59 - Surat Al-Hashr ()

|

(1) Vinamtakasa Mwenyezi Mungu vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Naye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

(2) Yeye ndiye aliyewatoa wale waliokufuru miongoni mwa Watu wa Kitabu katika nyumba zao wakati wa uhamisho wa kwanza. Hamkudhani kuwa watatoka, nao walidhani kuwa ngome zao zitawalinda dhidi ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu akawafikia kwa mahali ambako hawakutazamia, na akatia uwoga mkubwa katika nyoyo zao. Wakawa wanazibomoa nyumba zao kwa mikono yao na mikono ya Waumini. Basi zingatieni enyi wenye macho!

(3) Na lau kuwa Mwenyezi Mungu asingeliwaandikia kutoka, angeliwaadhibu katika dunia. Na katika Akhera watapata adhabu ya Moto.

(4) Hayo ni kwa sababu walimpinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumpinga Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

(5) Mtende wowote mlioukata au mliouacha umesimama vile vile juu ya mashina yake, basi ni kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, na ili awahizi wavukao mipaka.

(6) Na mali aliyoileta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwao hamkuikimbilia mbio kwa farasi wala ngamia. Lakini Mwenyezi Mungu huwapa mamlaka Mitume wake juu ya wowote awatakao. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza mno juu ya kila kitu.

(7) Mali aliyoileta Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kutoka kwa watu wa hivi vijiji ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na kwa ajili ya Mtume, na jamaa, na mayatima, na masikini, na msafiri, ili isiwe ikizunguka baina ya matajiri tu miongoni mwenu. Na anachokupeni Mtume, kichukueni. Na anachokukatazeni, jiepusheni nacho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.

(8) Wapewe mafakiri Wahajiri waliotolewa majumbani mwao na mali yao kwa ajili ya kutafuta fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake, na wanamsaidia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao ndio wakweli.

(9) Na wale walio na maskani zao na Imani yao kabla yao, wanawapenda wale waliohamia kwao, wala hawaoni choyo katika vifua vyao kwa walivyopewa (Wahajiri), bali wanawapendelea kuliko nafsi zao, ingawa wao wenyewe ni wahitaji. Na mwenye kuepushwa uchoyo wa nafsi yake, basi hao ndio wenye kufanikiwa.

(10) Na wale waliokuja baada yao wanasema: Mola wetu Mlezi! Tughufirie sisi na ndugu zetu waliotutangulia kwa Imani, wala usijaalie ndani ya nyoyo zetu undani kwa walioamini. Mola wetu Mlezi! Hakika Wewe ni Mpole na Mwenye kurehemu mno.

(11) Huwaoni wale wanaofanya unafiki wanawaambia ndugu zao waliokufuru katika Watu wa Kitabu: Mkitolewa, na sisi lazima tutatoka pamoja nanyi, wala hatutamtii yeyote kabisa dhidi yenu. Na mkipigwa vita, lazima tutakusaidieni. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa hao hakika bila ya shaka ni waongo.

(12) Pindi wakitolewa, hawatatoka pamoja nao. Na wakipigwa vita, hawatawasaidia. Na kama wakiwasaidia, basi watageuza mno migongo; kisha hawatanusuriwa.

(13) Hakika nyinyi ni kitisho zaidi katika vifua vyao kuliko Mwenyezi Mungu. Hayo ni kwa kuwa hao ni watu wasiofahamu kitu.

(14) Hawatapigana nanyi kwa mkusanyiko isipokuwa katika vijiji vilivyoimarishwa kwa ngome, au nyuma ya kuta. Wao kwa wao vita vyao ni vikali. Utawadhania kuwa wako pamoja, kumbe nyoyo zao ni mbali mbali. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiotumia akili.

(15) Ni kama mfano wa wale waliokuwa kabla yao hivi karibuni, walionja uovu wa mambo yao. Nao watapata adhabu iliyo chungu.

(16) Ni kama mfano wa Shetani anapomwambia mtu: 'Kufuru.' Na akikufuru, humwambia: 'Hakika mimi niko mbali zaidi nawe. Hakika mimi namwogopa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu wote.'

(17) Basi ikawa mwisho wa wote wawili hao ni kuingia Motoni, wadumu humo daima; na hayo ndiyo malipo ya madhalimu.

(18) Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kila nafsi iangalie inayo yatanguliza kwa ajili ya Kesho. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu anazo habari ya mnayoyatenda.

(19) Wala msiwe kama wale walio msahau Mwenyezi Mungu, na Yeye akawasahaulisha nafsi zao. Hao ndio wavukao mipaka.

(20) Hawawi sawa watu wa Motoni na watu wa Peponi. Watu wa Peponi ndio wenye kufuzu.

(21) Lau kuwa tumeiteremsha hii Qur'ani juu ya mlima, basi bila ya shaka ungeliuona ukinyenyekea, ukipasuka kwa hofu ya Mwenyezi Mungu. Na hiyo mifano tunawapigia watu ili wafikiri.

(22) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mwenye kuyajua yaliyofichikana na yanayoonekana. Yeye ndiye Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

(23) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu ambaye hapana mungu isipokuwa Yeye tu. Mfalme, Mtakatifu, Mwenye salama, Mtoaji wa amani, Mwenye kuyaendesha Mwenyewe mambo yake, Mwenye nguvu, Anayefanya analolitaka, Mkubwa, Ametakasika Mwenyezi Mungu na hayo wanayomshirikisha nayo.

(24) Yeye ndiye Mwenyezi Mungu, Muumbaji, Mtengenezaji, Mtia sura, Mwenye majina mazuri kabisa. Kila kilioko katika mbingu na ardhi kinamtakasa, naye ni Mwenye kushinda, Mwenye hekima.