11 - Surat Hud ()

|

(1) Alif Lam Ra. Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimefanywa kuwa sawa sawa, kisha zikapambanuliwa kwa kina, kilichotoka kwa Mwenye Hekima, Mwenye habari zote.

(2) Ili msimuabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi kwenu ni mwonyaji na mbashiri nitokaye kwake.

(3) Na ili mumwombe msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atawastarehesha starehe nzuri mpaka muda maalumu. Na atampa kila mwenye fadhila, fadhila yake. Na wakikengeuka, basi mimi ninawahofia adhabu ya hiyo Siku Kubwa.

(4) Marejeo yenu ni kwa Mwenyezi Mungu tu. Naye ni Muweza wa kila kitu.

(5) Hebu angalia! Ati wanafunika vilivyomo vifuani mwao ili wamfiche Mwenyezi Mungu! Jueni kuwa wanapojigubika nguo zao, Yeye anajua yale wanayoyaficha na yale wanayoyaweka hadharani. Hakika Yeye ni Mwenye kujua zaidi yaliyomo vifuani.

(6) Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi isipokuwa riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Naye anajua makao yake na mapitio yake. Yote hayo yamo katika Kitabu chenye kubainisha.

(7) Na Yeye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Na Kiti chake cha Enzi kilikuwa juu ya maji, ili awajaribu ni nani kati yenu ndiye mzuri zaidi wa matendo. Na wewe ukisema, "Hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa." Hakika wale waliokufuru watasema, "Haya si isipokuwa uchawi ulio wazi."

(8) Na hata tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliokwisha hisabiwa, wao hakika watasema, "Ni nini kinachoizuia?" Jueni! Siku itakapowajia, basi haitaondolewa kwao. Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

(9) Na tukimwonjesha mtu rehema kutoka kwetu, kisha tukaiondoa kwake, yeye hakika ni mwenye kukata tamaa, mwingi wa kufuru.

(10) Na tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyomgusa, hakika yeye husema, "Mabaya yamekwisha niondokea." Hakika yeye ni mwenye kufurahi, mwenye kujifahiri mno.

(11) Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema. Hao wana maghufira na malipo makubwa.

(12) Basi labda utaacha baadhi ya yale yaliyofunuliwa kwako, na kifua chako kikaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, "Mbona hakuteremshiwa hazina, au Malaika akaja pamoja naye?" Hakika, wewe ni mwonyaji tu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mtegemewa kwa kila kitu.

(13) Au wanasema, "Ameizua?" Sema, "Basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wake, na waiteni muwawezao isipokuwa Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi ni wakweli."

(14) Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba (hii Qur-ani) imeteremshwa kwa elimu ya Mwenyezi Mungu, na kwamba hakuna mungu isipokuwa Yeye. Basi je, nyinyi ni Waislamu?

(15) Yule ambaye anataka uhai wa dunia na mapambo yake, tutawalipa humo matendo yao kamili. Na wao humo hawatapunjwa.

(16) Hao ndio ambao hawana kitu katika Akhera isipokuwa Moto, na yataharibika yale waliyoyafanya humo, na yatabatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.

(17) Basi je, yule ambaye ana ushahidi ulio wazi kutoka kwa Mola wake Mlezi, na unaofuatwa na shahidi anayetoka kwake, na kabla yake kilikuwapo Kitabu cha Musa kilichokuwa mwongozi na rehema. Hao wanaiamini. Naye anayeikufuru katika makundi, basi Moto ndipo pahali pa miadi yake. Kwa hivyo, usiwe katika shaka juu yake. Hakika, hii ni haki itokayo kwa Mola wako Mlezi, lakini wengi wa watu hawaamini.

(18) Na ni nani aliye dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo? Hao wataletwa mbele ya Mola wao Mlezi, na mashahidi watasema, "Hawa ndio waliomdanganyishia Mola wao Mlezi. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iwapate madhalimu."

(19) Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu, na wanaitakia ijipinde, nao wanakufuru Akhera.

(20) Hao hawakuwa ni wa kushinda katika ardhi, wala hawana walinzi wowote kando na Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu. Kwa kuwa, hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.

