina ya mavi na damu, maziwa safi, mazuri kwa wanywao.
(67) Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza ulevi na riziki nzuri. Hakika katika hayo ipo Ishara kwa kaumu watumiao akili.
(68) Na Mola wako Mlezi alimfunulia nyuki kwamba: Jitengenezee majumba yako katika milima, na katika miti, na katika vile wanavyojenga watu.
(69) Kisha kula katika kila matunda, na upite katika njia za Mola wako Mlezi zilizofanywa nyepesi kuzipita. Na kutoka matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbalimbali; ndani yake kuna ponya kwa watu. Hakika katika haya ipo Ishara kwa kaumu wanaotafakari.
(70) Na Mwenyezi Mungu aliwaumba; kisha atawafisha. Na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri mbaya kabisa, hata akawa hajui kitu baada ya kuwa alikuwa anajua. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujua zaidi, Muweza.
(71) Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki. Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale iliowamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo. Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
(72) Na Mwenyezi Mungu amewaumbia wake kutokana na nyinyi wenyewe, na akawajaalia kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu, na akawaruzuku vitu vizuri. Basi je, wanaamini upotovu na wanazikufuru neema za Mwenyezi Mungu?
(73) Na badala ya Mwenyezi Mungu wanawaabudu wasiowamilikia riziki kutoka mbinguni wala kwenye ardhi, wala hawawezi kitu.
(74) Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua, na nyinyi hamjui.
(75) Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtumwa aliyemilikiwa, asiyeweza kitu, na mwingine tuliyemruzuku riziki njema inayotoka kwetu, naye akawa anatoa katika riziki hiyo kwa siri na dhahiri. Je, hao watakuwa sawa? Alhamdu Lillahi (Kuhimidiwa kote ni kwa Mwenyezi Mungu)! Lakini wengi wao hawajui.
(76) Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa wanaume wawili. Mmoja wao ni bubu, hawezi chochote, naye ni mzigo kwa mlezi wake. Popote anapomuelekeza, haleti heri yoyote. Je, huyo anaweza kuwa sawa na yule anayeamrisha uadilifu, naye yuko kwenye njia iliyonyooka?
(77) Na siri zote za katika mbingu na ardhi ni za Mwenyezi Mungu. Wala halikuwa jambo la Saa (ya Qiyama) isipokuwa kama kupepesa kwa jicho, au chini zaidi ya hivyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(78) Na Mwenyezi Mungu aliwatoa matumboni mwa mama zenu hali ya kuwa hamjui kitu, na akawajaalia masikio na macho na nyoyo ili mpate kushukuru.
(79) Je, hawawaoni ndege walivyotiishwa katika anga la mbingu? Hakuna mwenye kuwashika isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika katika haya zipo ishara kwa kaumu wanaoamini.
(80) Na Mwenyezi Mungu amewajaalia majumba yenu yawe ni maskani yenu, na amewajaalia ni kutokana na ngozi za wanyama, nyumba mnazoziona nyepesi wakati wa safari zenu na wakati wa kutua kwenu. Na kutokana na sufi zao, na manyoya yao, na nywele zao, mnafanya vyombo na mapambo ya kutumia kwa muda.
(81) Na Mwenyezi Mungu amewafanyia vivuli katika vitu alivyoviumba, na amewafanyia maskani milimani, na amewafanyia nguo za kuwakinga kutokana na joto, na nguo za kuwakinga katika vita vyenu. Ndivyo hivyo anawatimizia neema zake ili mpate kujisalimisha kwake.
(82) Kwa hivyo, wakikengeuka, basi lililo juu yako wewe ni kufikisha ujumbe wazi wazi tu.
(83) Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu, kisha wanazikanusha, na wengi wao ni makafiri.
(84) Na siku tutakapomtoa shahidi kutoka katika kila umma, kisha hawataruhusiwa wale waliokufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi.
(85) Na wale waliodhulumu watakapoiona adhabu, hawatapunguziwa adhabu hiyo, wala hawatapewa muhula.
(86) Na wale walioshirikisha watakapowaona hao waliowashirikisha na Mwenyezi Mungu, watasema: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaomba badala yako. Lakini hao watawatupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo!
(87) Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu, na yatapotea yale waliyokuwa wakiyazua.
(88) Wale waliokufuru na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu, tutawazidishia adhabu juu ya adhabu, kwa walivyokuwa wakifanya uharibifu.
(89) Na (waonye) siku tutakapomtoa shahidi katika kila umma kutokana na wao wenyewe, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hawa. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinachobainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu.
(90) Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa, na anakataza uchafu, na uovu, na dhuluma. Anawaaidhi ili mpate kukumbuka.
(91) Na timizeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapoahidi, wala msivunje viapo baada ya kuvifunga imara, ilihali mmekwisha mfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayajua myafanyayo.
(92) Wala msiwe kama mwanamke yule aliyeuzongoa uzi wake baada ya kwishausokota ukawa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa ati umma mmoja una nguvu zaidi kuliko mwingine? Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwa njia hiyo. Na bila ya shaka atawabainishia Siku ya Qiyama yale mliyokuwa mkihitalifiana ndani yake.
(93) Na Mwenyezi Mungu angelitaka, kwa yakini angeliwafanya kuwa umma mmoja. Lakini anampoteza amtakaye, na anamwongoa amtakaye. Na hakika mtaulizwa juu ya yale mliyokuwa mkiyatenda.
