(1) [Huku ni] kujiweka mbali kutokako kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kunawaendea wale mlioagana nao miongoni mwa washirikina.
(2) Basi tembeeni katika ardhi miezi minne, na jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu atawahizi makafiri.
(3) Na ni tangazo kutoka kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwaendea watu wote siku ya Hija Kubwa kwamba Mwenyezi Mungu yuko mbali na washirikina, na Mtume wake wake pia yuko mbali. Kwa hivyo, mkitubu, basi hilo ndilo heri kwenu. Na mkigeuka, basi jueni kuwa nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu. Na wabashirie wale waliokufuru adhabu chungu.
(4) Isipokuwa wale mlioahidiana nao katika washirikina, kisha hawakuwapunguza chochote, wala hawakumsaidia yeyote dhidi yenu. Basi hao watimizieni ahadi yao mpaka muda wao. Hakika, Mwenyezi Mungu huwapenda wachamungu.
(5) Na ikiisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote muwakutapo, na wachukueni na wazingireni, na wavizieni katika kila njia. Lakini wakitubu, na wakashika Sala, na wakatoa Zaka, basi waachilieni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(6) Na ikiwa yeyote miongoni mwa washirikina atakuomba ulinzi, basi mpe ulinzi ili apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Kisha mfikishe pahali pake pa amani. Haya ni kwa kuwa hao ni kaumu wasiojua kitu.
(7) Vipi washirikina watakuwa na agano kwa Mwenyezi Mungu na kwa Mtume wake, isipokuwa wale mliofanya agano nao kwenye Msikiti Mtakatifu? Basi maadamu watawawia wanyoofu, basi nanyi pia wawieni wanyoofu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wachamungu.
(8) Vipi, na wakiwa na ushindi dhidi yenu, hawachungi kwenu udugu wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, lakini nyoyo zao zinakataa hayo. Na wengi wao ni wavukao mipaka.
(9) Walinunua Ishara za Mwenyezi Mungu kwa thamani chache, kwa hivyo wakaizuilia njia yake. Hakika hao ni maovu waliyokuwa wakiyatenda.
(10) Hawachungi kwa Muumini udugu wala ahadi. Basi hao ndio wapindukiao mipaka.
(11) Kwa hivyo wakitubu, na wakasimamisha Sala, na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika Dini. Na tunazipambanua Aya kwa kaumu wanaojua.
(12) Na wakivunja viapo vyao baada ya agano lao, na wakaitia dosari Dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri. Hakika hao hawana viapo vya kweli. Huenda (kwa hayo) wakaacha.
(13) Je, hampigani na kaumu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume, nao ndio waliowaanza mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mmwogope, ikiwa nyinyi ni Waumini.
(14) Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awahizi na awanusuru dhidi yao, na aviponye vifua vya kaumu ya Waumini.
(15) Na aondoe hasira ya nyoyo zao. Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima kubwa.
(16) Je, mlidhani kuwa mtaachwa tu, na Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliopigana Jihadi miongoni mwenu, na wala hawakumfanya yeyote mwendani wao isipokuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Waumini wenziwe? Na Mwenyezi Mungu anazo habari za yote mnayoyatenda.
(17) Haikuwa kwa washirikina kwamba waiimarishe misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali ya kuwa wanazishuhudia nafsi zao wenyewe ukafiri. Hao matendo yao yaliharibika, na katika Moto wao watadumu.
(18) Hakika anayeimarisha tu misikiti ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemwamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na akasimamisha Sala, na akatoa Zaka, na wala hakumnyenyekea isipokuwa Mwenyezi Mungu. Basi huenda hao wakawa katika waongofu.
(19) Je, mnafanya kuwanywesha maji Mahujaji na kuimarisha Msikiti Mtakatifu ni sawa na mwenye kumuamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na akafanya Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu dhalimu.
(20) Wale walioamini, na wakahama, na wakafanya Jihadi katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, hao wana daraja kubwa zaidi kwa Mwenyezi Mungu. Na hao ndio waliofuzu.
(21) Mola wao Mlezi anawabashiria rehema zitokazo kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo wana neema za kudumu.
(22) Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo makubwa.