(21) Hao ndio waliozihasiri nafsi zao, na yakawapotea yale waliyokuwa wakiyazua.

(22) Hakuna shaka kwamba wao katika Akhera ndio waliohasiri zaidi.

(23) Hakika, wale walioamini, na wakatenda mema, na wakanyenyekea kwa Mola wao Mlezi, hao ndio wenza wa Pepo, humo watadumu.

(24) Mfano wa makundi mawili haya ni kama kipofu na kiziwi, na mwenye kuona na anayesikia. Je, wawili hawa wanakuwa sawa kwa kufananishwa? Basi, je, hamkumbuki?

(25) Na hakika, tulimtuma Nuhu kwa kaumu yake, akawaambia, "Hakika mimi ni mwonyaji aliye wazi kwenu."

(26) Ya kwamba msimuabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu tu. Hakika mimi ninawahofia adhabu ya Siku Chungu.

(27) Basi wakasema wakuu waliokufuru katika kaumu yake, "Hatukuoni wewe isipokuwa ni mtu tu mfano wetu, wala hatukuoni wamekufuata isipokuwa wale wetu walio duni, watu wasiokuwa na maoni. Wala hatuwaoni nyinyi kuwa mna ubora wowote kutushinda sisi. Bali tunawadhania nyinyi kuwa ni waongo."

(28) Akasema, "Enyi kaumu yangu! Hebu fikirini! Ikiwa mimi ninayo hoja wazi iliyotoka kwa Mola wangu Mlezi, na amenipa rehema kutoka kwake, nayo ikafichwa kwenu. Je, tuwalazimishe kuikubali ilhali nyinyi mnaichukia?"

(29) "Na enyi kaumu yangu! Mimi siwaombi mali kwa ajili ya haya. Mimi sina ujira isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu; na mimi sitawafukuza walioamini. Hakika wao watakutana na Mola wao Mlezi, lakini mimi nawaona mnafanya ujinga.

(30) Na enyi kaumu yangu! Ni nani atakayeninusuru kwa Mwenyezi Mungu nikiwafukuza hawa? Basi je, hamkumbuki?

(31) Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu, wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu, wala sisemi: Mimi ni Malaika. Wala sisemi kuhusu wale ambao yanawadharau macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa heri. Mwenyezi Mungu ndiye anayajua zaidi yaliyo katika nafsi zao. Hapo bila ya shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.

(32) Wakasema, "Ewe Nuhu! Umejadiliana nasi, na umekithirisha kutujadili. Basi tuletee hayo unayotuahidi, ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli."

(33) Akasema, "Hakika Mwenyezi Mungu tu ndiye atakayewaletea akipenda. Wala nyinyi si wenye kumshinda."

(34) "Wala nasaha yangu haitawafaa kitu nikitaka kuwanasihi, ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapoteza. Yeye ndiye Mola wenu Mlezi, na kwake mtarejeshwa."

(35) Au ndio wanasema, "Ameizua?" Sema, "Ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi niko mbali sana na makosa myatendayo."

(36) Na akafunuliwa Nuhu akaambiwa, "Hataamini yeyote katika kaumu yako isipokuwa wale waliokwisha amini. Basi usisikitike kwa yale waliyokuwa wakiyatenda."

(37) "Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa mujibu wa ufunuo wetu. Wala usiniongeleshe kuwatetea wale waliodhulumu. Kwani hao bila ya shaka watazamishwa."

(38) Na akawa anaunda jahazi, na kila walipopita karibu nayo wakuu kutoka kwa kaumu yake, wanamkejeli. Yeye akasema, "Ikiwa nyinyi mnatukejeli, basi sisi pia tunawakejeli kama mnavyotukejeli."

(39) "Nanyi mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na itakayemteremkia adhabu ya kudumu."

(40) Mpaka ilipokuja amri yetu, na tanuri ikafoka maji, tulisema, "Pakia humo katika kila kitu, jozi mbili ya dume na jike, na ahali zako, isipokuwa wale ambao imekwisha wapitia hukumu, na watu walioamini." Na hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache tu.

