(1) Alif Laam Miim Swaad
(2) Kitabu kilichoteremshwa kwako, basi isiwe dhiki yoyote katika kifua chako kwa sababu yake, ili uonye kwacho, na kiwe ni ukumbusho kwa Waumini.
(3) Yafuateni yale yaliyoteremshwa kwenu kutoka kwa Mola wenu Mlezi, wala msifuate marafiki wasaidizi wowote badala yake. Ni machache mnayoyakumbuka.
(4) Na ni miji mingapi tuliyoiangamiza, ikaifikia adhabu yetu usiku au walipokuwa wamelala adhuhuri.
(5) Basi haukuwa mwito wao wakati ilipowajia adhabu yetu, isipokuwa walisema, "Hakika sisi tulikuwa madhalimu."
(6) Na hakika tutawauliza wale waliotumiwa Ujumbe, na pia hakika tutawauliza hao Wajumbe.
(7) Tena hakika tutawasimulia kwa elimu. Wala Sisi si kwamba hatukuwepo.
(8) Na kipimo Siku hiyo kitakuwa kwa haki. Kwa hivyo yule ambaye vipimo vyake vitakuwa vizito, basi hao ndio waliofaulu.
(9) Na yule ambaye vipimo vyake vitakuwa hafifu, basi hao ndio waliozihasirisha nafsi zao kwa sababu ya vile walivyokuwa wakizifanyia Ishara zetu udhalimu.
(10) Na hakika tumewaimarisha katika dunia, na tukawajalia humo njia za kupatia maisha. Ni kidogo tu mnavyoshukuru.
(11) Na hakika tuliwaumba, kisha tukawatia sura, kisha tukawaambia Malaika, "Msujudieni Adam." Basi wakasujudu isipokuwa Iblisi, hakuwa miongoni mwa waliosujudu.
(12) (Mwenyezi Mungu) akasema, "Ni nini kilichokuzuia kusujudu nilipokuamrisha?" Akasema, "Mimi ni bora zaidi kumliko yeye. Uliniumba kwa moto, naye ulimuumba kwa udongo."
(13) Akasema, "Basi teremka kutoka humo! Haikufalii kufanya kiburi humo. Basi toka! Hakika wewe ni miongoni mwa walio duni."
(14) Akasema, "Nipe muhula mpaka siku watakapofufuliwa."
(15) Akasema, "Hakika wewe ni miongoni mwa waliopewa muhula."
(16) Akasema: Kwa kuwa umenipotosha, basi hakika nitawakalia katika Njia yako iliyonyooka.
(17) Kisha nitawajia kwa mbele yao na kwa nyuma yao na kuliani kwao kwote na kushotoni kwao kwote. Wala hutawakuta wengi wao wenye shukrani.
(18) Akasema: Toka humo ilhali umeshutumiwa, umefukuzwa. Hapana shaka atakayekufuata miongoni mwao, basi nitaijaza Jahannam kwa nyinyi nyote.
(19) Na wewe, Adam! Kaa wewe na mkeo Bustanini humo, na kuleni kwayo mpendapo. Wala msiukaribie mti huu, basi mkawa katika madhalimu.
(20) Basi Shetani akawatia wasiwasi ili awafichulie tupu zao walizofichwa, na akasema: hakuwakataza Mola wenu Mlezi mti huu isipokuwa mkaja kuwa Malaika, au mkawa katika wanaoishi milele.
(21) Naye akawaapia: Hakika mimi ni miongoni wa wanaowanasihi.
(22) Basi akawatumbukiza kwa hadaa. Na walipouonja ule mti, tupu zao zikawafichukia na wakaanza kujibandikia katika majani ya Bustani hiyo. Na Mola wao Mlezi akawaita, "Je, sikuwakataza mti huo, na kuwaambia ya kwamba hakika Shetani kwenu ni adui wa dhahiri?"
(23) Wakasema: Mola wetu Mlezi! Tumezidhulumu nafsi zetu, na kama hutatufutia dhambi na ukaturehemu, hakika tutakuwa katika waliohasirika.
(24) Akasema: Teremkeni! Nyinyi kwa nyinyi ni maadui. Nanyi katika ardhi mtakuwa na makao na starehe mpaka ufike muda.
(25) Akasema: Humo mtakuwa hai, na humo mtakufa, na kutoka humo mtatolewa.
(26) Enyi wanadamu! Hakika tumewateremshia vazi la kuficha tupu zenu, na vazi la pambo. Na vazi la uchamungu, hilo ndilo bora zaidi. Hilo ni katika Ishara za Mwenyezi Mungu ili mpate kukumbuka.
(27) Enyi wanadamu! Kamwe Shetani asiwafitini kama alivyowatoa wazazi wenu katika Bustani lile, akawavua vazi lao ili awaonyeshe tupu zao. Hakika yeye anawaona yeye na kabila yake kwa namna ambayo nyinyi hamuwaoni. Hakika Sisi tumewafanya Mashetani kuwa ni marafiki wasaidizi wa wale wasioamini.
(28) Na wanapofanya uchafu, husema: Tuliwakuta baba zetu juu yake, na Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuamrisha hayo. Sema: Hakika Mwenyezi Mungu haamrishi uchafu. Je, mnasema juu ya Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua?
(29) Sema: Mola wangu Mlezi ameamrisha uadilifu, na zielekezeni nyuso zenu kila mnaposujudu, na muombeni Yeye kwa kumfanyia yeye tu Dini. Kama alivyowaanzisha, ndivyo mtakavyorudi.
