(1) Wanakuuliza juu ya Ngawira. Sema: Ngawira ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na suluhisheni mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni Waumini.
(2) Hakika Waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu, nyoyo zao zinaingia hofu. Na wanaposomewa Aya zake, zinawazidishia Imani, na kwa Mola wao Mlezi wakamtegemea.
(3) Wale wanaosimamisha Swala, na wanatoa katika yale tunayowaruzuku.
(4) Hao ndio Waumini wa uhakika. Wana vyeo kwa Mola wao Mlezi, na kusitiriwa dhambi, na riziki tukufu.
(5) Kama alivyokutoa Mola wako Mlezi katika nyumba yako kwa haki, na hakika kundi moja katika Waumini linachukia.
(6) Wanakujadili kuhusu haki baada ya kwisha bainika, kama kwamba wanasukumwa kwenye mauti hali ya kuwa wanatazama.
(7) Na Mwenyezi Mungu alipowaahidi moja ya vikundi vile viwili kuwa ni chenu. Nanyi mkapenda kwamba kile kisichokuwa kikali ndicho kiwe chenu. Naye Mwenyezi Mungu anataka ahakikishe haki kwa maneno yake, na aikate mizizi ya makafiri.
(8) Ili aihakikishe haki na aibatilishe batili hata kama watachukia wahalifu.
(9) Mlipokuwa mnamuomba msaada Mola wenu Mlezi, naye akawaitikia kuwa Mimi hakika nitawasaidia kwa elfu moja miongoni mwa Malaika wakifuatana mfululizo.
(10) Na Mwenyezi Mungu hakufanya hayo isipokuwa yawe ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na nusura haiwi isipokuwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(11) Alipowafunika kwa usingizi uwe ni amani kutoka kwake, na akawateremshia maji kutoka mbinguni ili awasafishe kwayo na awaondolee uchafu wa Shetani, na ili azifunge nyoyo zenu, na aimarishe kwayo miguu yenu.
(12) Mola wako Mlezi alipowafunulia Malaika: Hakika Mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini. Nitatupa uoga katika nyoyo za wale waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.
(13) Hayo ni kwa sababu walimuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
(14) Ndivyo hivyo! Basi ionjeni! Na bila ya shaka makafiri wana adhabu ya Moto.
(15) Enyi Mlioamini! Mnapokutana na wale waliokufuru vitani, msiwageuzie migongo.
(16) Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo, isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi, basi hakika atakuwa amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu. Na pahali pake ni Jahannam, na huo ni mwisho muovu.
(17) Kwa hivyo, hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua. Nawe hukutupa ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, na ili awajaribu Waumini majaribio mazuri kutoka kwake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.
(18) Hayo! Na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kudhoofisha njama za makafiri.
(19) Mkiomba msaada wa ushindi, basi msaada wa ushindi ulikwisha wajia. Na mkikomeka, basi hilo ndilo heri kwenu. Na mkirejea, Sisi pia tutarejea. Na kundi lenu halitawanufaisha kitu hata kama yatakuwa mengi. Kwani hakika Mwenyezi yu pamoja na Waumini.
(20) Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msigeuke mkamuacha hali ya kuwa mnasikia.
(21) ala msiwe kama wale wanaosema, "Tumesikia" na hali hawasikii.
(22) Hakika waovu mno wa wanyama wote mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale viziwi, na mabubu wasiotumia akili zao.
(23) Na Mwenyezi Mungu angelijua heri yoyote ndani yao, angewasikilizisha, na lau angewasikilizisha, wangeligeuka hali ya kuwa wamepuuza.
(24) Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaitia yale yenye kuwahuisha. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huizuia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba hakika kwake Yeye mtakusanywa.
(25) Na jikingeni na mtihani ambao hautawasibu wale waliodhulumu pekee miongoni mwenu. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu.
(26) Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkidhoofishwa katika ardhi, mkiogopa kwamba watu watawanyakua, naye akawapa pahali pazuri pa kukaa, na akawaunga mkono kwa nusura yake, na akawaruzuku katika vilivyo vizuri ili mshukuru.
(27) Enyi mlioamini! Msimhini Mwenyezi Mungu na Mtume, na mkahini amana zenu, hali ya kuwa mnajua.
(28) Na jueni ya kwamba mali zenu na wana wenu ni mtihani, na kwamba Mwenyezi Mungu ana ujira mkubwa kwake.
(29) Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu, atawapa kipambanuo, na atawasitiria mabaya yenu,na awafutie dhambi, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye fadhila kubwa.
(30) Na walipokupangia vitimbi wale waliokufuru ili wakufunge, au wakuue, au wakutoe. Na wakapanga vitimbi vyao, naye Mwenyezi Mungu akapanga vitimbi vyake. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora wa wapangao vitimbi.