(41) Na akasema, "Pandeni humo kwa Bismillahi (Kwa Jina la Mwenyezi Mungu), kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu."

(42) Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuhu akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi, wala usiwe pamoja na makafiri.

(43) Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. (Nuhu) akasema: Leo hakuna wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu isipokuwa yule aliyemrehemu mwenyewe. Na wimbi likawatenganisha, basi akawa katika waliozama.

(44) Na ikasemwa: Ewe ardhi! Meza maji yako. Na Ewe mbingu! Jizuie. Basi maji yakadidimia chini, na amri hiyo ikapitishwa, na (jahazi) likasimama juu ya (mlima) wa Al Juudiy. Na ikasemwa: Wapotelee mbali kaumu madhalimu!

(45) Na Nuhu alimwomba Mola wake Mlezi: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika mwanangu ni katika ahali zangu, na hakika ahadi yako ndiyo ya haki. Na Wewe ndiye hakimu bora zaidi ya mahakimu wote.

(46) Akasema: Ewe Nuhu! Huyu si katika ahali zako. Hakika yeye mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usilo na elimu nalo. Mimi nakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga.

(47) Nuhu akasema: Ewe Mola wangu Mlezi! Mimi najikinga kwako nikuombe nisilo na elimu nalo. Na kama hunisamehe na ukanirehemu, nitakuwa katika waliohasiri.

(48) Ikasemwa: Ewe Nuhu! Shuka kwa salama itokayo kwetu, na baraka nyingi juu yako na juu ya umma miongoni mwa wale walio pamoja nawe. Na zitakuwapo umma tutakazozistarehesha, na kisha zitaguswa na adhabu chungu itokayo kwetu.

(49) Hizi ni katika habari za ghaibu tunazokufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala kaumu yako, kabla ya haya. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamungu.

(50) Na kwa kina 'Aadi tulimtuma ndugu yao Hud. Akasema, "Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu! Hamna mungu isipokuwa Yeye tu. Nyinyi si chochote isipokuwa ni wazushi tu."

(51) "Enyi watu wangu! Siwaombi ujira kwa ajili ya haya. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Yule aliyeniumba. Basi hamtumii akili?"

(52) "Na enyi kaumu yangu! Mwombeni msamaha Mola wenu Mlezi, kisha mtubie kwake. Atawatumia mbingu zenye kunyesha mvua ya kumiminika, na atawazidishia nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke mkawa wahalifu."

(53) Wakasema, "Ewe Hud! Hujatuletea ushahidi ulio wazi. Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kufuata kauli yako. Na wala sisi hatukuamini wewe."

(54) "Sisi tunasema: 'Baadhi ya miungu yetu imekusibu kwa baa.' Akasema, "Hakika, mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu, na nyinyi shuhudieni, ya kwamba mimi niko mbali na hao mnaowafanya washirika."

(55) "Badala ya Yeye. Basi nyinyi nyote nipangieni njama, na kisha msinipe muhula!"

(56) "Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Hakuna kiumbe yeyote isipokuwa Yeye anamwendesha atakavyo. Hakika Mola wangu Mlezi yuko kwenye njia iliyonyooka."

(57) Na wakikengeuka, "basi hakika mimi nimekwisha wafikishia yale niliyotumwa nayo kwenu. Na Mola wangu Mlezi atawaleta watu wengine badala yenu, wala nyinyi hamumdhuru kitu Yeye. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuhifadhi kila kitu."

(58) Na ilipofika amri yetu, tulimwokoa Hud na wale walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na tukawaokoa na adhabu kali.

(59) Na hao ndio kina 'Aadi. Walizikufuru Ishara za Mola wao Mlezi, na wakawaasi Mitume wake, na wakafuata amri ya kila jabari mkaidi.

(60) Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na Siku ya Qiyama. Basi tambueni mtanabahi kuwa hakika kina 'Aadi walimkufuru Mola wao Mlezi. Na tambueni mtanabahi kuwa hakika waliangamizwa kina 'Aadi, kaumu ya Hud.

