6 - Surat Al-An'am ()

|

(1) Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, ambaye aliumba mbingu na ardhi, na akafanya giza mbalimbali na nuru. Kisha wale waliokufuru wanawafanya wengine kuwa sawa na Mola wao Mlezi.

(2) Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na udongo, kisha akawahukumia muda, na muda maalumu uko kwake tu. Kisha nyinyi mnatia shaka.

(3) Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu katika mbingu na katika ardhi. Anajua ya siri yenu na ya dhahiri yenu. Na anajua mnayoyachuma.

(4) Na haiwajii ishara miongoni mwa ishara za Mola wao Mlezi isipokuwa walikuwa wakiipa mgongo.

(5) Basi hakika walikwisha ikadhibisha haki ilipowajia. Kwa hivyo, zitawajia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

(6) Je, hawakuona ni vizazi vingapi tulivyoviangamiza kabla yao? Tuliwaimarisha katika dunia namna ambavyo hatukuwaimarisha nyinyi; na tukawatumia mvua nyingi na tukaifanya mito inapita kwa chini yao. Mwishowe tukawaangamiza kwa madhambi yao; na tukaanzisha baada yao kizazi kingine.

(7) Na lau tungelikuteremshia kitabu cha karatasi, wakakigusa kwa mikono yao, wangelisema wale waliokufuru: Haya si chochote isipokuwa ni uchawi ulio wazi.

(8) Na walisema, "Mbona hakuteremshiwa Malaika?" Na kama tungelimteremsha Malaika, basi bila ya shaka ingeshahukumiwa amri, kisha wasingelipewa muhula.

(9) Na kama tungelimfanya Malaika, bila ya shaka tungelimfanya kuwa mwanamume, na tungeliwatilia matatizo yale wanayoyatatiza wao.

(10) Na hakika walifanyiwa mzaha Mitume waliokuwa kabla yako, lakini wale waliowafanyia mzaha yakawafika yale yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.

(11) Sema: Tembeeni katika dunia, kisha mtazame vipi ulikuwa mwisho wa wanaokadhibisha.

(12) Sema: Ni vya nani vilivyo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye ameiandika rehemu juu ya nafsi yake. Hakika atawakusanya hadi Siku ya Qiyama isiyokuwa na shaka. Wale waliojihasiri nafsi zao, wao hawaamini.

(13) Na ni vyake vilivyotulia katika usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

(14) Sema: Je, nimfanye rafiki mwandani asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba mwanzilishi wa mbingu na ardhi, naye ndiye anayelisha wala halishwi? Sema: Hakika Mimi nimeamrishwa kwamba niwe wa kwanza wa wenye kusilimu. Na wala kabisa usiwe miongoni wa washirikina.

(15) Sema: Hakika Mimi ninahofu nikimuasi Mola wangu Mlezi, adhabu ya Siku kubwa.

(16) Mwenye kuepushwa nayo Siku hiyo, basi hakika atakuwa amemrehemu. Na huko ndiko kufuzu kuliko wazi.

(17) Na ikiwa Mwenyezi Mungu akikugusa kwa madhara, basi hapana wa kuyaondoa isipokuwa Yeye. Na ikiwa akikugusa kwa heri, basi Yeye ndiye Muweza wa kila kitu.

(18) Naye ndiye Mwenye nguvu juu ya waja wake, naye ndiye Mwenye hekima, Mwenye habari zote.

(19) Sema: Ni kitu gani ushahidi wake ndio mkubwa kabisa? Sema: Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye shahidi baina yangu na nyinyi. Na imefunuliwa kwangu Qur-ani hii ili kwayo niwaonye nyinyi na kila inayemfikia. Ati kweli nyinyi mnashuhudia kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu wapo miungu wengine? Sema: Mimi sishuhudii hayo. Sema: Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu, nami hakika niko mbali na mnaowashirikisha.

(20) Wale tuliowapa Kitabu wanakijua kama wanavyowajua watoto wao. Wale waliozihasiri nafsi zao, basi wao hawaamini.

(21) Na nani dhalimu zaidi kuliko anayemzulia uongo Mwenyezi Mungu, au akazikadhibisha Ishara zake? Hakika madhalimu hawafaulu.

(22) Siku tutakapowakusanya wote pamoja, kisha tuwaambie wale walioshirikisha: Wako wapi washirikishwa wenu mliokuwa mkidai?

(23) Kisha hautakuwa udhuru wao isipokuwa ni kusema: Wallahi! Mola wetu Mlezi! Hatukuwa washirikina.

(24) Tazama jinsi wanavyosema uongo juu ya nafsi zao wenyewe. Na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.

(25) Na miongoni mwao wapo wanaokusikiliza; na tumezitia pazia kwenye nyoyo zao wasije kuyafahamu. Na upo uziwi katika masikio yao, na wakiona kila Ishara, hawaiamini. Mpaka wakikujia kwa kujadiliana nawe, wanasema wale waliokufuru: Hizi si chochote isipokuwa hadithi za watu wa kale.

(26) Nao huwazuia watu hayo, na wao wenyewe wanajitenga nayo. Nao hawaangamizi isipokuwa nafsi zao tu, wala wao hawatambui.