(94) Wala msifanye viapo vyenu kuwa njia ya kudanganyana baina yenu, mguu ukaja teleza baada ya kuwa thabiti, na mkaonja mabaya kwa sababu ya kule kuzuilia kwenu Njia ya Mwenyezi Mungu, na mkapata adhabu kubwa.
(95) Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndicho bora kwenu, ikiwa mnajua.
(96) Mlivyo navyo vitakwisha, na vilivyo kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobakia. Na kwa yakini Sisi tutawapa wale waliosubiri ujira wao kwa bora zaidi ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
(97) Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni Muumini, hakika tutamhuisha uhai mwema, na hakika tutawapa ujira wao kwa bora zaidi ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
(98) Na unaposoma Qur-ani, mwombe Mwenyezi Mungu akulinde kutokana na Shetani aliyelaaniwa.
(99) Hakika yeye hana mamlaka juu ya wale walioamini na wakamtegemea Mola wao Mlezi.
(100) Hakika mamlaka yake yako juu ya wale wanaomfanya kuwa rafiki yao msaidizi, na wale wanaofanya ushirika naye.
(101) Na tunapobadilisha Ishara pahala pa Ishara, na Mwenyezi Mungu anayajua anayoyateremsha, wanasema: Wewe si chochote ila ni mzushi tu, lakini wengi wao hawajui tu.
(102) Sema: Ameiteremsha Roho mtakatifu kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa haki, ili awaimarishe wale walioamini, na kuwa ni uwongofu, na bishara kwa Waislamu.
(103) Na Sisi hakika tunajua kwamba wanasema: Yuko mtu anayemfundisha. Lugha ya huyo wanayemuelekezea ni ya kigeni, na hii ni lugha ya Kiarabu iliyo bainifu.
(104) Hakika wale wasioziamini Ishara za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao wana adhabu chungu.
(105) Hakika wanazua uongo tu wale wasioziamini Ishara za Mwenyezi Mungu. Na hao ndio waongo.
(106) Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya kuamini kwake - isipokuwa yule aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya Imani, lakini yule aliyekifungulia kifua chake ukafiri - basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ipo juu yao, na wao wana adhabu kubwa.
(107) Hayo ni kwa sababu wameupendelea uhai wa dunia hii kuliko Akhera, na kwa sababu Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu makafiri.
(108) Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu ameziziba nyoyo zao na masikio yao na macho yao. Na hao ndio walioghafilika.
(109) Hakuna shaka ya kwamba hao ndio waliohasirika.
(110) Kisha hakika Mola wako Mlezi, kwa wale waliohama makwao baada ya kuteswa, kisha wakapigania Dini na wakasubiri, bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.
(111) Siku ambayo kila nafsi itakuja ikijitetea, na kila nafsi italipwa kikamilifu yale iliyotenda, nao hawatadhulumiwa.
(112) Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa wingi kutokea kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hivyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
(113) Na alikwisha wajia Mjumbe kutoka miongoni mwao. Lakini wakamkadhibisha; basi ikawachukua adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.
(114) Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu, vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema za Mwenyezi Mungu, ikiwa kweli mnamuabudu Yeye tu.
(115) Hakika amewaharimishia tu nyamafu, na damu, na nyama ya nguruwe, na mnyama aliyechinjwa kwa ajili isiyokuwa ya Mwenyezi Mungu. Lakini anayelazimishwa bila ya kuasi, wala kuvuka mipaka, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.
(116) Wala msiseme uongo, kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali, na hiki ni haramu - mkimzulia uongo Mwenyezi Mungu. Hakika wale wanaomzulia uongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu.
(117) Ni starehe ndogo tu, nao wana adhabu chungu.
(118) Na Mayahudi tuliwaharimishia yale tuliyokuhadithia zamani. Na Sisi hatukuwadhulumu, bali walikuwa wakijudhulumu wenyewe.
(119) Kisha hakika Mola wako Mlezi kwa wale waliotenda mabaya kwa ujinga, kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mazuri; bila ya shaka Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwingi wa kusamehe, Mwingi wa kurehemu.
(120) Hakika Ibrahim alikuwa mfano mwema, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mnyoofu kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
(121) Mwenye kuzishukuru neema zake. Yeye alimteua, na akamwongoa kwenye Njia iliyonyooka.
(122) Na tukampa mazuri katika dunia, naye hakika Akhera atakuwa miongoni mwa walio wema.
(123) Kisha tukakufunulia ya kwamba ufuate mila ya Ibrahim, mnyoofu kwa Mwenyezi Mungu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.
(124) Hakika siku ya Sabato (Jumamosi) waliwekewa wale waliohitalifiana kuhusiana nayo. Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka atahukumu baina yao Siku ya Qiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana.
(125) Lingania kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hekima na mawaidha mazuri, na ujadiliane nao kwa namna iliyo nzuri zaidi. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anayemjua zaidi yule aliyeipotea Njia yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi wale walioongoka.
(126) Na mkilipiza, basi lipizeni sawa na vile mlivyoadhibiwa. Na ikiwa mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri.
(127) Na subiri. Na kusubiri kwako kusiwe isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Wala usiwahuzunikie, wala usiwe katika dhiki kwa njama wanazozifanya.
(128) Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kumcha, na wale watendao mazuri.