(61) Na kina Thamud tuliwatumia ndugu yao Saleh. Akasema: Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu yeyote isipokuwa Yeye. Yeye ndiye aliyewaumba kutoka katika ardhi, na akawaweka humo imara. Basi mwombeni msamaha, kisha mtubu kwake. Hakika Mola wangu Mlezi yupo karibu, anaitikia maombi.

(62) Wakasema: Ewe Saleh! Hakika kabla ya haya ulikuwa unatarajiwa heri kwetu. Je, unatukataza kuwaabudu wale ambao baba zetu walikuwa wakiwaabudu? Na hakika sisi tuna shaka na wasiwasi kwa hayo unayotuitia.

(63) Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwaonaje ikiwa ninao ushahidi ulio wazi kutoka kwa Mola wangu Mlezi, naye akawa amenipa rehema kutoka kwake, je, ni nani atakayeninusuru kutokana na Mwenyezi Mungu nikimuasi? Basi nyinyi hamnizidishii isipokuwa kuhasirika tu.

(64) Na enyi kaumu yangu! Huyu ni ngamia wa Mwenyezi Mungu kama Ishara kwenu. Basi mwacheni ale katika ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimguse kwa ubaya, ikaja kuwaangamiza adhabu iliyo karibu.

(65) Lakini wakamchinja. Basi (Saleh) akasema: Stareheni katika makazi yenu muda wa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokuwa ya uongo.

(66) Basi ilipokuja amri yetu, tulimwokoa sawasawa Saleh na wale walioamini pamoja naye kwa rehema yetu kutokana na hizaya ya siku ile. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mtukufu.

(67) Na ukelele uliwaangamiza wale waliodhulumu, basi wakaishia majumbani mwao wamekufa kifudifudi!

(68) Kama kwamba hawakuishi kwa ustawi huko. Hebu zingatieni! Hakika kina Thamud walimkufuru Mola wao Mlezi. Hebu zingatieni! Thamud walipotelea mbali!

(69) Na hakika wajumbe wetu walimjia Ibrahim kwa bishara njema, wakasema, "Salama!" Naye akasema, "Salama!" Kisha hakukaa isipokuwa mara hiyo akaja na ndama wa kuchoma.

(70) Basi alipoiona mikono yao haimfikii, akawatilia shaka, na akawahofu. Wakasema, "Usihofu! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut."

(71) Na mkewe alikuwa amesimama wima, akacheka. Basi tukambashiria kuhusu (kuzaliwa kwa) Is-haq, na baada ya Is-haq Yaaqub.

(72) Akasema, "Ole wangu! Mimi nizae ilhali mimi ni ajuza? Na tena huyu mume wangu ni mzee? Hakika haya ni mambo ya ajabu!"

(73) Wakasema: Je, unastaajabia amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake ziwe juu yenu, enyi watu wa nyumba hii! Hakika Yeye ndiye Msifika, Mtukufu.

(74) Basi hofu ilipomwondoka Ibrahim, na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya kaumu ya Lut.

(75) Hakika Ibrahim alikuwa mvumilivu sana, mwenye huzuni kubwa, na mwepesi wa kurejea kwa Mwenyezi Mungu.

(76) (Akaambiwa): Ewe Ibrahim! Achilia mbali haya! Hakika amri ya Mola wako Mlezi imekwisha kuja, na hakika hao itawafikia adhabu isiyorudishwa nyuma.

(77) Na wajumbe wetu walipomjia Lut, yakamuwia mabaya kwa sababu yao na akaona dhiki kubwa kwa sababu yao. Akasema: Hii si ni siku ngumu sana!

(78) Wakamjia kaumu yake mbio mbio. Na kabla ya haya walikuwa wakitenda mabaya. Yeye akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu, ndio wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi mbele ya wageni wangu. Hivyo je, hakuna hata mtu mmoja miongoni mwenu aliyeongoka?

(79) Wakasema: Bila shaka umekwisha jua hatuna haki yoyote juu ya binti zako, na hakika wewe unayajua yale tunayoyataka.

(80) Akasema: Laiti ningelikuwa na nguvu kwenu, au nijilinde kwenye nguzo yenye nguvu!