(27) Na lau ungeona waliposimamishwa kwenye Moto, wakawa wanasema: Laiti tungelirudishwa, wala tusizikadhibishe tena Ishara za Mola wetu Mlezi, na tuwe miongoni wa Waumini.

(28) Bali yamewadhihirikia yale waliyokuwa wakiyaficha zamani. Na lau wangelirudishwa, bila ya shaka wangeliyarejea yale yale waliyokatazwa. Na hakika wao ni waongo.

(29) Na walisema: Hakuna mengine isipokuwa maisha yetu haya ya duniani, wala sisi hatutafufuliwa.

(30) Na lau utaona walivyosimamishwa mbele ya Mola wao Mlezi, akasema, "Je, huu si uhakika?" Na wao wakasema, "Ndiyo? Tunaapa kwa Mola Mlezi wetu (ni uhakika)." Yeye akasema: Basi onjeni adhabu kwa sababu ya vile mlivyokuwa mnakufuru.

(31) Hakika wamehasirika wale waliokadhibisha kukutana na Mwenyezi Mungu, mpaka ilipowajia Saa kwa ghafla, wakasema: Ee majuto yetu kwa yale tuliyoyapuuza! Nao watabeba mizigo yao juu ya migongo yao. Tazama! Ni maovu mno hayo wanayoyabeba.

(32) Na maisha ya dunia si chochote isipokuwa ni mchezo na pumbao tu. Na hakika Nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wale wanaomcha Mwenyezi Mungu. Basi, je, hamtumii akili?

(33) Hakika tunajua ya kwamba yanakuhuzunisha yale wanayoyasema. Basi hakika wao hawakukadhibishi wewe, lakini hao madhalimu wanazikataa Ishara za Mwenyezi Mungu.

(34) Na hakika walikadhibiwa Mitume wa kabla yako. Nao wakavumilia kule kukanushwa, na kuudhiwa, mpaka ilipowafikia nusura yetu. Na hapana wa kubadilisha maneno ya Mwenyezi Mungu. Na hakika imekwisha kujia katika habari za Mitume hao.

(35) Na ikiwa ni makubwa kwako huku kupeana kwao mgongo, basi kama unaweza kutafuta njia ya chini kwa chini ya ardhi, au ngazi kwendea mbinguni ili uwaletee Ishara. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, angeliwakusanya kwenye uwongofu. Basi kamwe usiwe miongoni mwa wajinga.

(36) Hakika wanaoitikia ni wale wanaosikia. Na ama wafu, Mwenyezi Mungu atawafufua, kisha kwake Yeye ndiko watakakorejeshwa.

(37) Na walisema: Kwa nini hakuteremshiwa muujiza kutoka kwa Mola wake Mlezi? Sema: Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kuteremsha muujiza. Lakini wengi wao hawajui.

(38) Na hakuna mnyama yeyote katika ardhi, wala ndege anayepaa kwa mbawa zake mbili, isipokuwa ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza kitu chochote katika Kitabu. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa.

(39) Na wale waliozikadhibisha Ishara zetu ni viziwi na mabubu wamo katika giza mbalimbali. Yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka, anampoteza, na yule ambaye anataka, anamuweka katika Njia iliyonyooka.

(40) Sema: Mwaonaje ikiwajia adhabu ya Mwenyezi Mungu, au ikawajia hiyo Saa, asiyekuwa Mwenyezi Mungu ndiye mtakayemuomba, ikiwa nyinyi ni wakweli?

(41) Bali Yeye ndiye mtakayemuomba, naye atawaondolea mnachomwombea akipenda. Na mtasahau hao mnaowafanya washirika wake.

(42) Na kwa yakini tuliwatuma Mitume kwa kaumu zilizokuwa kabla yako, kisha tukawatia katika dhiki na mashaka ili wanyenyekee.

(43) Kwa nini wasinyenyekee ilipowafika adhabu yetu? Lakini nyoyo zao zilikuwa ngumu, na Shetani akawapambia waliyokuwa wakiyafanya.

(44) Basi waliposahau yale waliyokumbushwa, tuliwafungulia milango ya kila kitu. Mpaka walipofurahia yale waliyopewa, tukawashika kwa ghafla, na mara wakawa wenye kukata tamaa.

(45) Ikakatwa mizizi ya kaumu waliodhulumu, na kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa viumbe vyote.

(46) Sema: Mwaonaje Mwenyezi Mungu akinyakua kusikia kwenu, na kuona kwenu, na akaziziba nyoyo zenu, ni mungu gani asiyekuwa Mwenyezi Mungu atakayewaletea hayo tena? Angalia vipi tunavyozieleza Ishara, kisha wao wanapuuza.

(47) Sema: Mwaonaje, ikiwafikia adhabu ya Mwenyezi Mungu kwa ghafla, au kwa dhahiri, je wataangamizwa isipokuwa kaumu waliodhulumu?

(48) Na hatuwatumi Mitume isipokuwa huwa ni wabashiri na waonyaji. Basi mwenye kuamini na akatengenea, haitakuwa hofu yoyote juu yao, wala hawatahuzunika.

(49) Na wale waliozikadhibisha Ishara zetu itawagusa adhabu kwa vile walivyokuwa wakivuka mipaka.