(31) Na wanaposomewa Aya zetu, wao husema: Hakika tumesikia. Lau tungetaka, tungesema mfano wa haya. Haya si chochote isipokuwa ngano za wa mwanzo.
(32) Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ndiyo haki kutoka kwako, basi tunyeshee mawe kutoka mbinguni, au tujie na adhabu yoyote iliyo chungu.
(33) Na Mwenyezi Mungu hakuwa wa kuwaadhibu hali ya kuwa uko miongoni mwao, na Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwaadhibu hali ya kuwa wanaomba kusitiriwa dhambi.
(34) Lakini wana nini hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu, na hali ya kuwa wanawazuilia watu Msikiti Mtakatifu, wala wao hawakuwa ndio walinzi wake? Bali walinzi wake si isipokuwa wachamungu tu, lakini wengi wao hawajui.
(35) Na hakukuwa kuswalia kwao kwenye hiyo Nyumba (Al-Kaaba) isipokuwa ni kupiga miunzi na makofi. Basi onjeni adhabu kwa vile mlivyokuwa mkikufuru.
(36) Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili waizuilie Njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam.
(37) Ili Mwenyezi Mungu awapambanue waovu kutokana na wazuri, na awaweke waovu juu ya waovu wengine, na awarundike wote pamoja, na awatie katika Jahannam. Hao ndio waliohasirika.
(38) Waambie wale waliokufuru ikiwa watakoma, watasitiriwa yale yaliyokwisha pita. Na wakiyarudia, basi hakika imekwisha pita mifano ya wa mwanzo.
(39) Na piganeni nao mpaka kusiwepo majaribio na Dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Lakini wakiacha, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayayatenda.
(40) Na kama wakigeuka basi jueni kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola Mwema na Msaidizi Mwema.
(41) Na jueni ya kwamba ngawira yoyote mnayoipata, basi humusi yake ni ya Mwenyezi Mungu na ni ya Mtume, na ni ya jamaa, na mayatima, na masikini, na wasafiri, ikiwa nyinyi mlimwamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyoyateremsha kwa mja wetu siku ya kipambanuo, siku yalipokutana makundi yale mawili. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(42) Kumbukeni pale mlipokuwa nyinyi kwenye ng'ambo ya karibu ya bonde, na wao wakawa kwenye ng'ambo ya mbali, na msafara ulipokuwa chini yenu. Na ingelikuwa mliagana, basi mngelihitalifiana katika miadi. Lakini (mkakutana) ili Mwenyezi Mungu atimize jambo liliokuwa lazima litendwe. Ili aangamie wa kuangamia kwa ushahidi ulio wazi, na asalimike wa kusalimika kwa ushahidi ulio wazi. Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.
(43) Kumbuka Mwenyezi Mungu alipokuonyesha wao katika usingizi wako kwamba wao ni wachache, na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi, basi mngeliingiwa na woga, na mngelizozana katika jambo hilo. Lakini Mwenyezi Mungu akawapa salama. Hakika Yeye ni Mwenye kuyajua vyema yaliyo vifuani.
(44) Na alipowaonyesha mlipokutana, katika macho yenu kuwa wao ni wachache, na akawafanya nyinyi ni wachache katika macho yao, ili Mwenyezi Mungu atimize jambo lililokuwa lifanywe. Na kwa Mwenyezi Mungu yatarejeshwa mambo yote.
(45) Enyi mlioamini! Mkikutana na kikundi, basi kueni imara, na mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana ili mfaulu.
(46) Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msizozane mkaingiwa woga, na zikapotea nguvu zenu. Na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaosubiri.
(47) Wala msiwe kama wale waliotoka katika majumba yao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na wakiwazuilia watu Njia ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka yote wanayoyafanya.
(48) Na wakati Shetani alipowapambia vitendo vyao, na akasema, "Hakuna yeyote wa kuwashinda leo hii katika watu, nami hakika ni mlinzi wenu." Basi yalipoonana makundi mawili hayo, akarudi nyuma juu ya visigino vyake, na akasema, "Hakika mimi niko mbali sana nanyi. Hakika mimi naona msiyoyaona. Hakika mimi ninamhofu Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu."
(49) Waliposema wanafiki, na wale wenye ugonjwa katika nyoyo zao, "Watu hawa dini yao imewadanganya." Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(50) Na laiti ungeliona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakiwapiga nyuso zao na migongo yao, (na kuwaambia), "Ionjeni adhabu iunguzayo!"
(51) Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyotangulizwa na mikono yenu, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.
(52) Kama ada ya watu wa Firauni na wale waliokuwa kabla yao, walizikufuru Ishara za Mwenyezi Mungu. Basi Mwenyezi Mungu akawachukua kwa madhambi yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mkali wa kuadhibu.