(81) (Wajumbe) wakasema: Ewe Lut! Sisi ni wajumbe wa Mola wako Mlezi. Hawa hawatakufikia. basi wewe ondoka pamoja na ahali zako usiku ungalipo. Wala yeyote miongoni mwenu asitazame nyuma, isipokuwa mkeo, kwani yeye utamfika msiba utakaowafika hao. Hakika miadi yao ni asubuhi. Je, asubuhi si karibu?

(82) Basi ilipokuja amri yetu, tuliigeuza nchi juu chini, na tukaiteremshia mvua ya changarawe za udongo mgumu uliokamatana wa Motoni.

(83) Zilizotiwa alama kwa Mola wako Mlezi. Na haya hayako mbali na madhalimu wengineo.

(84) Na kwa watu wa Madyana tuliwatumia ndugu yao Shua'ib. Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu yoyote isipokuwa Yeye, wala msipunguze vipimo na mizani. Mimi ninawaona mmo katika hali njema, nami ninawahofia adhabu ya Siku kubwa hiyo itakayowazunguka.

(85) Na enyi kaumu yangu! Timizeni vipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msienee katika ardhi mkifanya uharibifu.

(86) Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ndiyo bora kwenu, ikiwa nyinyi ni Waumini. Wala mimi siye mlinzi wenu.

(87) Wakasema: Ewe Shua'ibu! Je, ni sala zako ndizo zinazokuamrisha tuyaache yale waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu, au tuache kufanya tupendavyo katika mali zetu? Ama hakika wewe ni mstahamilivu kweli na mwongofu mno!

(88) Akasema: Enyi kaumu yangu! Mwaonaje ikiwa ninao ushahidi ulio wazi kutoka kwa Mola wangu Mlezi, na ikawa Yeye ameniruzuku riziki njema kutoka kwake? Wala mimi sitaki kuwahalifu nikafanya yale ninayowakataza. Sitaki isipokuwa kutengeneza kiasi ninavyoweza. Na sipati kuwezeshwa haya isipokuwa na Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye ninategemea, na kwake Yeye ninarudi.

(89) Na enyi kaumu yangu! Kuhalifiana nami kusiwapelekee hata mkasibiwa na mfano wa yale waliyosibiwa kaumu ya Nuhu, au kaumu ya Hud, au kaumu ya Saleh. Na kaumu ya Lut si mbali nanyi.

(90) Na ombeni msamaha kwa Mola wenu Mlezi, tena tubuni kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kurehemu sana, Mwenye upendo mkubwa.

(91) Wakasema: Ewe Shu'aibu! Mengi katika hayo unayoyasema hatuyafahamu. Na sisi tunakuona dhaifu miongoni mwetu. Na lau kuwa si jamaa zako, tungekupiga mawe, wala wewe si mtukufu kwetu.

(92) Akasema: Enyi kaumu yangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemueka nyuma ya migongo yenu! Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kuyazunguka yote mnayoyatenda.

(93) Na enyi kaumu yangu! Fanyeni katika mahali penu, na mimi pia ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumhizi, na ni nani mwongo. Na ngojeni, mimi pia ninangoja pamoja nanyi.

(94) Na amri yetu ilipokuja, tulimwokoa sawasawa Shu'aibu na wale walioamini pamoja naye kwa rehema kutoka kwetu. Na ukelele uliwanyakua wale waliodhulumu, na wakaishia wamekufa kifudifudi katika majumba yao!

(95) Kama kwamba hawakuishi kwa ustawi humo. Zingatia ilivyoangamia Madyana, kama ilivyoangamia Thamud!

(96) Na hakika tulimtuma Musa pamoja na Ishara zetu na uthibitisho ulio wazi.

(97) Kwa Firauni na waheshimiwa wake. Lakini wao wakafuata amri ya Firauni, na amri ya Firauni haikuwa yenye uwongofu.

(98) Siku ya Qiyama atawatangulia kaumu yake na atawaingiza Motoni. Na muingio mbaya zaidi ulioje huo unaoingiwa!