(50) Sema: Mimi siwaambii kuwa ninazo hazina za Mwenyezi Mungu. Wala sijui mambo yaliyofichikana. Wala siwaambii kuwa mimi ni Malaika. Mimi sifuati isipokuwa yanayofunuliwa kwangu. Sema: Je, wanakuwa sawa, kipofu na mwenye kuona. Basi hamfikiri?

(51) Na waonye kwayo wale wanaohofu kuwa watakusanywa kwa Mola wao Mlezi, hali ya kuwa hawana kando naye mlinzi wala mwombezi, ili wamche Mwenyezi Mungu.

(52) Wala usiwafukuze wale wanaomwomba Mola Mlezi wao asubuhi na jioni kwa kutaka radhi yake. Si juu yako hisabu yao hata kidogo, wala hisabu yako si juu yao hata kidogo, hata uwafukuze na uwe miongoni mwa wenye kudhulumu.

(53) Na hivi ndivyo tunavyowajaribu wao kwa wao, ili waseme: Ni hao ndio Mwenyezi Mungu amewafadhilisha miongoni mwetu? Kwani Mwenyezi Mungu hawajui wanaoshukuru?

(54) Na wanapokujia wanaoziamini Ishara zetu waambie: Assalamu alaikum! (Amani iwe juu yenu!) Mola wenu Mlezi amejilazimisha rehema, ya kwamba atakayefanya uovu miongoni mwenu kwa ujinga, kisha akatubu baada yake na akatengenea, basi hakika Yeye ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

(55) Na ndivyo hivyo tunavyozieleza Ishara, na ili ibainike njia ya wahalifu.

(56) Sema: Mimi nimekatazwa kuwaabudu hao mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu. Sema: mimi sifuati matamanio yenu. Hivyo nitakuwa nimepotea, na sitakuwa miongoni mwa walioongoka.

(57) Sema: Mimi nipo kwenye sheria iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu Mlezi, nanyi mnaikanusha. Mimi sina hicho mnachokihimiza. Hapana hukumu ila ya Mwenyezi Mungu. Yeye anasimulia yaliyo kweli; naye ni Mbora wa kuhukumu kuliko wote.

(58) Sema: Lau kuwa ninacho hicho mnachokihimiza, ingelikwisha katwa shauri baina yangu na nyinyi. Na Mwenyezi Mungu ndiye anayewajua zaidi madhalimu.

(59) Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilicho katika nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.

(60) Naye ndiye anayewafisha usiku, na anakijua mlichokifanya mchana. Kisha Yeye huwafufua humo mchana ili muda uliowekwa utimizwe. Kisha kwake Yeye ndiyo marejeo yenu, kisha atawaambia yale mliyokuwa mkiyafanya.

(61) Naye ndiye Mwenye nguvu za kushinda, aliye juu ya waja wake. Na huwapelekea (nyinyi) waangalizi, mpaka mmoja wenu yakimjia mauti wajumbe wetu humfisha, nao hawafanyi taksiri.

(62) Kisha watarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, Mola wao wa Haki. Hakika, hukumu ni yake. Naye ni Mwepesi kuliko wote wanaohisabu.

(63) Sema: Ni nani anayewaokoa kutoka katika giza la nchi kavu na baharini? Mnamwomba kwa unyenyekevu na kwa siri, mkisema: Kama akituokoa na haya bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

(64) Sema: Mwenyezi Mungu hukuwaokoa kutoka katika hayo, na kutoka kila mashaka, na kisha nyinyi mnamshirikisha!

(65) Sema: Yeye ndiye Muweza wa kuwatumia adhabu kutoka juu yenu au kutoka chini ya miguu yenu, au awavishe fujo la mfarakano, na awaonjeshe baadhi yenu jeuri ya wenzi wenu. Tazama vipi tunavyozieleza Aya ili wafahamu.

(66) Na kaumu yako waliikadhibisha, nayo ndiyo Haki. Sema: Mimi si wakili juu yenu.

(67) Kila habari ina kipindi chake. Nanyi mtakuja jua.

(68) Na unapowaona wanaoziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingilie mazungumzo mengine. Na kama Shet'ani akikusahaulisha, basi baada ya kutanabahi usikae pamoja na watu madhalimu.

(69) Wala hakuna jukumu lolote kwa wale wamchao Mungu, lakini ni kukumbusha tu, asaa wapate kumcha Mwenyezi Mungu.

(70) Waachilie mbali walioifanya dini yao ni mchezo na pumbao, na uhai wa dunia ukawaghuri. Nawe kumbusha kwayo, isije nafsi ikaangamizwa kwa sababu ya iliyoyachuma, nayo haina mlinzi wala mwombezi ila Mwenyezi Mungu. Na ingetoa kila fidia haitokubaliwa. Hao ndio walioangamizwa kwa sababu ya yale waliyoyachuma. Wao watapata kinywaji cha maji ya moto kabisa, na adhabu chungu.

