(1) Kinamtakasa Mwenyezi Mungu kila kilichomo katika mbingu na katika ardhi. Ufalme ni wake, na sifa njema ni zake. Na Yeye ni Mwenye uweza juu ya kila kitu.
(2) Yeye ndiye aliyekuumbeni. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mno mnayoyatenda.
(3) Ameziumba mbingu na ardhi kwa haki, na akakupeni sura, na akazifanya nzuri sura zenu. Na marudio ni kwake.
(4) Anajua vilivyomo katika mbingu na ardhi, na anajua mnayoyaficha na mnayoyaweka hadharani. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa yaliyomo vifuani.
(5) Kwani haikukujieni habari ya wale waliokufuru kabla, wakaonja matokeo mabaya ya mambo yao? Na wao wana adhabu iliyo chungu.
(6) Hayo ni kwa kuwa Mitume wao walikuwa wakiwajia kwa hoja zilizo wazi, nao wakasema: 'Hivyo binadamu ndio atuongoe?' Basi wakakufuru, na wakageuka upande. Mwenyezi Mungu akawa hana haja nao. Na Mwenyezi Mungu ni Mkwasi, si mhitaji, naye ni Msifiwa.
(7) Wale waliokufuru wanadai kuwa hawatafufuliwa. Sema: Kwani? Ninaapa kwa Mola wangu Mlezi! Hapana shaka mtafufuliwa, na kisha hapana shaka mtaambiwa mliyoyatenda. Na hayo ni mepesi kwa Mwenyezi Mungu.
(8) Basi muaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Nuru tuliyoiteremsha. Na Mwenyezi Mungu anazo habari za mnayoyatenda.
(9) Siku atakayokukusanyeni kwa ajili ya Siku ya Mkusanyiko. Hiyo ni siku ya kupunjana. Na anayemuamini Mwenyezi Mungu na akatenda mema, atamfutia maovu yake, na atamuingiza katika Mabustani ya mbinguni yenye kupitiwa kati yake mito, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(10) Na wale waliokufuru na wakakadhibisha Ishara zetu, hao ni watu wa Motoni, watadumu humo milele. Na hayo ndiyo marejeo mabaya mno.
(11) Haufiki msiba wowote ila kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, huuongoa moyo wake. Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi kila kitu.
(12) Na mtiini Mwenyezi Mungu, na mtiini Mtume. Mkigeuka, basi hakika juu ya Mtume wetu ni kufikisha (Ujumbe wake) kwa uwazi tu.
(13) Mwenyezi Mungu, hapana mungu isipokuwa Yeye. Na juu ya Mwenyezi Mungu, basi na wategemee Waumini.
(14) Enyi mlioamini! Hakika miongoni mwa wake zenu na watoto wenu wamo maadui zenu. Basi tahadharini nao. Na mkisamehe, na mkapuuza, na mkaghufiria basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghfira, Mwenye kurehemu.
(15) Hakika mali yenu na watoto wenu ni jaribio. Na kwa Mwenyezi Mungu upo ujira mkubwa.
(16) Basi mcheni Mwenyezi Mungu kama mwezavyo, na sikieni, na tiini, na toeni, itakuwa heri kwa nafsi zenu. Na mwenye kuepushwa na uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio waliofanikiwa.
(17) Mkimkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mzuri, atakuzidishieni maradufu, na atakusameheni. Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa shukrani, Mstahamilivu.
(18) Mwenye kujua siri na dhahiri, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.