(1) Tw'aa Siin Miim.
(2) Hizi ni Aya za Kitabu kinachobainisha.
(3) Huenda ukaihiliki nafsi yako kwa kuwa hawawi Waumini.
(4) Tungependa, tungeliwateremshia kutoka mbinguni Ishara zikashinda zimezinyenyekea shingo zao.
(5) Wala hauwafikii ukumbusho mpya kutoka kwa Arrahman (Mwingi wa rehema), isipokuwa wao huupa mgongo.
(6) Kwa yakini wamekwisha kanusha; kwa hivyo zitakuja wafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.
(7) Je, hawakuiona ardhi, ni mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri?
(8) Hakika katika haya zipo Ishara. Lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
(9) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(10) Na Mola wako Mlezi, alipomwita Musa, akamwambia: Nenda kwa kaumu madhalimu.
(11) Kaumu wa Firauni. Kwani hawamchi Mwenyezi Mungu?
(12) Akasema: Mola wangu Mlezi, hakika mimi ninachelea kwamba watanikadhibisha.
(13) Na kifua changu kina dhiki, na ulimi wangu haukunjuki vyema. Basi mtumie ujumbe Harun.
(14) Na wao wana dhambi niliyowafanyia, kwa hivyo ninahofu wanaweza kuniua.
(15) Akasema: Sivyo hivyo kabisa! Nendeni na miujiza yetu. Hakika Sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.
(16) Basi nendeni kwa Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni Mitume wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(17) Kwamba: Waachilie Wana wa Israili waende pamoja nasi.
(18) (Firauni) akasema: Je, sisi hatukukulea wewe utotoni, na ukakaa miongoni mwetu katika umri wako miaka mingi?
(19) Na ukatenda kitendo chako ulichotenda, nawe ukawa miongoni mwa wenye kukufuru?
(20) (Musa) akasema: Nilitenda hayo hapo nilipokuwa miongoni mwa wale waliopotea.
(21) Basi nikawakimbia nilipowahofu, tena Mola wangu Mlezi akanitunukia hukumu, na akanijaalia niwe miongoni mwa Mitume.
(22) Na hiyo ndiyo neema ya kunisumbulia, na wewe umewatia utumwani Wana wa Israili?
(23) Firauni akasema: Na ni nani huyo Mola Mlezi wa walimwengu wote?
(24) Akasema: Ndiye Mola Mlezi wa mbingu na ardhi, na vilivyo baina yake, ikiwa nyinyi ni wenye yakini.
(25) (Firauni) akawaambia waliomzunguka: Kwani hamsikilizi?
(26) (Musa) akasema: Ndiye Mola wenu Mlezi, na Mola Mlezi wa baba zenu wa kwanza.
(27) (Firauni) akasema: Hakika huyu Mtume wenu aliyetumwa kwenu ni mwendawazimu.
(28) (Musa) akasema: Ndiye Mola Mlezi wa Mashariki na Magharibi na vilivyo baina yake, ikiwa nyinyi mnatia akilini.
(29) (Firauni) akasema: Ukijifanyia mungu mwengine asiyekuwa mimi, basi bila ya shaka nitakufunga gerezani.
(30) Akasema: Je, hata kama nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?
(31) Akasema: Kilete basi, kama wewe ni katika wakweli.
(32) Basi akaitupa fimbo yake, mara ikawa nyoka wa kuonekana dhahiri.
(33) Na akautoa nje mkono wake, mara ukawa mweupe kwa watazamao.
(34) (Firauni) akawaambia waheshimiwa waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mtaalamu.
(35) Anataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wake. Basi mna shauri gani?
(36) Wakasema: Mpe muda yeye na kakaye na uwatume mijini wakusanyao watu.
(37) Wakuletee kila mchawi bingwa mtaalamu.
(38) Basi wakakusanywa wachawi kwa ajili ya miadi ya siku maalumu.
(39) Na watu wakaambiwa: Je, mtakusanyika?
(40) Huenda tutawafuata wachawi ikiwa wao ndio watakaoshinda.
(41) Basi walipokuja wachawi, wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira ikiwa sisi ndio tutakaoshinda?
(42) Akasema: Naam! Na hakika mtakuwa katika watu wa mbele.
(43) Musa akwaambia: Tupeni mnavyotaka kutupa.
(44) Basi wakatupa kamba zao na fimbo zao, na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi hapana shaka ni wenye kushinda.