(71) Sema: Je, tumuombe asiyekuwa Mwenyezi Mungu ambaye hatufai wala hatudhuru, na turejee nyuma baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuongoa? Tuwe kama ambao mashetani wamempumbaza katika ardhi, amebabaika? Anao marafiki wanaomwita aende kwenye uwongofu, wakimwambia: Njoo kwetu! Sema: Hakika uwongofu wa Mwenyezi Mungu ndio Uwongofu. Nasi tumeamrishwa tusilimu kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.

(72) Na mshike Sala, na mcheni Yeye, na kwake Yeye ndiko mtakakokusanywa

(73) Naye ndiye aliyeziumba mbingu na ardhi kwa Haki. Na anaposema: Kuwa! Basi huwa. Kauli yake ni Haki. Na ufalme wote ni wake Siku litakapopulizwa barugumu, Mjuzi wa yaliyofichikana na yanayoonekana. Naye ndiye Mwenye hekima na Mwenye habari.

(74) Na pale Ibrahim alipomwambia baba yake, Azar: Unayafanya masanamu kuwa ni miungu? Hakika mimi nakuona wewe na watu wako mmo katika upotovu ulio wazi.

(75) Na kadhaalika tulimwonyesha Ibrahim ufalme wa mbingu na ardhi, na ili awe miongoni mwa wenye yakini.

(76) Na ulipomwingilia usiku aliona nyota, akasema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Na ilipotua, akasema: Siwapendi wanaotua.

(77) Alipouona mwezi unachomoza alisema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Na ulipotua, akasema: Kama Mola Mlezi wangu hataniongoa, basi hakika nitakuwa miongoni mwa kaumu waliopotea.

(78) Na alipoliona jua linachomoza, akasema: Huyu ndiye Mola wangu Mlezi. Huyu ni mkubwa zaidi. Na lilipotua, akasema: Enyi kaumu yangu! Mimi niko mbali na hayo mnayoshirikisha.

(79) Hakika mimi nimeuelekeza uso wangu kwa yule aliyeziumba mbingu na ardhi, kwa unyoofu, wala mimi si miongoni mwa washirikina.

(80) Na kaumu yake wakamhoji. Akasema: Je, mnanihoji kuhusiana na Mwenyezi Mungu, na ilhali Yeye hakika amekwisha niongoa? Wala siogopi hao mnaowashirikisha naye, isipokuwa ikiwa Mola wangu Mlezi akipenda kitu. Mola wangu Mlezi amekusanya elimu ya kila kitu. Basi je, hamkumbuki?

(81) Na vipi nivihofu hivyo mlivyovishirikisha, ilhali nyinyi hamhofu kuwa nyinyi mmemshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu ambacho hakuwateremshia uthibitisho juu yake. Basi ni kundi gani katika mawili haya lina haki zaidi kupata amani, ikiwa nyinyi mnajua?

(82) Wale ambao waliamini, na hawakuchanganya imani yao na dhuluma, hao ndio wana amani, na wao ndio walioongoka.

(83) Na hizo ndizo hoja zetu tulizompa Ibrahim dhidi ya kaumu yake. Tunamnyanyua tumtakaye daraja mbalimbali. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye hekima kubwa, Mwenye kujua yote.

(84) Na tukamtunuku (Ibrahim) Is-haq na Yaakub. Kila mmoja wao tulimwongoa. Na Nuhu tulimwongoa kabla. Na katika kizazi chake tulimwongoa Daud na Suleiman na Ayyub na Yusuf na Musa na Harun. Na hivi ndivyo tunavyowalipa wafanyao mazuri.

(85) Na Zakaria, na Yahya, na Isa, na Ilyas. Kila mmoja wao ni miongoni mwa walio wema.

(86) Na Ismail, na Al-Yasaa, na Yunus, na Lut'. Na kila mmoja wao tulimfadhilisha juu ya walimwengu wote.

(87) Na katika baba zao, na vizazi vyao, na ndugu zao. Na tukawateua na tukawaongoa kwenye njia iliyonyooka.

(88) Huo ni uwongofu wa Mwenyezi Mungu, anaongoa kwao amtakaye katika waja wake. Na lau wangelimshirikisha, basi yangeliwaharibikia yale waliyokuwa wakiyatenda.

(89) Hao ndio tuliowapa Kitabu, na hukumu, na Unabii. Kwa hivyo, ikiwa hawa watayakufuru, basi hakika tumekwisha yawakilisha kwa kaumu wasioyakufuru.

(90) Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoa. Basi fuata uwongofu wao. Sema: Mimi siwaombi ujira wowote juu yake. Haya si isipokuwa ni ukumbusho kwa walimwengu wote.

(91) Na hawakumkadiria Mwenyezi Mungu kwa haki ya kadri yake, waliposema: Mwenyezi Mungu hakumteremshia mwanaadamu chochote. Sema: Nani aliyekiteremsha Kitabu alichokuja nacho Musa, chenye nuru na uwongofu kwa watu, mlichokifanya kurasa kurasa mkizionyesha, na mengi mkiyaficha? Na mkafunzwa mliyokuwa hamyajui nyinyi wala baba zenu? Sema: Mwenyezi Mungu. Kisha waache wacheze katika porojo lao.

(92) a hiki ni Kitabu tulichokiteremsha, kilichobarikiwa, chenye kusadikisha yale yaliyokitangulia, na ili uuonye Mama wa Miji na wale walio pembezoni mwake. Na wale wanaoiamini Akhera wanakiamini, nao wanazihifadhi Swala zao.