(23) Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa marafiki walinzi wenu ikiwa wanaupendelea ukafiri kuliko Imani. Na mwenye kuwafanya marafiki walinzi miongoni mwenu, basi hao ndio madhalimu.
(24) Sema: Ikiwa baba zenu, na wana wenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mlizozichuma, na biashara mnazohofia kuharibika kwake, na makazi mnayoyaridhia, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kufanya Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu aje na amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu wavukao mipaka.
(25) Hakika Mwenyezi Mungu aliwanusuru katika maeneo mengi, na siku ya Hunayni wakati wingi wenu uliwapa majivuno, lakini haukuwafaa kitu, na ardhi ikawa finyu kwenu pamoja na upana wake. Kisha mkageuka mkapeana migongo.
(26) Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya Waumini. Na akateremsha majeshi ambayo hamkuyaona, na akawaadhibu wale waliokufuru. Na hayo ndiyo malipo ya makafiri.
(27) Kisha baada ya hayo Mwenyezi Mungu atamkubalia toba amtakaye. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(28) Enyi mlioamini! Hakika washirikina ni najisi, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakatifu baada ya mwaka wao huu. Na ikiwa mnahofia umasikini, basi Mwenyezi Mungu atawatajirisha kutoka katika fadhila zake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima kubwa.
(29) Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala Siku ya Mwisho, wala hawaharamishi yale aliyoharimisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki Dini ya haki, miongoni mwa wale waliopewa Kitabu, mpaka watoe kodi kwa hiari yao, hali wametii.
(30) Na Mayahudi walisema: Uzeir ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Na Wakristo walisema: Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ni kauli yao tu kwa vinywa vyao. Wanayaiga maneno ya wale waliokufuru kabla yao. Mwenyezi Mungu awaangamize! Wanageuzwa namna gani hawa!
(31) Waliwafanya makuhani wao na wamonaki wao kuwa ni mabwana badala ya Mwenyezi Mungu, na pia Masihi bin Maryamu. Na wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwabudu Mungu Mmoja, hapana mungu isipokuwa Yeye. Subhanahu, Ametakasika na hayo wanayoyashirikisha.
(32) Wanataka kuizima Nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, na Mwenyezi Mungu anakataa isipokuwa aitimize Nuru yake hata makafiri wakichukia.
(33) Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uwongofu na Dini ya haki ili aipe ushindi juu ya dini zote, hata washirikina wakichukia.
(34) Enyi mlioamini! Hakika wengi katika makuhani na wamonaki wanakula mali za watu kwa batili na wanazuilia Njia ya Mwenyezi Mungu. Na wale wanaolimbika dhahabu na fedha, wala hawazitumii katika Njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu chungu.
(35) Siku zitakapotiwa moto katika Moto wa Jahannamu, na kwazo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, wakaambiwa: Haya ndiyo mliyozilimbikia nafsi zenu. Basi onjeni mliyokuwa mkilimbika.
(36) Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na miwili katika andiko la Mwenyezi Mungu tangu alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko minne mitakatifu. Hiyo ndiyo Dini iliyonyooka sawa. Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamungu.
(37) Hakika kuahirisha (miezi) ni kuzidi tu katika kukufuru; wanapotezwa kwa hilo wale waliokufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuharimisha mwaka mwingine, ili wafanye kuwa sawa idadi ya ile (miezi) aliyoitukuza Mwenyezi Mungu, ndiyo wahalalishe yale aliyoyaharimisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao hivi. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu makafiri.
(38) Enyi mlioamini! Mna nini mnapoambiwa: Nendeni katika Njia ya Mwenyezi Mungu, mnajitia uzito katika ardhi? Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na Akhera siyo isipokuwa chache.
(39) Kama hamuendi, atawaadhibu adhabu chungu, na atawabadilisha na kaumu wasiokuwa nyinyi, wala nyinyi hamtamdhuru chochote. Na Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
(40) Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Mwenyezi Mungu alikwisha mnusuru walipomtoa wale waliokufuru, akiwa ni wa pili wa wawili walipokuwa katika pango, alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike. Hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja nasi. Basi Mwenyezi Mungu akauteremsha utulivu wake juu yake, na akamuunga mkono kwa majeshi ambayo hamkuyaona, na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na Neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(41) Tokeni muende mkiwa wepesi na wazito, na piganeni Jihadi kwa mali zenu na nafsi zenu katika Njia ya Mwenyezi Mungu. Hayo ni heri kwenu ikiwa mnajua.
