62 - Surat Al-Jumu'ah ()

|

(1) Vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(2) Yeye ndiye aliyemtuma Mtume kwenye watu wasiojua kusoma na kuandika, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hekima, ijapokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhahiri.

(3) Na kwa wengine ambao bado hawajaungana nao. Na Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(4) Hiyo ni fadhila ya Mwenyezi Mungu anayompa amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye fadhila kubwa.

(5) Mfano wa wale waliobebeshwa Taurati kisha wasiibebe, ni mfano wa punda anayebeba vitabu vikubwa vikubwa. Mfano muovu mno wa watu waliokadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu madhalimu.

(6) Sema: Enyi mlio Mayahudi! Ikiwa nyinyi mnadai kuwa ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu pasipokuwa watu wengine, basi yatamanini mauti, ikiwa mnasema ukweli.

(7) Wala hawatayatamani kabisa, kwa sababu ya iliyokwisha yatanguliza mikono yao. Na Mwenyezi Mungu anawajua mno madhalimu.

(8) Sema: Hayo mauti mnayoyakimbia, bila ya shaka yatakukuteni. Kisha mtarudishwa kwa Mwenye, mjuzi wa yaliyofichikana na yanayoonekana. Hapo atakwambieni mliyokuwa mkiyatenda.

(9) Enyi mlioamini! Ikiadhiniwa kwa ajili ya Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye utajo wa Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua.

(10) Na itakapokwisha Sala, tawanyikeni katika nchi mtafute fadhila za Mwenyezi Mungu, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufanikiwa.

(11) Na wanapoiona biashara au pumbao wanayakimbilia hayo na wakakuacha umesimama. Sema: Yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ni bora kuliko pumbao na biashara. Na Mwenyezi Mungu ni Mbora wa watoa riziki.