(99) Nao walifuatishwa laana hapa (duniani) na Siku ya Qiyama. Ni kipawa kibaya zaidi kilichoje walichopewa!

(100) Hizi ni katika habari za miji, tunakusimulia. Mingine ipo bado na mingine ilifyekwa.

(101) Na Sisi hatukuwadhulumu, lakini wao wenyewe walizidhulumu nafsi zao. Na miungu yao waliyokuwa wakiiomba badala ya Mwenyezi Mungu haikuwafaa kitu ilipokuja amri ya Mola wako Mlezi. Na hiyo miungu haikuwazidishia isipokuwa maangamio tu.

(102) Na hivyo ndivyo ulivyo mshiko wa Mola wako Mlezi anapoishika miji inapokuwa imedhulumu. Hakika mshiko wake ni mchungu na mkali.

(103) Hakika katika hayo ipo ishara kwa yule anayehofu adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo Siku itakayokusanyiwa watu, na hiyo ndiyo Siku itakayoshuhudiwa

(104) Na wala hatuiahirishi isipokuwa kwa muda unaohisabiwa.

(105) Siku hiyo itakapokuja, nafsi yoyote haizungumza isipokuwa kwa idhini yake. Basi miongoni mwao watakuwamo waliomo mashakani na wenye furaha.

(106) Ama wale wale walijitia mashakani, hao watakuwa Motoni, humo watavuta pumzi na kuitoa kwa ugumu mkubwa.

(107) Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa atakavyo Mola wako Mlezi. Hakika Mola wako Mlezi hutenda atakavyo.

(108) Na ama wale waliofurahishwa, wao watakuwa katika Pepo wakidumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa atakavyo Mola wako Mlezi. Hicho ni kipawa kisicho na kikomo.

(109) Basi usiwe katika shaka juu ya yale wanayoyaabudu hawa. Hawaabudu isipokuwa kama walivyoabudu baba zao zamani. Na hakika Sisi tutawatimilizia fungu lao bila ya kupunguzwa.

(110) Na hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini kukazuka kuhitilafiana ndani yake. Na lau kuwa si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka juu yake inayowahangaisha.

(111) Na hakika Mola wako Mlezi atawatimilizia malipo ya matendo yao wote. Hakika Yeye anayo habari ya wayatendayo.

(112) Basi, nyooka kama ulivyoamrishwa, wewe na wale wanaotubia kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe, wala msivuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo.

(113) Wala msiwategemee wale waliodhulumu, mkaja kuguswa na Moto. Wala nyinyi hamna walinzi wowote kando na Mwenyezi Mungu, wala tena hamtanusuriwa.

(114) Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mazuri huondoa mabaya. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.

(115) Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wafanyao mazuri.

(116) Basi mbona hawakuwamo katika vizazi vya kabla yenu wenye vyeo na wasaa wanaokataza uharibifu katika nchi, isipokuwa wachache tu, miongoni mwa wale tuliowaokoa miongoni mwao? Na wale waliodhulumu walifuata yale waliyostareheshwa kwayo, na walikuwa wahalifu.

(117) Wala hakuwa Mola wako Mlezi wa kuiangamiza miji kwa dhuluma tu ilhali watu wake ni watenda mema.

(118) Na Mola wako Mlezi angelitaka, angewafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kuhitalifiana.

(119) Isipokuwa wale ambao Mola wako Mlezi amewarehemu. Na kwa hiyo ndiyo Mwenyezi Mungu amewaumba. Na lilitimia neno la Mola wako Mlezi kwamba hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.

(120) Na yote tunayokusimulia katika habari za Mitume yale tunayokuimarisha kwayo moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini.

(121) Na waambie wale wasioamini, "Fanyieni mahali penu, nasi hakika pia tunafanya."

(122) Na ngojeni, na sisi hakika tunangoja.

(123) Na ni ya Mwenyezi Mungu tu ghaibu ya mbinguni na ardhi, na mambo yote yatarejeshwa kwake. Basi muabudu Yeye na umtegemee Yeye. Na Mola wako Mlezi haghafiliki na yale mnayoyatenda.