(30) Kundi moja ameliongoa, na kundi jingine limethibitikiwa na upotovu. Kwa hakika hao waliwafanya mashetani kuwa ndio marafiki walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, na wanadhani kuwa wao wameongoka.
(31) Enyi wanadamu! Chukueni pambo lenu kwenye msikiti, na kuleni, na kunyweni, wala msipitilize. Kwa hakika Yeye hapendi wanaopitiliza.
(32) Sema: Ni nani aliyeharimisha pambo la Mwenyezi Mungu alilowatolea waja wake, na vile vilivyo vizuri katika riziki? Sema: hivyo ni kwa wale walioamini katika uhai wa duniani, na Siku ya Qiyama vitakuwa vyao wao tu. Namna hivyo ndivyo tunavyoeleza Ishara kwa kaumu wanaojua.
(33) Sema: Hakika Mola wangu Mlezi ameharimisha machafu, yaliyodhihiri yake na ya siri, na dhambi, na kuvuka mipaka bila ya haki, na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na ambacho hakukiteremshia uthibitisho wowote, na kusema juu ya Mwenyezi Mungu yale msiyoyajua.
(34) Na kila umma una muda wake. Na unapokuja muda wao, basi hawakawii hata saa moja, wala hawatangulii.
(35) Enyi wanadamu! Watakapowajia Mitume miongoni mwenu wakiwasimulia Ishara zangu, basi mwenye kumcha Mungu na akatengenea, haitakuwa hofu kwao, wala wao hawatahuzunika.
(36) Na wale waliozikadhibisha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hao ndio wenza wa Moto, wao humo watadumu.
(37) Basi ni nani dhalimu zaidi kuliko yule anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, au akazikadhibisha Ishara zake? Hao litawafikia fungu lao waliloandikiwa, mpaka watakapowajia wajumbe wetu kuwafisha, watawaambia: Wako wapi wale mliokuwa mkiwaomba badala ya Mwenyezi Mungu? Watasema: Wametupotea! Na watajishuhudia dhidi yao wenyewe kwamba walikuwa makafiri.
(38) Mwenyezi Mungu atasema: Ingieni (Motoni) pamoja na umma zilizopita kabla yenu miongoni mwa majini na watu. Kila utakapoingia umma, utalaani dada yake. Mpaka watakapokusanyika wote humo, wa mwisho wao atasema juu ya wa mwanzo wao: Mola wetu Mlezi! Hawa ndio waliotupoteza. Basi wape adhabu ya Motoni marudufu. Atasema: Kila mmoja ana marudufu, lakini nyinyi hamjui tu.
(39) Na wa mwanzo wao atamwambia wa mwisho wao: Basi nyinyi pia hamkuwa na ubora wowote kuliko sisi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyachuma.
(40) Hakika wale waliozikadhibisha Ishara zetu na wakazifanyia kiburi, hawatafunguliwa milango ya mbingu, wala hawataingia Bustanini mle mpaka aingie ngamia katika tundu ya sindano. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wahalifu.
(41) Wana kitanda chao katika Jahannamu, na juu yao nguo za moto za kujifunika. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa madhalimu.
(42) Na wale walioamini na wakatenda mema, hatuitwiki nafsi yoyote isipokuwa kwa kiasi cha uwezo wake. Hao ndio wenza wa Bustani ile. Wao watadumu humo.
(43) Na tutaondoa kilicho katika vifua vyao ya chuki, na chini yao itapita mito. Na watasema: Alhamdulillah (kuhimidiwa ni kwa Mwenyezi Mungu), ambaye alituongoa kuyafikia haya. Wala hatukuwa wenye kuongoka wenyewe lau kuwa Mwenyezi Mungu hakutuongoa. Hakika Mitume wa Mola wetu Mlezi walikuja na haki. Na watanadiwa kwamba: Hiyo ndiyo Bustani mliyorithishwa kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyafanya.
(44) Na wenza wa Bustani ile watawanadi wenza Moto kwamba, "Sisi tumeshakuta yale aliyotuahidi Mola wetu Mlezi kuwa ni kweli. Na je, nyinyi pia mmekuta yale aliyowaahidi Mola wenu Mlezi kuwa ni kweli?" Watasema: "Ndiyo!" Basi mtangazaji atatangaza kati yao kwamba, "Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu."
(45) Wale wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu, na wanataka ipotoke, nao wanaikufuru Akhera.
(46) Na baina yao (makundi mawili hayo) patakuwapo pazia. Na juu ya Minyanyuko patakuwa watu watakaomjua kila mmoja kwa alama zao, na wao watawaita watu wa Peponi: Salamu Alaykum (amani iwe juu yenu)! Wao bado hawajaingia humo, lakini wanatumai.
(47) Na yanapogeuzwa macho yao kuelekea watu wa Motoni, watasema: Mola wetu Mlezi! Usitujaalie kuwa pamoja na kaaumu madhalimu.
(48) Na watu hao wa Minyanyukoni watawaita watu wanaowajua kwa alama zao. Watasema: Kujumuika kwenu hakukuwafaa kitu, wala hicho mlichokuwa mnakifanyia kiburi.
(49) Je, hawa ndio wale mliokuwa mkiwaapia kuwa Mwenyezi Mungu hatawafikishia rehema? Ingieni Peponi, hapana hofu kwenu, wala hamtahuzunika!
(50) Na watu wa Motoni watawaita watu wa Peponi: Tumiminieni maji, au chochote alichowaruzuku Mwenyezi Mungu. Nao watasema: Hakika Mwenyezi Mungu ameviharimisha hivyo kwa makafiri.