(93) Na ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia uwongo Mwenyezi Mungu, au anayesema: Mimi nimeletewa wahyi; na ilhali hakuletewa wahyi wowote. Na yule anayesema: Nitateremsha kama alivyoteremsha Mwenyezi Mungu. Na lau ungeliwaona madhalimu wanapokuwa katika mahangaiko ya mauti, na Malaika wamewanyooshea mikono wakiwambia: Zitoeni roho zenu! Leo mtalipwa adhabu ya kudunisha kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyasema juu ya Mwenyezi Mungu yasiyo ya haki, na mlivyokuwa mkizifanyia kiburi Ishara zake.

(94) Nanyi mlitujia wapweke kama tulivywaumba mara ya kwanza. Na mkayaacha nyuma yenu yote tuliyowapa, na wala hatuwaoni hao waombezi wenu, ambao mlidai kuwa ni washirika wa Mwenyezi Mungu kwenu. Yamekatika mahusiano baina yenu, na yamekupoteeni mliyokuwa mkiyadai.

(95) Hakika Mwenyezi Mungu ndiye mpasuaji nafaka na mbegu za tende, zikachipua. Humtoa aliye hai kutokana na maiti, na mwenye kumtoa maiti kutokana na aliye hai. Huyo ndiye Mwenyezi Mungu. Basi vipi mnadanganywa?

(96) Ndiye anayepambaza mwangaza wa asubuhi; na ameufanya usiku kwa mapumziko, na jua na mwezi kwenda kwa hesabu. Hayo ndiyo makadirio ya Mwenye nguvu kubwa, Mwenye kujua yote.

(97) Na Yeye ndiye aliyewawekea nyota ili mwongoke kwazo katika giza mbalimbali ya bara na bahari. Hakika tumezieleza kwa kina Ishara hizi kwa kaumu wanaojua.

(98) Na Yeye ndiye aliyewazalishia kutokana na nafsi moja. Pako pahali pa kutulia na pa kupita njia. Hakika tumezichambua Ishara hizi kwa watu wanaofahamu.

(99) Na Yeye ndiye aliyeteremsha maji kutoka mbinguni; na kwayo tukatoa mimea ya kila kitu. Na kutokana na baadhi yake tukatoa mimea ya kijani, tukatoa ndani yake punje zilizopandana; na kutokana na mitende katika makole yake yakatoka mashada yaliyo karibu; na mabustani ya mizabibu na mizaituni, na makomamanga, yanayofanana na yasiyofanana. Angalieni matunda yake yanapozaa na yakaiva. Hakika katika hayo kuna Ishara kwa kaumu wanaoamini.

(100) Lakini walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika, majini, ilhali Yeye ndiye aliyewaumba. Na wakamzulia kuwa ana wana wa kiume na wa kike, bila ya kuwa na elimu yoyote. Yeye Ametakasika, na ametukuka juu ya hayo wanayomsifu kwayo!

(101) Yeye ndiye Muumbaji mwanzilishi wa mbingu na ardhi. Vipi awe na mwana, ilhali hakuwa na mke? Naye ndiye aliyeumba kila kitu. Naye ni Mwenye kujua vyema kila kitu.

(102) Huyo ndiye Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi, hapana mungu isipokuwa Yeye, Muumba wa kila kitu. Basi muabuduni Yeye tu. Naye ni Mtegemewa wa kila kitu.

(103) Hazungukwi na macho, naye anayazunguka macho. Naye ni Mjua siri, Mwenye habari zote.

(104) Hakika zimekwishawajia hoja wazi wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo, mwenye kuona, basi ni kwa faida yake mwenyewe. Na mwenye kupofuka, basi ni hasara yake. Wala mimi si mtunzaji wenu.

(105) Na namna hivyo tunazisarifu Aya, na wao wakwambie: Umesoma. Na ili tuyabainishe kwa watu wanaojua.

(106) Fuata yale yaliyofunuliwa kwako kutoka kwa Mola wako Mlezi. Hakuna mungu isipokuwa Yeye. Na jitenge na washirikina.

(107) Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelimshirikisha. Na Sisi hatukukufanya wewe uwe mtunzaji wao. Wala wewe si mlinzi juu yao.

(108) Wala msiwatukane hao ambao wao wanawaomba badala ya Mwenyezi Mungu, nao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao ni kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia yale waliyokuwa wakiyatenda.

(109) Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu viapo vyao vikali zaidi, kuwa ikiwajia Ishara, bila shaka wataiamini. Sema: Hakika Ishara hizo ziko kwa Mwenyezi Mungu. Na ni nini kitawajulisha kuwa zikija, hawataamini?

(110) Na tutazigeuza nyoyo zao na macho yao kama vile hawakuiamini mara ya kwanza. Kisha tutawaacha katika upotovu wao wakitangatanga kwa upofu.

(111) Na lau kuwa tungeliwateremshia Malaika, na maiti wakazungumza nao, na tukawakusanyia kila kitu mbele yao, bado hawakuwa ni wa kuamini, isipokuwa Mwenyezi Mungu atake. Lakini wengi wao wanafanya ujinga.

