32 - Surat As-Sajdah ()

|

(1) Alif Laam Miim

(2) Huu ni mteremsho wa Kitabu kisicho kuwa na shaka yoyote kinachotoka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote.

(3) Au wanasema: Amekizua? Bali hiki ni kweli iliyotoka kwa Mola wako Mlezi ili uwaonye watu wasiofikiwa na mwonyaji kabla yako; huenda wakaongoka.

(4) Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yake kwa siku sita, na akatawala kwenye Kiti cha Enzi. Nyinyi hamna mlinzi wala mwombezi isipokuwa Yeye tu. Basi, je, hamkumbuki?

(5) Anapitisha mambo yote yaliyo baina ya mbingu na ardhi, kisha yanapanda kwake kwa siku ambayo kipimo chake ni miaka elfu kwa mnavyohesabu nyinyi.

(6) Huyu ndiye Mwenye kuyajua yasiyoonekana na yanayoonekana. Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

(7) Ambaye ametengeneza vizuri umbo la kila kitu na akaanzisha kumuumba mtu kwa udongo.

(8) Na kisha akajaalia uzao wake utokane na kizazi cha maji madhaifu.

(9) Kisha akamtengeneza sawasawa, na akampulizia katika roho yake, na akawajalieni kusikia na kuona, na nyoyo za kufahamu. Ni uchache mnavyoshukuru.

(10) Nao husema: Tutapokwisha potea chini ya ardhi, ni kweli tutarudishwa katika umbo jipya? Bali wao wanakanusha kwamba watakutana na Mola wao Mlezi.

(11) Sema, "Atakufisheni Malaika wa mauti aliyewakilishwa juu yenu; kisha mtarejeshwa kwa Mola wenu Mlezi."

(12) Na ungeliwaona wakosefu wanavyoinamisha vichwa vyao mbele ya Mola wao Mlezi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Tumeshaona, na tumeshasikia. Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwisha kuwa na yakini sasa.

(13) Na lau tungelitaka, tungempa kila mtu uwongofu wake. Lakini imekwisha kuwa kauli iliyotoka kwangu: Kwa yakini nitaijaza Jahannamu kwa wote hawa, majini na watu.

(14) Basi onjeni kwa vile mlivyousahau mkutano wa Siku yenu hii. Na Sisi hakika tunakusahauni. Basi onjeni adhabu ya milele kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.

(15) Hakika wanaoziamini Aya zetu ni hao tu ambao wakikumbushwa hizo, basi wao huanguka kusujudu, na humsabihi Mola wao Mlezi kwa kumhimidi, nao hawajivuni.

(16) Mbavu zao zinaachana na vitanda kwa kumwomba Mola wao Mlezi kwa khofu na kutumaini, na hutoa kutokana na tulivyowaruzuku.

(17) Nafsi yoyote haijui waliyofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho - ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

(18) Ati aliye Muumini atakuwa sawa na aliye mpotovu? Hawawi sawa.

(19) Ama walioamini na wakatenda mema, watakuwa nazo Bustani za makazi mazuri. Ndio pa kufikia kwa waliyokuwa wakiyatenda.

(20) Na ama wale waliotenda uovu, basi makazi yao ni Motoni. Kila wakitaka kutoka humo, watarudishwa humo humo. Na wataambiwa: Onjeni adhabu ya Moto ambayo mlikuwa mkiikanusha.

(21) Na hakika tutawaonjesha katika adhabu hafifu kabla ya adhabu kubwa, huenda labda watarejea.

(22) Na ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule anayekumbushwa kwa Ishara za Mola wake Mlezi, kisha akazikataa? Hakika Sisi tutajilipiza kwa wakosefu.

(23) Hakika Sisi tulikwisha mpa Musa Kitabu. Basi usiwe na shaka kuwa kakipokea. Na tukakifanya kuwa ni uwongofu kwa Wana wa Israili.

(24) Na tukawafanya miongoni mwa waongozi wanaoongoa watu kwa amri yetu, waliposubiri na wakawa na yakini na Ishara zetu.

(25) Hakika Mola wako Mlezi ndiye atakayefafanua baina yao Siku ya Kiyama katika yale waliyokuwa wakihitalifiana ndani yake.

(26) Ee! Haijawabainikia kwamba kaumu ngapi tuliziangamiza kabla yao, nao wanapita katika maskani zao hizo? Hakika katika hayo zipo Ishara. Basi, je, hawasikii?

(27) Je, hawaoni ya kwamba tunayapeleka maji kwenye ardhi kavu, kisha kwayo tunaitoa mimea wanayokula wanyama wao na wao wenyewe? Je, hawaoni?

(28) Wanasema: Ushindi huu ni lini, kama nyinyi ni wakweli?

(29) Sema: Siku ya Ushindi, wale waliokufuru imani yao haitawafaa kitu, wala wao hawatapewa muhula.

(30) Basi wapuuze, nawe ngonja; hakika wao wanangoja.