(51) Ambao waliifanya dini yao kuwa ni pumbao na mchezo, na maisha ya dunia yakawadanganya. Basi leo sisi tunawasahau kama walivyousahau mkutano wa Siku yao hii, na kwa sababu ya kule kuzikataa Ishara zetu.
(52) Na hakika tumewaletea Kitabu tulichokipambanua kwa elimu, uwongofu na rehema kwa watu wenye kuamini.
(53) Je, lipo wanalolingojea isipokuwa matokeo yake? Siku yatatapofika matokeo yake watasema wale waliokisahau: Kweli Mitume wa Mola Mlezi wetu walileta Haki! Je, tunao waombezi ili watuombee? Au turudishwe ili tufanye yasiyokuwa yale tuliyokuwa tukiyafanya? Bila ya shaka wamejihasiri nafsi zao, na yamewapotea waliyokuwa wakiyazua.
(54) Hakika Mola wenu Mlezi ni Mwenyezi Mungu ambaye aliziumba mbingu na ardhi katika siku sita. Kisha akatawala juu ya Kiti cha Enzi. Huufunika usiku kwa mchana, ufuatao upesi upesi. Na jua, na mwezi, na nyota zinazotumika kwa amri yake. Fahamuni! Ni kwake kuumba na amri. Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa baraka, Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(55) Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika Yeye hawapendi wavukao mipaka.
(56) Wala msifanye uharibifu katika dunia baada ya kutengenea kwake. Na mwombeni kwa hofu na kutumai. Hakika rehema ya Mwenyzi Mungu iko karibu na wafanyao uzuri.
(57) Na Yeye ndiye anayetuma pepo (za kuvuma) kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata hizo pepo zinapobeba mawingu mazito, tunayapeleka kwenye nchi iliyokufa. Kisha tunateremsha kwayo maji, na tukatoa kwayo kila aina ya matunda. Basi namna hiyo ndivyo tunavyowafufua wafu, ili mkumbuke.
(58) Na ardhi nzuri hutoka mimea yake kwa idhini ya Mola Mlezi wake. Nayo ardhi ambayo ni mbaya haitoki isipokuwa mimea michache, isiyokuwa na faida, tena kwa shida. Na hivyo ndivyo tunavyozipambanua Ishara (Aya) kwa kaumu wanaoshukuru.
(59) Tulimpeleka Nuhu kwa kaumu yake, naye akasema: Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika mimi ninawahofia adhabu ya Siku iliyo kuu.
(60) Wale watukufu katika kaumu yake wakasema: Hakika sisi tunakuona wewe umo katika upotofu ulio dhahiri.
(61) Akasema: Enyi watu wangu! Mimi simo katika upotofu, lakini mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(62) Nawafikishia Ujumbe wa Mola Mlezi wangu, na ninawanasihi; na ninayajua kwa Mwenyezi Mungu msiyoyajua nyinyi.
(63) Je, mnastaajabu kukujieni mawaidha yanayotoka kwa Mola Mlezi wenu kwa njia ya mtu aliye ni mmoja katika nyinyi, ili akuonyeni na ili mumche Mungu, na ili mpate kurehemewa?
(64) Basi walimkanusha. Nasi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye katika jahazi. Na tukawazamisha wale waliozikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu vipofu.
(65) Na kwa 'Aadi tulimpeleka ndugu yao, Huud. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna mungu ila Yeye. Basi je, hamumchi?
(66) Wakasema watukufu wa wale waliokufuru katika kaumu yake: Sisi tunakuona umo katika upumbavu, na hakika sisi tunakufikiria kuwa wewe ni katika waongo.
(67) Akasema: Enyi watu wangu! Mimi sina upumbavu. Lakini mimi ni Mtume niliyetoka kwa Mola Mlezi wa viumbe vyote.
(68) Nawafikishia ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Na mimi kwenu ni mwenye kuwanasihi, mwaminifu
(69) Mnaona ajabu kukufikieni mawaidha yanayo toka kwa Mola wenu Mlezi kwa mtu aliye mmoja wenu nyinyi ili awaonye? Na kumbukeni alivyo kufanyeni mshike pahala pa kaumu ya Nuhu, na akawazidishia katika umbo. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu ili mpate kufanikiwa.
(70) Wakasema: Je! Umetujia ili tumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu? Basi tuletee hayo unayotuahidi, ukiwa miongoni mwa wasemao kweli.
(71) Akasema: Bila ya shaka adhabu na ghadhabu zimekwisha kuwaangukia kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Mnabishana nami kwa ajili ya majina tu mliyoyaita nyinyi na baba zenu ambayo kwayo Mwenyezi Mungu hakuteremsha uthibitisho? Basi ngojeni, mimi pia ni pamoja nanyi katika wanaongoja
(72) Basi tukamwokoa yeye na waliokuwa pamoja naye kwa rehema zetu, na tukaikata mizizi ya wale waliozikanusha Ishara zetu, na hawakuwa wenye kuamini.
(73) Na kwa Thamud tulimpeleka ndugu yao, Swaleh. Akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Nyinyi hamna Mungu ila Yeye. Hakika imekwisha wafikia Ishara iliyo wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Huyu ni ngamia jike wa Mwenyezi Mungu aliye Ishara kwenu. Basi mwachieni ale kwenye ardhi ya Mwenyezi Mungu, wala msimdhuru, isije kukushukieni adhabu chungu.
(74) Na kumbukeni alivyowafanya wa Makhalifa wa A'adi na akawaweka vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Mwenyezi Mungu wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi.
(75) Waheshimiwa wa kaumu yake wanaojivuna waliwaambia wanaoonewa wenye kuamini miongoni mwao: Je, mnaitakidi ya kwamba Swaleh ametumwa na Mola wake Mlezi? Wakasema: Hakika sisi tunayaamini yale aliyotumwa nayo.