(53) Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu hakuwa ni wa kuibadilisha neema aliyowaneemesha kwayo kaumu, mpaka wao wabadilishe yale yaliyoko katika nafsi zao, na kwamba hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.
(54) Ni kama ada ya watu wa Firauni na wale walio kabla yao, walizikadhibisha Ishara za Mola wao Mlezi, basi tukawaangamiza kwa madhambi yao, na tukawazamisha watu wa Firauni. Na kila mmoja wao walikuwa madhalimu.
(55) Hakika waovu zaidi ya wanyama wote mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale waliokufuru, basi hao hawaamini.
(56) Wale ambao miongoni mwao ulifanya agano nao, kisha wanavunja agano lao katika kila mara, wala wao hawamchi Mungu.
(57) Kwa hivyo, ukiwakuta katika vita, basi wakimbize kwa hawa wale walio nyuma yao ili wapate kukumbuka.
(58) Na ukichelea hiana kwa kaumu fulani, basi watupilie ahadi yao kwa usawa. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wahaini.
(59) Wala kamwe wasidhanie wale waliokufuru kwamba wao wametangulia mbele. Hakika, wao hawatashinda.
(60) Na waandalieni muwezavyo katika nguvu, na kwa farasi waliofungwa tayari tayari, ili muwatie hofu kwavyo maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu, na wengineo kando na hao ambao hamwajui, lakini Mwenyezi Mungu anawajua. Na mnachotoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mtarudishiwa kikamilifu, nanyi hamtadhulumiwa.
(61) Na wakiielekea amani, basi nawe pia ielekee, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ndiye Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.
(62) Na wakitaka kukufanyia hiana, basi hakika Mwenyezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndiye aliyekuunga mkono kwa nusura yake, na kwa Waumini.
(63) Na akaziunga pamoja nyoyo zao. Lau wewe ungelitoa vyote vilivyo katika dunia, usingeliweza kuziunga pamoja nyoyo zao, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaunganisha. Hakika Yeye ndiye Mwenye nguvu, Mwenye hekima kubwa.
(64) Ewe Nabii! Mwenyezi Mungu anakutosha wewe na mwenye kukufuata miongoni mwa Waumini.
(65) Ewe Nabii! Wahimize Waumini juu ya kupigana vita. Wakiwapo miongoni mwenu ishirini wanaosubiri, watawashinda mia mbili. Na wakiwapo miongoni mwenu mia, watawashinda elfu moja katika wale waliokufuru, kwa sababu wao ni kaumu wasiofahamu.
(66) Sasa Mwenyezi Mungu amewapunguzia, na alijua kuwa ndani yenu upo udhaifu. Kwa hivyo, wakiwapo watu mia moja miongoni mwenu wenye kusubiri, watawashinda mia mbili. Na wakiwapo elfu moja, watawashinda elfu mbili, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye kusubiri.
(67) Haikuwa kwa Nabii yeyote kwamba awe na mateka, mpaka awe ameshinda sawasawa katika ardhi. Mnataka vitu vya dunia, na Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima kubwa.
(68) Lau lisingelikuwa andiko lililokwisha tangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ingewagusa adhabu kubwa kwa vile mlivyochukua.
(69) Basi kuleni katika mlivyoteka, ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(70) Ewe Nabii! Waambie wale walio katika mikono yenu miongoni mwa mateka: Kama Mwenyezi akijua heri yoyote katika nyoyo zenu, atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kutoka kwenu, na atawasitiria dhambi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(71) Na ikiwa wanataka kukufanyia hiana, basi hakika walikwisha mfanyia hiana Mwenyezi Mungu kabla, naye akawawezesha nyinyi kuwashinda. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.
(72) Hakika wale walioamini na wakahama na wakaipigania Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, na wale waliotoa pahali pa kukaa, na wakanusuru, hao ni marafiki na walinzi wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhama, nyinyi hamna wajibu wa ulinzi kwao hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiomba msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa juu ya kaumu ambao lipo agano baina yenu na wao. Na Mwenyezi Mungu anayaona vyema yale mnayoyatenda.
(73) Na wale waliokufuru ni marafiki wenyewe kwa wenyewe. Msipofanya hivi, itakuwepo fitina katika ardhi na uharibifu mkubwa.
(74) Na wale walioamini, na wakahama, na wakapigana Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wale waliotoa pahali pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Wana kusitiriwa dhambi na riziki njema.
(75) Na wale walioamini baadaye, na wakahama, na wakapigana Jihadi pamoja nanyi, basi hao ni miongoni mwenu. Na jamaa wa nasaba wanastahikiana zaidi wenyewe kwa wenyewe katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika, Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua kila kitu.