(42) Lau ingelikuwa ipo faida ya papo kwa hapo, na safari fupi, basi hakika wangelikufuata. Lakini wameona ni mbali na kuna mashaka. Nao wataapa kwa Mwenyezi Mungu: Tungeliweza, basi bila ya shaka tungelitoka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo.
(43) Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini ukawapa ruhusa kabla ya kukubainikia wale wanaosema ukweli, na ukawajua waongo?
(44) Hawakuombi ruhusa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho ili wafanye Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema wachamungu.
(45) Hakika wanakuomba ruhusa tu wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu, na Siku ya Mwisho, na nyoyo zao zikatia shaka. Basi hao wanasitasita katika shaka yao.
(46) Na wangelitaka kweli kutoka, basi bila ya shaka wangelikuandalia maandalizi. Lakini Mwenyezi Mungu alichukia kutoka kwao, kwa hivyo akawazuia na ikasemwa: Kaeni pamoja na wanaokaa!
(47) Lau wangelitoka kati yenu, wasingeliwazidisha isipokuwa mchafuko, na wangetangatanga kati yenu wakiwatakia fitina. Na miongoni mwenu wapo wanaowasikiliza sana. Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.
(48) Hakika, walikwisha taka fitina tangu zamani, na wakakugeuzia mambo, mpaka ikaja haki na ikadhihirika amri ya Mwenyezi Mungu hali kuwa wao wamechukia.
(49) Na miongoni mwao wapo wanaosema: Niruhusu wala usinifitini. Kwa yakini wao hivyo wamekwishatumbukia katika fitina. Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri.
(50) Likikupata zuri, linawawia baya. Na ukikusibu msiba, wanasema: Sisi hakika tuliangalia mambo yetu vizuri tangu zamani. Na wanageuka kwenda zao hali ya kuwa wamefurahi.
(51) Sema: Halitusibu isipokuwa yale aliyotuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye Mola wetu Mlinzi. Na kwa Mwenyezi Mungu, basi na wategemee Waumini!
(52) Sema: Hivyo mnatutazamia litupate lolote isipokuwa moja katika mazuri mawili? Na sisi tunawatazamia kuwa Mwenyezi Mungu atawasibu kwa adhabu kutoka kwake, au kwa mikono yetu. Basi tazamieni, nasi hakika tunatazamia pamoja nanyi.
(53) Sema: Toeni kwa kupenda au kwa kuchukia. Kamwe hakitakubaliwa kutoka kwenu. Kwani hakika nyinyi mmekuwa kaumu wavukao mipaka.
(54) Na hawakuzuiliwa kukubaliwa kutoa kwao isipokuwa kwa kuwa walimkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawaji kwenye Sala isipokuwa huku ni wavivu, wala hawatoi isipokuwa nao wamechukia.
(55) Basi zisikufurahishe mali zao wala wana wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwazo katika maisha ya dunia hii, na zitoke roho zao na hali wao ni makafiri.
(56) Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, wala wao si katika nyinyi. Lakini wao ni kaumu wanaoogopa.
(57) Lau kama watapata pa kukimbilia au mapango au pahala pa kuingia, basi hakika wangeligeuka kwenda huko huku wanakimbia mbio zisizozuilika.
(58) Na miongoni mwao kuna yule anayekusengenya katika kuhusiana na sadaka. Kwa hivyo wakipewa kwayo, wanaridhika. Na wasipopewa kwayo, tazama, wanakasirika.
(59) Na lau kuwa waliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila yake, na pia Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu!
(60) Hakika sadaka ni za mafakiri tu, na masikini, na wanaozitumikia, na wa kutiwa nguvu nyoyo zao, na katika kukomboa watumwa, na waliogharamika, na katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na wasafiri. Huu ni waajibu uliofaridhiwa na Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.
