35 - Surat Fatir ()

|

(1) Sifa zote njema ni za Mwenyezi Mungu, Muumba wa mbingu na ardhi, aliyewafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili mbili, na tatu tatu, na nne nne. Huzidisha katika kuumba apendavyo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza juu ya kila kitu.

(2) Rehema ambayo Mwenyezi Mungu anawafungulia watu, hapana wa kuizuia. Na anayoizuia, hapana wa kuiachilia isipokuwa Yeye. Naye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(3) Enyi watu! Kumbukeni neema za Mwenyezi Mungu juu yenu. Ati yupo muumba mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu anayekupeni riziki kutoka mbinguni na kwenye ardhi? Hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Basi wapi mnakogeuzwa?

(4) Na wakikukanusha, basi walikwisha kanushwa Mitume kabla yako. Na mambo yote yatarudishwa kwa Mwenyezi Mungu.

(5) Enyi watu! Hakika ahadi ya Mwenyezi Mungu ni ya kweli. Basi kamwe yasikudanganyeni maisha ya dunia, wala kamwe mdanganyifu asikudanganyeni juu ya Mwenyezi Mungu.

(6) Hakika Shetani ni adui yenu, basi mfanyeni kuwa ni adui. Kwani yeye analiita kundi lake liwe katika watu wa Moto wenye mwako mkali.

(7) Wale waliokufuru watakuwa na adhabu kali; na wale walioamini na wakatenda mema watapata msamaha na ujira mkubwa.

(8) Je, yule aliyepambiwa matendo yake mabaya na akayaona ni mema - basi hakika Mwenyezi Mungu humpoteza amtakaye, na humwongoa amtakaye. Basi, nafsi yako isijihiliki kwa kuwasikitikia. Hakika Mwenyezi Mungu anajua vyema wanayoyafanya.

(9) Na Mwenyezi Mungu ndiye anayezituma Pepo ziyatimue mawingu, nasi tukayafikisha kwenye nchi iliyokufa, tukaifufua ardhi baada ya kufa kwake. Ndivyo kama hivyo kutakavyokuwa kufufuliwa.

(10) Mwenye kutaka utukufu, basi utukufu wote uko kwa Mwenyezi Mungu. Kwake Yeye hupanda neno zuri, na tendo jema Yeye hulitukuza. Na wanaopanga vitimbi vya maovu, watapata adhabu kali. Na vitimbi vyao vitaondokea patupu.

(11) Na Mwenyezi Mungu amewaumba kutokana na udongo. Kisha kwa tone la manii. Kisha akawafanya mwanamume na mwanamke. Na mwanamke yeyote hachukui mimba, wala hazai, isipokuwa kwa elimu yake. Na wala hapewi umri mwenye umri mrefu, wala hapunguziwi katika umri wake, isipokuwa yamo hayo katika Kitabu. Hakika hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.

(12) Na bahari mbili haziwi sawa; haya ni matamu yenye ladha, mazuri kunywa. Na haya ni ya chumvi, machungu. Na kutokana na bahari zote mnakula nyama mpya (isiyochacha). Na mnatoa mapambo mnayoyavaa. Na unaona ndani yake merikebu zinakata maji ili mtafute fadhila zake, na ili mpate kushukuru.

(13) Anauingiza usiku katika mchana, na anauingiza mchana katika usiku. Na amelifanya jua na mwezi kutumikia, kila kimoja kinakwenda kwa muda maalumu. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu Mola wenu Mlezi. Ufalme ni wake. Na hao mnaowaomba badala yake hawamiliki hata ugozi wa kokwa ya tende.

(14) Mkiwaomba hawasikii maombi yenu, na hata wakisikia, hawawajibu. Na Siku ya Kiyama watakataa ushirikina wenu. Na hapana atakayekupa habari vilivyo kama Yeye Mwenye habari.

(15) Enyi watu, nyinyi ndio wenye haja kwa Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kujitosha, Msifiwa.

(16) Akitaka, atawaondoa na alete viumbe vipya.

(17) Na hilo si gumu kwa Mwenyezi Mungu.

(18) Na mbebaji hatabeba mzigo wa mwengine. Na aliyetopewa na mzigo wake akiomba uchukuliwe, hautachukuliwa hata kidogo, hata kama ni jamaa yake. Hakika wewe unawaonya wale wanaomcha Mola wao Mlezi kwa ghaibu, na wanashika Swala. Na mwenye kujitakasa, basi anajitakasa kwa ajili ya nafsi yake. Na marejeo ni kwa Mwenyezi Mungu.

(19) Na kipofu na mwenye kuona hawalingani.

(20) Wala giza na mwangaza.

(21) Wala kivuli na joto.