(112) Na kadhalika tumemfanyia kila Nabii maadui mashetani wa kiwatu, na kijini, wanafundishana wao kwa wao maneno ya kupambapamba, kwa udanganyifu. Na angelipenda Mola wako Mlezi, wasingelifanya hayo. Basi waache na hayo wanayoyazua.

(113) Na ili ziyaelekee hayo nyoyo za wale wasioiamini Akhera, nao wayaridhie, na wayachume yale wanayoyachuma.

(114) Je, nimtafute hakimu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, naye ndiye aliyewateremshia Kitabu hiki kilichoelezwa kwa kina? Na wale tuliowapa Kitabu wanajua ya kwamba kimeteremshwa kutoka kwa Mola wako Mlezi kwa Haki. Basi kamwe usiwe katika wale wanaotia shaka.

(115) Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa ukweli na uadilifu. Hakuna yeyote wa kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.

(116) Na ukiwatii wengi wa hawa waliomo katika dunia, watakupoteza na Njia ya Mwenyezi Mungu. Hawa hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa isipokuwa ni wenye kusema uwongo tu.

(117) Hakika Mola wako Mlezi ndiye Anayejua vyema yule aliyepotea Njia yake, naye ndiye Anayejua vyema wale walioongoka.

(118) Basi kuleni katika yale yaliyotajiwa jina la Mwenyezi Mungu, ikiwa mnaziamini Aya zake.

(119) Na mna nini msile katika yale yaliyotajiwa jina la Mwenyezi Mungu, naye amekwisha wabainishia kwa kina vile alivyowaharimishia, isipokuwa vile mnavyolazimishwa? Na hakika wengi wanapotea kwa matamanio yao bila ya kuwa na elimu. Hakika Mola wako Mlezi ndiye Mwenye kujua vyema wale wanaopindukia mipaka.

(120) Na acheni dhambi iliyo dhahiri na iliyofichikana yake. Hakika wale wanaochuma dhambi watalipwa kwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

(121) Wala msile katika vile ambavyo halikutajwa jina la Mwenyezi Mungu juu yake. Kwani huko hakika ni kuvuka mipaka. Na kwa yakini mashetani wanawaletea wahyi marafiki zao ili wabishane nanyi. Na mkiwatii, basi nyinyi kwa hakika mtakuwa washirikina.

(122) Je, yule aliyekuwa maiti, kisha tukamhuisha, na tukamfanyia nuru akatembea kwayo katika watu, ni kama yule ambaye mfano wake yuko katika giza mbalimbali, sio wa kutoka humo? Kama hivyo ndivyo makafiri walivyopambiwa yale waliyokuwa wakiyafanya.

(123) Na namna hivi tumeweka katika kila mji wakubwa wa wahalifu ili wafanye vitimbi ndani yake. Na wala hawafanyii vitimbi isipokuwa nafsi zao ilhali hawatambui.

(124) Na inapowajia Ishara, wao husema: Hatutaamini mpaka tupewe mfano wa yale waliyopewa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye anayejua zaidi ni wapi anaweka ujumbe wake. Itawafikia wale waliofanya uhalifu udhalili kwa Mwenyezi Mungu, na adhabu kali kwa sababu ya vitimbi walivyokuwa wakivifanya.

(125) Basi yule ambaye Mwenyezi Mungu anataka kumuongoa, humfungulia kifua chake kwa Uislamu. Na yule anayetaka kumpoteza, hukifanya kifua chake kuwa kifinyu, kimebana, kama kwamba anapanda katika mbingu. Namna hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anaweka uchafu juu ya wale wasioamini.

(126) Na hii ndiyo Njia ya Mola wako Mlezi iliyonyooka. Tumeshazieleza Aya kwa kina kwa kaumu wanaokumbuka.

(127) Hao watapata nyumba ya salama kwa Mola Mlezi wao. Naye ndiye Rafiki Mlinzi wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyatenda.

(128) Na ile Siku atakapowakusanya wote, “Enyi kundi la majini! Hakika nyinyi mmechukua wafuasi wengi katika wanadamu.” Na marafiki zao katika wanadamu watasema: Mola Mlezi wetu! Tulinufaishana baadhi yetu kwa wenzi wetu, na tumefikia muda wetu uliotuwekea. Basi Mwenyezi Mungu atasema: Moto ndiyo makazi yenu, mtadumu humo, isipokuwa apendavyo Mwenyezi Mungu. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye hekima kubwa, Mwenye kujua zaidi.

(129) Na namna hivi ndivyo tunavyowafanya baadhi ya madhalimu wapendane wao kwa wao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

(130) Enyi kundi la majini na watu! Je, hawakuwajia Mitume kutokana na nyinyi wenyewe wakiwabainishia Aya zangu, na wakiwasimulia kukutana na Siku yenu hii? Nao watasema, “Tumeshuhudia juu ya nafsi zetu.” Na yaliwadanganya maisha ya dunia. Nao watajishuhudia wenyewe ya kwamba walikuwa makafiri.

(131) Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi hakuwa ni wa kuiangamiza miji kwa dhuluma, hali ya kuwa wenyewe wameghafilika.