(76) Wakasema wale wanaojivuna: Sisi tunayakataa hayo mnayoyaamini.
(77) Na wakamuua yule ngamia, na wakaiasi amri ya Mola Mlezi wao, na wakasema: Ewe Saleh! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume.
(78) Basi tetemeko la ardhi likawanyakua, na kulipokucha wakawa majumbani mwao kifudifudi wamekwisha kufa.
(79) Basi Swaleh akawaacha na akasema: Enyi watu wangu! Niliwafikishia Ujumbe wa Mola wangu Mlezi, na nikawanasihi, lakini nyinyi hamwapendi wenye nasaha.
(80) Na Lut alipowaambia kaumu yake, "Je, mnafanya uchafu ambao hajawatangulia kwa huo yeyote katika walimwengu?"
(81) Hakika nyinyi mnawaingilia wanaume kwa shahawa na mnawaacha wanawake? Bali nyinyi ni watu wapitilizao!
(82) Na halikuwa jibu la kaumu yake isipokuwa walisema, "Watoeni kutoka katika mji wenu. Maana wao hakika ni watu wanaojitakasa."
(83) Basi tukamwokoa yeye na ahali zake, isipokuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa walioangamia.
(84) Na tukawanyeshea mvua. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wahalifu.
(85) Na kwa (watu wa) Madyana tulimtuma ndugu yao Shu'aib. Akasema, "Enyi kaumu yangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu yeyote isipokuwa Yeye. Hakika imekwisha wajia hoja wazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi timizeni sawasawa vipimo na mizani, wala msiwapunje watu vitu vyao, wala msifanye uharibifu katika ardhi baada ya kutengenea kwake. Hayo ndiyo bora kwenu ikiwa nyinyi ni Waumini.”
(86) Wala msikae katika kila njia mkitishia, na mkiizuia njia ya Mwenyezi Mungu wale waliomuamini, na mkiitaka ipotoke. Na kumbukeni mlipokuwa wachache, naye akawafanya kuwa wengi. Na tazameni jinsi ulivyokuwa mwisho wa waharibifu.
(87) Na kama liko kundi miongoni mwenu lililoamini haya niliyotumwa nayo, na kundi jingine halikuamini, basi subirini mpaka Mwenyezi Mungu ahukumu baina yetu. Naye ndiye Mbora zaidi wa wenye kuhukumu.
(88) Wakasema waheshimiwa waliotakabari katika kaumu yake, "Lazima tutakutoa ewe Shu'aib na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu, au lazima mtarejea katika mila yetu." Akasema, "Je, hata kama tunachukia?"
(89) "Bila ya shaka tutakuwa tumemzulia uwongo Mwenyezi Mungu ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya Mwenyezi Mungu kwisha tuokoa kutokana nayo. Wala haiwi kwetu sisi kuirejea mila hiyo, isipokuwa akitaka Mwenyezi Mungu, Mola wetu Mlezi. Mola wetu Mlezi umekienea kila kitu kwa elimu. Kwa Mwenyezi Mungu tumetegemea. Mola wetu Mlezi, hukumu baina yetu na kaumu yetu kwa haki, nawe ndiwe Mbora zaidi wa wanaohukumu."
(90) Na wakasema waheshimiwa waliokufuru katika kaumu yake, "Mkimfuata Shu'aib, basi hakika nyinyi mtahasiri."
(91) Basi tetemeko la ardhi likawachukua, kwa hivyo wakawa katika makazi yao wameanguka kifudifudi.
(92) Wale waliomkadhibisha Shu'aib ni kama kwamba hawakuishi humo. Wale waliomkadhibisha Shu'aib walikuwa ndio waliohasiri.
(93) Basi akawaachilia mbali na akasema, "Enyi kaumu yangu! Hakika nimewafikishia jumbe za Mola wangu Mlezi, na nimewanasihi. Basi vipi niwahuzunikie kaumu makafiri?"
(94) Na hatukumtuma katika mji wowote Nabii yeyote isipokuwa tuliwachukua wakazi wake kwa umaskini na maradhi ili wanyenyekee.
(95) Kisha tukabadilisha pahali pa ubaya kwa wema, mpaka wakazidi, na wakasema, "Hakika ziliwafikia baba zetu taabu na raha." Basi tukawachukua kwa ghafla hali ya kuwa hawatambui.
(96) Na lau kuwa watu wa miji wangeliamini na wakamcha Mungu, basi hakika tungeliwafungulia baraka za kutoka mbinguni na ardhi. Lakini walikadhibisha, basi tukawachukua kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
(97) Je, wakazi wa vijijini wana amani ya kuwa iwajie adhabu yetu usiku hali ya kuwa wamelala?
(98) Au wakazi wa vijijini wana amani ya kuwa iwajie adhabu yetu mchana hali ya kuwa wanacheza?
(99) Je, wana amani dhidi ya mipango ya Mwenyezi Mungu? Kwani hawawi na amani dhidi ya mipango ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kaumu waliohasiri.
(100) Kwani haijawabainikia wale wanaoirithi ardhi baada ya wale wenyewe kwamba tukitaka tunawasibu kwa madhambi yao, na tukaziba nyoyo zao, kwa hivyo hawatasikia?
(101) Vijiji hivyo, tunakusimulia katika habari zake. Na hakika waliwajia Mitume wao na hoja zilizo waziwazi. Lakini hawakuwa wenye kuamini yale waliyoyakadhibisha zamani. Namna hivi ndivyo Mwenyezi Mungu anavyoziba kwenye nyoyo za makafiri.