(61) Na miongoni mwao kuna wale wanaomuudhi Nabii na wanasema: Yeye ni sikio tu. Sema: Basi ni sikio la heri kwenu. Anamwamini Mwenyezi Mungu, na ana imani na Waumini, naye ni rehema kwa wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu, wana adhabu chungu.
(62) Wanawaapia kwa Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe nyinyi, ilhali Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndio wanaostahiki zaidi kwamba wao wawaridhishe ikiwa wao ni Waumini.
(63) Je, hawajui ya kwamba anayempinga Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo hakika ana Moto wa Jahannam adumu humo? Hiyo ndiyo hizaya kubwa.
(64) Wanafiki wanaogopa kwamba iteremshwe Sura juu yao itakayowaambia yale yaliyo katika nyoyo zao. Sema: Fanyeni stihizai! Hakika Mwenyezi Mungu atayatoa nje hayo mnayoyaogopa.
(65) Na ukiwauliza, bila shaka watasema: Hakika tulikuwa tukipiga porojo na kucheza tu. Sema: Kwani mlikuwa mkimfanyia masikhara Mwenyezi Mungu, na ishara zake, na Mtume wake?
(66) Msitoe udhuru. Hakika mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu! Tukilisamehe kundi moja miongoni mwenu, tunaliadhibu kundi jingine kwa kuwa wao wamekuwa wahalifu.
(67) Wanaume wanafiki na wanawake wanafiki, wote ni hali moja. Huamrisha maovu na hukataza mema, na huifumba mikono yao. Walimsahau Mwenyezi Mungu, basi na Yeye pia akawasahau. Hakika wanafiki ndio wavukao mipaka.
(68) Mwenyezi Mungu amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri Moto wa Jahannamu watadumu humo. Hiyo ndiyo inawatosha, na Mwenyezi Mungu amewalaani; nao wana adhabu ya kudumu.
(69) Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa wana nguvu na mali na watoto zaidi kuwaliko nyinyi. Basi walistareheka na fungu lao, na nyinyi mnastareheka na fungu lenu, kama walivyostareheka kwa fungu lao wale waliokuwa kabla yenu. Na nyinyi mkazama katika maovu kama wao walivyozama. Hao, matendo yao yaliharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio waliohasiri.
(70) Je, hazikuwajia habari za wale waliokuwa kabla yao, kaumu ya Nuhu, na A'ad, na Thamud, na kaumu ya Ibrahim, na watu wa Madyana, na miji iliyopinduliwa chini juu? Mitume wao waliwajia na hoja zilizo wazi. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.
(71) Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na husimamisha Sala, na hutoa Zaka, na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
(72) Mwenyezi Mungu amewaahidi Waumini wanaume na Waumini wanawake Bustani zipitiazo mito chini yake, watadumu humo. Na makazi mema katika Bustani za kudumu, na Radhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi kuliko yote. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(73) Ewe Nabii! Pambana na makafiri na wanafiki, na wawiye mgumu. Na makazi yao ni Jahannamu, na hapo ndipo pabaya zaidi pa kuishia.
(74) Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema; nao hakika wamekwisha sema neno la ukafiri, na wakakufuru baada ya kusilimu kwao. Na wakawa na utashi mkubwa juu ya yale ambayo hawakuweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila kwa kuwa Mwenyezi Mungu aliwatajirisha, na Mtume wake pia kutokana na fadhila zake. Basi wakitubu, itakuwa heri kwao. Na wakigeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu chungu katika dunia na Akhera. Na wala hawana katika ardhi mlinzi yeyote wala wa kuwanusuru.
(75) Na miongoni mwao kuwa wale waliomuahidi Mwenyezi Mungu kwamba: Akitupa katika fadhila yake, hapana shaka tutatoa sadaka, na tutakuwa katika waliotengenea.
(76) Basi alipowapa katika fadhila yake, wakaifanyia ubahili na wakageuka hali ya kuwa wamepeana mgongo.
(77) Basi akawafuatisha unafiki katika nyoyo zao mpaka Siku watakapokutana naye, kwa sababu ya kuwa walimvunjia Mwenyezi Mungu yale waliyomuahidi, na kwa sababu ya kusema kwao uongo.
(78) Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong'ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua sana ya ghaibu?