(45) Basi Musa akatupa fimbo yake, nayo mara ikavimeza vile walivyovizua.
(46) Hapo wachawi hao walipinduka wakasujudu.
(47) Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(48) Mola Mlezi wa Musa na Harun.
(49) (Firauni) akasema: Je, mmemuamini kabla ya kuwaruhusu? Bila ya shaka yeye basi ndiye mkubwa wenu aliyewafunza uchawi. Basi mtakuja jua! Nitakatakata mikono yenu na miguu yenu kwa kutofautisha. Na nitawasulubisha misalabani nyote.
(50) Wakasema: Haidhuru, kwani sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
(51) Hakika sisi tunatumai kwamba Mola wetu Mlezi atatusamehe makosa yetu, kwa kuwa tumekuwa wa kwanza wa Waumini.
(52) Na tulimuamrisha Musa kwa ufunuo: Nenda na waja wangu wakati wa usiku. Kwa hakika mtafuatwa.
(53) Basi Firauni akawatuma mijini wakusanyaji.
(54) (Wakieneza): Hakika hawa ni kikundi kidogo.
(55) Nao kwa hakika wanatuudhi.
(56) Na sisi ni wengi, wenye kuchukua hadhari.
(57) Basi tukawatoa katika mabustani na chemchemi.
(58) Na mahazina, na vyeo vya heshima,
(59) Vivyo hivyo, na tukawarithisha hayo Wana wa Israili.
(60) Basi wakawafuata lilipochomoza jua.
(61) Na yalipoonana majeshi mawili haya, watu wa Musa wakasema: Hakika sisi bila ya shaka tumekutwa!
(62) (Musa) akasema: Hasha! Hakika yu pamoja nami Mola wangu Mlezi. Yeye ataniongoa!
(63) Na tulimletea Musa ufunuo tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana, na kila sehemu ikawa kama mlima mkubwa.
(64) Na tukawasongesha hapo karibu wale wengine.
(65) Tukawaokoa Musa na wale waliokuwa pamoja naye wote.
(66) Kisha tukawazamisha hao wengine.
(67) Hakika bila ya shaka katika hayo ipo Ishara; lakini wengi wao si wenye kuamini.
(68) Na kwa hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(69) Na wasomee habari za Ibrahim.
(70) Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?
(71) Wakasema: Tunaabudu masanamu, daima tunayanyenyekea.
(72) Akasema: Je, yanawasikia mnapoyaita?
(73) Au yanawafaa, au yanawadhuru?
(74) Wakasema: Bali tuliwakuta baba zetu wakifanya hivyo hivyo.
(75) Akasema: Je, mmewaona hawa mnaowaabudu?
(76) Nyinyi na baba zenu wa zamani?
(77) Kwani hakika hao ni adui zangu, isipokuwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(78) Ambaye ndiye aliyeniumba, na Yeye ndiye ananiongoa
(79) Na ambaye ndiye ananilisha na kuninywesha.
(80) Na ninapougua, ni Yeye ndiye anayeniponesha.
(81) Na ambaye atanifisha, na kisha atanihuisha.
(82) Na ambaye ndiye ninayemtumai kunisamehe makosa yangu Siku ya Malipo.
(83) Mola wangu Mlezi! Nitunukie hukumu na uniunganishe na walio wema.
(84) Na unijalie nitajwe kwa wema na watu watakaokuja baadaye.
(85) Na unijalie katika warithi wa Bustani za neema.
(86) Na umsamehe baba yangu, kwani hakika alikuwa miongoni mwa wapotovu.
(87) Wala usinihizi Siku watakapofufuliwa.
(88) Siku ambayo kwamba mali haitafaa kitu wala wana.
(89) Isipokuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi.
(90) Na Pepo itasogezwa kwa wachamungu.
(91) Na Jahannamu itadhihirishwa kwa wapotovu.
(92) Na wataambiwa: Wako wapi mliokuwa mkiwaabudu
(93) Badala ya Mwenyezi Mungu? Je, wanawasaidia, au wanajisaidia wenyewe?
(94) Basi watavurumizwa humo wao na hao wakosefu.
(95) Na majeshi ya Ibilisi yote.
(96) Watasema, na hali ya kuwa wanazozana humo:
(97) Wallahi! Kwa yakini tulikuwa katika upotovu ulio dhahiri.
(98) Tulipowafanya nyinyi ni sawa na Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(99) Na hawakutupoteza isipokuwa wale wakosefu.