(102) Wala hatukuwapata wengi wao wakiwa ni wenye ahadi yoyote, bali kwa hakika tuliwapata wengi wao ni wavukao mno mipaka.
(103) Kisha tukamtuma baada yao Musa na Ishara zetu kwa Firauni na waheshimiwa wake. Nao wakazifanyia dhuluma. Basi tazama namna ulivyokuwa mwisho wa waharibifu.
(104) Na Musa akasema, "Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume kutoka kwa Mola Mlezi wa walimwengu wote "
(105) Inastahiki zaidi juu yangu kwamba nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki tu. Hakika nimewajia na Ishara za waziwazi kutoka kwa Mola wenu Mlezi. Basi waachilie pamoja nami Wana wa Israili.
(106) Akasema (Firauni), "Ikiwa umekuja na ishara yoyote, basi ilete ikiwa wewe ni katika wakweli."
(107) Basi akaitupa fimbo yake, na tazama, ikawa joka lililo dhahiri.
(108) Na akautoa nje mkono wake, na tazama ulikuwa mweupe kwa watazamao.
(109) Wakasema waheshimiwa kutoka katika kaumu ya Firauni, "Hakika huyo ni mchawi ajuaye vyema."
(110) Anataka kuwatoa katika nchi yenu. Basi mnaamrisha nini?
(111) Wakasema: Mwache kidogo yeye na kaka yake, na watume mijini wakusanyaji.
(112) Wakujie na kila mchawi ajuaye vyema.
(113) Na wakamjia wachawi Firauni, wakasema: Hakika tutapata ujira ikiwa tutakuwa sisi ndio washindi.
(114) Akasema: Ndiyo! Nanyi bila ya shaka ni katika waliotiwa karibu nami.
(115) Wakasema: Ewe Musa! Ima utupe wewe, au tuwe sisi ndio watupao?
(116) Akasema: Tupeni! Basi walipotupa, waliyafanyia uchawi macho ya watu na wakawatia hofu, na wakaleta uchawi mkubwa.
(117) Nasi tukamfunulia Musa kumwambia: Itupe fimbo yako, na tazama, ikawa inavimeza vyote vile walivyovizulia uwongo.
(118) Basi haki ikathibiti na yakabatilika yale waliyokuwa wakiyatenda.
(119) Kwa hivyo wakashindwa huko, na wakageuka kuwa wadogo.
(120) Na wachawi wakatupwa chini wakisujudu
(121) Wakasema: Tumemuamini Mola Mlezi wa walimwengu vyote.
(122) Mola Mlezi wa Musa na Haarun.
(123) Akasema Firauni: Mmemuamini kabla mimi kuwapa idhini? Hakika, hii ni njama mliyoipangia huko mjini ili muwatoae humo wenyewe. Basi karibu mtajua!
(124) Lazima nitaikata mikono yenu na miguu yenu kwa kutofautisha. Kisha lazima nitawasulubisha nyote.
(125) Wakasema: Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu Mlezi.
(126) Nawe hutushutumu kwa chuki isipokuwa kwa kuwa tumeziamini Ishara za Mola wetu Mlezi pindi zilipotujia. Ewe Mola wetu Mlezi! Tumiminie subira na utufishe hali ya kuwa ni Waislamu.
(127) Na wakasema waheshimiwa kutoka kwa kaumu ya Firauni: Je, unamuacha Musa na kaumu yake ili wafanye uharibifu katika ardhi na akuache wewe na miungu yako? Akasema: Tutawauaua wavulana wao, na tuwaache hai wanawake wao. Na bila ya shaka sisi ni wenye nguvu juu yao.
(128) Musa akawaambia kaumu yake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu, na subirini. Hakika ardhi ni ya Mwenyezi Mungu, anairithisha amtakaye katika waja wake. Na mwisho mwema ni wa wacha Mungu.
(129) Wakasema: Tumeudhiwa kabla wewe kutujia, na baada ya wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamuangamiza adui wenu, na akawafanya nyinyi ndio wa kufuatia kushika ardhi, ili atazame mtakavyokuja tenda nyinyi.
(130) Na hakika tuliwachukua watu wa Firauni kwa miaka (ya ukame), na kwa upungufu katika mazao, huenda wakakumbuka.
(131) Basi wakijiwa na zuri, wanasema, "Ni haki yetu hii." Na likiwasibu ovu, wanaona mkosi kwa Musa na wale walio pamoja naye. Tazama! Hakika mkosi huo unatoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.
(132) Na walisema, "Hata ukitujia na Ishara yoyote ile kutufanyia uchawi kwazo, basi sisi hatutakuamini."
(133) Basi tukawatumia tufani, na nzige, na chawa, na vyura, na damu, ziwe ni Ishara za kina. Lakini wakatakabari, na wakawa kaumu wahalifu.
(134) Na ilipowaangukia adhabu, wakasema, "Ewe Musa! Tuombee kwa Mola wako Mlezi kwa yale aliyokuahidi. Ukituondolea adhabu hii, hapana shaka tutakuamini, na tutawaachilia Wana wa Israili waende pamoja nawe."
(135) Basi tulipowaondolea adhabu mpaka muda fulani wao waufikie, tazama! Wakavunja ahadi yao.
(136) Basi tukawapatiliza, tukawazamisha katika bahari kwa sababu walizikadhibisha Ishara zetu, na wakawa wanazighafilikia.
(137) Na tukawarithisha kaumu wale waliokuwa wakidhoofishwa, mashariki ya ardhi na magharibi yake ambayo tulibariki ndani yake. Na likatimia neno jema la Mola wako Mlezi juu ya Wana wa Israili, kwa vile walivyosubiri. Na tukayaangamiza yale aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake, na yale waliyokuwa wakiyajenga.