(79) Wale wanaowabeua Waumini wanaotoa sadaka nyingi na wasio nacho cha kutoa ila kiasi cha juhudi yao, hivyo wanawafanyia masikhara. Mwenyezi Mungu atawakejeli wao! Nao wana adhabu chungu!
(80) Waombee kusitiriwa dhambi, au usiwaombee kusitiriwa dhambi. Hata ukiwaombea kusitiriwa dhambi mara sabini, Mwenyezi Mungu hatawasitiria dhambi. Hayo ni kwa sababu ya kuwa wao walimkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu wavukao mipaka.
(81) Walifurahi walioachwa nyuma kwa kule kukaa kwao nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Na wakachukia kupigana Jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na wakasema: Msitoke kwenda katika joto! Sema: Moto wa Jahannamu una joto kubwa zaidi, laiti wangelikuwa wanafahamu!
(82) Basi na wacheke kidogo, na walie sana. Hayo ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.
(83) Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kikundi kimoja miongoni mwao - na wakakutaka idhini ya kutoka - basi sema: Nyinyi hamtatoka pamoja nami kabisa, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Hakika nyinyi mliridhia kukaa nyuma mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na hao waliobakia nyuma.
(84) Wala usimsalie kabisa yeyote katika wao akifa, wala usisimame kaburini kwake. Hakika hao walimkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakafa na hali ni wamevuka mipaka.
(85) Wala zisikupendeze mali zao na watoto wao. Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwa hayo katika dunia; na zitoke roho zao na hali wao ni makafiri.
(86) Na inapoteremshwa Sura kwamba muaminini Mwenyezi Mungu na piganeni Jihadi pamoja na Mtume wake, wale wenye nguvu miongoni mwao hukutaka ruhusa na wanasema: Tuache tuwe pamoja na wanaokaa nyuma!
(87) Waliridhia kwamba wawe pamoja na wabakiao nyuma, na nyoyo zao zikafunikwa, kwa hivyo hawafahamu.
(88) Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye, walifanya Jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na hao ndio wana heri nyingi. Na hao ndio waliofaulu.
(89) Mwenyezi Mungu amewaandalia Bustani zipitazo mito kwa chini yake, watadumu humo. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(90) Na walikuja wenye kutoa udhuru miongoni mwa Mabedui ili wapewe ruhusa, na wakakaa wale waliomdanganya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Itawafika wale waliokufuru miongoni mwao adhabu chungu.
(91) Hakuna lawama juu ya wanyonge, wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutoa, maadamu wanamsafia nia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakuna njia ya kuwalaumu wanaofanya mazuri. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(92) Wala wale wanaokujia ili uwape kipando, ukasema: Sina kipando cha kuwakubebea juu yake, kwa hivyo wanageuka kwenda huku macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kwamba hawatapata cha kutoa.
(93) Hakika njia ya lawama iko tu juu ya wale wanaokuomba ruhusa wasiende vitani ilhali wao ni matajiri. Waliridhia kwamba wawe pamoja na wanaosalia nyuma. Na Mwenyezi Mungu akaiziba mioyo yao. Kwa hivyo hawajui.
(94) Watawatolea udhuru mtakapowarudia. Sema: Msitoe udhuru; hatutawaamini. Mwenyezi Mungu amekwisha tujulisha habari zenu. Na Mwenyezi Mungu na Mtume wake wataviona vitendo vyenu. Kisha mtarudishwa kwa Mjuzi wa ya siri na ya dhahiri; naye atawaambia mliyokuwa mkiyatenda.
(95) Watawaapia kwa Mwenyezi Mungu mtakaporudi kwao ili muwaachilie mbali. Basi waachilieni mbali. Hakika hao ni najisi, na makaazi yao ni Jahannam, kuwa ni malipo kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.
(96) Wanawaapia ili muwe radhi nao. Lakini hata mkiwa radhi nao nyiye, basi hakika Mwenyezi Mungu hawi radhi na kaumu wavukao mipaka.
(97) Mabedui ndio wenye ukafiri mkubwa zaidi na unafiki, na wameelekea zaidi kutojua mipaka ya yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu juu ya Mtume wake. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua zaidi, Mwenye hekima.