(100) Basi hatuna waombezi wowote.
(101) Wala rafiki wa dhati.
(102) Laiti tungelipata kurejea tena, tungelikuwa katika Waumini.
(103) Hakika katika haya ipo Ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.
(104) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu Mwingi wa kurehemu.
(105) Kaumu ya Nuhu waliwakadhibisha Mitume.
(106) Alipowaambia ndugu yao, Nuhu: Je, hamumchi Mwenyezi Mungu?
(107) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
(108) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
(109) Na siwaulizi juu yake ujira, kwani ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(110) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
(111) Wakasema: Je, tukuamini wewe, ilhali wanaokufuata ni watu duni?
(112) Akasema: Ninayajuaje waliyokuwa wakiyafanya?
(113) Hesabu yao haiko isipokuwa kwa Mola wao Mlezi, laiti mngelitambua!
(114) Wala mimi si wa kuwafukuza Waumini.
(115) Mimi si chochote isipokuwa ni Mwonyaji wa dhahiri shahiri.
(116) Wakasema: Ikiwa huachi, ewe Nuhu, bila ya shaka utapigwa mawe.
(117) Akasema: Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wamenikadhibisha.
(118) Basi hukumu baina yangu na wao kwa hukumu yako, na uniokoe mimi na walio pamoja nami miongoni mwa Waumini.
(119) Kwa hivyo tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika marikebu iliyosheheni.
(120) Kisha tukawazamisha baadaye waliobakia.
(121) Hakika katika haya ipo Ishara, lakini si wengi wao waliokuwa Waumini.
(122) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(123) Kina 'Aad waliwakanusha Mitume.
(124) Alipowaambia ndugu yao, Hud: Je, hamchi Mungu?
(125) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
(126) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
(127) Wala siwaulizi juu yake ujira wowote, kwani ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(128) Je, mnajenga juu ya kila mnyanyuko kumbusho la kufanyia upuuzi?
(129) Na mnajenga majengo ya kifahari kama kwamba mtaishi milele!
(130) Na mnapotumia nguvu, mnatumia nguvu kwa ujabari.
(131) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini.
(132) Na mcheni aliyewapa haya mnayoyajua.
(133) Aliwapa wanyama wa kufuga na wana.
(134) Na mabustani na chemchemi.
(135) Hakika mimi ninawahofia adhabu ya Siku Kubwa.
(136) Wakasema: Ni mamoja kwetu, ukitupa mawaidha au hukuwa miongoni mwa watoao mawaidha.
(137) Haya si chochote isipokuwa ni mtindo wa watu wa tokea zamani.
(138) Wala sisi hatutaadhibiwa.
(139) Wakamkadhibisha; nasi tukawaangamiza. Hakika bila ya shaka katika haya ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
(140) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(141) Kina Thamud waliwakadhibisha Mitume.
(142) Alipowaambia ndugu yao Saleh: Je, hamumchi Mungu?
(143) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
(144) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini.
(145) Wala siwaulizi ujira wowote juu yake. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(146) Je, mtaachwa salama usalimina katika haya yaliyopo hapa?
(147) Katika mabustani, na chemchemi?
(148) Na konde na mitende yenye makole yaliyowiva.
(149) Na mnachonga milimani majumba kwa ustadi.
(150) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
(151) Wala msitii amri za waliopitiliza mipaka
(152) Ambao wanafanya uharibifu katika nchi, wala hawatengenezi.
(153) Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa.
(154) Wewe si chochote isipokuwa ni mtu kama sisi. Basi leta Ishara ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.
(155) Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa, na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalumu.
(156) Wala msimguse kwa wovu, ikawashika adhabu ya Siku Kubwa.
(157) Lakini wakamuua, na wakawa wenye kujuta.
(158) Basi ikawapata adhabu. Hakika katika hayo ipo Ishara. Lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
(159) Na hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(160) Watu wa Luti waliwakadhibisha Mitume.
(161) Alipowaambia ndugu yao, Luti: Je, hamumchi Mungu?
(162) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu kwenu.
(163) Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini mimi.
(164) Wala mimi sikuwauliza ujira wowote juu yake; ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(165) Je, katika viumbe vyote mnawaingilia wanaume?
(166) Na mnaacha alichowaumbia Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Ama kweli nyinyi ni watu mnaoruka mipaka!
(167) Wakasema: Ewe Luti! Usipoacha, hapana shaka utakuwa miongoni mwa wanaotolewa mji!