(138) Na tukawavusha bahari Wana wa Israili, kisha wakajia kaumu waliokuwa wanayaabudu masanamu yao. Wakasema, "Ewe Musa! Tufanyie mungu kama hawa walivyo na miungu." Musa akasema: Hakika nyinyi ni kaumu msiojua kitu.
(139) Hakika hawa, haya waliyomo yatakuja angamia, na ni batili hayo waliyokuwa wakiyafanya.
(140) Akasema, "Je, niwatafutie mungu asiyekuwa Mwenyezi Mungu, ilhali Yeye ndiye aliyewafadhilisha juu ya walimwengu wote?"
(141) Na pale tulipowaokoa kutoka kwa watu wa Firauni waliowatia adhabu mbaya zaidi. Wakiwaua wavulana wenu, na wakawaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo yalikuwa majaribio makubwa kutoka kwa Mola wenu Mlezi.
(142) Na tulimuahidi Musa masiku thelathini na tukayatimiza kwa kumi; basi ikatimia miadi ya Mola wake Mlezi masiku arabaini. Na Musa akamwambia kaka yake, Haarun: Shika pahali pangu katika kaumu yangu na utengeneze, wala usifuate njia ya waharibifu.
(143) Na alipokuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamuongelesha, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutaniona. Lakini utazame huo mlima. Ikiwa utabaki mahali pake, basi utaniona. Basi alipojionyesha Mola wake Mlezi kwa mlima huo, akaufanya upasukepasuke, na Musa akaanguka chini akazimia. Basi alipozindukana, akasema: Subhanaka (Umetakasika)! Nimetubia kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.
(144) (Mwenyezi Mungu) akasema: Ewe Musa! Hakika Mimi nilikuteua uende kwa watu na jumbe zangu na maneno yangu. Basi chukua hayo niliyokupa na kuwa katika wanaoshukuru.
(145) Na tukamuandikia kwenye mbao zile katika kila kitu, mawaidha na maelezo ya kina ya kila kitu. (Tukamwambia): Basi yachukue kwa nguvu na uwaamrishe kaumu yako wayachukue kwa ubora wake. Nami nitawaonyesha makazi ya wale waliovuka mipaka.
(146) Nitawaepusha na Ishara zangu wale wanaotakabari katika ardhi bila ya haki. Na wao wakiona kila Ishara, hawaiamini. Wakiiona njia ya uwongofu, hawaichukui kuwa ndiyo njia. Lakini wakiiona njia ya ukengeufu, wanaichukua kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu walizikadhibisha Ishara zetu, na walikuwa wakizighafilikia.
(147) Na wale waliozikadhibisha Ishara zetu na kukutana na Akhera, matendo yao yameharibika. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?
(148) Na kaumu ya Musa wakamfanya baada yake kutoka katika mapambo yao ndama mwenye kiwiliwili, mwenye kutoa mlio wa ng'ombe. Kwani hawakuona kuwa hawasemeshi wala hawaongoi njia yoyote? Walimchukua (kamuabudu), na wakawa madhalimu.
(149) Na wakati mambo yalipoangushwa katika mikono yao, na wakaona ya kwamba wamekwisha potea, wakasema: Ikiwa Mola wetu Mlezi hataturehemu na akatufutia dhambi, basi bila ya shaka tutakuwa miongoni mwa waliohasiri.
(150) Na wakati aliporudi Musa kwa kaumu yake hali ya kuwa ameghadhibika na kuhuzunika, akasema: Ni mabaya mno mliyonifanyia nyuma yangu! Je, mmeiharakisha amri ya Mola wenu Mlezi? Na akazitupa chini mbao zile, na akamkamata kaka yake kichwa akimvuta kwake. (Haarun) akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Hakika kaumu hawa waliniona kuwa mimi ni dhaifu, na walikaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui zangu, wala usinifanye pamoja na kaumu madhalimu.
(151) (Musa) akasema: Mola wangu Mlezi! Nifutie dhambi mimi na kaka yangu, na utuingize katika rehema yako. Nawe ni Mwenye kurehemu zaidi kuliko wote wenye kurehemu.
(152) Hakika wale waliojifanyia (na kumuabudu) ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao Mlezi, na udhalilifu katika maisha ya dunia. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazuao uongo.
(153) Na wale waliotenda mabaya, kisha wakatubia baada yake na wakaamini, hakika Mola wako Mlezi baada ya hayo ni Mwenye kufuta dhambi, Mwenye kurehemu.
(154) Na wakati ghadhabu ilipomtulia Musa, akazichukua mbao zile. Na katika maandiko yake kuna uwongofu na rehema kwa wale ambao wao wanaomhofu Mola wao Mlezi.
(155) Na Musa akawateua kaumu wake wanaume sabiini kwa ajili ya miadi yetu. Na ulipowachukua mtetemeko mkubwa, akasema: Mola wangu Mlezi! Ungelitaka, ungeliwaangamiza wao hapo kabla na hata mimi. Unatuangamiza kwa yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi? Haya si chochote isipokuwa ni majaribio yako, unampoteza kwayo umtakaye, na umuongoa umtakaye. Wewe ndiye rafiki mlinzi wetu. Basi tusitiri dhambi na uturehemu. Na Wewe ndiwe Mbora zaidi wa wasitirio dhambi.