(132) Na kila mmoja ana daraja mbalimbali kutokana na yale waliyoyatenda. Na Mola wako Mlezi si mwenye kughafilika na yale wanayoyatenda.

(133) Na Mola wako Mlezi ndiye Asiyemhitaji yeyote, Mwenye rehema. Akitaka, atawaondoa na awaweke nyuma yenu wengine awatakao, kama vile alivyowatoa kutokana na dhuria ya kaumu wengine.

(134) Hakika, yale mnayoahidiwa yatafika, wala nyinyi hamtaweza kushinda.

(135) Sema: Enyi kaumu yangu! Fanyeni pahali penu mlipo, na hakika mimi ninafanya. Mtakuja jua ni ya nani yatakuwa makaazi mema mwishoni. Hakika, madhalimu hawafaulu.

(136) Na walimwekea Mwenyezi Mungu fungu katika mimea na wanyama alioumba, wakasema: Hii ni sehemu ya Mwenyezi Mungu - kwa madai yao - na hii ni ya washirikishwa wetu. Basi vile vilivyokuwa vya washirikishwa wao, havimfikii Mwenyezi Mungu, vile vilivyokuwa vya Mwenyezi Mungu, huwafikia washirikishwa wao. Ni uovu mno hayo wanayoyahukumu.

(137) Na kadhalika hao washirika wao wamewapambia wengi katika washirikina kuwaua watoto wao ili kuwaangamiza na kuwachanganyia dini yao. Na lau kuwa Mwenyezi Mungu angelipenda, wasingelifanya hayo. Basi waache na hayo wanayozua ya uongo.

(138) Nao walisema: "Mifugo hawa na mimea ni miiko. Hawavili isipokuwa tumtakaye" - kwa madai yao tu. Na mifugo wengine imeharimishwa migongo. Na mifugo wengine hawalitaji jina la Mwenyezi Mungu juu yao, kwa kumzulia uongo tu. Atawalipa kwa hayo ya uongo waliyokuwa wakiyazua.

(139) Na walisema: Vile vilivyo katika matumbo ya mifugo hawa ni ya wanaume wetu tu, na vimeharimishwa kwa wake zetu. Lakini wakiwa nyamafu, basi wanashirikiana ndani yake. Atawalipa maelezo yao hayo. Hakika Yeye ni Mwenye hekima kubwa, Mwenye kujua vyema.

(140) Hakika walipata hasara wale waliowaua watoto wao kwa upumbavu bila ya elimu, na wakaharimisha vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu kwa kumzulia Mwenyezi Mungu uongo. Hakika walipotea, wala hawakuwa wenye kuongoka.

(141) Na Yeye ndiye aliyeziumba mabustani yenye kutambaa kwenye fito, na yasiyotambaa kwenye fito, na mitende, na mimea yenye vyakula mbali mbali, na mizaituni na mikomanga inayofanana na isiyofanana. Kuleni katika matunda yake inapozaa, na toeni haki yake siku ya kuvunwa kwake. Wala msitumie kwa kupitiliza. Hakika Yeye hawapendi watumiao kwa kupitiliza.

(142) Na katika mifugo kuna wale wabebao mizigo na kutoa matandiko. Kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu, wala msifuate nyayo za Shetani. Hakika yeye kwenu ni adui wa wazi.

(143) (Amewaumbia) majozi manane: katika kondoo ni wawili, na katika mbuzi ni wawili. Sema: je, ameharimisha madume wawili hawa au majike wawili hawa, au wale waliomo matumboni mwa majike yote mawili haya? Niambieni kwa elimu ikiwa nyinyi ni wakweli.

(144) Na katika ngamia ni wawili, na katika ng'ombe ni wawili. Sema: Je, ameharamisha yote madume wawili au majike wawili, au waliomo matumboni mwa yote majike? Au, nyinyi mlishuhudia Mwenyezi Mungu alipowausia haya? Basi ni nani dhalimu mkubwa kuliko yule aliyemzulia Mwenyezi Mungu uoongo, ili awapoteze watu bila ya elimu? Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu madhalimu.

(145) Sema: Sipati katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilichoharimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa ikiwa ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani huo ni uchafu; au kilichovukiwa mipaka kilichochinjwa kwa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako Mlezi ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.

(146) Na wale waliotubu (yani Mayahudi) tuliwaharamishia kila mwenye kwato au mguu usio na mgawanyiko. Na katika ng'ombe, na kondoo, na mbuzi tuliwaharamishia shahamu yao, isipokuwa ile iliyobeba migongo yao au matumbo yao, au iliyochanganyika na mifupa. Hayo tuliwalipa kwa sababu ya uasi wao. Nasi bila ya shaka ni wakweli.

(147) Na wakikukadhibisha, basi wewe sema: Mola wenu Mlezi ni Mwenye rehema iliyoenea. Wala haizuiwi adhabu yake kwa kaumu wahalifu.

(148) Watasema wale walioshirikisha, "Lau kuwa Mwenyezi Mungu angetaka, tusingelishirikisha, wala baba zetu, wala tusingeliharamisha kitu chochote." Hivyo ndivyo walivyokadhibisha wale waliokuwa kabla yao mpaka walipoionja adhabu yetu. Sema: Je, nyinyi mnayo elimu yoyote mtutolee hiyo? Nyinyi hamfuati isipokuwa dhana. Wala hamfanyi isipokuwa kukisia tu.