(168) Akasema: Hakika mimi ni katika wanaokichukia hiki kitendo chenu.
(169) Mola wangu Mlezi! Niokoe mimi na ahali zangu na haya wayatendayo.
(170) Basi tukamwokoa yeye na ahali zake wote.
(171) Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma.
(172) Kisha tukawaangamiza wale wengine.
(173) Na tukawanyeshea mvua, basi ni ovu mno mvua ya waliyoonywa.
(174) Hakika katika hayo ipo Ishara. Na hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
(175) Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(176) Watu wa Machakani waliwakanusha Mitume.
(177) Shuaibu alipowaambia: Je, hamumchi Mungu?
(178) Hakika mimi kwenu ni Mtume muaminifu.
(179) Basi mcheni Mwenyezi Mungu, na nitiini mimi.
(180) Wala siwaulizi ujira wowote juu yake. Ujira wangu hauko isipokuwa kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(181) Timizeni kipimo sawasawa, wala msiwe katika wanaopunja.
(182) Na pimeni kwa haki iliyonyooka.
(183) Wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye jeuri katika ardhi kwa kufanya uharibifu.
(184) Na mcheni aliyewaumba nyinyi na vizazi vilivyotangulia.
(185) Wakasema: Hakika wewe ni katika waliorogwa.
(186) Na wewe si chochote isipokuwa ni mtu tu kama sisi, na kwa yakini tunakuona wewe ni katika waongo.
(187) Hebu tuangushie vipande kutoka mbinguni ikiwa wewe ni miongoni mwa wakweli.
(188) Akasema: Mola wangu Mlezi anajua zaidi mnayoyatenda.
(189) Basi walimkanusha, na ikawashika adhabu ya Siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya Siku kubwa.
(190) Hakika katika hayo ipo Ishara, lakini hawakuwa wengi wao wenye kuamini.
(191) Na hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ndiye Yeye Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(192) Na bila ya shaka hii ni Uteremsho wa Mola Mlezi wa walimwengu wote.
(193) Ameuteremsha Roho muaminifu.
(194) Juu ya moyo wako, ili uwe katika Waonyaji.
(195) Kwa ulimi wa Kiarabu ulio wazi.
(196) Na hakika bila ya shaka haya yamo katika Vitabu vya kale.
(197) Je, haikuwa kwao ni Ishara kwamba wanayajua haya wanauchoni wa Wana wa Israili?
(198) Na lau kuwa tungeliiteremsha juu ya mmoja wa wasiokuwa Waarabu.
(199) Na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuamini.
(200) Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wahalifu.
(201) Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.
(202) Basi itawafikia kwa ghafla, na hali hawana habari.
(203) Na watasema: Je, tutapewa muhula?
(204) Basi je, wanaihimiza adhabu yetu?
(205) Waonaje kama tukiwastarehesha kwa miaka.
(206) Kisha yakawafikia waliyokuwa wakiahidiwa.
(207) Yatawafaa nini yale waliyostareheshewa?
(208) Wala hatukuangamiza mji wowote isipokuwa ulikuwa na waonyaji.
(209) Kuwa ni ukumbusho. Wala Sisi hatukuwa wenye kudhulumu.
(210) Wala Mashetani hawakuteremka nayo.
(211) Wala haitakiwi kwao, na wala hawawezi.
(212) Hakika hao wametengwa na kusikia.
(213) Basi usimwombe mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.
(214) Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe.
(215) Na watwae kwa upole wanaokufuata miongoni mwa Waumini.
(216) Na ikiwa watakuasi, basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyatenda.
(217) Na umtegemee Mtukufu Mwenye nguvu, Mwingi wa kurehemu.
(218) Ambaye anakuona unaposimama.
(219) Na mageuko yako kati ya wanaosujudu.
(220) Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua zaidi.
(221) Je, niwaambieni nani wanawashukia Mashetani?
(222) Wanamshukia kila mzushi mkubwa mwingi wa dhambi.
(223) Wanawapelekea yale wanayoyasikia; na wengi wao ni waongo.
(224) Na watungaji mashairi ni wapotofu ndio wanawafuata.
(225) Je, huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?
(226) Na kwamba wao husema wasiyoyatenda?
(227) Isipokuwa wale walioamini, na wakatenda mema, na wakamkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, na wakajitetea wanapodhulumiwa. Na wanaodhulumu watakuja jua mgeuko gani watakaogeuka.