(156) Na tuandikie mazuri katika dunia hii na katika Akhera. Hakika sisi tumerejea kwako. (Mwenyezi Mungu) akasema: Adhabu yangu nitamsibu kwayo nimtakaye. Na rehema yangu imeenea kila kitu. Basi nitaiandika hii hasa kwa wale wanaomcha Mungu, na wanaotoa Zaka, na wale ambao wanaziamini Ishara zetu.
(157) Wale ambao wanamfuata huyo Mtume, Nabii, asiyesoma wala kuandika, ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili, anayewaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawahalalishia vizuri, na anawaharimishia viovu, na anawaondolea mizigo yao na minyororo ambayo ilikuwa juu yao. Basi wale waliomwamini yeye, na wakampa taadhima, na wakamnusuru, na wakaifuata nuru ambayo iliteremshwa pamoja naye, hao ndio waliofaulu.
(158) Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote, Yeye ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi. Hapana mungu isipokuwa Yeye. anahuisha na anafisha. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Nabii asiyejua kusoma na kuandika, ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni yeye ili muongoke.
(159) Na katika kaumu ya Musa upo umma unaowaongoa watu kwa haki, na kwayo wanafanya uadilifu.
(160) Na tukawakatakata makabila kumi na mawili, mataifa mbali mbali. Na tulimfunulia Musa wakati kaumu yake walipomwomba maji kwamba: Lipige hilo jiwe kwa fimbo yako. Mara zikabubujika kutoka humo chemchemi kumi na mbili, na kila watu wakajua pahali pao pa kunywea. Na tukawafunika kivuli kwa mawingu, na tukawateremshia Manna na Salwa. Kuleni katika vizuri hivi tulivyowaruzuku. Na hawakutudhulumu Sisi, bali walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
(161) Na pale walipoambiwa: Ukaeni mji huu, na mle humo popote mpendapo, na semeni: Tufutie dhambi zetu. Na uingieni mlango wake kwa kusujudu, tutawasitiria makosa yenu. Walio wema tutawazidishia.
(162) Lakini wakabadilisha wale waliodhulumu miongoni mwao kauli isiyo ile waliyoambiwa. Basi tukawatumia adhabu kutoka mbinguni kwa vile walivyokuwa wakidhulumu.
(163) Na waulize kuhusu kijiji kilichokuwa kando ya bahari, walipokuwa wakiivunja Sabato (Jumaamosi ya mapumziko). Walipokuwa samaki wakiwajia juu juu siku ya Sabato, na siku isiyokuwa ya Sabato hawawajii. Kwa namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakivuka mipaka.
(164) Na kikundi miongoni mwao walisema: Kwa nini mnawawaidhi watu ambao tangu hapo Mwenyezi Mungu atawaangamiza au atawaadhibu adhabu kali? Wakasema: Ili uwe ni udhuru kwa Mola wenu Mlezi, na huenda nao wakamcha Mungu.
(165) Basi walipoyasahau yale waliyokumbushwa kwayo, tukawaokoa wale waliokuwa wakikataza mabaya, na tukawachukua wale waliodhulumu kwa adhabu mbaya mno kwa vile walivyokuwa wakivuka mipaka.
(166) Walipotakabari na kuasi yale waliyokatazwa, tukawaambia, "Kuweni manyani, mliodharauliwa."
(167) Na wakati alipotangaza Mola wako Mlezi kwamba hakika atawatumia dhiki yao hadi Siku ya Qiyama mwenye kuwaadhibu kwa adhabu mbaya sana. Hakika Mola wako Mlezi ni Mwepesi wa kuadhibu, na hakika Yeye ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu sana.
(168) Na tukawagawanya katika ardhi umma umma. Miongoni mwao kuna wale walio wema, na miongoni mwao kuna walio kinyume cha hivyo. Na tukawajaribu kwa mazuri na mabaya huenda wakarejea.
(169) Basi wakafuatia baada yao wafuatizi waliokirithi Kitabu. Wanachukua anasa za haya maisha duni, na wanasema, "Tutasitiriwa dhambi!" Na ikiwajia tena anasa mfano wake, wanaichukua pia. Je, halikuchukuliwa juu yao agano la Kitabu kuwa wasiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki tu? Nao wamekwishasoma yale yaliyomo humo. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi kwa wachao. Basi je, hamtii akilini?
(170) Na wale wanaokikamata sawasawa Kitabu, na wakasimamisha Swala, hakika Sisi hatupotezi ujira wa watengenezao.
(171) Na pale tulipounyanyua mlima juu yao ukawa kama kwamba ni kiwingu kilichowafunika, na wakadhani kuwa utawaangukia, (tukawaambia): Chukueni yale tuliyowapa kwa nguvu, na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mche.
(172) Na pale Mola wako Mlezi alipochukua kutoka kwa wanadamu kutoka katika migongo yao dhuria zao na akawashuhudisha juu ya nafsi zao (na kuwaambia), "Je, mimi si Mola wenu Mlezi?" Wakasema, "Ndiyo, tumeshuhudia." Mje mkasema Siku ya Qiyama, "Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika na haya."
(173) Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha kabla yetu, na sisi ni dhuriya zao tu baada yao. Basi utatuangamiza kwa sababu ya waliyoyafanya wapotovu?
(174) Na ndiyo kama hivyo tunavyozieleza Ishara kwa kina, ili huenda wakarejea.
(175) Na wasomee habari za yule ambaye tulimpa Ishara zetu, naye akajivua kutoka kwazo, basi Shetani akamfuata. Kwa hivyo, akawa miongoni mwa waliopotea.