(98) Na katika Mabedui hao kuna yule anayefikiri kuwa kile wanachotoa ni gharama ya bure, na anawatazamia nyinyi mambo yawageukie. Mageuko maovu yatakuwa juu yao! Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote.
(99) Na katika Mabedui kuna yule anayemwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na anakichukulia kile anachotoa kuwa ni cha kuwasogeza karibu kwa Mwenyezi Mungu na ya kupatia dua za Mtume. Ndiyo! Hizo hakika ni mambo ya kuwasogeza wao karibu. Mwenyezi Mungu atawaingiza katika rehema yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusitiri dhambi, Mwenye kurehemu.
(100) Na wale waliotangulia, wa kwanza, katika Wahajiri na Ansari, na wale waliowafuata kwa uzuri, Mwenyezi Mungu aliwaridhia, na wao walimridhia, na amewaandalia Bustani zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele. Huko ndiko kufuzu kukubwa.
(101) Na katika mabedui walio jirani zenu kuna wanafiki; na katika wakazi wa Madina pia wapo wale waliobobea katika unafiki. Wewe huwajui. Sisi tunawajua. Tutawaadhibu mara mbili, kisha watarudishwa kwenye adhabu kubwa.
(102) Na wengine walikiri dhambi zao, walichanganya matendo mema na mengine mabaya. Huenda Mwenyezi Mungu akakubali toba zao. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
(103) Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na uwatakase kwayo, na waombee dua. Hakika kuomba dua kwako ni utulivu kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia vyema, Mwenye kujua yote
(104) Je! Hawajui ya kwamba Mwenyezi Mungu anakubali toba ya waja wake, na anazichukua sadaka, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kukubali toba, Mwenye kurehemu sana?
(105) Na sema: Tendeni matendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake, na Waumini watayaona matendo yenu. Na mtarudishwa kwa Mwenye kujua siri na dhahiri; basi naye atawaambia yale mliyokuwa mkiyatenda.
(106) Na wapo wengine wanaongojea amri ya Mwenyezi Mungu. Ima atawaadhibu au atawakubalia toba. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua zaidi, Mwenye hekima.
(107) Na wapo waliojenga msikiti kwa ajili ya madhara, na ukafiri, na kuwafarikisha Waumini, na pa kuvizia kwa ajili ya wale waliompiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake hapo kabla. Na bila ya shaka wataapa kwamba: Hatukukusudia isipokuwa uzuri tu. Na Mwenyezi Mungu anashuhudia kuwa wao hakika ni waongo.
(108) Usisimame ndani yake kabisa. Msikiti uliojengwa juu ya msingi wa uchamungu tangu siku ya mwanzo unastahiki zaidi wewe usimame ndani yake. Humo wamo wanaume wanaopenda kujitakasa. Na Mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitakasa.
(109) Je, mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya uchaji utokao kwa Mwenyezi Mungu na radhi zake ni bora zaidi au mwenye kuweka msingi wa jengo lake juu ya ukingo wa shimo unaoporomoka? Kwa hivyo ukaporomoka naye ndani ya Moto wa Jahannamu? Na Mwenyezi Mungu hawaongoi kaumu madhalimu.
(110) Na jengo lao hilo walilolijenga halitaacha kuwa shaka katika nyoyo zao mpaka nyoyo zao hizo zikatike vipande vipande. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema, Mwenye hekima.
(111) Hakika Mwenyezi Mungu alinunua kutoka kwa Waumini nafsi zao na mali zao kwa kuwa wao wana Pepo. Wanapigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu, kwa hivyo wanaua na wanauawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Taurati, na Injili, na Qur-ani. Na nani atimizaye zaidi ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.
(112) Wale wanaotubia, wanaoabudu, wanaohimidi, wanaokimbilia heri, wanaorukuu, wanaosujudu, wanaoamrisha mema na wanaokataza maovu, na wanaolinda mipaka ya Mwenyezi Mungu. Na wabashirie Waumini.
(113) Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, hata wakiwa ni jamaa zao, baada ya kwisha wabainikia kuwa hao ni watu wa Motoni.