(22) Wala hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini.

(23) Hukuwa wewe isipokuwa ni mwonyaji.

(24) Hakika Sisi tumekutuma wewe kwa Haki, kuwa ni mbashiri na mwonyaji. Na hapana umma wowote isipokuwa ulipata mwonyaji kati yao.

(25) Na wakikukadhibisha, basi walikwisha kanusha wale waliokuwa kabla yao. Mitume wao waliwajia kwa ushahidi wa waziwazi na kwa maandiko na Kitabu chenye nuru.

(26) Kisha nikawakamata wale waliokufuru. Basi kuchukia kwangu kulikuwaje?

(27) Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni, na kwayo tumeyatoa matunda yenye rangi mbalimbali. Na katika milima imo mistari myeupe na myekundu yenye rangi mbali mbali, na myeusi sana.

(28) Na katika watu, na wanyama, na mifugo, pia rangi zao zinahitalifiana. Kwa hakika wanaomcha Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wanazuoni. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye kusamehe.

(29) Hakika wale wanaosoma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Swala, na wakatoa kwa siri na kwa dhahiri katika vile tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyobwaga.

(30) Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani kubwa.

(31) Na hayo tuliyokufunulia kutoka Kitabuni ni Kweli, yenye kusadikisha yale yaliyokuwa kabla yake. Hakika Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Mwenye habari na Mwenye kuona.

(32) Kisha tumewarithisha Kitabu hao ambao tuliwateua miongoni mwa waja wetu. Kati yao yupo aliyejidhulumu, na yupo wa katikati, na yupo aliyetangulia katika mambo ya heri, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo fadhila kuu.

(33) Mabustani ya milele watayaingia. Huko watavikwa vikuku vya dhahabu na lulu, na nguo zao humo ni za hariri.

(34) Na watasema: Alhamdulillahi (Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu) aliyetuondolea huzuni wote. Hakika Mola wetu Mlezi bila ya shaka ni Mwenye kusamehe, Mwenye shukrani.

(35) Ambaye kwa fadhila yake ametuweka makao ya kukaa daima; humu haitugusi taabu wala humu hakutugusi kuchoka.

(36) Na wale waliokufuru watakuwa na Moto wa Jahannamu. Hawahukumiwi wakafa, wala hawatapunguziwa adhabu yake. Hivyo ndivyo tunavyomlipa kila mwenye kuzidi ukafiri.

(37) Na humo watapiga makelele: 'Mola wetu Mlezi! Tutoe tufanye mema siyo yale tuliyokuwa tukiyafanya.' Kwani hatukukupeni umri wa kutosha kukumbuka mwenye kukumbuka? Na akakukujieni Mwonyaji? Basi onjeni! Kwani wale waliodhulumu hawana wa kuwanusuru.

(38) Kwa hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa siri za mbinguni na ardhi. Hakika Yeye ni Mjuzi wa yaliomo vifuani.

(39) Yeye ndiye aliyekufanyeni manaibu katika ardhi. Na anayekufuru, basi kufuru yake ni juu yake. Na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila hasara.

(40) Sema: Mnawaona hawa miungu wenu wa kishirikina mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu! Nionyesheni wameumba sehemu gani katika ardhi? Au wana ushirika wowote katika mbingu? Au tumewapa Kitabu nao kwa hicho wakawa na hoja zilizo wazi? Lakini madhalimu hawaahidiani wao kwa wao ila udanganyifu tu.

(41) Hakika Mwenyezi Mungu ndiye anayezuilia mbingu na ardhi zisiondoke. Na zikiondoka hapana yeyote wa kuzizuia isipokuwa Yeye. Hakika Yeye ni Mpole Mwenye kusamehe.

(42) Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu ukomo wa kuapa kwao, kwamba akiwajia mwonyaji, bila ya shaka watakuwa waongofu zaidi kuliko taifa jingine lolote. Lakini alipowajia mwonyaji, hakuwazidishia ila kuikimbia hiyo Haki.

(43) Kwa kutakabari kwao katika nchi, na kufanya vitimbi vya uovu. Na vitimbi viovu havimsibu ila mwenyewe aliyevifanya. Hebu, hawangojei yale yaliowasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu.

(44) Je, hawakusafiri katika ardhi wakaona vipi ulikuwa mwisho wa wale waliokuwa kabla yao? Na hao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko wao. Na hapana kitu kinachoweza kumshinda Mwenyezi Mungu mbinguni wala katika ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kujua zaidi, Mwenye uweza wote.

(45) Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa yale waliyoyachuma, basi asingelimuacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja. Lakini Yeye anawachukulia mpaka ufike muda maalumu. Na muda wao ukifika, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaona waja wake baraabara.