(176) Na lau kuwa tungelitaka, tungelimwinua kwazo, lakini yeye alizama katika ulimwengu na akafuata matamanio yake. Basi mfano wake ni kama mfano wa mbwa. Ukimhujumu hupumua na kutoa ulimi nje, na ukimwacha, pia hupumua na kutoa ulimi nje. Huo ni mfano wa kaumu ambao walizikadhibisha Ishara zetu. Basi simulia hadithi, huenda wakatafakari.
(177) Mfano mbaya zaidi ni wa kaumu waliozikadhibisha Ishara zetu na walikuwa wakizidhulumu nafsi zao.
(178) Yule ambaye Mwenyezi Mungu amemuongoa, basi huyo ndiye mwongofu. Na yule aliyempoteza, basi hao ndio waliohasiri.
(179) Na hakika tumeiumbia Jahannamu wengi katika majini na watu. Wana nyoyo wasizofahamu kwazo. Na wana macho wasiyoona kwayo. Na wana masikio wasiyosikia kwayo. Hao ni kama wanyama wa mifugo, bali wao ni wapotofu zaidi. Hao ndio walioghafilika.
(180) Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri kabisa, basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopindukia mipaka katika majina yake. Watakuja lipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.
(181) Na katika wale tuliowaumba wako umma wanaoongoza kwa haki, na kwayo wanafanya uadilifu.
(182) Na wale waliokadhibisha Ishara zetu, tutawapeleka katika maangamio pole pole kutokea pale wasipojua.
(183) Nami nitawapa muda. Hakika njama yangu ni madhubuti.
(184) Je, hawafikirii? Huyu mwenzao hana wazimu. Yeye siyo isipokuwa ni mwonyaji aliye dhahiri.
(185) Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi, na vile vyote alivyoviumba Mwenyezi Mungu katika vitu, na kwamba huenda muda wao umekwisha karibia? Basi maneno gani baada ya haya watayaamini?
(186) Yule Mwenyezi Mungu alimpoteza, basi hana wa kumwongoa. Atawaacha hao katika upotovu wao wakitangatanga.
(187) Wanakuuliza kuhusu hiyo Saa (ya Qiyama) kusimama kwake ni lini? Sema: Elimu yake iko kwa Mola wangu Mlezi. Haidhihirishi hiyo kwa wakati wake isipokuwa Yeye. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitawajia isipokuwa kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama kwamba wewe una pupa ya kuijua. Sema: Elimu yake iko tu kwa Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wa watu hawajui.
(188) Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara, isipokuwa apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu, ningalitenda mema sana, wala ubaya usingenigusa. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mbashiri kwa kaumu wanaoamini.
(189) Yeye ndiye aliyewaumba kutoka katika nafsi moja; na katika hiyo hiyo akamfanya mwenzi wake, ili ajitulize kwake. Na alipomuingilia, akabeba mimba nyepesi, akitembea nao. Anapokuwa mjamzito, wote wawili humwomba Mwenyezi Mungu, Mola wao Mlezi: Kama ukitupa mwana mwema hakika tutakuwa katika wanaoshukuru.
(190) Basi alipowapa mwana mwema, wakamfanyia washirikina Mwenyezi Mungu katika kile kile alichowapa. Basi Mwenyezi Mungu ametukuka na huko kushirikisha kwao.
(191) Ati wanashirikisha kisichoumba kitu, hali ya kuwa wao wanaumbwa?
(192) Wala hawawezi kuwanusuru wala wao wenyewe hawajinusuru.
(193) Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawawafuati. Ni mamoja kwenu ikiwa mtawaita au mkae kimya.
(194) Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu nyinyi. Basi waombeni, nao wawaitikie ikiwa nyinyi ni wakweli.
(195) Je, wao wanayo miguu wanayotembea kwayo? Au wanayo mikono wanayokamata kwa nguvu kwayo? Au wanayo macho wanayoona kwayo? Au wanayo wanayosikia kwayo? Sema: Waiteni washirika wenu hao, kisha nifanyieni mimi njama, na wala msinipe muhula.
(196) Hakika Mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu ambaye aliteremsha Kitabu. Naye ndiye anayewalinda walio wema.
(197) Na wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi hawawezi kuwanusuru, wala hawajinusuru wao wenyewe.
(198) Na mkiwaita kwenye uwongofu, hawasikii. Na utawaona wanakutazama hali ya kuwa hawaoni.
(199) Chukua yaliyo mepesi (katika matendo yao), na amrisha mema, na jitenge na majahili.
(200) Na kama uchochezi kutoka kwa Shetani utakuchochea, basi tafuta ulinzi wa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Msikizi mzuri, Mwenye kujua vyema.
(201) Hakika wale wamchao Mungu, zinapowagusa pepesi kutoka kwa Shetani, mara huzindukana na hapo huwa wenye kuiona haki.
(202) Na ndugu zao wanawavuta kwenye upotovu, kisha wao hawaachi.
(203) Na usipowajia na Ishara, wanasema: Kwa nini hukuibuni? Sema: hakika mimi ninafuata tu yale yanayofunuliwa kwangu kutoka kwa Mola wangu Mlezi. Hii (Qur'ani) ni hoja zinazotoka kwa Mola wenu Mlezi, na uwongofu, na rehema kwa kaumu wanaoamini.
(204) Na inaposomwa Qur-ani, basi isikilizeni na mnyamaze ili mrehemewe.
(205) Na mkumbuke Mola wako Mlezi katika nafsi yako kwa unyenyekevu na hofu, na bila ya kuinua sauti juu kwa kauli, asubuhi na jioni, wala usiwe miongoni wa walioghafilika.
(206) Hakika wale walio kwa Mola wako Mlezi hawajivuni wakaacha kumuabdu, na wanamtakasa, na wanamsujudia Yeye.