(114) Wala haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake isipokuwa kwa sababu wa ahadi aliyomuahidi. Lakini ilipombainikia kwamba yeye ni adui ya Mwenyezi Mungu, alijiweka mbali naye. Hakika Ibrahim alikuwa mwingi wa kuomba, mnyenyekevu, mvumilivu.
(115) Na haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwapotosha kaumu baada ya kwisha waongoa mpaka awabainishie ya kujiepusha nayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kujua vyema kila kitu.
(116) Hakika Mwenyezi Mungu anao ufalme wa mbingu zote na ardhi; huhuisha na hufisha. Nanyi hamna mlinzi yeyote wala msaidizi kando na Mwenyezi Mungu.
(117) Mwenyezi Mungu alikwisha kubali toba ya Nabii na Wahajiri na Ansari waliomfuata katika saa ya ugumu, baada ya kwamba nyoyo za kundi miongoni mwa zilikuwa zimekaribia kukengeuka. Basi akakubali toba yao. Hakika Yeye kwao ni Mpole, Mwenye kurehemu.
(118) Na pia wale watatu walioachwa nyuma hata ardhi wakaiona kuwa ni finyu juu yao pamoja na ukunjufu wake, na nafsi zao zikawabana, na wakayakinika kuwa hakuna kimbilio kutoka kwa Mwenyezi Mungu isipokuwa kwake Yeye. Kisha akawakubalia toba ili nao watubu. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kukubali toba sana, Mwenye kurehemu.
(119) Enyi mlioamini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli.
(120) Haiwafailii watu wa Madina na Mabedui walio kando kando yao kusalia nyuma wasitoke na Mtume, wala kujipendelea nafsi zao kuliko nafsi yake. Hayo ni kwa sababu wao hakiwapati kiu, wala machovu, wala njaa, katika Njia ya Mwenyezi Mungu, wala hawendi mahali panapowaghadhibisha makafiri, wala hakiwapati chochote kutokana na maadui, isipokuwa huandikiwa kuwa ni kitendo chema. Hakika Mwenyezi Mungu haupotezi ujira wa wanaofanya uzuri.
(121) Wala hawatoi masurufu madogo wala makubwa, wala hawalivuki bonde, isipokuwa huandikiwa, ili Mwenyezi Mungu awalipe bora zaidi ya yale waliyokuwa wakiyatenda.
(122) Na haiwapasi Waumini kutoka wote pamoja. Lakini kwa nini hawatoki baadhi katika kila kundi miongoni mwao, wakajifunze vyema Dini, na kisha waje kuwaonya wenzao watakapowarudia, ili wajihadharishe?
(123) Enyi mlioamini! Piganeni na wale walio karibu yenu miongoni mwa makafiri, na wakute ugumu kwenu. Na jueni ya kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamungu.
(124) Na inapokwisha teremshwa Sura, basi wapo miongoni mwao wasemao: Ni nani miongoni mwenu Sura hii imemzidishia Imani? Ama wale walioamini iliwazidishia Imani, nao wanafurahi.
(125) Na ama wale wenye maradhi katika nyoyo zao, basi iliwazidishia uovu juu ya uovu wao; na wanakufa hali ya kuwa wao ni makafiri.
(126) Je, hawaoni ya kwamba wanajaribiwa kila mwaka mara moja au mara mbili? Kisha hawatubu, wala hawakumbuki.
(127) Na ikishateremka Sura, hutazamana wao kwa wao, (kama kwamba wanasema:) Je, yuko yeyote anayewaona nyinyi? Kisha huondoka wakaenda. Mwenyezi akaziondoa nyoyo zao kwa kuwa hao ni kaumu wasiofahamu.
(128) Hakika amekwisha wajia Mtume kutokana na nyinyi wenyewe; yanamhuzunisha yale yanayowataabisha, anawajali sana, kwa Waumini ni mpole na mwenye huruma.
(129) Kwa hivyo, wakigeuka, basi wewe sema, ”Mwenyezi Mungu ananitosha. Hakuna mungu isipokuwa Yeye tu. Mimi ninamtegemea Yeye, na Yeye ndiye Mola Mlezi wa Kiti Kikuu cha Enzi.