(149) Sema: Basi Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye hoja ya kukata. Na kama angelitaka, angeliwaongoa nyote.

(150) Sema: Waleteni mashahidi wenu ambao wanashuhudia kuwa Mwenyezi Mungu amewaharamisha hawa. Kwa hivyo, wakishuhudia, basi wewe usishuhudie pamoja nao. Wala usifuate matamanio ya wale waliozikadhibisha Ishara zetu, na ambao hawaamini katika Akhera, nao wanamlinganisha Mola wao Mlezi na wengine.

(151) Sema: Njooni niwasomee yale aliyowaharimishia Mola wenu Mlezi. Kwamba msimshirikishe Yeye na chochote, na wazazi wawili wafanyieni uzuri, wala msiwauwe watoto wenu kwa sababu ya umasikini. Sisi tunawaruzuku nyinyi na wao. Wala msikaribie machafu, yaliyo dhahiri yake, na yaliyofichikana yake. Wala msiiue nafsi ambayo Mwenyezi Mungu aliiharimisha isipokuwa kwa haki. Hayo aliwausia ili myatie akilini.

(152) Wala msiikaribie mali ya yatima isipokuwa kile kilicho kizuri kabisa mpaka afike utu uzima wake. Na timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu. Hatuibebeshi nafsi isipokuwa kwa uwezo wake. Na mnaposema, basi fanyeni uadilifu hata kama ni jamaa. Na ahadi ya Mwenyezi Mungu,itimizeni. Hayo amewausia ili mkumbuke.

(153) Na kwamba hakika hii ndiyo Njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Wala msifuate njia nyinginezo, zikawatengeni na Njia yake. Haya amewausia ili mmche (Mwenyezi Mungu).

(154) Tena tulimpa Musa Kitabu kwa kumtimizia (neema) yule aliyefanya uzuri, na kuwa ni maelezo kina ya kila kitu, na uwongofu na rehema, ili waamini katika kukutana na Mola wao Mlezi.

(155) Na hiki ni Kitabu tulichokiteremsha, kilichobarikiwa. Basi kifuateni, na mcheni, ili mrehemewe.

(156) Mkaja kusema, “Hakika waliteremshiwa Kitabu makundi mawili tu kabla yetu, na sisi tulikuwa hatuna habari ya waliyokuwa wakiyasoma.”

(157) Au mkasema: "Lau hakika sisi tungeteremshiwa Kitabu hicho, basi tungelikuwa waongofu zaidi kuwaliko wao." Basi hakika imekwisha wajia hoja iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema. Kwa hivyo, ni nani aliye dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule anayekadhibisha Ishara za Mwenyezi Mungu, na akajitenga nazo? Tutawalipa wale wanaojitenga na Ishara zetu adhabu mbaya kabisa kwa sababu ya walivyokuwa wakijitenga.

(158) Je, wanangoja isipokuwa kwamba wajiwe na Malaika, au awajie Mola wako Mlezi, au ziwajie baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi? Siku zitakapowajia baadhi ya Ishara za Mola wako Mlezi, kuamini kwa nafsi hapo hakutaifaa kitu, ikiwa haikuwa imeamini kabla yake, au imefanya heri katika Imani yake. Sema, "Ngojeni, nasi hakika pia ni wenye kungoja."

(159) Hakika wale waliofarakisha Dini yao na wakawa makundi makundi, wewe si miongoni mwao katika chochote. Bila ya shaka jambo lao liko kwa Mwenyezi Mungu; kisha atawajulisha yale waliyokuwa wakiyatenda.

(160) Mwenye kuja na jema, basi ana mara kumi mfano wake. Na mwenye kuja na baya, basi hatalipwa isipokuwa mfano wake. Na wao hawatadhulumiwa.

(161) Sema: Hakika mimi, Mola wangu Mlezi ameniongoa kwenye njia iliyonyooka, dini iliyo sawa kabisa, mila ya Ibrahim aliyekuwa mnyoofu, wala hakuwa miongoni mwa washirikina.

(162) Sema: Hakika Swala yangu, na kuchinja kwangu , na uhai wangu, na kufa kwangu, ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wa walimwengu."

(163) Hana mshirika yeyote. Na hayo ndiyo niliyoamrishwa, na mimi ni wa kwanza wa Waislamu.

(164) Sema: Je nimtafute Mola Mlezi asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ilhali Yeye ndiye Mola Mlezi wa kila kitu? Na wala haichumi kila nafsi isipokuwa ni juu yake. Na wala hatabeba mbeba mzigo, mzigo wa mwingine. Kisha kwa Mola wenu Mlezi ndiyo marejeo yenu, kisha atawajulisha yale mliyokuwa mkihitalifiana ndani yake.

(165) Naye ndiye aliyewafanya kuwa mahalifa katika dunia, na amewanyanyua baadhi yenu juu ya wengine daraja mbalimbali ili awajaribu katika hayo aliyowapa. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kufuta dhambi zaidi, Mwenye kurehemu sana.